Juu mfanyabiashara maarufu na muumini wa maendeleo ya kijamii nchini, BW. Mustapha Jaffar Sabodo akimkabidhi hundi ya shilingi milioni 100 Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA Mh.Freeman Mbowe aliyeambatana na Katibu Mkuu wake Dr Wilibrod Slaa leo jijini Dar.
Chini Bw. Sabodo akiongea na Mh. Mbowe na Dk. Slaa
*ASIFU UMAKINI WAKE NDANI NA NJE YA BUNGE
*AWAPONGEZA MBOWE NA DR SLAA
*AAHIDI KUCHANGIA ZAIDI
Mfanyabiashara maarufu na muumini wa maendeleo ya kijamii nchini, Mustapha Jaffar Sabodo amekichangia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo-CHADEMA shilingi milioni mia moja ili kuimarisha upinzani na demokrasia nchini.
Bw. Sabodo amekabidhi hundi ya kiasi hicho cha fedha leo jijini Dar kwa Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA Bw. Freeman Mbowe aliyeambatana na Katibu Mkuu wake Dr Wilibrod Slaa na Mkurugenzi wa Fedha wa chama hicho Bw. Antony Komu.
Akikabidhi hundi hiyo Bw. Sabodo amesema pamoja na kwamba yeye ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi lakini anapenda kuona upinzani na demokrasia vinaimarika nchini huku akikitaja CHADEMA kuwa ni chama makini na safi cha upinzani.
Bw. Sabodo amekuwa mmoja wa wazee walio wazi katika kukosoa utendaji wa serikali ya chama chake CCM hasa inapokiuka misingi ya utawala bora iliyojengwa na Mwasisi wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere.
“Mimi ni mwanachama wa CCM lakini napenda kuona demokrasia ikikua huku kambi ya upinzani ikiimarika kwa kuwa na wabunge wengi bungeni ili kushamirisha maendeleo nchini……na nawachangia CHADEMA kwa kuwa natambua umakini wenu katika siasa za hapa nchini na hasa Bungeni”, Alisema.
Bw. Sabodo amesema kuongezeka kwa wabunge wa upinzani bungeni ni jambo la muhimu katika kutoa upinzani kwa CCM na kusukuma maendeleo ya wananchi huku akikitaka CHADEMA kuongeza nguvu zaidi katika harakati zake za kisiasa na kumwelezea Dr Slaa kuwa ni mwanasiasa mwenye uchungu wa kweli na watanzania.
Aidha Bw. Sabodo amesema ana mpango wa kuichangia fedha zaidi CHADEMA ili kuimarisha harakati zake za kisiasa na kuahidi kufanya hivyo atakaporejea nchini akitokea India kwenye matibabu.
Akizungumza katika makabidhiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwa Bw. Sabodo Mtaa wa Upanga Jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe ameshukuru na kutaja msaada huo kuwa ni wa kihistoria katika siasa za vyama vingi nchini.
Amesema mara nyingi imekuwa ni vigumu kwa wafanyabiashara wakubwa wa kada ya Bw. Sabodo kuchangia kwa uwazi tena kiasi kikubwa cha fedha na kutaka hatua hiyo kuigwa na wafanyabiashara wengine nchini.
“Kwa kweli tunashukuru sana hii ni historia mpya katika siasa za vyama vingi nchini, ni wajibu wa wafanyabiashara wakubwa kuona umuhimu wa kusaidia vyama vyote makini nchini bili kuwa na ubaguzi wala woga, Mzee ameonyesha njia naamini itakuwa ni mfano kwa wengine wenye uwezo, Alisema Bw. Mbowe.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Dr Slaa ameshukuru kwa mchango huo na kudokeza kwamba mchango utatumika kwa kadiri ya vipaumbele vitakavyopangwa kwenye Kamati Kuu ya chama inayotarajiwa kufanyika tarehe 20 Julai 2010 ikilenga zaidi katika kutekeleza mipango endelevu ya kuimarisha chama kama Operesheni Sangara na utekelezaji wa mikakati ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
“Nawaomba watanzania wengine wa kada na uwezo mbalimbali kuichangia CHADEMA ili kuondokana na ukiritimba wa chama kimoja kwani ni hatari kwa maendeleo na usalama wa nchi kama michango yote ikielekezwa kwa chama tawala pekee.
“Natoa mwito kwa vyombo vya dola kuacha kuwatisha watanzania wenye mapenzi mema wanaochangia vyama mbadala kama CHADEMA kwani kufanya hivyo ni kuhujumu taifa na kukwamisha maendeleo ya nchi”, alisema
Imetolewa tarehe 12 Julai na:
Erasto Tumbo
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
0 comments:
Post a Comment