Thursday, August 12, 2010

DR SLAA APASULIWA MKONO

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbroad Slaa, amepasuliwa mkono katika Hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam ili kurekebisha mkono alioumia, hali yake inaendelea vizuri.

Akizungumza na mwandishi wetu jana, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, alisema baada ya upasuaji huo, mgombea huyo alipumzishwa katika wadi ya Kitengo cha Mifupa Muhimbili (Moi), Muhimbili.

“Hali yake inaendelea vizuri na leo (jana) saa sita mchana, alifanyiwa upasuaji mdogo kwa ajili ya merekebisho kwenye mkono alioumia na tunatarajia baadaye ataruhusiwa,” alisema Lwakatare.

Mwandishi wetu alikwenda katika hospitali hiyo ili kuweza kumwona, lakini mmoja wa maofisa wa Kitengo cha Habari cha Moi, alisema mgombea huyo aliomba waandishi wa habari wasiruhusiwe kumwona na kwamba taarifa za ugonjwa wake zitatolewa na chama chake baadaye.

“Ugonjwa wa mtu ni siri yake, hivyo siwezi kusema lolote zaidi ya kukiri kuwa kweli tunaye hapa hospitalini amelazwa, tayari alishatoa agizo kuwa waandishi wa habari wasiruhusiwe kumwona na taarifa zozote kuhusu hali yake zitatolewa makao makuu ya chama hicho, kitaitisha mkutano wa waandishi wa habari,” alisema ofisa huyo ambaye pia alikataa kutaja jina lake.

Hivi karibuni Dk Slaa, aliumia mkono wa kushoto baada ya kuanguka bafuni ambapo alipewa matibabu katika hospitali ya Bugando, Mwanza na kuendelea na mikutano yake ya kutafuta wadhamini.

Lucy Lyatuu anaripoti kwamba Kamati Kuu ya Chadema, imethibitisha wagombea ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema hayo jana Dar es Salaam katika mkutano huo na kuongeza kuwa Baraza Kuu pamoja na mambo mengine, litapitia Ilani ya chama hicho. Alisema leo mkutano mkuu utapitisha wagombea wote.

Katika taarifa ya juzi, Msimamizi wa Uchaguzi wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Dk. Kitila Mkumbo, alisema kutokana na kufutwa kwa uchaguzi huo, atapeleka taarifa kamili kuhusu mchakato wa uchaguzi huo kwa Katibu

Mkuu ambaye ataishauri Kamati Kuu hatua za kuchukuliwa yakiwamo mapendekezo ya jinsi ya kupata wabunge wa viti maalumu.

Habari hizi ni kwa mujibu wa gazeti la HabariLeo

1 comments:

Harry said...

Ni kweli kabisa Dr Slaa anendelea vizuri maana kama rafiki wa Dr. Slaa nilipata nafasi ya kumtembelea leo asubuhi na kumkuta imara kabisa. Anatoa salaam nyingi kwa marafiki zake wote popote walipo na namnukuu " Mungu awabariki sana marafiki zangu" mwisho wa kunukuu.

Post a Comment