Saturday, August 14, 2010

Slaa kubadili Katiba

Slaa kubadili Katiba

• Asema ndani ya siku 100

na Mwandishi wetu

MGOMBEA wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.. Wilbrod Slaa, amesema kazi ya kwanza itakayofanywa na chama chake kama kitafanikiwa kuingia madarakani, ni kubadilisha Katiba ambayo inaonekana kuwa kikwazo cha maendeleo.

Akizungumza mara baada ya kuthibitishwa na Mkutano Mkuu Maalum kuwa mgombea wa nafasi hiyo, Dk. Slaa, alisema chama chake kitaanza mchakato wa kubadilisha Katiba baada ya miezi mitatu baada ya kuingia madarakani.

Alisema Katiba iliyopo sasa, haitoi fursa kwa wananchi kuwa na mamlaka ya kumiliki uchumi wao.

“Inawezekana Watanzania wengi hawajui kuwa Katiba inachangia vipi kudumaza au kukuza uchumi, lakini ndio chanzo kikubwa cha umaskini kwa Watanzania wengi.

“Hivyo kazi ya kwanza tutakayoifanya tukiingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu ni kubadilisha Katiba ili kuwawezesha wananchi wote kumiliki uchumi wao,” alisema Dk.. Slaa.

Huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo, Dk.. Slaa ambaye ameidhinishwa pamoja na mgombea mwenza, Said Mzee Said, alieleza kuwa CCM imeshindwa kuondoa umaskini kwa kuwa imewaondolea Watanzania umilikaji wa uchumi kwa kulinda Katiba ambayo imepitwa na wakati.

Katika hotuba yake, Dk. Slaa alisema CCM imekuwa ikitoa takwimu nyingi zinazoelezea kukua kwa uchumi kwa kujenga shule, zahanati na majengo mbali mbali bila kuoanisha na uchumi ulivyokua kwa wananchi wake.

“Hawa CCM wamekuwa wanatulaumu kuwa hatuna macho, hatuoni waliyoyafanya, lakini sisi tunasema, hauwezi kuelezea kukua kwa uchumi kwa kujenga shule au zahanati, wanajenga maghorofa wakati wananchi wanaishi kwenye nyumba za ‘matembe’, huko si kukua kwa uchumi,” aliongeza.

Alisema Watanzania wamechoshwa na utaratibu wa CCM wa kutoa takwimu ambazo haziwasaidii katika maisha yao.

“Watanzania hawawezi kushiba takwimu wala kuvaa takwimu, wanachotaka ni kuona takwimu hizo zinaoana na kukua kwa uchumi kwa mwananchi mwenyewe.

Dk. Slaa aliidhinishwa na Mkutano Mkuu Maalum kwa kura za wazi 752 kati ya kura 758 dhidi ya kura 6 zilizomkataa.

Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa matokeo ya kura za maoni za Chama cha Mapinduzi (CCM), zimeonyesha jinsi chama hicho kilivyopoteza mwelekeo wa kuliongoza taifa.

Alisema kukumbatia rushwa ndani ya chama hicho ni sehemu ya kielelezo cha kuondoka madarakani katika uchaguzi mkuu ujao, kwa kuwa kimeshindwa kutekeleza matakwa ya Watanzania ambao wamepoteza matumaini ya maisha yao.

“CHADEMA kamwe haikumbatii rushwa au ufisadi, ndio maana katika uchaguzi wetu wa Viti Maalum kulipandikizwa suala la ufusadi, lakini tulipogundua tu tukasimamisha uchaguzi mara moja,” alifafanua huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo.

Katika hatua nyingine, zaidi ya Watanzania mil. 1.3 wenye sifa na vigezo vya kupiga kura wamemdhamini Dk. Wilbrod Slaa kugombea urais, wakati wa ziara yake ya kutafuta wadhamini iliyofanyika mikoa mbalimbali hivi karibuni.

Akitoa taarifa ya ziara hiyo katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, alisema idadi hiyo ilipatikana katika mikoa 19 waliyoitembelea.

Alisema kwa idadi hiyo CHADEMA imejipatia mtaji mkubwa wa kushinda urais kwani kila mdhamini akitafuta wapiga kura wenzake saba tu Dk. Slaa atakuwa amepata kura za kutosha kumwingiza Ikulu.

Aidha, katika mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Kiramuu Mbezi Beach, Dar es Salaam , Dk. Slaa alipitishwa rasmi kwa kishindo kuwa mgombea urais.

“Ni kura sita za hapana ndizo zimemkataa Dk. Slaa ambaye amethibitishwa rasmi kuwa mgombea wetu wa urais kwa kupata asilimia 99.2 ya kura zote zilizopigwa,” alisema Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, wakati akitangaza matokeo hayo.

Katika hatua nyingine, wajumbe wa mkutano huo pia walimthibitisha Said Mzee Saida kuwa mgombea mwenza wa urais wakiridhia pendekezo lililotolewa na Dk. Slaa mwenyewe.

Akizungumza baada ya uthibitisho huo, Dk.Slaa aliushukuru mkutano huo kwa kumthibitisha na kusema kuwa sasa amepata ujasiri na jeuri ya kutembea kifua mbele baada ya kuungwa mkono na idadi kubwa ya Watanzania.

“Uchumi wetu umedorola, hatuwezi kuendelea kwa uchumi uliohodhiwa na asilimia tatu tu ya Watanzania wote huku wengine wakiteketea kwa umaskini. “Huko nyuma tulikuwa sawa na wenzetu Rwanda, wakaingia kwenye vita lakini sasa uchumi umeimarika kuliko wa kwetu, kwa nini tusijiulize sababu?

CCM inasingizia mtikisiko wa uchumi, ni mtikisiko gani huo unaoiangusha Tanzania na si nchi nyingine?” alihoji Dk. Slaa.

Naye, mgombea mwenza, alisema akiwa Makamu wa Rais atasaidia sana kuundwa kwa muungano wa serikali tatu na kukosoa mabadiliko ya 10 ya katiba ya Zanzibar yaliyofanyika hivi karibuni ambayo alidai yanahatarisha uhai wa Muungano.

Awali, mwakilishi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mkutano huo, Nape Nnauye, akitoa salamu za chama chake aliisifu CHADEMA kwa kudhihirisha ukomavu wa kidemokrasia na kusema kuwa taasisi hivyo ni mfano wa kuigwa na vyama vingine.

“Mmejijenga na kuifanya CHADEMA kuwa chama taasisi, endeleeni kuimarisha taasisi yenu, msirudi nyuma. Uimara wa CCM unategemea sana vyama pinzani, wanaodhani upinzani ni ugomvi au uhaini wanakosea, mimi siamini hivyo,” alisema hivyo na kubainisha kuwa alikuwa akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.

Mbali na CCM vyama na taasisi nyingine zilizohudhuria mkutano huo ni APPT-Maendeleo kilichowakilishwa na Elizabeth Masanja na Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA), kilichowakilishwa na Huba Pondo.

Naye waziri wa zamani wa serikali ya Tanzania na aliyekuwa mwanasiasa nguli wa CCM, Arcado Ntagazwa, alipokelewa rasmi katika mkutano huo kama mwanachama mpya wa CHADEMA.

“Kama alivyosema Mwalimu, CCM sio mama yangu, nimeamua kuiacha ili historia isije ikanihukumu kuwa miongoni mwa wale waliolitumbukiza taifa hili katika uovu na umaskini,” alisema Ntagazwa na kushangiliwa na umati mkubwa.

Mkutano huo pia ulipitisha rasimu ya ilani ya chama hicho kwa mwaka 2010-2015 yenye vipaumbele vinane, ambavyo ni elimu bora, huduma bora za jamii, kilimo bora, uchumi imara na shirikishi, mfumo bora wa utawala, ajira na ujira bora, kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi na ushirikiano wa kimataifa.

0 comments:

Post a Comment