Wednesday, August 11, 2010

Mchango wa Zitto Kabwe katika Bajeti ya Serikali 2010/2011

Dodoma, 11/6/2010.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Bajeti, hotuba ya mwisho ya bajeti kwa Serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi katika kipindi chake cha miaka 5 toka wameingia madarakani. Toka Serikali hii imeingia madarakani kwa miaka 4 iliyopita Bunge limeidhinisha zaidi ya shilingi trilioni 26 kama bajeti, [2006/2007 Tshs 4tr, 2007/2008 Tshs 6tr, 2008/2009 Tshs 7tr na 2009/2010 Tshs 9tr] toka mwaka 2006/2007 mpaka mwaka 2009/2010. Leo na mpaka Jumatatu tunajadili na kwa wingi wa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi humu kwa vyotevyote vile watatoa hundi nyingine ya shilingi trilioni 11. Kwa hiyo jumla katika miaka 5 tutakuwa tumewapa [serikali] jumla ya shilingi trilioni 37 kwa ajili ya kuweza kuleta maendeleo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika kipindi cha miaka 4 iliyopita jumla ya Watanzania milioni 1.9 wamekuwa maskini zaidi na kuongeza idadi ya watu maskini mpaka kufikia watu milioni 13. Kwa hiyo tunapojadili bajeti hii tunazungumza bajeti ambayo tuna Watanzania zaidi ya milioni 13 ambao wanaishi chini ya Dola moja kwa siku na bajeti hii haijibu matarajio yao. Bajeti hii haielezi ni jinsi gani Watanzania hawa wataweza kushiriki katika uchumi na kukua na kuondoka katika wimbi la umaskini.

Bajeti hii ni the longest suicide letter ambayo Chama cha Mapinduzi imejiandikia mbele ya wananchi. Kwa sababu ni bajeti ambayo inatoa faida zaidi kwa watu ambao tayari wana uwezo [rich people] na haielezi jinsi ya kuondoa changamoto kwa watu ambao ni maskini [impoverished people] zaidi ya milioni 13.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa aliyetoka kuzungumza hivi sasa [mheshimiwa Mzindakaya] alizungumza kuhusiana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi.

Mwaka 2005 Chama cha Mapinduzi kiliwaahidi Watanzania kwamba watahakikisha kwenye ilani yao sekta ya kilimo inakua kwa asilimia 20 [!]. Kwa mujibu wa MKUKUTA wa kwanza ambao tunaumaliza sasa ilitakiwa sekta ya kilimo ikue kwa asilimia kati ya 8 mpaka 10 ili kuweza kuwaondoa nusu ya Watanzania kwenye umaskini [wa kutupwa].

Kwa masikitiko makubwa kwa taarifa ya hali ya uchumi ambayo Waziri wa Fedha ameisoma jana sekta ya kilimo ilikua kwa asilimia 3.2 tu mwaka 2009 [ukiweka na wastani wa ukuaji wa idadi ya watu pamoja na madhara ya mfumuko wa bei ukuaji huu ni hasi (negative growth)].

Katika kipindi cha miaka 5 toka Serikali ya awamu ya 4 iingie madarakani sekta ya kilimo imekua kwa wastani wa asilimia 4 peke yake. Mmeshindwa hata kufikia nusu ya malengo yenu ya ilani ya Chama cha Mapinduzi. Mmeshindwa hata kufikia nusu ya ahadi kwa mujibu wa MKUKUTA. Hii ni aibu kubwa sana na tumewapa jumla ya shilingi trilioni 26 kwa miaka 4 iliyopita na mmeshidwa kukuza kilimo angalau kufikia nusu ya mambo ambayo nyinyi mlikuwa mmeyatarajia.

Faida kama za Dodoma University, nilikuwa naomba nitoe challenge. Kwa Mbunge yoyote wa Chama cha Mapinduzi asimame na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi aonyeshe ni wapi Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi imesema itajenga Chuo Kikuu Dodoma?

Yeyote miongoni mwenu asimame nam-challenge, hakuna. Mtu yeyote asimame na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi aseme Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi iliahidi University of Dodoma, hakuna. Kwa hiyo hamuwezi kufaidika na kutaka kujisifu kwa vitu ambavyo wala hamkuwaambia wananchi. UDOM wazo la ujenzi na kugeuza Dodoma kuwa University City ni wazo ambalo lilitolewa na CHADEMA toka mwaka 1992. Huo ndio ukweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha ametusomea bajeti ya mapato ya ndani kuongezeka kwa zaidi ya shilingi trilioni moja (Domestic Revenue). Tofauti kati ya Recurrent Budget [Bajeti ya kawaida] peke yake kwa mujibu wa takwimu ambazo amezisoma Waziri wa Fedha zinaonyesha kwamba asilimia 23 ya Recurrent Budget ita-financi-wa [itagharamiwa] kutokana na mikopo na misaada kutoka nje. Recurrent yaani Mishahara, Mafuta jumla ya shilingi trilioni 1.8 ni a black hole kwenye Recurrent Budget.

Huko nyuma tulifikia wakati ambapo (Domestic Revenue) au fedha za ndani ziliweza kuendesha matumizi ya kawaida. Sasa hivi tunakwenda katika hali ambayo fedha za ndani hazitoshi kuendesha matumizi ya kawaida. Hii ni hali mbaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani katika kila shilingi 100 tunaitumia katika matumizi ya kawaida shilingi 23 inabidi twende tukakope, tunakopa kulipa mishahara, tunakopa kulipa posho, tunakopa kununua mafuta ya magari yetu, hii ni nchi ya namna gani?

Kama alivyosema Waziri Kivuli wa Fedha na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Fedha na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni [Hamad Rashid Mohammed] bajeti hii ni moja ya bajeti mbaya kuliko zote katika historia ya nchi yetu. Kwa sababu ni bajeti ya kuchumia tumbo, ni bajeti ya chote tunachokikusanya tunakila hatuendelei na bado tunabakia na gap ya kwenda kutafuta na kwenda kukopa na misaada kwa ajili ya kula na sio kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa sababu asilimia 65 ya bajeti ya maendeleo bado inategemea wafadhili na ukichukua recurrent na development budget asilimia 44 ya bajeti yetu na sio 33 kama Waziri alivyosema bajeti bado tunategemea wafadhili.

[Bajeti ya matumizi ya kawaida ina nakisi ya Tshs 1.8tr ambayo itazibwa na misaada ya wafadhili na mikopo kutoka ndani na nje. Inasemekana mwaka huu Serikali itafanya Deficit Financing (PRINTING MONEY!!!) ya thamani ya takribani 350bn. Katika Bajeti ya Maendeleo kuna nakisi ya Tsh 2.4tr ambayo ni sawa na asilimia 65 ya Bajeti ya Maendeleo na itazibwa na misaada na mikopo kutoka ndani na nje ya nchi].

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Serikali ikubali sio sifa kuwa na bajeti kubwa sana. Kwa sababu bajeti hii inapelekea kwa mfano kodi ambazo zitaongezeka kwa ajili ya kuziba kuongeza mwanya wa makusanyo shilingi bilioni 300 zinatoka Large Tax Payers Department. [ Kodi mpya zinazopendekezwa kukusanywa za jumla ya shilingi 1tr, 300bn zitatoka kwa walipa kodi wakubwa, 300bn kodi za biashara ya kimtaifa ie trade taxes na 110bn kutokana na PAYE. Shilingi 300bn nyingine zitatoka ‘non-tax revenue ambapo 153bn ni mrahaba wa Madini]. Kwa Shilingi biloni 300 zitakazotoka trade taxes na hali ya uchumi sio nzuri kiasi hicho [itabidi tutegemee importation]. Maana yake ni kwamba tunategemea watu wa import zaidi ili tuweze kukusanya zaidi. Ni hali ambayo sio nzuri ni hali ambayo inaweza kuleta matatizo zaidi katika uchumi wa Taifa letu. [kwa kodi kutoka walipaji wakubwa na PAYE makadirio yanaweza yasifikiwe maana zitategmea mazingira ya biashara na hasa ukizingatia kuwa Serikali itaenda kukopa katika mabenki na crowding out effect itakosesha private sector mikopo na hata kupunguza uzalishaji na kupunguza ajira].

[mapendekezo ya kutatua changamoto hizi ni pamoja na kupunguza matumizi ya kawaida kwa kiasi kikubwa ikiwemo kupunguza sana posho zikiwemo posho kwa Wabunge na viongozi wa Serikali na matumizi makubwa ya mafuta ya magari (fuel bill). Pili, badala ya kukopa katika Benki za Biashara Serikali itoe Infrastructure Bond kwa ajili ya kupata fedha za kutengeneza mfumo wa usafirishaji umeme, kuimarisha gridi ya Taifa na kujenga Gridi mpya ya Kaskazini Magharibi. Tatu, Uzalishaji wa Umeme (power generation) ufanywe na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama ambavyo wameelekezwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma. Nne, Serikali iuze 25% ya hisa zake katika Kampuni ya simu ya Zain Tanzania kupitia IPO. Uuzwaji wa sehemu ya hisa za serikali katika Benki ya NBC bado haupo wazi kwani mapato ambayo serikali inasema itapata ni kidogo mno kulingana thamani ya Benki hiyo (serikali ina hisa 30% na wanasema watapata Tshs 30bn. Serikali ikiuza asilimia 20 ya hisa NBC kwa njia ya IPO itapata zaidi ya Tshs 100bn). Tano, EuroBond ilete mapato yatakayotumika kujenga Barabara na Reli peke yake ili kupata manufaa ya mkopo huu ambao utakuwa ghali sana].

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha amezungumza kuhusu kuuzwa kwa hisa za NBC na Serikali kupata zaidi ya shilingi bilioni 30. Lakini nimeangalia kitabu namba moja Revenue Book hiyo source of revenue haimo. Kwa hiyo nilikuwa naomba Waziri wa Fedha aweze kutoa ufafanuzi ? [Kila shilingi inayotarajiwa kukusanywa na Serikali ni lazima ionyeshwe katika Kitabu Na 1 cha Mapato ya Serikali. Tshs 30bn zimetajwa katika Hotuba ya Bajeti lakini haimo katika kitabu hicho.....!!!!].

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu na la mwisho kwa sababu ya muda. Waziri wa Fedha jana alizungumza kurejesha misamaha ya kodi ya mafuta kwa Kampuni za Madini. Madhara ya uamuzi ambao umeufanya ambao ni kwamba tunarudi nyuma, ile goodwill ambayo tumeitengeneza kwenye Sheria Mpya ya Madini tunaiua. Naelewa kwamba Serikali inaogopa kushtakiwa kwa sababu watu wamesaini zile MDA[mineral development agreements]. Lakini kuna namna za kuhakikisha kwamba sekta ya madini inafungamanishwa na sekta nyingine za uchumi.

Ukiruhusu Makampuni ya Madini yaagize mafuta kuzalisha umeme wao bila kulipa kodi maana yake ni kwamba hawatanunua umeme kutoka TANESCO. Sasa hivi kuna kazi ambayo imefanyika tayari Wizara ya Nishati na Madini. Migodi yote isipokuwa mmoja sasa unaweza kupata umeme kutoka TANESCO. Lakini kwa kuwaruhusu kuagiza mafuta ya kuzalisha umeme wao wenyewe tunaingia kwenye tatizo la fungamanisho kati ya sekta ya madini na sekta ya umeme. [Migodi hutumia takribani asilimia 13 ya gharama zake za uzalishaji katika Umeme]

[Vile vile, Kwa kuwa msamaha huu hautahusisha wakandarasi wa ndani wanaofanya biashara na Kampuni za Madini (local contractors), hivyo hapatakuwa na vivutio kwa kampuni za madini kutumia wakandarasi wa ndani. Kampuni za madini zitaona ni rahisi zaidi (less costly) kufanya shughuli ya kuchimba wenyewe (owner mining). Hii inaua (kills) dhana ya fungamanisho kati ya sekta ya madini na sekta ya ujenzi (construction sector) ambayo ilikuwa ni dhumuni mojawapo la Sheria mpya ya madini ili kujibu changamoto ya fungamanisho dogo la sekta ya Madini na sekta nyingine za Uchumi (low integration of the mining sector to other sectors of the economy). Katika muundo wa gharama za uzalishaji kwa Kampuni za madini, takribani asilimia 30 ni gharama za kuchimba].

[Napendekeza kama ifuatavyo]

Kuhusu Umeme; Sheria ya fedha iseme wazi kuwa mara baada ya migodi yote kupata Umeme kutoka TANESCO, msamaha wa mafuta utakwisha.

Kuhusu Makandarasi wa ndani;

Ama (a) Msamaha huu uendelezwe mpaka kwa kampuni za ujenzi katika migodi (local contractors [worst case scenario].

Au (b) Katika Finance Bill, kuanzishwe (introduce) 15% withholding tax on technical services kwa kampuni za madini zitakazofanya “owner mining” (second best case scenario).

Kwa kuwa local contractors wamatozwa 5% withholding tax on technical services, itakuwa ni rahisi (cheap) kwa kampuni za madini kutoa zabuni (tender) kwa kampuni za ndani. Hata hivyo pendekezo hili litaathiriwa na MDAs zilizopo.

Kwa hiyo kuna haja ya kuwa na measures maalum ya ku-mitigate huo uamuzi ambao Serikali imeufanya [kurejesha msamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni za madini] na kwa vyovyote vile si uamuzi sahihi na uamuzi ambao haukufikiriwa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, siungi Bajeti mkono.

0 comments:

Post a Comment