Sunday, August 8, 2010

wajibu wa viongozi wa kata, vijiji na vitongoji katika uchaguzi mkuu 2010

Hotuba ya Mhe Anthony Komu, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala juu ya wajibu wa viongozi wa kata, vijiji na vitongoji katika uchaguzi mkuu 2010

Ukumbi wa Mississipi Resort - Moshi Vijijini


Waheshimiwa viongozi wa CHADEMA na wale Serikali, awali ya yote nawapa hongera sana kwa kuchaguliwa katika uchaguzi uliyopita wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kupitia chama chetu, hasa kutokana na uchaguzi mzima kutawaliwa na hila na mizengwe.

Ninatambua ilivyo ghali kuwa katika upinzani katika nchi yetu. Nyote mnajua bila shaka yeyote mizengwe ambayo huelekezwa kwetu na watumishi wa umma wasiotimiza matakwa ya utawala wa sheria. Pamoja na adha hizo, ninyi mmekuwa mfano wa kuigwa. Mmesimama imara kutimiza wajibu wenu wa kikatiba.

Ninafahamu jinsi mlivyopambana kulinda haki zenu. Hamkujali, hila, hadaa wala vitisho vya baadhi ya wanachama na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake waliotumia baadhi ya watendaji wa vijiji, kata na wilaya kudhulumu haki zenu.

Waheshimiwa viongozi, ndani ya serikali zenu, mko viongozi wanaotokana na vyama tofauti, hivyo ni wajibu wenu sasa kuzika tofauti zenu za kisiasa ili muweze kutimiza wajibu wenu wa kuwatumikia wananchi waliowachagua.

Ninyi wote hapa, na wale ambao hawapo hapa waliotokana na vyama vingine, wakati mliomba uongizi ni wazi kwamba mlikuwa na lengo moja la kuwatumikia wananchi. Naowaomba sana timizeni wajibu huo. Vilevile, ninaimani kwamba mtayatumia vema mafunzo haya ya siku moja katika uchaguzi ujao ili kuwezesha wananchi kupata viongozi bora, wenye uchungu na rasilimali za taifa na ambao wananena wanachokitenda.

Mkiwa viongozi wa serikali mliokaribu na wananchi, katu msikubali wananchi wenu kuwapa nafasi viongozi wanafiki, wezi wa mali ya umma, eti kwa sababu wamehongwa pombe au doti ya kanga.

Kwa zaidi ya miaka 40 sasa, taifa letu limekuwa nyuma kimaendeleo kutokana na vitendo haramu vya kutumia fedha kuingia madarakani vinavyofanywa na baadhi ya wanasiasa.

Ninawaomba sana, tena sana kwamba tumieni kila uwezo wenu, kufanya fedha kuwa mtaji wa kuvuna kura katika uchaguzi ujao ukome. Kwa kufanya hivyo, kutasaidia taifa kupata viongozi bora.

Ni wajibu wenu kuwauliza wale wanaokuja na fedha: Wamepata wapi mabilioni yote hayo? Je, kama wanataka kutumia fedha kuingia madarakani, watawezaje kuzirudisha wakati katika siasa hakuna biashara?

Swali hili ni muhimu sana hasa katika kipindi hiki ambacho taifa letu limetumbukizwa na baadhi ya wanasiasa katika dhahama ya mikataba michafu, kama vile Richmond, EPA na ununuzi wa Rada.

Kuibuka kashfa hizi katika kipindi hiki ambacho viongozi wa CCM wamekiri kwamba rushwa ni donda dugu ndani ya serikali, kunathibitisha kwamba fedha nyingi zinazotumika katika uchaguzi zimepatikana kwa njia ya wizi.

Kuendelea kuchagua viongozi wanaootumia fedha kuingia madarakani kutazidi kuangamiza taifa kwa kuibua mikataba mingine ya hovyo. Hali kama hiyo ipo pia katika Jimbo letu, yapo maeneo kadhaa mali za wananchi zimepewa watu wachache kwa manufa binafsi.

Aidha, ninaomba nichukue fursa hii nijibu swali moja ambalo nimekuwa naulizwa karibu kila mahali katika Jimbo la Moshi-Vijijini, kwamba nitagombea tena ubunge mwaka 2010? Swali hili limekuwa likiulizwa kwa namna mbalimbali kama ombi, kama lawama, kama onyo, kuwa nataka kuwaacha katika mataa au kuwasusa watu wangu.

Yote hayo katika tafakari zangu na baadhi ya wananchi inaonyesha kuwa kuna walakini katika uwakilishi tulionao bungeni.

Waheshimiwa viongozi ni lazima kama viongozi tujibu kiu ya wananchi hao. Ni lazima nitoe majibu kwa kila swali ninaloulizwa na wananchi. Na huo ndiyo msingi wa kuwa kiongozi.

Waheshimiwa viongozi, watu wa Moshi-Vijijini wanasema nisiwaache kwa kuwa wana matatizo ya msingi ambayo hayajapatiwa ufumbuzi na hakuna matumaini ya kupatiwa ufumbuzi chini ya utawala na uwakilishi wa sasa.

Sote hapa ni mashahidi, kwamba hali ya uchumi wa jimbo letu inaporomoka kila kukicha, vyanzo vya mapato vimekufa kabisa, zao la kahawa linateketea, miundo mbinu kwa ajili ya umwagiliaji inaendelea kutoweka; hivyo hata mazao kwa ajili ya chakula kwa kiasi kikubwa yanashindikana.

Si hivyo tu, kuna tatizo jingine kubwa na la msingi. Uwezo wa wananchi Moshi-Vijijini kusomesha watoto wao unapungua kila mwaka. Ni lazima tutoe majibu sahihi.

Wananchi wengi, hasa ninyi mliopo hapa mnasema kwamba Chama Cha Mapinduzi kimeshindwa kutoa majibu sahihi kwa matatizo haya. Nakubaliana nanyi.

Hatuhitaji miujiza kuondokana na matatizo yanayolikabili jimbo letu, tunahitaji uongozi na uwakilishi wenye nia ya dhati ya kumwendeleza mwananchi wa kawaida. Kwa mfano, ni kwanini vihamba (Mashamba yetu) yasipimwe tukapata uwezo wa kufanya biashara na mabenki? Kwa nini viongozi wetu wasisimamie hili na Moshi Vijijini ikarudi katika enzi zake?

Waheshimiwa viongozi kutokana na matatizo hayo na ombwe kubwa la uongozi lilipo ndani na nje ya Bunge, ninachukua nafasi hii kuutangazia ulimwengu kwa ushahidi wenu kupitia kwa wanahabari wetu kuwa sitawaacha watu wangu wa Moshi-Vijijini.

Ninatangaza rasmi kama mnavyotaka kuwa kwa kufuata taratibu zilizowekwa na chama changu, nitakuwa miongoni mwa wanachama watakaomba ridhaa ya chama ya kugombea ubunge katika jimbo hili. Iwapo chama kitaniteuwa, ninawahikishia kuwa nitasimama imara katika kutatua matatizo yaliyoorodheshwa.

Naamini tukiwa wamoja, hatuna cha kupoteza. Tutasimama imara kupambana na ulaghai, ufisadi, uzandiki na ufedhuli wa muda mrefu uliowekwa na viongozi tulionao.

Mwisho, ninawatakia safari njema ya kurudi huko mlikotoka kwa salama na amani ili kuweza kuendelea na majukumu yenu mengine mliyonayo ya ujenzi wa taifa na chama chetu.

Pamoja tutashinda.

0 comments:

Post a Comment