Sunday, August 8, 2010

Mkono Achemsha kwa Dr Slaa ashindwa kumstaki

Saturday, 22 September 2007

Mwanasheria maarufu nchini, Bw. Nimrodi Mkono amekanusha madai yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa kuwa yeye ni mkurugenzi wa makampuni mbalimbali hapa nchini yanayotuhumiwa kuiba fedha za serikali.

Hata hivyo, Bw. Mkono amesema hana nia ya kumfikisha Dk. Slaa mahakamani kwa kumchafulia jina lake kwa kile alichosema hana hela ya kumlipa.

Bw. Mkono aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi kupitia kwa waandishi wa habari juu ya tuhuma za kutafuna fedha za serikali kupitia kesi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Valambhia zilizotolewa dhidi yake na Dk. Slaa hivi karibuni.

Juzi Bw. Mkono alikaririwa na gazeti moja la kila siku
akisema hatokubali tuhuma hizo ziishie hewani.

Hata hivyo, Bw. Mkono alikiri kulipwa kiasi kikubwa cha fedha kutoka BoT lakini alisema hiyo ni sehemu ya malipo halali kwa kuitetea serikali isipoteze mamilioni ya fedha.

Mwanasheria huyo ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Vijijini Mkoani Mara alisema anaona uchungu kuambiwa kuwa yeye ni mfisadi pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali.

Alisema ana ushahidi wa wazi kwamba fedha anazolipwa na serikali kwa kuitetea BoT dhidi ya Valambhia ni halali na wala hazina dalili za rushwa.

Aidha, Bw. Mkono alisema, gharama za kuendesha kesi hiyo zimekuwa kubwa kutokana na kuendeshwa muda mrefu bila kufikia mwisho.

Alisema kesi hiyo ina mawakili wanane ambao kila mmoja analipwa Dola za Marekani 500 kwa saa na anafanya kazi saa nane ambapo kwa ujumla analipwa Dola 4,000.

Aliongeza kuwa kila wakili katika kesi hiyo analipwa Dola 1,000 kwa saa inapofanyika nje ya nchi ambapo malipo yanafikia Dola 8,000 kwa hizo saa.

Dola moja ya Marekani ni sawa na Sh. 1280 ambapo akilipwa Dola 500 ni sawa na Sh. 640,000 kwa saa na akilipwa Dola 1000 akiwa nje ya nchi ni sawa na Sh.1,280,000 kwa saa.

Kwa ujumla Bw. Mkono analipwa fedha na BoT kila anapohudhuria mahakamani katika saa nane akiwa nchini Sh. 5,120,000 na nje ya nchi Sh. 10,240,000 na kwamba haijulikani kesi hiyo itakwisha lini.

Alifafanua kuwa Dk. Slaa ambaye mara kwa mara alimuita `Father` alikurupuka kumtaja kwamba yeye ni mkurugenzi wa makampuni mbalimbali bila kwenda kuangalia kwa Wakala wa Usajili wa Makampuni na Leseni, (BRELA).

Bw. Mkono aliwakejeli wapinzani kwa kuwaambia kuwa hawajui kusoma wala kuandika ndiyo maana wameshindwa kujua kumtukana Rais wa nchi kwenye majukwaa ya siasa ni kosa.

Alimwambia Dk. Slaa aende kanisani kuungama makosa yake kwa kuwa aliwahi kuwa Padri kutokana na dhambi alizofanya kwa kusema uongo dhidi yake.

`Huyu ni `Father` nimemuita aje tuongee mezani nimweleze ukweli amekataa lakini mimi nasema aende tu kanisani na Mungu atamsamehe makosa yote,` alisema.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Dk. Slaa alitoa madai dhidi ya Bw. Mkono kupitia kampuni yake ya uwakili kuwa anatafuna fedha nyingi za serikali.

Dk. Slaa alisema, BoT inadaiwa Sh. bilioni 60 dhidi ya Valambhia ambapo hadi sasa Bw. Mkono amelipwa Sh. bilioni nane kama sehemu ya gharama ya kuitetea benki hiyo.

Hata hivyo, Bw. Mkono alisema, lazima aendelee kuitetea BoT na kwamba asipolipwa kiasi hicho atajitoa katika kesi hiyo ambayo inafanyika ndani na nje ya nchi. (Chanzo Nipashe)

0 comments:

Post a Comment