Wednesday, August 18, 2010

Ndiyo, watu washindane kwa hoja, si vioja

Ndiyo, watu washindane kwa hoja, si vioja

John Bwire
Agosti 18, 2010

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa nchini kutobeba sanamu, kinyago na vitu vingine vinavyoweza kutumika kumkashifu mgombea wa chama pinzani katika kampeni za Urais na Ubunge zilizopangwa kuanza Agosti 20, 2010, nchi nzima.

Mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Rajabu Kiravu amesema vyama vya siasa vinatakiwa kuheshimu maadili ya uchaguzi yaliyotiwa saini na viongozi wa vyama vyote vitakavyoshiriki katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 31, mwaka huu.

NEC imefanya jambo jema kuvikumbusha vyama vya siasa juu ya umuhimu wa kuheshimu maadili ya uchaguzi ili mikutano ya kampeni isigeuzwe kuwa uwanja wa kupigana vijembe visivyostahili.

Pamoja na kuipongeza NEC, tunadhani kuna umuhimu pia kwa vyombo vya usalama na hasa Jeshi la Polisi kuwa makini wakati wa mikutano ya kampeni kuwakamata watu ambao watakwenda kinyume na maagizo ya NEC.

Mambo kama hayo ndiyo yanayohatarisha amani kwa kuleta vurugu wakati wa mikutano ya kampeni hivyo, polisi wakiwa macho watanusuru mikutano mingi ambayo pengine ingemalizika kwa vurugu kutokana na kujitokeza kwa watu wanaokusudia kuendesha kampeni za kashfa.

Sote tu mashahidi wa vituko vilivyopata kufanywa katika chaguzi ndogo mbalimbali za ubunge. Watu walifikia hata hatua ya kuvalisha mbwa bendera za chama pinzani katika kuonyeshana kejeli na kukafishiana.

Ni muhimu mno kwa wagombea, wapambe na mashabiki wa vyama ya siasa kuzingatia maadili wakati wa kampeni. Watambue kwamba kutofautiana kimawazo, kiitikadi na kiushabiki juu ya mgombea si kosa bali ni kukomaa kwa demokrasia tunayojitahidi kuijenga katika nchi yetu.

Watu washindane kwa hoja si kwa vioja katika kushabikia, kushangilia na kukosoana ili hatimaye mbunge atakayechaguliwa awe ni yule ambaye amekubalika na wapiga kura wengi kutokana ushawishi wake wa staha aliouonyesha wakati wa kampeni.

Sote ni lazima tuwajibike si tu katika kuifanya Tanzania yetu mahala salama pa kuishi, bali pia katika kuwapata viongozi wazuri katika mazingira mazuri. Hivyo kila mtu aseme ‘hapana’ kwa kampeni chafu.

http://www.raiamwema.co.tz/news.php?d=2507

0 comments:

Post a Comment