Monday, August 30, 2010

Chagueni watu sio vyama


UMOJA ya Makanisa ya Kikristo mkoani Kilimanjaro, umetoa waraka unaowataka wananchi kuchagua viongozi bora, huku wakisisitiza umuhimu wa kuchagua watu badala ya vyama vilivyowasimamisha.

Waraka huo ni mwongozo wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu na umesainiwa na Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo la Moshi, Isaack Amani, Dk. Martin Shao wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini (KKKT) na Glorius Shoo wa Kanisa la Tanzania Assembies Of God (TAG) .

Waraka huo ambao Tanzania Daima ina nakala yake, ulianza kusambazwa juzi kwenye makanisa yote huku ukiwahimiza waumini wao kuona umuhimu wa kudumisha amani na upendo hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
“Mtu yeyote mwenye sifa ya uongozi achaguliwe bila kuangalia yeye anatoka dini gani au kabila fulani ama sehemu anayotokea ama chama chake,” unasomeka sehemu ya waraka huo.

Maaskofu hao wamewataka wananchi kuepuka vitendo vya rushwa kwa kile walichosema kuwa mbali na kuwa hufunika ukweli na kuwakosesha haki wengine lakini pia ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu.

Aidha viongozi hao wa dini walihimiza jamii kuona umuhimu wa kujitokeza na kuwa waangalifu katika kuweka mawakala waaminifu watakaosimamia zoezi la upigaji na kuhesabu kura ili haki itendeke.

Waraka huo pia unaeleza umuhimu wa wananchi kushiriki mikutano ya kampeni ya wagombea mbalimbali, jambo litakalowawezesha kuwapima na kujua uwezo wao na uchungu walionao katika kuwakomboa kutoka katika umaskini unaowakabili.

0 comments:

Post a Comment