Wednesday, August 11, 2010

MSITUZINGUE NA: 'UWEPO AU USIWEPO MDAHALO?

Na Subi Sabato.

Kwa dhana ya taaluma, mdahalo ni kitendo cha watu kujadili aidha kwa kukubali au kukataa mada iliyowekwa mbele yao; Na kwa dhana ya siasa, mdahalo ni kitendo cha wahusika wakuu kujadili hoja kwa kutetea zao au kupinga za wenzao kwa kufuata mrengo wa wauliza maswali (wananchi).

Yamekuwepo malumbano baina ya wadau wa vyama vikuu viwili vya siasa nchini, CHADEMA na CCM, wengine wakitaka mdahalo il hali wengine wakisema, aghalabu kudharau umuhimu wa mdahalo.

Ifahamike kuwa, tofauti na dhana iliyojengeka kwa baadhi ya watu ambao wanataka kuuambia umma ukubaliane nao, ya kuwa kufanya mdahalo ni kupoteza muda, ukweli uli haki ni kwamba, katika siasa ya dunia ya sasa inayohimiza demokrasia na ambayo kwa kiasi kikubwa nchi ya Tanzania huifuata, mdahalo ni fursa pekee na heshima kubwa ya kuwapa wananchi nafasi ya kuwaona na kusemezana viongozi wa vyama kadha wa kadha kwa pamoja, wakapata kuwasikiliza hoja zao na tetezi zao.

Ni njia mahsusi ya raia kutumia uhuru wao wa kuzungumza, wakapata kusikizwa na hao watarajiwa wanaowaomba wawapatie dhamana ya uongozi. Ni nafasi nzuri ya kuwaruhusu wananchi kuuliza maswali yanayowatatiza waliyokosa nafasi ya kuyawakilisha kutokana na sababu kadha wa kadha zisizozuilika, ikiwemo ya kujibiidisha makazini ili kutokukupoteza muda kufuatilia masuala ya siasa kwenye muda wa kazi.

Kufanya mdahalo si ada useme ni kitendo cha siku baada ya siku kama zilivyo kampeni hata mtu alalame kuwa inachosha, la! Ni kuwawezesha wananchi kutenga siku moja au mbili maalumu, wakaacha vingine vyote ili wapate kuwasikiza Wawakilishi ambao mmoja kati yao atakuwa kiongozi wao Mkuu mtoa amri.

Kwa takwimu za nchi mbalimbali duniani, siku ya mdahalo ni siku ambayo watazamaji wa luninga na wasikilizaji wa redio huongezeka sana na magazeti kuuzika sana kesho yake kufuatia mdahalo na hata watu kuhifadhi kumbukumbu hizo muhimu. Watu hufanya hivi kwa kuwa wanafahamu kuwa watapata fursa ya kuwasikiliza wagombea wote kwa pamoja kwa wakati mmoja. Nafasi hii hutokea kwa nadra sana. Je, viongozi wa vyama hawaoni kuwa hii ni heshima na nafasi ya pekee kuwaenzi wananchi kwa muda mfupi tu?

Viongozi wengi wa nchi za nje wa mataifa yanayotajwa kuwa yameendelea, mathalan Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Japan nk, heshima hii ya kuzungumza na wananchi kwa njia ya mdahalo imesaidia kukuza demokrasia na kuongeza ufahamu wa wananchi kuhusiana na maswala mbalimbali na hivyo kufahamu njia na muelekeo wa Taifa lao. Mtu mwenye siasa safi hawezi kukwepa majadiliano na umma.

Kufanya mdahalo si dharau.
Kufanya mdahalo si udhalilishaji.
Mdahalo si kipimo cha nani anajua kuzungumza zaidi ya nani.
Kufanya mdahalo si kipimo cha kukubalika au kiashirio cha ushindi, la hasha.
Kama 'livyosema awali, ni sehemu ya kuwakilisha sera, mipango na matazamio ya wagombea uongozi, ili wananchi wapate kufahamu.

Nimalize kwa kusema kuwa, nimesikitishwa sana na kauli zinazotolewa na baadhi ya watu kwa kusema ati Raisi wa sasa wa Tanzania hawezi kulinganishwa wala kufanyiwa mdahalo na wagombea wengine wa kiti hicho kwa kuwa tu, yeye amekuwa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano na, amefanya mengi. Nionavyo mimi, hili si sahihi hata kidogo. Huu ni sawa na ukwepaji au utetezi usio na tija, nachelea kusema ni sawa na ukiherehere. Tena nidhaniavyo mimi, aliyekuwa madarakani kwa muda ndiye haswa anapaswa mhusika mkuu katika mdahalo, kwani pamoja na utaratibu uliopo wa kuufahamisha umma kuhusu mafanikio ya malengo yake katika kipindi hicho, wapo wananchi wengi wanaoishi maeneo ya mbali ambao kuzipata taarifa hizo ni nadra, kama siyo haiwezekani kabisa; Ila kupitia mdahalo, wananchi wengi wanapata kwa ufupi kufahamu yaliyotendeka na yasiyotendeka na mikakati iliyopo. Pia, si sahihi kusema kwamba yaliyofanywa yanaonekana dhahiri; Wapo ambao hawaoni yaliyotendeka makwao, hivyo wangependa kufahamishwa kwa wakati huu. Wawakilishi na Wabunge wanaweza kujibu maswali hayo, ndiyo, lakini ni dhahiri hawawezi kufikia uzito na hadhi ya kukat akiu anayopewa asemapo aidha, Kiongozi Mkuu au Kiongozi Mkuu Mtarajiwa.

Tafadhalini viongozi wa vyama vyote, jifunzeni kusikiliza, kujadiliana, kuchambua hoja na kufikiri vyema kabla ya kuzungumza. Wakale walisema, 'kuchamba kwingi huondoka na mavi' kwa maana kuwa, kusema sana ndani yake huwepo uongo na kupotosha maana kusudiwa
(soma Mithali za Nabii Suleman sura ya 10 katika Biblia utauona mstari ufananao na maneno hayo); hivyo wasemaji au wenye dhamana ya chama chochote, tendeni na neneni kwa haki. Msipende kukurupuka kwa jazba zinazojawa na hisia za kutaka kujitetea nafsi zenu ninyi binafsi, au kuwakingia kifua wakuu wenu ama vyama vyenu, hata kama kujitetea huko yabidi kusema porojo tu. Siasa zenyewe zilivyo tu, ni kizungumkuti tosha!, kuongeza maneno yasiyo na mantiki ni kuharibu zaidi.

Ikiwa mwisho wa Siasa ni kulitakia mema Taifa letu, basi ni vyema kila mhusika wa chama chochote akuchambua mashambulizi ya wapinzani wao kwa kuzingatia faida na hasara ya Kitaifa, ndipo akaamua jambo la mbolea la kuzungumza. Tujenge hoja za nguvu, na si ubabe na nguvu kwenye hoja. Siasa za kupinga lolote atakalosema mpinzani wako ati kwa kuwa tu ni mpinzani na si vinginevyo, hazitufai. Tukumbuke kuwa sisi sote ni Watanzania na lengo letu ni moja, nchi iliyoendelea ambapo raia wake wanapata huduma zote muhimu bila bughudha wala usumbufu kama uliopo sasa. Sasa lengo ingawa laweza kuwa moja, njia za kulifikia zaweza kutofautiana, basi tukubaliane katika kutofautiana huko.

Waislam wote, wenye kuzitii amri za Mola, nakutakieni mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

0 comments:

Post a Comment