----------
1.0 UTANGULIZI
Ndugu Wafanyakazi, SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) ni Muungano wa Vyama huru vya Wafanyakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bara, ambavyo kwa pamoja vimejitoa kwa moyo kulinda,kutetea na kuendeleza haki za wafanyakazi ili kufanya maisha yao na familia zao kuwa yenye usalama, afya na ustawi.
Aidha kwa pamoja SHIRIKISHO limeazimia kujenga mshikamano na heshima miongoni mwa wafanyakazi katika kutetea hadhi ya kazi kama msingi imara wa harakati za wafanyakazi. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Toleo la 2005 inatambua kuwa kila mtu bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake. Pia kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki pamoja na haki ya kupata hifadhi sawa chini ya Sheria.
Katika kutambua wajibu huo muhimu kwa Wafanyakazi, Mkutano Mkuu wa Kazi wa TUCTA uliofanyika Arusha Oktoba 24 na 25 mwaka 2009, uliazimia na kutoa Tamko la kuipa Serikali muda wa miezi mitatu mpaka Januari 2010 ishughulikie matatizo sugu ya Mshahara duni, Kodi kubwa na Mafao ya Uzeeni vinginevyo TUCTA ingeandaa mgomo. Katika kikao cha Baraza Kuu la TUCTA lilofanyika Morogoro tarehe 4 na 5 Machi Mwaka huu, Baraza Kuu likatoa agizo la kuandaa mgomo mara moja baada ya kukosa majibu kutoka Serikalini.
2.0 HOTUBA YA MHESHIMIWA RAIS
2.1 RAIS KUKUTANA NA WAZEE WA DAR ES SALAAM
Ndugu Wafanyakazi, katika mada kuu mbili alizoongea Rais, mada moja na iliyochukuwa uzito kwenye Hotuba yake ilikuwa inawahusu Wafanyakazi na Shirikisho lao na hasa Viongozi wao. Pamoja na kwamba TUCTA kwa niaba ya Wafanyakazi ilikubali kurudi kwenye meza ya majadiliano kwa kuitikia wito wake, Rais hakutupa nafasi ya kutusikiliza badala yake akaamua kusikiliza upande mmoja. Kwa hili tunaona kwamba Rais hakututendea haki na ni kinyume cha maadili ya nchi iliyoridhia misingi ya Utawala Bora.
2.2 UHALALI WA MGOMO SHINIKIZI (PROTEST ACTION) ULIOTARAJIWA KUFANYIKA TAREHE 05.5.2010
Ndugu Wafanyakazi, TUCTA imesikitishwa na Kauli ya Mhe. Rais kutangaza kuwa Mgomo ni batili. Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004, Rais hana Mamlaka ya kubatilisha au kuhalalisha Mgomo. Chombo pekee chenye Mamlaka hayo ni Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
TUCTA inawahakikishia wanachama wake na Watanzania kwa ujumla kuwa Mgomo Shinikizi ni halali na uliitishwa kwa mujibu wa Sheria. Kwa taarifa TUCTA iliitisha Mgomo Shinikizi (Protest Action) kwa kuwasilisha kwenye Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO), Notisi iliyozingatia matakwa ya kifungu cha 85 (1) (a), (b), (c) na (d) ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya Mwaka 2004. Baraza hilo liliitishwa mnamo tarehe 25.3.2010 na kwa kuzingatia sababu saba zilizoambatanishwa kwenye Notisi ya Mgomo. Baraza lilijadili kwa kina na kuridhishwa na sababu hizo na ndiyo maana halikubatilisha wala kupinga notisi ile. Ili kukidhi hitaji la Sheria ya Ajira Na Mahusiano Kazini Na.6 ya Mwaka 2004 kifungu cha 85 (4) (b) Baraza liliamua kumteua Msuluhishi Ndugu Cosmas Msigwa, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.
Msuluhishi alitekeleza wajibu wake na kuitisha kikao cha pande zote mbili mnamo tarehe 06.4.2010. Kikao hicho kilipokea na kujadili suala hilo. Baada ya hapo kikao kiliahirishwa hadi tarehe 13.4.2010. Kwenye kikao hicho makubaliano yalifikiwa ya jinsi ya kushughulikia Madai ya TUCTA kwa niaba ya Wafanyakazi kuwa yafikie tamati kabla ya siku ya Mei Mosi. Hivyo kwa mujibu wa Sheria hiyo na utaratibu uliofuatwa Mgomo Shinikizi ni halali.
Ndugu Wafanyakazi, kauli ya Mheshimiwa Rais kwamba, TUCTA imetangaza Mgomo katikati ya Majadiliano siyo ya kweli, kwani Mgomo huu ulitangazwa kabla ya kurudi kwenye meza ya Majadiliano. Vile vile ikumbukwe kwamba Mgomo wetu uliitishwa kabla ya Mhe. Rais kutuomba kurudi kwenye Meza ya Majadiliano.
2.3 AJENDA YA MGOMO SHINIKIZI (PROTEST ACTION)
Ndugu Wafanyakazi, Mheshimiwa Rais katika Hotuba yake alieleza kuwa Mgomo ni ajenda ya Viongozi wa TUCTA na haikuwa kwenye ajenda za vikao vya Shirikisho bali ilikuja kama mengineyo. Maneno haya si ya kweli kwani Ajenda hii haikuanzia kwenye Kikao cha Baraza Kuu Mjini Morogoro Mwezi Machi 2010, bali ilianzia kwenye Mkutano Mkuu wa Kazi mjini Arusha Oktoba 24 na 25 mwaka 2009. Mkutano huo uliazimia kutoa Tamko na kuipa Serikali muda wa miezi mitatu mpaka Januari 2010 ili ishughulikie matatizo ya mshahara usiokidhi mahitaji ya msingi, Kodi kubwa inayokatwa kwenye Mishahara hiyo na Mafao duni yanayotolewa na baadhi ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mkutano Mkuu ulifikia azimio hilo kutokana na Serikali kwa muda mrefu kushindwa kuyatolewa ufumbuzi matatizo haya.
Hadi ilipofika mwishoni mwa Januari 2010 TUCTA ilikuwa haijapata majibu yeyote toka Serikalini. Hivyo katika kikao cha Baraza Kuu la TUCTA lilofanyika Mjini Morogoro Machi 2010, Baraza Kuu lilitoa agizo la kuandaa Mgomo mara moja.
Kwa mujibu wa Katiba ya TUCTA, Mkutano Mkuu ndiyo chombo cha juu cha Maamuzi kinachowakilisha wanachama wa Vyama Huru mbalimbali vya Wafanyakazi. Maamuzi yake yanapaswa kuheshimiwa na kutekelezwa na wanachama wote. Agizo la kuitisha Mgomo Shinikizi (Protest action) lililotolewa na Baraza Kuu mjini Mororgoro kwa Wafanyakazi nchi nzima haukuwa uamuzi wa viongozi bali ni utekelezaji wa MAAGIZO ya Mkutano Mkuu. Mnamo tarehe 15.3.2010 TUCTA ilitoa Notisi ya Siku therathini (30) kwa Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO), ya Mgomo Shinikizi (Protest Action) ambao ungefanyika tarehe 05.5.2010. Mgomo Shinikizi (Protest Action) huo ambao ungehusisha Wafanyakazi wote nchini ulizingatia Madai makuu ya Wafanyakazi yaliyohusu kuboresha kima cha chini cha mishahara kufikia shs 315,000/=, Kupunguza Kodi ya mishahara (PAYE) kwenye Mishahara ya wafanyakazi na Kuboresha Mafao yatolewayo na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
2.4 LUGHA ALIYOITUMIA MHESHIMIWA RAIS
Ndugu Wafanyakazi, Mheshimiwa Rais alitumia lugha ya vitisho, akatudhalilisha, akatushutumu na kutuhukumu. Mheshimiwa Rais alidai kwamba sisi ni waongo, wanafiki na wazandiki na tuna letu jambo katika kufanya haya yote.
Tungependa kuwafahamisha wafanyakazi na watanzania wote kwa ujumla kwamba Viongozi wa TUCTA hatuna letu jambo zaidi ya kuwatetea wafanyakazi wa nchi hii waliotuchagua ili kutetea na kulinda haki zao kwa kupitia vyama vyao, kwa mujibu wa Katiba zetu ambazo zinalindwa na Katiba ya nchi. Pamoja na kwamba wanachama wa Vyama vya Wafanyakazi wana Uhuru na Haki ya kujiunga na Vyama vya Siasa, wanapotetea haki zao hawafungamani na Chama chochote cha Siasa.
2.5 MADAI YA MHESHIMIWA RAIS KUWA VIONGOZI WA TUCTA NI WAONGO
Ndugu Wafanyakazi, tungetaka ifahamike kwamba Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi siyo waongo kama Mheshimiwa Rais alivyoelezwa na akaueleza Umma wa Watanzania. Kwa mfano Mheshimiwa Rais alidai kwamba Viongozi wa TUCTA walialikwa kuhudhuria Mkutano Hazina saa nne asubuhi na wakafika pale saa nane mchana.
Ukweli ni kwamba tulilalikwa kuhudhuria huo Mkutano kuanzia saa nane na nusu mchana kama barua Na. TYC/B/280/69 ya tarehe 22 Aprili 2010 inavyojidhihirisha, wakati makundi ya wenzetu wengine yalialikwa saa nne. Hii inaonyesha kuwa ilikuwa ni njama ya kutotaka kutushirikisha kwenye Mkutano huo kwa sababu tulifika wakati Mkutano unakaribia kumalizika. TUCTA inalaani vikali mtu au kundi la watu waliomdanganya Mheshimiwa Rais katika hili.
2.6 MADAI YA MHESHIMIWA RAIS KUWA VIONGOZI WA TUCTA NI WANAFIKI
Ndugu Wafanyakazi, katika hili tunapenda kuufahamisha Umma wa Watanzania kwamba kuna Sheria na Kanuni zinazosimamia Majadiliano, na moja wapo ya kanuni hizo ni kutotangaza matokeo wakati majadiliano hayajafikia mwisho na ndio maana TUCTA isingeweza na haitaweza kutangaza mpaka hapo majadiliano yatakapofikia mwisho.
Vile vile ieleweke kwamba Majadiliano hayo, kiutaratibu yalitakiwa yawe yamefanyika kabla ya tarehe 15 Disemba 2009. Hayakufanyika mpaka Rais alipoingilia kati baada ya TUCTA kutangaza mgomo. Na hata yanapofanyika hayakuzingatia hiyo notisi ya mgomo kwa sababu kwa watu wanaojadiliana kwa nia njema, matokeo ya majadiliano yalitakiwa yazingatie tarehe iliyokusudiwa kuitishwa mgomo ili kuuepusha. Sasa katika hili, nani mnafiki kati ya Serikali na Viongozi wa TUCTA?
Ili kuonyesha kuwa TUCTA ina nia njema, Kamati ya Utendaji iliyokutana tarehe 04/05/2010 iliamua kuahirisha Mgomo ili kusubiri matokeo ya majadiliano ya tarehe 08/05/2010. Mategemeo ya TUCTA ni kuwa Majadiliano tarehe 08.5.2010 yatafikia TAMATI siku hiyo na kutoa matunda yanayotegemewa kwa nia ya kuondoa mgogoro huo.
2.7 MATUMIZI YA LUGHA YA VITISHO
Ndugu Wafanyakazi, Mheshimiwa Rais akiwa Amiri Jeshi Mkuu, siyo jambo zuri kutumia mabavu, vitisho kwa jamii anayoiongoza ambavyo vinaweza kuchochea vurugu kwa wafanyakazi na wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Rais inafaa afahamu kwamba mgomo ni haki ya mfanyakazi kisheria, kwa hiyo anapofanya hivyo akiwa ametimiza Sheria zote hastahili kwa hali yoyote kupigwa virungu, kutupiwa mabomu au kufyatuliwa Risasi za aina yoyote, isipokuwa Serikali ina wajibu wa kumhakikishia usalama wake kwa kumpa ulinzi wa kutosha ili atimize azma yake ya mgomo wa amani.
Jambo kubwa la msingi tulilotegemea kutoka kwa Mhe. Rais lilikuwa ni kutoa majibu ya namna ya kutatua matatizo sugu ya Wafanyakazi ambayo hayakuanza leo wala jana kuliko kutoa vitisho.
2.8 TANGAZO LA MHE. WAZIRI WA KAZI JUU YA KIMA CHA CHINI CHA MISHAHARA KWENYE SEKTA BINAFSI
Ndugu Wafanyakazi, mnamo tarehe 19/04/2010 Waziri wa Kazi (Mhe. Juma Kapuya) alitangaza kwenye Vyombo vya Habari ongezeko la asilimia mia moja ya Kima cha Chini cha Mshahara katika Sekta Binafsi. Kutokana na Tangazo hilo TUCTA ilieleza kuwa hatua hiyo haikufuata taratibu za Sheria Na. 7 ya 2004. Sheria hii inamtaka Mhe. Waziri kutoa tangazo la ongezeko la mshahara baada ya kupata ushauri na mapendekezo kutoka kwenye Bodi za Mishahara za Kisekta na Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO). Ongezeko alilotangaza Mhe.Waziri Kapuya halikupitia Bodi za Mishahara ya Kisekta. Waziri anatakiwa pia kupata Mapendekezo yaliyowasilishwa kwenye Baraza la Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO).
Pia, pamoja na Ndugu Nicholaus Mgaya kuwa Mjumbe wa LESCO hakuwahi kuhudhuria kikao chochote cha Baraza hilo kikiwemo kilichofanyika tarehe 14/04/2010. Zaidi ya hayo ndugu Mgaya hakutia saini katika Viwango Vipya vya Kima cha Chini cha Mishahara kama ilivyoelezwa na Mhe. Rais katika hotuba yake.
2.9 MAJADILIANO JUU YA KIMA CHA CHINI CHA SHS 315,000/= KWA WAFANYAKAZI WA SEKTA YA UMMA
Ndugu Wafanyakazi, kupitia makubaliano ya Serikali na TUCTA yaliyofanyika tarehe 13/04/2010 chini ya Msuluhishi Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Ndugu Cosmas Msigwa, Serikali na TUCTA walikubaliana kuitisha Kikao Maalum cha Baraza la Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Umma (Public Service Negitiation Machinery) tarehe 27/04/2010. Kikao hicho kilifanyika na kikaendelea tarehe 30.4.2010.
Katika kikao hicho Pendekezo la kima cha chini kuwa shs. 315,000/- liliwasilishwa. Hata hivyo kiwango hicho hakikukubaliwa na upande wa Serikali. Pamoja na upande wa wafanyakazi kukubali kushusha kiwango Wawakilishi wa Serikali walizidi kukataa na Majadiliano kuishia kukubaliana kutokubalina.
Kutokana na utaratibu wa Majadiliano, Makubaliano ya kukubaliana kutokubaliana yalipaswa kufikishwa kwa Mhe. Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma ili ndani ya siku ishirini na moja (21) aweze kutoa tuzo. Hivyo wajumbe wa kikao hicho kwa namna yoyote ile na kwa mujibu wa Sheria ya Majadiliano katika Utumishi wa Umma hawakupaswa kutangaza chochote kwa Wafanyakazi juu ya Makubaliano ndani ya kipindi hicho. Aidha ni kinyume cha Sheria hata Mhe. Rais kutangaza matokeo ya Majadiliano yaliyofanyika ndani ya kikao hicho. Aidha TUCTA tunamshangaa Mhe. Rais kusema kwamba upande wa Wafanyakazi walipunguza kiwango mara mbili, kwani huo siyo utaratibu wa Majadiliano.
Pia maneno ya Mhe. Rais kuwa TUCTA ilisema kuwa iwapo Serikali haitatangaza kima cha chini cha sh. 315,000/= ndani ya siku mbili wafanyakazi wagome siyo ya kweli, kwani katika Risala ya wafanyakazi kwa Mgeni Rasmi ilitamkwa kuwa Mwaka 2006, TUCTA ilifanya utafiti na kuona kuwa Sh. 315,000/= ndiyo kiwango cha chini cha mshahara ambacho kingemwezesha mfanyakazi kumudu mahitaji muhimu kwa mwezi. Hivyo si kwenye Risala wala Hotuba iliyotaja juu ya siku mbili kufanyika Mgomo.
2.10 KAULI YA MHE. RAIS JUU YA KIMA CHA CHINI CHA MSHAHARA CHA SH. 315,000/=
Ndugu Wafanyakazi, kauli ya Mheshimiwa Rais katika Hotuba yake kuwa ‘ Serikali haiwezi kuwalipa wafanyakazi wake kima cha chini cha shs.315,000/= hata wakigoma miaka nane (8) ni ya kushtua na ya kukatisha tamaa kwa vile inaonyesha jinsi gani Serikali hii isivyo na mipango na mikakati madhubuti ya jinsi ya kuongeza pato la Taifa na hatimaye kuongeza Mishahara ya Watumishi wake ambao ni muhimu katika ukuzaji uchumi. Hii pia ni kinyume cha dhamira ya Serikali ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania kama hiyo dhamira bado ipo basi tabaka la Wafanyakazi wa nchi hii limetengwa kwenye dhamira hiyo.
2.11 UWEZO WA SERIKALI KULIPA MSHAHARA KIMA CHA CHINI CHA SHS. 315,000/=
Ndugu Wafanyakazi, TUCTA bado inasisitiza kuwa kima hicho cha Mshahara kwa watumishi wake kinawezekana iwapo Serikali itachukua hatua zifuatazo;
- Kuziba mianya yote ya upotevu wa fedha za Serikali ambazo ni zaidi ya Bilioni 50 ( Rejea; A General Report of The Controller and Auditor General for the Year ended 30th. June,2009).
- Kupunguza posho kwa Watumishi wa ngazi za juu na badala yake posho hizo zihamishiwe kwenye Mishahara. Mfano Mwaka 2009/10 Serikali ilitenga asilimia 59% ya Bajeti yote ya Mishahara kwa ajili ya posho. Serikali ina kila sababu ya kuweka kipaumbele kwenye Mishahara kuliko posho inazolipa kwa watumishi wachache.
- Kupunguza Misamaha ya Kodi, Mfano Hotuba ya Bajeti ya Mwaka 2007/8 ilibainisha kwamba Misamaha ya Kodi ilifikia wastani wa asilimia therathini (30) ya Mapato yanayotokana na Kodi au asilimia 3.5 ya Pato la Taifa (GDP).
- Kuzuia Ukwepaji Kodi, Mfano kwa miaka ya hivi karibuni Tanzania imekuwa ikipoteza wastani wa Tshs. 52 bilioni kila mwaka.
- Kuondoa Matumizi ya anasa na yasiyo ya lazima, Mfano ununuzi wa Magari ya kifahari, Uagizaji wa vifaa vya ofisini kutoka nchi za nje kwa matumizi ya Serikali na baadhi ya viongozi kulipwa posho ya Mafuta kwa bei ya Tsh.2,500/= kwa lita wakati bei ya Mafuta haijafikia kiwango hicho.
- Kupunguza muachano (gap) kati ya kima cha juu na kima cha chini cha Mishahara ya Wafanyakazi Serikalini. Jambo hili linaweza kufanya fedha iliyotengwa kwenye Gharama ya Mishahara kuwanufaisha wote.
Haya yote yaliyotajwa hapo juu 1-5, yakisimamiwa vyema na kutekelezwa, Serikali yetu inao uwezo wa kulipa Mshahara wa Kima cha chini tunachodai mara moja bila kuathiri huduma nyingine na siyo kwamba hata tukisubiri Miaka minane ijayo hakitaweza kupatikana.
2.12 KAULI MBIU YA MEI MOSI KUHUSISHWA NA MAMBO YA KISIASA
Ndugu Wafanyakazi, tunapenda kusisitiza kuwa TUCTA haifungamani na Chama chochote cha Siasa bali wanachama wake ambao ni Wafanyakazi wanao uhuru na haki ya kuwa wanachama wa Chama chochote cha Siasa wanachokipenda bila kushurutishwa na mtu yeyote. Katika kipindi hiki cha kuelekea katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu, makundi mbalimbali ya kijamii yanapokutana yanatumia nafasi hiyo kuhamasishana juu ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu.
Kauli mbiu ya Mei Mosi Mwaka huu haikuwa na lengo lolote la kisiasa isipokuwa kuwahamasisha wafanyakazi kushiriki kikamilifu kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka huu na pia kuwa makini kuchagua viongozi wanaojali Maslahi ya nchi hii ikiwa ni pamoja na Wafanyakazi.
TUCTA imesikitishwa na kauli ya Mheshimiwa Rais kudai kuwa haitaji kura za Wafanyakazi wakati Wafanyakazi wanahamasishana kuchagua viongozi bora. Tueleweje?
2.13 KAULI YA MHESHIMIWA RAIS KUWA MFANYAKAZI ASIYERIDHIKA NA MSHAHARA HUU USIOTOSHA AACHE KAZI
Ndugu Wafanyakazi, kauli hii kwa viwango vyovyote vile haikuwa ya kiungwana na haikustahili kutolewa na kiongozi wa ngazi ya juu wa nchi kama Rais. Kauli hii iliwahi kutolewa na kiongozi Mwandamizi katika Serikali yake na matokeo yake tunayaona na tutaendelea kuyaona. Mhe. Rais akiwa katika Ziara nchi za nje amekuwa akiwahimiza watanzania walioko nje warudi kujenga nchi yao, wakati huku nyumbani akisisitiza kuwa Serikali haina uwezo wa kulipa mishahara inayokidhi na kumudu mahitaji ya msingi ya maisha. Kauli hizi zinakinzana na kutia mashaka.
Aidha kauli ya Mhe. Rais ya kuwafukuza kazi Wafanyakazi wote watakao shiriki Mgomo na kuwahimiza Waajiri wengine wafanye hivyo ni kinyume cha kifungu cha 83 (1), (2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya
Mwaka 2004.
3.0 HITIMISHO
Ndugu Wafanyakazi, leo mmepata nafasi ya kupata ufafanuzi kutoka kwa viongozi wenu juu ya Hotuba ya Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete kuhusu Mgomo ulioitishwa na SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi, TUCTA.
Tunaendelea kuwashauri na kuwasisitiza kuendelea kuwa na subira wakati tukisubiri matokeo ya Majadiliano ya tarehe 08.5.2010 tukiwa na matumaini kuwa majadiliano hayo yatazaa matunda yanayotarajiwa kuhusu masuala yetu matatu.
Ndugu Wafanyakazi, Mhe.Rais aliwahi kusema katika moja ya Hotuba zake kuwa ukipigana vita ya haki ushindi ni lazima. Na sisi kwa vile tunapigana vita ya haki tuna uhakika Mungu yupo nasi, hivyo tutashinda vita hii.
Asanteni kwa kunisikiliza.
MSHIKAMANO DAIMA
0 comments:
Post a Comment