Wednesday, August 18, 2010

Tuimarishe Demokrasia tuepuke Ufisadi

13 Machi 2008

Tuimarishe Demokrasia tuepuke Ufisadi

na
Edwin I.M. Mtei
Mwenyekiti Taifa Mwanzilishi

Mjadala uliozuka Tanzania kuhusu ufisadi hivi karibuni, ambao ulipelekea kuundwa kwa Baraza la Mawaziri upya, Mhe. Mizengo Pinda akiwa ni Waziri Mkuu, umedhihirisha umuhimu wa kutathmini kwa kina Katiba ya nchi yetu na sheria zinazohusu ubunge na vyama vya siasa. Nitajieleza kidogo.

Kwanza, licha ya kwamba mafisadi wanasiasa waliobainika ni wanachama wa Chama cha Mapinduzi na Kamati Teule ya Bunge iliyochambua ufisadi wa Richmond ilikuwa na Wana-CCM wengi, hakuna pendekezo lolote lililotolewa hadharani kwamba hawa mafisadi wafukuzwe toka chama chao cha siasa. Swali: Je CCM, kama chama, kinakumbatia mafisadi?

Hapa ni lazima nikiri kwamba nimefadhaishwa sana na tamko la Mheshimiwa Rais wetu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, kwamba Waziri Mkuu aliyelazimika kujiuzulu “alipatwa na ajali kazini”, katika kushughulikia kampuni ya Richmond. Siwaelewi Watanzania jinsi mnavyochukulia kama mzaha, kuporwa kwa Shilingi milioni 152 kila siku (Shilingi 55 bilioni kwa mwaka) toka kwa walipiaji wa umeme ili kufidia TANESCO wawalipe kampuni ya Richmond kwa huduma hewa. Mzaha huu umeendelea hata mtuhumiwa mkuu wa uzembe kupokewa “kifalme” aliporejea makwao! Narudia kusema kwamba nafadhaishwa na dalili hizi za kupuuza mambo yanayoathiri maslahi ya umma kwa kiwango kikubwa hivyo.

Kufadhaika kwangu kumeongezeka pale niliposoma magazetini kwamba juhudi zilifanywa na CCM Kyela kuzuiya mapokezi mazuri na wapenzi wake Mhe. Harrison Mwakyembe ambaye alijizolea sifa kitaifa kwa jinsi alivyoongoza uchambuzi wa ufisadi katika kampuni ya Richmond. Kulikoni? Ni watu gani wanafaidika na wizi na ufisadi wa Richmond unaoendelea kutunyonya fedha kulipia umeme hewa? Aidha kuhusu fedha zilizoibiwa kutoka katika akaunti ya EPA, Benki Kuu ya Tanzania, eti zinarejeshwa kimya kimya na Waziri wa Fedha ametangaza kiasi cha Shilingi 50 bilioni kati ya zile Shilingi 133 bilioni zimekwisha rejeshwa.

Swali: Mbona hawa wezi walioshirikiana na maofisa wa Benki Kuu wasitiwe mbaroni na kushtakiwa? Sijapata kusikia serikali yoyote duniani ikifumbia macho wizi wa fedha za umma na kusema eti ni siri kati yake na huyo mhalifu! Tungekuwa na Bunge jasiri linalojali maslahi ya wananchi na umma, Serikali ingepigiwa kura ya kukosa imani nayo.

Sasa nigusie Bunge na siasa za sasa. Katika Bunge letu, hususan katika ile Kamati Teule iliyochunguza Richmond, kulionekana wana-siasa ambao walionyesha kuchukizwa kwa dhati na ufisadi na kutamka dhamira yao ya kuupiga vita. Aidha kwa miezi kadhaa sasa kumekuwa na mijadala hadharani, hasa katika redio na televisheni ambapo wana-CCM mashuhuri, kwa mfano Joseph Warioba, Peter Kisumo na Joseph Butiku, wameonyesha kukerwa na jinsi Chama tawala na Serikali, wanavyoshughulikia rushwa na ufisadi. Wana-siasa wa upinzani wanaoamini kwamba ufisadi ndio kiini cha umaskini na kukosekana kwa maendeleo kunakoikumba Tanzania wanafarijika kwa dalili hizi za kubadilika kwa baadhi ya wanachama wa chama tawala.

Mimi kama mwana-Mageuzi, nimepata kushauri baadhi ya hawa wana-CMM ambao tumefahamiana kwa miaka mingi, wakihame chama chao na kujiunga na chama kama Chadema ambacho kimedhihirisha kwamba kinakubaliana na msimamo wao wa kupinga rushwa na kiliibua mjadala huu. Baadhi yao wamenieleza kwamba kuna misimamo mingine ya CCM ambayo inawavutia, na suala la rushwa peke yake haliwezi kuwafanya wakihame chama.

Labda lao hilo ni jibu sahihi, ingawa kwa kweli nakiri sijui mvuto wa CCM kwa Mtanzania mzalendo thabiti kwa sasa ni nini. Labda wanadhani wanaweza kubadilisha mwenendo wa chama hicho wakibaki ndani.

Ukitafakari kwa kina siasa za Tanzania na hali za wana-siasa, utaweza kubaini kwamba Katiba na Sheria ya Uchaguzi zinawabana wawakilishi, wakiwepo wabunge, kuendelea na chama chao hata pale chama na uongozi wake wanakiuka misimamo ya awali, wanashindwa kutekeleza ahadi na/au wanatenda mbambo kinyume na maslahi ya taifa na dhamiri (conscience) njema. Katika nchi zinazozingatia demokrasia ya kweli, chama kama hicho kinaachia ngazi kutokana na Bunge kupitisha azimio la kukosa imani na uongozi au chama. Lakini hapa kwetu jambo kama hilo halifanyiki; sio kutokana na kwamba chama hakikiuki maadili, bali kutokana na Katiba, sheria na taratibu mbovu.

Kwa hiyo pendekezo langu la kwanza ni kwamba Katiba, sheria na taratibu zirekebishwe ili umma kupitia wawakilishi wao, yaani Bunge, kuweza kuiondoa madarakani Serikali yoyote wakati wowote inapodhihirika imekiuka maadili, ahadi na maslahi ya taifa kama ilivyotokea kuhusu Richmond, ulipaji wa fedha za EPA katika Benki Kuu na kukubali mikataba mibovu mingine inayowaumiza na kuwaathiri wananchi sana. Isiwe ni lazima kungojea mpaka miaka mitano ipite.

Ningetaka kusisitiza kwamba Mbunge au Diwani anachaguliwa na umma. Hapa ninamaanisha kwamba wanachama wa vyama vya siasa katika jimbo/kata ni wachache sana kulingana na idadi ya wananchi wapigao kura. Wengi wa wabunge au madiwani huchaguliwa kutokana na haiba na mahusiano yao na umma na jinsi wanavyoweza kutatua matatizo ya kijamii. Licha ya ukweli huu, Mbunge akiamua kujiuzulu kutoka chama kilichomsimamisha, anapoteza ubunge wake. Vivyo hivyo kama diwani akifanya hivyo, anapoteza udiwani wake. Hii inamaanisha kwamba hawa wawakilishi kila wakati wanahofia kujiuzulu ili kujiunga na kambi ya kutetea maslahi ya umma kwa vile wanatambua ni vigumu kupinga chama tawala na kurudia katika nyadhifa zao mara tu baada ya kukihama.

Kwa hiyo pendekezo langu la pili ni kwamba Katiba yetu na Sheria ya Uchaguzi virekebishwe kuruhusu Mbunge au Diwani kujiuzulu toka chama chake bila kupoteza uwakilishi wake. Naamini hatua hii itaimarisha uhuru wa wawakilishi na demokrasia thabiti katika nchi yetu. Bunge likiimarika, Serikali itatekeleza majukumu yake kwa uadilifu, uzembe utapungua na maendeleo na huduma za kijamii zitanoga kwa manufaa ya wote. Narudia kwamba Katiba yetu inayotamka kwamba Bunge ndicho chombo kikuu kitakachokuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kusimamia na kushauri Serikali, itatekelezwa kwa ukamilifu zaidi endapo wabunge hawatawekewa vizingiti na vikwazo katika kukosoa Serikali.

Kama tunadhamiria kwa dhati kusimika demokrasia ya kweli hapa nchini, ni lazima wabunge wawe na uhuru wa kweli kuchangia na kutoa mawazo kulingana na dhamiri yao (conscience), na wakiona ni lazima, basi wahame toka chama chao hasa ikiwa, kwa maoni yao, chama kinakwenda kinyume na maslahi ya umma na taifa. Viongozi wa chama chochote tawala, wakidhihirisha ni waroho wa madaraka na wanatumia nyadhifa zao kujinufaisha binafsi, ni lazima wanachama wazalendo wa kweli wapinge mwenendo huo na wawaondoe katika uongozi huo. La sivyo, basi hao wazalendo wawaachie chama chao hao viongozi mafisadi, wahamie kingine au waunde chama kipya, bila hofu ya kufukuzwa Bungeni.

Hata hivyo, natambua kwamba kama maamuzi ya Mahakama Kuu ya hivi karibuni kuhusu mgombea wa kujitegemea yatazingatiwa na kuingizwa katika Katiba ya nchi na Sheria ya Uchaguzi, basi hata kipengele kinachotaka Mbunge au Diwani aachie uwakilishi wake pale anapojiuzulu kutoka chama chake cha awali, utakuwa hauna mantiki. Kuingia Bungeni hakutategemea tena ulazima wa kuteuliwa na chama cha siasa.

Hapa nieleweke pia kwamba ni lazima vyama vya siasa viwepo na viwe ni vyama imara kama tunataka kuimarisha michango ya mawazo na uchambuzi wa kina katika miswada iletwayo Bungeni na Serikali. Hii haipingani na msimamo kuwa demokrasia ya kweli na uhuru kamili unaweza kuwepo tu pale wanasiasa kibinafsi wanapokuwa huru kwa dhati kutoa maoni yao kwa ujasiri na uzalendo kwa manufaa ya umma.

0 comments:

Post a Comment