Monday, August 9, 2010

Mushengezi J.J. Nyambele - TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI - Kujiunga CHADEMA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UTANGULIZI:

Kwa muda mrefu nimeulizwa na baadhi ya Wananchi wa Wilaya yetu ya Ngara ni kwa nini sigombei ubunge wa Wilaya hii. Kila nilipoulizwa hivyo nilijibu kuwa mimi nimekuwa mbunge wa Ngara tangu nikiwa shuleni hadi sasa. Nimekuwa nikitoa mifano michache ifuatayo:

Tarehe 4 Oktoba 1968 ilichapishwa kwenye gazeti la “ The Standard “ barua yangu kwa wasomaji iliyokuwa na kichwa cha habari “NGARA - A PART OF TANZANI ?” nikiuliza iwapo Ngara ni sehemu ya Tanzania. Katika barua hiyo nilieleza kuwa Wilaya ya Ngara imesahaulika kimaendeleo na kwamba kiasi cha kodi ya kichwa (Shs. 56/= kila mtu mzima kwa mwaka) kilikuwa juu kuliko Wilaya nyingine ya Tanzania. Aidha nilieleza masikitiko yangu kuwa mara kadhaa viongozi wa kitaifa walikuwa wanatembelea Wilaya za Bukoba, Karagwe na Biharamulo bila kufika Ngara.

Mwezi Januari, 1969 niliandika barua nyingine kwenye gazeti hilo hilo. Barua hiyo ilichapishwa tarehe 31 Januari, 1969 chini ya kichwa cha habari ‘ANOTHER CRY FROM NGARA’ yaani kilio kingine kutoka Ngara. Katika barua hiyo ‘nilijiunga mkono’ kwa ile barua ya kwanza na kusisitiza kuwa Wilaya ya Ngara imetelekezwa na Serikali na wanasiasa, huku watu wakiumizwa na kiwango kikubwa sana cha kodi bila kuona maendeleo yanayotokana na kodi hiyo. Nilieleza kwamba hospitali chache zilizokuwapo wakati huo zilikuwa zinatoa huduma mbovu kutokana na kukosa vifaa na maawa ya kutosha. Nililalamikia pia huduma mbovu za posta ndogo ambayo wakati huo ilikuwa inatumika kutunza fedha huku ikishindwa kulipa wateja pale walipotaka kuchukua sehemu ya fedha zao.

Ukiacha “uwakilishi” huo wa kwenye ujana, baada ya kuhitimu na kuanza kazi, mimi nimekuwa sehemu ya Ngara zaidi ya nilivyokuwa sehemu ya ughaibuni nilikokuwa ninafanya kazi. Kila mwaka nimekuwa nakuja nyumbani na kukaa na wananchi na pia viongozi wa Wilaya na kubadilishana mawazo juu ya maendeleo ya watu wetu.

Sipendi kujisifia juu ya mchango wangu binafsi kwa Wilaya ya Ngara, lakini ni dhahiri kwa wote wanaonifahamu kuwa nimewekeza zaidi katika Wilaya hii kuliko sehemu nyingine yoyote. Kwa muda wa miaka 20 na zaidi nimekuwa nawekeza wilayani si pungufu ya Shs milioni 20 kila mwaka hivyo kuinua uchumi wa wilaya yetu na kutoa ajira kwa baadi ya watu wake.

MCHANGO WANGU KITAIFA

Pamoja na kwamba niliondoka katika utumishi wa umma kutokana na vitendo vya shari na kibaguzi vya baadhi ya viongozi katika serikali ya awamu iliyopita, mimi nimeendelea kutoa mchango wangu katika ujenzi wa taifa hili. Wengi mtakuwa mmesoma makala yangu katika gazeti la RAIA MWEMA mwezi Julai, 2010. Katika makala hiyo nilieleza kwa kirefu njia mbalimbali ambazo Serikali inaweza kutumia kupunguza matumizi ili kuboresha maslahi ya watumishi wake na pia kuongeza bajeti ya maendeleo.

Hata hivyo baada ya uzoefu niliopata katika siasa za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Mlimani) wakati nikigombea urais wa serikali ya wanafunzi, nimekuwa mwoga wa kushiriki siasa za ushindani. Hii haina maana kwamba sijashiriki siasa za nchi hii. Kwa mfano mimi nilishirikiana nyuma ya pazia na wanasiasa wa kundi lililojulikana kama G.55 lililoshinikiza (bila mafanikio) kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika. Aidha nilishiriki vivyo hivyo nyuma ya pazia kwenye mkakati wa kuleta mageuzi yaliyolazimisha marekebisho ya Katiba ya nchi hii na kuruhusu mfumo wa vyama vingi.

UANACHAMA WA CCM

Mwaka 1976 nilijiunga na TANU nikiwa Chuo cha Chama cha Kivukoni na kupewa kadi namba E 735352. Kwa maana hiyo nilikuwa muasisi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya TANU kuungana na ASP mwaka 1977. Kadi hiyo hiyo iliendelea kutumika kama ya CCM baada ya kupewa Kumb. Na. B 321241.

Tarehe 21 Julai 2010 nilifika hapa Wilayani Ngara si kwa sababu ya kupumzika au kufuatilia mchakato wa uteuzi wa wagombea wa udiwani na ubunge kwa tiketi ya CCM. Nililetwa na mapenzi yangu kwa Padri Marcel Bashaka ambaye alikuwa amelazwa hospitali na hatimaye kufariki na kuzikwa Rulenge juzi tarehe 3 Agosti, 2010. Hata hivyo nikiwa hapa Ngara sikuweza kujizuia kufuatilia kampeni zilivyokwenda. Katika kufanya hivyo nimeshuhudia uchafu wa kila aina katika mchakato wa wana-CCM kutaka kuteuliwa kugombea nafasi hizo. Uchafu huo ni pamoja na rushwa kwa viongozi na wanachama wenzangu ndani ya CCM. Mashindano ya nani anaweza kuhonga zaidi wakati mwingine yalikuwa yanachefua! Nimeshuhudia jinamizi la ukabila likirejea na kutumika kwa uwazi wa kutisha. Siyo siri kuwa sasa Wilaya ya Ngara imegawanyika katika vipande viwili na itachukua muda mrefu na umakini wa hali ya juu kwa watu wa Ngara kurejea kujiona kama familia moja badala ya kuwa Washubi au Wahangaza.

Nimesikitishwa sana kuona wachezaji wa timu moja wakiraruana na kuvunjana viungo kabla ya kucheza na timu pinzani. Sina shaka tena kwamba mustakabali wa Chama changu na Taifa zima uko katika hali ya kutetereka. Nimepatwa na woga zaidi baada ya kugundua kuwa kilichotokea Ngara ndicho kimetokea nchi nzima. Tuliyoyaona katika nchi ya jirani ya Kenya wakati wa uchaguzi uliopita yanatunyemelea. Angalau wao wameweza kupata suluhu hasa baada ya kutunga katiba mpya. Sina hakika iwapo sisi tuko salama.

HITIMISHO
Kutokana na maelezo hayo hapo juu, Leo tarehe 5 Agosti 2010 nimeona ni vema nirejeshe kadi yangu ya CCM kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwa nina hakika kwamba uongozi wa CCM wilayani na hata kitaifa hauwezi kuipokea kadi hiyo kwa uwazi ninaoutaka kama ningeamua kwenda huko. Nimeomba viongozi wa CHADEMA hapa wilayani wanisaidie kufanya hivyo na baada ya hapo wao watanipima na wakiona kuwa ninafaa kuwa mwanachama wao wataniambia.

Mungu Ibariki Tanzania

Mushengezi J.J. Nyambele
NGARA

0 comments:

Post a Comment