Tuesday, August 10, 2010

Barua kwa walioshindwa kura za maoni CCM 2010

John Malecela
Wasalaam mlioshindwa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi ‘CCM’ kwa mizengwe. Ingawa nimeambiwa mchakato ulikuwa na ufisadi mwingi kiasi cha kuwafanya mchoke kimwili na kiakili, ninyi pia mmenichosha kwa kutopatikana kwenu uswahilini.

Leo ni siku ya tano nawatafuta niwape ujumbe kutoka ndani ya akili zangu nilizopewa na Mungu kama zawadi, lakini mmekuwa hamuonekani kabisa. Kila nilipofika nyumbani kwenu niliambiwa mmelala kwa uchovu na mmepiga marufuku msiamshwe na mtu yeyote, eti mnapumzika.

Mnalala wakati taifa linateketea, mnataka mimi mwenye akili niamini nini kuhusu nia yenu ya kutaka kuteuliwa kuwa wagombea? Kwamba mlihitaji vyeo na si kuwatumikia wananchi? Hapana mzee Arcado Ntagazwa usitake kunidanganya, nina akili nyingi …sisemi kuliko wewe lakini zinazidi.

Kama alivyosema Lucas Selelii, katika vita yenu ya mchakato wa kuwapata wagombea ndani ya chama chenu mmegombana na ‘mashehe’, lakini si ‘uislam’. Hii ina maana kwamba walioiba kura zenu, waliocheza rafu ni ‘mashehe’, ila ‘uislam’ kwa maana ya chama ni safi.

‘Mashehe’ hawa waliochakachua kura zenu kwenye chama chenu wapo kila chama, mkitaka ushahidi muulizeni Fredy Mpendazoe ambaye aliondoka CCM kwa mbwembwe na kukimbilia Chama Cha Jamii na hatimaye CHADEMA, ambako nako aliwakuta ‘mashehe’ anaowalalamikia leo kumuibia kura za ubunge Jimbo la Segerea.

Hivi kushindwa kwenye kura za maoni kuna maana gani ukilinganisha na nia yenu ya kuwatumikia wananchi kama ni kweli? Nijuavyo mimi heshima ya mtu kwenye jamii si uongozi, bali ni wajibu safi wenye lengo la kizalendo kwa taifa lake.

Sitaki kuamini kwamba nafasi ya kusaidia jamii iko kwenye siasa, uongozi, ubunge au urais pekee, kama ingekuwa hivyo, Reginald Mengi asingesaidia jamii mpaka Watanzania wamchague awe rais.
Kwa akili zangu naamini walioshindwa kwenye kura za maoni, wengi wao wanaumia kwa sababu ya ulevi wa madaraka na imani potofu kwamba usipokuwa na cheo huwezi kuongoza.

Kasoro hii ya imani ndiyo inayowafanya baadhi ya watu kutumia uwezo wao wote kupata nguvu ndani ya chama ili kujihakikishia ufalme wa nchi, kiasi cha kuwaburuza Watanzania zaidi ya milioni 45 watumike kama vibaraka wao, kwa lengo la kulinda maslahi yao binafsi. Kwa hili wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Nashangaa leo tunapokutana kwenye vikao vyetu vya kahawa tunajadili kuanguka kwa mpiganaji Joel Bendera, ……na kusahau kuwa jamii imeangushwa na mafisadi kabla ya mchakato wa kuwapata viongozi bora.
Kwenye kura za maoni tumesikia baadhi ya matokeo yakitangazwa kinyume na wananchi walivyotarajia, na kwingine kiongozi mmoja wa chama akiamua kugeuza matokeo na kumpa ushindi mgombea aliyempenda kabla ya kiongozi mwingine hajatumia wadhifa wake kubatilisha matokeo hayo.

Mambo yote hayo yamefanywa huku jamii iliyolazwa usingizi ikiangalia na kushindwa kutetea haki yake ya msingi ya kuchagua viongozi bora. Katika hali hii, mtetezi wa viongozi bora wasiotakiwa na mafisadi ni nani kama si nguvu ya umma inayonunuliwa leo kwa pesa?

Bila shaka tiba ya uovu huu haipatikani kwa wote kuvutana ndani ya vyama vya siasa ambavyo mpaka sasa vina wenyewe, dawa sahihi ya gonjwa hili ni kwenu ninyi mlioshindwa kwenye kura za maoni ilhali mna nia njema kwa jamii, kurudi kutumikia wananchi kwa mfumo wa kuongoza bila cheo ‘leading without title’.

Naamini mfumo huu ukitengenezwa na kumuwezesha kila Mtanzania kuwa kiongozi mahali alipo, kukawa na viongozi shambani, ofisini, shuleni, mitaani, kwenye familia na wote wakahakikisha maslahi ya taifa yanalindwa, tutakuwa tumepata dawa ya kuondoa mfumo wa watu wachache ndani ya vyama kuendesha nchi wapendavyo.

Uamuzi wa kuhama chama unaweza kuwa na shabaha ya kulipa maumivu ya kisiasa tu, lakini usiwe tiba ya kunyausha mizizi ya mizegwe na hivyo kuwaacha wafalme wakiendelea kutawala watakavyo.

Natangulia kuiongoza jamii bila cheo, karibuni waheshimiwa wengine tujenge shule, zahanati, tuweke mabomba ya maji, tufungue kliniki na tuhamasishane kulinda maslahi ya taifa letu. Bila shaka tukifanya hivyo tutakuwa viongozi wa kijamii tutakaoheshimika na vizazi vyote, kuliko kulilia nafasi ya ubunge.

http://www.globalpublishers.info/profiles/blogs/barua-kwa-walioshindwa-kura-za

0 comments:

Post a Comment