Sunday, August 8, 2010

HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE WAKATI AKIZUNGUMZA NA WAZEE WA MKOA WA DAR ES SALAAM

HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI AKIZUNGUMZA NA WAZEE WA MKOA WA
DAR ES SALAAM, TAREHE 3 MEI 2010

Mhe. Makamu wa Rais,
Mhe. Waziri Mkuu,
Waheshimiwa Mawaziri,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Mstahiki Meya,
Viongozi wa Serikali,
Wazee wangu,
Ndugu Wananchi,

Nianze kwa kumshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuniandalia fursa ya kukutana na Wazee wa Dar es Salaam. Nawashukuru wazee wangu kwa kuitikia wito wangu huu wa kukutana nanyi na nimefarijika sana kwa mahudhurio yenu makubwa. Asanteni sana.

Nimewaiteni wazee wangu nizungumze nanyi mambo mawili na kupitia kwenu nizungumze na wananchi wote wa Tanzania. Jambo la kwanza, linahusu mkutano mkubwa wa kimataifa kuhusu masuala ya uchumi utakaofanyika hapa Dar es Salaam kuanzia keshokutwa tarehe 5 Mei mpaka tarehe 7 Mei. Mkutano huo ulioandaliwa na shirika moja la kimataifa lijukanalo kama World Economic Forum, lenye makao yake makuu nchini Uswisi, unafanyika hapa nchini kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 20 ya mikutano hiyo kufanyika Barani Afrika. Pia ni mara ya kwanza kwa mikutano hiyo kufanyika nje ya Cape Town, Afrika Kusini.

Ndugu zangu, Watanzania Wenzangu,

Hii ni heshima kubwa sana ambayo taifa letu limepewa. Ni kielelezo cha imani kubwa waliyokuwa nayo kwetu, wenzetu kwingineko duniani, kwani zilikuwepo nchi nyingine zilizotaka kuwa wenyeji wa mkutano huu lakini wakaiteua Tanzania. Ni jambo la fahari kwetu lakini ni jambo ambalo pia lina wajibu mkubwa kwetu. Wajibu wenyewe si mwingine bali ni ule wa kuwapokea vizuri na kuwa wakarimu kwa wageni wetu kama ilivyo desturi yetu na sifa yetu Watanzania. Lazima tuhakikishe kuwa wageni wetu wanaondoka nchini wakiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu na sisi watu wake.
Ndugu Wananchi,

Mwitikio wa watu kushiriki katika mkutano huu wa Dar es Salaam umekuwa mkubwa sana hata kuwashangaza waandaaji. Wanasema wameshaandaa mikutano hii kwa zaidi ya miaka 50 sasa, lakini hawajapata mwitikio kama huu wa mkutano wa Tanzania. Walikuwa na lengo la kupata washiriki 750, lakini mpaka tarehe 29 Aprili, 2010 washiriki 959 walikuwa wamethibitisha kushiriki na wengine kadhaa wamekosa nafasi. Haya yote ni kielelezo cha kukubalika na kuheshimika kwa nchi yetu kimataifa.

Ndugu Wananchi;

Tunatarajia kupokea Wakuu wa Nchi na Serikali wapatao, 11 na Mawaziri 23 wa kutoka nchi mbalimbali duniani. Aidha, wajumbe kutoka mashirika makubwa ya kimataifa, kama Umoja wa Kimataifa, Benki ya Dunia, WTO n.k. Kuna washiriki kutoka makampuni makubwa, ya kati na madogo ya kimataia na watu binafsi wakiwemo watu mashuhuri duniani. Washiriki wa mkutano huu kwa ujumla wao wanatoka katika mataifa 85 duniani. Katika mikutano hii hufanyika mikutano ya Viongozi Vijana wanaoongozwa na Mwana wa Mfalme wa Norway, Prince Magnus Haakon. Mkutano huo nao umevunja rekodi ya ushiriki, awali walitegemea washiriki 200 lakini washiriki waliothibitisha mpaka sasa ni 350. Kwa sababu ya ugeni mkubwa kiasi hiki, kutatokea usumbufu wa magari kusimamishwa ili kuruhusu misafara ya wageni wetu kupita. Naomba ndugu zangu muelewe hilo na kuwa wavumilivu. Natanguliza kuwataka radhi kwa usumbufu mtakaoupata katika siku tatu za mkutano huu.

Agenda kubwa ya mkutano wa mwaka huu ni kuangalia jinsi ya kurekebisha na kukuza uchumi wa nchi za Afrika baada ya kutikiswa na hali mbaya ya uchumi duniani. Masuala yatakayoongelewa ni pamoja na jinsi ya kuongeza uwekezaji; kukuza uzalishaji na tija kwenye kilimo; uwekezaji kwenye viwanda na uongezaji wa thamani kwenye bidhaa za kilimo; kuendeleza sekta binafsi ili iweze kuchangia kwenye ukuzaji wa uchumi; kuboresha miundombinu; kuendeleza elimu n.k.

Kwa ujumla mkutano huu ambao miaka ya nyuma umekuwa unafanyika Cape Town, Afrika Kusini una faida kwa nchi yetu. Faida kubwa ni kuitangaza nchi yetu na vivutio vyake duniani na hivyo kuwafanya wawekezaji na watalii watambue uwepo wetu. Wapo watakaoijua Tanzania kwa kufika na kujionea wenyewe na wapo watakaoijua nchi yetu kupitia vyombo vya habari ambavyo vitawakilishwa kwa wingi sana. Faida itakayopatikana haraka sana wakati na baada ya mkutano huu ni mahoteli na vyombo vya uchukuzi na maduka nchini kupata kipato kutokana na wageni watakaohudhuria mkutano huu kutumia huduma hizo. Naambiwa karibu wageni wetu wote wa nje watatembelea mbuga za wanyama na visiwa vya Zanzibar baada ya mkutano.


Ndugu Wazee na Viongozi,

Jambo la pili linahusu TUCTA na mgomo. Sikupenda kulizingumzia suala hili, lakini nimelazimika kuzungumza baada ya kuwasikiliza viongozi wa TUCTA wakati wa Maadhimisho ya Sherehe ya Mei Mosi hivi majuzi. Nimewasikia wakirudia kuwashawishi wafanyakazi kugomo kuanzia tarehe 5 Mei, 2010 kwa sababu ati sisi katika Serikali hatusikii wala hatujali maslahi ya wafanyakazi.

Katika hotuba yangu niliyoitoa mwishoni mwa mwezi Machi, 2010, nilielezea kwa kirefu jinsi gani Serikali inavyowathamini na kuwajali wafanyakazi. Nilitaja na kufafanua kwa kina hatua mbalimbali ambazo Serikali imechukua na inazoendelea kuchukua katika kuboresha maslahi ya mfanyakazi. Nilisema kuwa madai ya viongozi wa TUCTA kuwa Serikali hii siyo sikivu na haiwajali wafanyakazi si kweli kwani mema yote tuliyoyafanya kwa wafanyakazi hayangefanyika kama sisi hatusikii wala kujali.

Kadhalika nimeelezea dhamira yetu ya kuongeza mishahara ya wafanyakazi katika bajeti ijayo. Ukweli ni kwamba tangu tuingie madarakani, tumeongeza kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 62.5 kutoka shilingi 65,000 hadi kufikia shilingi 104,000 hivi sasa.

Nilielezea pia mambo mazuri yaliyofanywa na Serikali kuendeleza maslahi ya wafanyakazi wa sekta binafsi. Taliziunda Bodi nane za kisekta ambazo hazikuwepo kabla ili ziweze kushughulikia kupanga viwango vya mishahara ya kima cha chini kwa wafanyakazi wa sekta binafsi. Kwa ajili hiyo, wafanyakazi wa sekta binafsi wameanza kunufaika kwa mishahara kupanda tangu wale wa mashambani na majumbani mpaka viwandani na kwingineko. Hivi majuzi tena kumetolewa nyongeza nyingine, wapo ambao wametoka kwenye shilingi 45,000 mpaka shilingi 80,000 au hata 150,000, wapo waliotoka kwenye mshahara wa shilingi 48,000 kwa mwezi hadi shilingi 350,000 kwa mwezi mwaka 2009. Bodi hizi zinafikia maamuzi haya kwa kuzingatia uwezo wa sekta binafsi kumudu gharama hizo.

Ndugu Wananchi;

Jambo kubwa nililowaomba viongozi wa TUCTA ni kwamba, katika hotuba ya Machi, 2010 niliwasihi viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi kutumia njia ya mazungumzo kwa sababu ilikuwa bado haijatumika na kushindikana. Aidha, nilikumbusha kuwa hata kama watagoma mwishowe watalazimika kurudi mezani kuzungumza, ndipo wapate wanayoyataka. Niliwatahadharisha pia kwamba ni bora kuzungumza sasa kuliko kufanya hivyo baada ya mgomo kwani hujui katika kipindi cha mgomo mambo yatakuwaje. Inawezekana hata mazingira ya kuzungumza yakawa mabaya.

Wazee Wangu;

Napenda kueleza furaha yangu na shukrani zangu kuwa maombi yangu yalikubaliwa na pande zetu tatu zimekuwa zinazungumza tangu wakati ule kwa mujibu wa sheria ya Mahusiano Kazini na Sheria ya Taasisi Kazi. Napenda kusema pia kuwa, mazungumzo yamekwenda vizuri, yapo mambo yaliyokamilika na yapo yanayoendelea kuzungumzwa na naamini nayo yatakamilika. Nadhani mnashangaa kuelezea furaha na kusema yapo mambo yaliyokamilika na kuonesha matumaini kuwa yaliyobakia nayo yatakamailika. Hii ni sahihi kabisa .

Naomba nifafanue kidogo. Tarehe 6 Aprili, 2010 kulifanyika kikao cha Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambapo TUCTA iliwasilisha rasmi hoja zao zinazowafanya waitishe mgomo wa wafanyakazi wote nchi nzima kuanzia tarehe 5 Mei, 2010. Hoja hizo ziliwasilishwa na kuzungumzwa na kuamuliwa ipasavyo.

a. Madai kuwa Bodi za Kisekta zilikuwa zimemaliza muda wake yalifutwa na TUCTA baada ya kugundua kuwa walikosea tarehe.
b. Kuhusu madai ya kuchelewa kutangazwa kima cha chini nalo halikuwa tatizo la Serikali bali ni LESCO kupata mamlaka ya Bunge.
c. LESCO kutokukutana kwa sababu ya mazungumzo kuchelewa kumalizika ndani ya siku 60, hivyo kibali cha Bunge kilihitajika ambacho kilipatikana Februari, 2010. Kinachosubiriwa sasa ni tarehe ya mazungumzo kupangwa.
d. Ripoti ya Tume ya Ntukamazina kupewa TUCTA; wakaambiwa Tume aliunda Rais imshauri yeye kama wanahitaji ripoti wakamuombe yeye.
e. Kima cha chini kiwe shilingi 315,000/=; wakaambiwa lizungumzwe kwenye baraza husika.
f. Kodi kuwa kubwa mno; wapeleke kwenye Mamlala husika.
g. Ukokotoaji wa malipo ya uzeeni uhuishwe ili ufanane katika mifuko yote. Waliambiwa ili nalo likazungumzwe.

Tarehe 14 Aprili, 2010, LESCO ilikutana kujadili taarifa ya CMA na kuelekeza ipasavyo. Matokeo ya uamuzi wa LESCO ni:-
a. Kukubali mapendekezo ya kima cha chini cha mishahara kwa sekta binafsi na kuelekeza Waziri wa Kazi atangaze kabla ya tarehe 30 Aprili, 2010; Waziri akafanya hivyo, lakini cha ajabu mara baada ya Waziri kutangaza, TUCTA wakamshutumu Waziri Kapuya na kudai hiyo ni danganya toto. Lakini wakati wanafanya hivyo, maamuzi hayo yamefanywa katika vikao ambavyo TUCTA wameshiriki kwa ukamilifu. Waziri si mjumbe wa vikao vyote hivyo, bali yeye ndiye mtanganzaji.
b. Ikaafiki uamuzi wa CMA kuwa suala la kima cha chini cha mshahara wa watumishi wa umma lipelekwe kwenye Baraza la Majadiliano la Pamoja la Utumishi wa Umma kuzungumzwa.

Tarehe 27 Aprili, 2010, kikao cha Baraza hilo kikaitishwa na mazungumzo kuendelea tena tarehe 30 Aprili, 2010. Baada ya kikao cha tarehe 30 Aprili, 2010 walikubaliana wakutane tena tarehe 8 Mei, 2010. Jambo la kustaajabisha, tarehe 1 Mei, wale wale waliokubaliana wakutane tarehe 8 mwezi Mei, wanatoa siku mbili kwa wenzao kutoa majibu na isipofanyika hivyo tarehe 5 mwezi Mei wafanyakazi wote wagome.

Lingine la ajabu ni la viongozi wa TUCTA kuendelea kudai hadharani kima cha chini cha shilingi 315,000/= , wakati siku ya kwanza ya mazungumzo walielezwa ugumu wake, nao wakakubali na kupendekeza kiwango kingine cha chini, ambacho nacho Serikali iliona hakitekelezeki. Hivyo tarehe 30 Aprili, viongozi wa TUCTA wakapendekeza kiwango kipya cha chini zaidi. Upande wa Serikali nao walipendekeza kiwango wanachoamini kuwa mapato yetu yanaweza kumudu. Licha ya mwenendo mzuri wa mazungumzo, bado hakujawa na muafaka kati ya kiwango kipya cha chini walichopendekeza viongozi wa TUCTA na kiwango kilichopendekezwa na Serikali. Kutokana na hali hiyo walikubaliana wakutane tarehe 8 Mei, 2010 kuendelea na mazungumzo.

Ndugu Wananchi;

Iweje tena tarehe 1 Mei, 2010 mtu yule yule anageuka na kuzungumzia kima kile kila cha mwanzo wa mazungumzo na iamuliwe ndani ya siku mbili? Tunayo kila sababu ya kuhoji dhamira zao, wana nia njema kweli wenzetu hawa? Wana hili hili au wana lao jambo lingine?

Kima cha Shilingi 315,000/=

Kima cha chini cha shilingi 315,000/= hakitekelezeki kwa sababu Serikali haitakuwa nazo pesa hizo. Kwa kima hicho, Serikali itatakiwa kutumia shilingi bilioni 6,852.93 kwa mishahara peke yake wakati mapato yanayotarajiwa katika bajeti ijayo ni shilingi bilioni 5,773.1, ambazo zinapaswa kutumika kwa mishahara pamoja na shughuli zingine za kuendesha Serikali na maendeleo. Hivyo basi, italazimika kukopa shilingi bilioni 1,233.52 zaidi ili zitosheleze mahitaji ya mishahara peke yake. Hii haiwezekani kwa sababu Serikali itakuwa haifanyi shughuli nyingine ila kulipa mishahara. Tutakuwa ni watu wa ajabu sana. Huko tutakapokwenda kukopa watatushangaa na tutaonekana kichekezo. Na viongozi wa TUCTA tumewaambia hivyo.

Hata kama ningetaka kuwafurahisha akina mzee Mgaya, kwa jambo hili haiwezekani. Na, kama wanavyodai kwamba watampigia kura kiongozi na chama atakayewapa fedha hizo, kura hizo sisi tunahesabu tumeshazikosa. Ni afadhali kuzikosa kura za akina Mgaya kuliko kuwaumiza wananchi walio wengi kwa kutumia fedha zote za nchi kuwapa akina Mgaya wagawane na kuwakosesha wananchi huduma muhimu. Jambo hili sitalifanya.

Hatutafanya hivyo, kwa vile fedha za Serikali ni za Watanzania wote milioni 40 na siyo kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi 350,000 tu. Ni kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wote kwa ajili ya maendeleo yao. Kuwalipa mishahara wanayodai viongozi wa TUCTA inamaanisha kwamba serikali isitishe kutoa huduma yoyote ile kwa wananchi; madawa hospitalini yasiwepo, ruzuku za mbegu, mbolea na madawa ya kuulia wadudu visiwepo, ujenzi wa majosho, barabara, zahanati, mashule, maji na umemenk usitishwe, shuguli za ulinzi na usalama wa raia pia zisimamishwe. Na wafanyakazi wenyewe wakifika maofisini mwao watakuwa ni watu wa kupiga gumzo tu bila kufanya kazi yoyote kwa sababu hakutakuwapo fedha za kununulia vitendea kazi. Hii haiwezekani. Hii ni sawa na kusema serikali iwe imekufa. Hakuna serikali inaweza kufanya hivyo. Hata hao ambao wanawapigia debe hivi sasa kama wangebahatika kuwa madarakani wasingeweza na hawataweza kamwe kukubali miujiza hii.

Wazee Wangu, Wananchi Wenzangu;

Naomba muelewe ugumu tulionao katika mazungumzo na viongozi wa TUCTA. Hawataki kuwaambia wafanyakazi na wanachama wao ukweli. Viongozi hawa hawana muamana, kwenye majadiliano wanakubaliana jambo moja, wakitoka nje wanasema jingine. Viongozi hawa wanakosa moja ya nguzo muhimu ya uongozi bora. Nguzo ya uongozi bora ni kuwaambia watu unaowaongoza ukweli hata kwa yale mambo wasiyopenda kuyasikia. Hawana sababu ya kuacha kuwaeleza wanachama wao ukweli. Tayari viongozi hao wamekubaliana na Serikali kukutana tarehe 8 Mei. Hawana sababu tena ya kuipa Serikali siku mbili kutekeleza mambo yale yale yaliyopangwa kujadiliwa baina yao na Serikali tarehe 8 Mei.

Uhalali wa Mgomo

Ndugu Wananchi;

Mgomo unaoshinikizhwa na viongozi wa TUCTA ni batili na kinyume cha sheria. Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini (Employment and Labour Relations Act,) No. 6 ya 2004 inaainisha pamoja na mambo mengine utaratibu wa kutatua mizozo na migogoro kazini na haki za mwajiri na mwajiriwa. Utaratibu wa mgomo ulioainishwa katika sheria hiyo, unazingatia maslahi ya wafanyakazi, waajiri pamoja na wananchi. Unatambua umuhimu wa kufanya majadiliano na unasisitiza kwamba huduma muhimu hazipaswi kuathirika kutokana na migomo. Aidha, imetamka kuwapo kiwango fulani cha huduma wakati wa mgomo. Uratatibu huo unaelekeza kwamba mgomo wenyewe utekelezwe kwa kiwango ambacho kitasaidia kutatua tatizo mahsusi lililopo kati ya mwajiri na mwajiriwa. Mambo ya msingi ya kuzingatia ni kwamba kabla mfanyakazi hajagoma, au mwajiri hajaamua kufunga eneo la kazi (lock out) kuwe na majadiliano yatakayofanyika kwa nia njema kati ya mwajiri na mwajiriwa na kwamba majadiliano hayo yawe yameshindwa kutoa suluhisho. Kamishna wa Kazi awe amearifiwa hiyo. Wafanyakazi wasilazimishwe kugoma, badala yake wao wenyewe wawe wameamua kwa ridhaa yao kwa kura, kushiriki katika mgomo.

Bahati mbaya sana mgomo huu uliotangazwa na Chama cha Wafanyakazi siyo halali kabisa. Umeitishwa wakati ambao majadiliano bado yanaendelea. Hawaonyeshi kuwa na nia njema katika majadiliano kwani mambo yanayokubalika kwenye majadiliano ni tofauti na yale wanayowaambia wafanyakazi wao. Pili, wanawalazimisha wafanyakazi wote kushiriki katika mgomo, hata wale ambao sheria inasema kwamba huduma zao ni muhimu hivyo hawatakiwi kugoma. Tatu mgomo wenyewe hauna muda. Nne, viongozi wamejitwalia mamlaka ya kisheria kutangaza mgomo bila kuzihusisha mamlaka za kazi jambo ambalo kwa kweli siyo zuri wala la kistaarabu. Kutokana na kushindwa kutekeleza masharti haya ya Sheria ya Ajira na mahusiano kazini mgomo huu ni kuvunja Sheria za nchi, ni haramu. Hatuwezi kukubali jeuri ya watu wanaovunja sheria za nchi.

Ndugu Wananchi;

Nimalize kwa kutoa ushauri wangu kwa wafanyakazi wa Serikali, wafanyakazi wa sekta binafsi na viongozi wa TUCTA. Kwa wafanyakazi wa Serikali hakuna sababu ya msingi kugoma kwa madai yasiyotekelezeka ya kulipwa kima cha chini cha shilingi 315,000/=. Kwa vile mazungumzo baina ya Serikali na TUCTA bado yanaendelea, hakuna sababu za msingi za kugoma. Kwa vile ni dhahiri kuwa siyo halali. Atakayegoma atakuwa amekiuka taratibu na kanuni za ajira na atachukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu na kanuni za utumishi Serikalini. Na yule ambaye atakwenda kazini lakini ataacha kufanya kazi atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Kwa wafanyakazi wa sekta binafsi, tumeunda Bodi za kisekta zimeshafanya kazi yake na Waziri wa Kazi ameshatangaza tuzo stahiki kisheria. Tangazo la TUCTA nyie mgome ili mlipwe shilingi 315,000/= linavunja sheria. Msiwasikilize. Mtapoteza ajira zenu na Mgaya hamtamwona. Ndugu zangu mshahara unategemea uwezo wa mwajiri kulipa, usidai kiasi ambacho hawezi kukulipa. Bodi ya Kisekta ndiyo muamuzi kwa mujibu wa sheria. Madai mengine yote nje ya utaratibu huu ni batili.
Changamoto kwa viongozi wa TUCTA, ni kuwa wakweli kwa watu wanaowaongoza na wawe tayari kusema hata yale mambo magumu ambayo wafuasi wao hawapendi kuyasikia.

Ahsanteni Sana kwa Kunisikiliza!
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!

0 comments:

Post a Comment