Saturday, August 14, 2010

Matukio 10 Yaliyotikisa Bunge 2006-2010

Bunge la tisa linamalizika likiwa na matukio mengi yaliyoitikisa na
kukumbukwa katika historia ya Tanzania. BUNGE hili la tisa lilikuwa na
Wabunge 320 kati yao tisina na nane(98) walikuwa ni Wanawake na 44 walikuwa
ni wa Kambi ya Upinzani wa Vyama vya CUF,UDP,CHADEMA na TLP,ambacho baadaye
kiti chao kimoja kilipotea baada ya Mbunge wake pekee Phares kabuye kufariki
dunia mwaka jana na kiti hiki kuchukiliwa na CCM.

Bunge hili liliongozwa na mbunge wa Urambo Mashariki Samwel Sitta akisaidiwa
na Naibu Spika Mama Anna Makinda Mbunge wa Njombe Kusini.
Viongozi hawa walikuwa pia wakisaidiwa na Wenyeyviti Jenista Mhagama Mbunge
wa Peramiho,Job Ndugai Mbunge wa Kongwa na Zuberi Maulid Mbungewa
Kwamtipura. Wote tunafahamu kuwa Wabunge wengine hawatarudi tena Bungeni
wengine wakiwa wameaga kuwa hawatagombea tena. Wengine hawatarudi kwakuwa
watapoteza viti vyao.

Matukio hayo yakukumbukwa ni kama ifuatavyo;

*1. **Kujiuzulu kwa aliyekuwa waziri Mkuu Edward Lowassa-Feb 2008*
*
*Itakumbukwa kuwa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa Mbunge wa Monduli
alituhumiwa kuhusika katika kashfa ya utoaji wa Zabuni ya kuzalisha umeme
kwa Kampuni ya Richmond. Lowassa alijiuzulu pamoja na Mawaziri wengine
wawili,Ibarhimu Msabaha na Nazir Karamagi waliowahi kuwa Mawaziri wa Nishati
na Madini. Kujiuzulu kwa Lowassa kulimfanya Rais Kikwete kuunda Baraza jipya
la Mawaziri chini ya Mbunge wa Mpanda Mizengo Peter Kayanza Pinda.

*2. **Kusimamishwa kwa ZittoKabwe*
Tukio la Kusimimsihwa bungeni Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe mwaka
2007 ni moja ya matukio yaliyotikisa Bunge na nchi kwa ujumla baada ya Zitto
kufungiwa kuhudhuria Vikao vyote vya Bunge kwa muda wa miezi mitatu kuanzia
Agosti-2007. Zitto alisimamishwa baada ya kudaiwa kulidanganya Bunge
alipomtuhumu aliyekuwa Waziri wa Nishati na madini Nazir Karamagi kudanganya
kuhusu Mkataba wa madini aliotia saini Hotelini London Uingereza. Miezi
michache baadye Nazir Karamagi alijiuzulu nafasi hiyo.

*3*.* Wabunge wa CUF Kugomea Vikao*
Itakumbukwa pia Aprili 2008 Wabunge wa CUF waligomea bunge na kutoka nje ya
ukumbi wa Bunge wakipinga kucheleweshwa kwa mazungumzo ya muafaka baina ya
Viongozi wa CCM na CUF.

1. *Vifo vya Wabunge*
Katika Bunge hili la tisa wabunge tisa walifariki dunia katika mazingira
tofauti tofauti. Wabunge hao ni Amina Chifupa, Chacha Wangwe, Benedict
Lusorutia, Salome Mbatia, Richard Nyaulawa, Faustine Rwilomba, Sigfrid
Ng'itu, Juma Akukweti na Phares Kabuye. Itakumbukwa kuwa vifo vya Amina
Chifupa,Chacha Wangwe,Salome Mbatia na Phares Kabuye viliacha gumzo kubwa
mpaka hii leo.

5. *Waziri Mkuu Pinda kulia Bungeni*
Mwanzoni mwa mwaka jana Waziri Mkuu Pinda alijikuta akiangua kilio alipokuwa
akitetea hoja ya kuhusu matatatizo yanayowapata Wenye Ulemavu wa
Ngozi(Albino). Pinda liangua kilio hicho alipokuwa akijibu hoja ya wapinzani
kupinga kauli yake alipoeleza kwamba wauaji wa Albino nao pia wauawe.

6.* Wabunge Kuchukua Posho mbili*
Itakumbukwa kuwa kulikuwa na mivutano baada ya wabunge na Edward Hosea
mkurugenzi wa TAKUKURU aliyetaka wabunge wachunguzwe kwa kupokea posho mara
mbili .Hosea alikuwa akiwalenga Wabunge waliokuwa wamejipambanua kama
Makamanda wa kupinga ufisadi hasa baada ya sakata la Richomd.

*7. Hofu ya Ushirikina*
Itakumbukwa pia Bunge lilikumbwa na hofu ya ushirikina baada ya baadhi ya
wabunge kudai kwamba kuna unga uliomwagwa katika viti vyao ambao ulidhaniwa
kwamba haukuwa salama. Hofu hiyo ilipelekea Spika Sitta kuamua kwamba unga
huo upimwe na Mkemia Mkuu wa Serikali. Lakini ilibainika kuwa Unga ule
hakuwa na madhara yeyote.

*8. Ajali ya Mudhihir*
Tukio jingine la kukumbukwa ni lile la ajali ya Mudhihir Mudhihir Mbunge wa
Mchinga.Mudhihir alilazimika kukatwa mkono na baadaye kuwekwa mkono wa
bandia. Ajali ilikuzua gumzo katika vyombo mbalimbali vya habari na
mawasiliano.

*9. Kuzima kwa Vipaza Sauti*
Itakumbukwa hivi karibuni jengo jipya la Bunge lilipata hitilafu na
kusababisha vipaza sauti kushindwa kufanya kazi.Bunge lililazimika kuhamia
kwenye ukumbi wa zamani wa Pius Msekwa ili kuendlea na shughuli za Bunge
baada ya kusbiri kwa takribani saa moja wakisubiri vitengamae.Ikumbukwe kuwa
jengo hili ni miongoni mwa majengo ya kisasa barani Afrika.

*10. John Cheyo kuvuliwa kuwa Msemaji wa kambi ya Upinzani*
Mbunge wa Bariadi John Cheyo ameingia katika historia mpya ya kuvuliwa
uwaziri kivuli wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi baada ya kuwa kinyume
na msimamo wa kambi ya upinzani.Uamuzi huu ulifanyika baada ya Cheyo
kubainika kuwa alisaliti uamuzi wa pamoja wa kutounga mkono bajeti ya
Serikaliiliyokuwaikiptishwa.

0 comments:

Post a Comment