Mwandishi Wetu | Agosti 18, 2010 |
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, sasa anaundiwa mkakati maalumu wa kumshughulikia, mkakati unaowashirikisha baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa na baadhi ya maofisa wa Serikali, Raia Mwema, imeelezwa.
Hata hivyo, pamoja na mikakati hiyo michafu kuandaliwa na kufahamika na CHADEMA, katika mahojiano maalumu na Raia Mwema, Dk. Slaa mwenyewe amesema hana wasiwasi wowote kutokana na kujiamini kuwa ni msafi na kwamba wanaotumika wanafahamika na hawana hoja.
Kwa mujibu wa habari za uhakika zilizotufikia, mbali na wanasiasa hao pamoja na maofisa wa dola, wamo pia baadhi ya wanasiasa wafanyabiashara ndani ya CCM ambao baadhi yao wakiwa ni wagombea ambao kwa pamoja wanajipanga kutumia mbinu zote kumdhibiti ikiwamo propaganda na hata vitisho.
“Sioni chochote cha kunishitua, ukishituka una madhambi Fulani, kama unajiamini huna dhambi zozote huhitaji kushituka na maneno ya watu hata kama unawafahamu na unafahamu mipango yao michafu.
“Bahati nzuri tunawafahamu wote na tulikuwa nao kule Tarime (kwenye uchaguzi mdogo)… maneno hayo walianza nayo Tarime yakashindikana baada ya Watanzania kuwashitukia,” alisema Dk. Slaa akirejea uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime ambako CHADEMA walishinda.
Akizungumza na Raia Mwema kwenye mahojiano ya simu jana Jumanne, Dk. Slaa alisema tayari anazo nyaraka zote zilizoandaliwa dhidi yake na kwamba hana wasiwasi na wanaojipanga kumtengenezea ‘zengwe’ kwa kuwa ana uhakika hakuna mwenye uwezo wa kuthibitisha madai yoyote dhidi yake.
“Nimesoma karatasi zao dhidi yangu…lakini nilikwishakusema ni kazi rahisi sana kusema nitamchafua mtu fulani lakini ni kazi ngumu kutoa ushahidi…kama mtu anao ushahidi auseme hadharani… mimi wakati wa EPA (Mfuko wa Fedha za Madeni ya Nje Benki Kuu) nilitoa (ushahidi) wa hadi tarehe, cheki namba na mahali zilipoingia sasa kama mtu anataka tu kuimba na aimbe hatotusumbua,” alisema Dk. Slaa.
Dk. Slaa ambaye uteuzi wake umeibua changamoto kwa wagombea wengine akiwamo wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, amezungumzia taarifa za kuwapo vitisho dhidi yake na vikiwamo hata vitisho vya kuwapo taarifa za ushirikina.
“Hatima ya yote mlinzi pekee ni Mwenyezi Mungu… kama Mungu hajakubali hata waende kwa waganga ama mbinu zote hakuna wa kukudhuru maisha. Katika sakata la EPA nilisema hata risasi inaweza isifanye kazi kama Mungu hajataka. Kwa hiyo na mimi siogopi, kama Nyerere (Baba wa Taifa, Mwalimu Julius) angeogopa tusingepata uhuru maana yeye alikubali kufungwa,” alisema Dk. Slaa.
Raia Mwema limeelezwa kwamba wanaofanya mikakati ya kumshughulikia Dk. Slaa wanahofia kampeni zake zitakapoanza anaweza kutumia baadhi ya nyaraka ambazo zinawahusisha kwenye masuala ya ufisadi mkubwa dhidi ya uchumi wa Taifa.
Mkakati huo unalenga kumpunguzia kasi katika kampeni zake za urais ambazo baadhi ya hoja atakazotumia zitaathiri kampeni za CCM, hususan mgombea urais wa chama hicho, Rais Kikwete, wabunge pamoja na madiwani.
Miongoni mwa watu wanaotajwa kuhusishwa kwenye mkakati huo ni Mwenyekiti wa Chama Cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema na wagombea wengine ambao baadhi wamekwishachukua fomu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwania urais.
Mwishoni mwa wiki, Mrema alifanya mkutano wa hadhara mjini Moshi ambako alimshambulia Dk. Slaa akijaribu kuonyesha kuwa ni mgombea mwenye kasoro za kiuadilifu akiibua kasoro hiyo kwenye mwenendo wake wakati akiwa Padri wa Kanisa Katoliki.
Hata hivyo, makombora hayo ya Mrema yalijibiwa na mgombea mwenzake katika jimbo la Vunjo, Mkurugenzi wa masuala ya Bunge na Halmashauri ndani ya CHADEMA, John Mrema. Mrema pia anatajwa kuwania ubunge Jimbo la Vunjo.
Katika majibu yake, John Mrema alimwelezea Augustine Mrema kuwa ni mmoja wa mapandikizi wa CCM katika kambi ya Upinzani akitoa changamoto mpya kwamba kama anaweza aeleze Watanzania lini alirejesha kadi ya CCM.
Mrema aliingia kambi ya Upinzani akitokea CCM ambako licha ya kuwa Mbunge kwa tiketi ya chama hicho alikuwa pia Waziri wa Mambo ya Ndani. Alijiunga na NCCR-Mageuzi na baadaye kuhamia TLP baada ya kuibuka mgogoro kwenye NCCR-Mageuzi, mgogoro uliohitimishwa kwa vurugu kubwa katika hoteli ya Raskazone mkoani Tanga.
Mgogoro wa NCCR-Mageuzi uliunda kambi mbili moja ikiongozwa na Mrema lakini nyingine ikiongozwa na Mabere Marando, ambaye kwa sasa amejiunga na CHADEMA, akitokea NCCR-Mageuzi.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa kundi la wafanyabiashara wanaohusishwa na kashfa za ufisadi serikalini, limekuwa likijipanga na kupanga baadhi ya vyombo vya habari kumdhibiti Dk. Slaa.
Lakini wakati wakijipanga kudhibiti baadhi ya magazeti wanayohofia si rahisi kutii wanachokitaka, mkakati wa kuhakikisha nyakati fulani magazeti hayo hayawafikii wananchi pia umeanza kufikiriwa.
Dk. Slaa anahofiwa kuharibu mwenendo wa kampeni za wagombea ubunge wenye dosari za ufisadi, pindi atakapokuwa akifanya mikutano ya hadhara kwenye majimbo ya wagombea hao.
Akiwa Mbunge wa Karatu, Dk. Slaa alikuwa kinara wa hoja dhidi ya ufisadi bungeni na hadi anamaliza muda wake wa ubunge alikuwa hajaridhishwa na hatua ya Serikali kutoweka bayana ufisadi uliohusisha baadhi ya wanasiasa wakitumia jina la Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika kampuni ya Meremeta.
Kabla ya Meremeta, Dk. Slaa ndiye aliyeibua sakata la EPA bungeni na amekuwa akisimamia kwa nguvu kubwa matumizi ya fedha katika halmashauri zote akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali na akiwa Naibu Kiongozi wa Upinzani bungeni.
http://www.raiamwema.co.tz/news.php?d=2505
0 comments:
Post a Comment