Monday, August 30, 2010

Edwin Mtei - Majukumu Makuu ya Chadema

Nilipofunga kompyuta yangu asubuhi leo ili nishughulikie mambo binafsi yanayoniletea kipato, nilikuwa nimechangia kwa ufupi topic kwamba "Watanzania si Mabwege" any more. Mhe. Kinana alikuwa amenukuliwa au alijieleza kuhusu misimamo ya chama chake cha CCM, kwamba WaTz. si mabwege, na eti Chadema wanadhani hivyo, kwa kuteua mgombea mwenza asiye na degree.

Kama Muasisi wa Chadema, nilisisitiza ni jukumu la Chadema hasa wakati huu wa kampeni za uchaguzi, kufichua uoza wa CCM na kuonyesha weaknesses za viongozi wao, tukiwataja majina pale tulipo na ushahidi. Hiyo ndio demokrasia. Tunahitaji ujasiri na uzalendo ili wananchi wapate viongozi adilifu.

Nilipofungua kompyuta baadaye nilimkuta Mhe. Kinana akizunguzia Chadema 'Kupotoka' kwa kutaja watu ambao kesi zao za ufisadi ziko mahakamani. Kinana namheshimu sana kwa vile amepata kuongoza wizara nyeti serikalini kama mimi. Lakini serikali wakati wetu, ikimshutumu mtu yeyote, ingeshauri CCM ya wakati huo isimteue Mgombea! Sisi Chadema tunasema "Mafisadi pamoja na Watuhumiwa wa ufisadi Ziiiiii". Watanzania msikubali kupotoshwa na wakina Kinana Oktoba 2010. Hawakubaliki!

Nataka kuongezea kuwa jukumu jingine kuu la Chadema sasa ni kujiandaa kuchunga kura tutakazopigiwa na Watanzania wanaoridhika kwamba sisi ni chama m'badala wa CCM na kwamba Dk. Slaa atafaa zaidi kuliko Kikwete.

Ni lazima kila kituo cha kupigia kura kiwe na wakala wetu shupavu, mkali na jasiri. Ahakikishe ni mpiga kura stahiki tu anapiga kura, na mara moja tu. Ujanja wa CCM kuleta watu wao kurudia kupiga kura, au kununua vitambulisho ili wapenzi wetu washindwe kupiga kura vifichuliwe mapema. Hakuna kulala, mpaka kieleweke.

Namalizia kuwatahadharisha wananchi wenzangu kwamba yaliyotokea pale Jangwani juzi, ambapo wafanyakazi wa TBC walirushiwa mawe na wapenzi wa Chadema wakati TBC walipositisha matangazo 'live' ya mkutano wao, yanaashiria uvumilivu wa WaTz. unafikia kikomo.

Endapo dalili za kutumia vyombo vya umma, kama TBC, ili kuhujumu au kukandamiza upinzani halali zitaendelezwa na serikali, CCM na viongozi wake watabeba lawama kwa lolote litakalotokea. Mimi binafsi nashauri wapenzi wa Chadema wawe watulivu na wapenda amani. Lakini wenye uwezo wa kuepusha vurugu ni wale walio madarakani sasa.

Ahsanteni

1 comments:

Unknown said...

Asante kwa maneno mazito, mazuri na yenye kutoa muongozo.

Tutalala tu pale kitakapoeleweka!

Post a Comment