Wednesday, August 18, 2010

Waraka kwa Watanzania

13 Juni 2007
Freeman Aikaeli Mbowe
Mwenyekiti Taifa

LEO napenda kuelekeza waraka na tafakuri yangu kwa Watanzania wote.

Rais wetu ana majukumu mengi na ni busara nimpe nafasi, kwa nia njema, atafakari kama akipenda, yale yote niliyoainisha kwenye tafakuri na nyaraka zangu kwake.

Waraka wangu leo haumlengi yeyote kipekee, bali unakusudia kutoa ufafanuzi wa jambo moja la msingi. Hakika, kama yupo mwenye uelewa zaidi na mwenye kuamini maelezo yangu, leo ni ya kupotosha, ingekuwa busara ajitokeze na aseme, “Mbowe unadanganya.”

Katika waraka wangu namba sita kwa Rais wetu, Jakaya Kikwete, niliouandika kupitia gazeti hili la siku ya Jumatano Mei 9, 2007, niliainisha sehemu tu ya ukubwa wa gharama zinazotokana na safari za rais nchi za nje.

Ukubwa wa gharama zile zimeonekana kushtua baadhi ya watu. Mimi nasema, gharama nilizoainisha ni sehemu tu na wala si gharama kamili zinazotumika kwenye safari hizi. Aidha, muungwana mmoja alinisihi nisome ufafanuzi uliotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati akifunga mkutano wa saba wa Bunge kule Dodoma, Mei 20, mwaka huu, kwani ingeweza kuondoa hofu yangu. Namshukuru sana.

Kwa bahati mbaya hata hivyo, hoja ya muungwana huyu haikuwa majibu rasmi toka serikalini. Mara nyingi nimeomba ufafanuzi wa hofu zinazojengeka, ili pengine tusiwajengee viongozi wetu taswira hasi mbele ya jamii. Wao mara nyingi wamechagua “kula jiwe”. Tutaendelea kuwakumbusha pale inapobidi, kwani ndio wajibu wetu sisi watawaliwa.

Hoja ya muungwana huyu, inaweza vilevile kuwakilisha fikra zilizofichama za viongozi wetu, wasaidizi au wapambe wao. Hata kama hawatasema kwa kauli, ukimya au muendelezo wa vitendo hivyo bila kuonyesha dalili ya kuvijutia, ni kiashiria tosha kuwa fikra za muungwana zaweza kushabihiana na zao.

Tafsiri rahisi ni kuwa, ni vigumu kwa yeyote asiye mbia kwa njia moja au nyingine kudiriki kuushabikia na kuhalalisha ufujaji wa kiwango hiki kwa nchi masikini mithili ya Tanzania.

Pengine kwa faida ya tafakuri ya leo, na uelewa wa wasomaji, ninukuu maneno yaliyokuwa sehemu ya hotuba ya Waziri Mkuu, Edward Lowassa wakati akifunga mkutano wa saba wa Bunge kule Dodoma Aprili 20, 2007 kwa mujibu wa kumbukumbu za Bunge, (hansard). Nanukuu:

“Mheshimiwa Spika,
Katika mkutano huu yametolewa maelezo ndani ya Bunge lako tukufu kuhoji safari za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nje ya nchi. Napenda kutoa ufafanuzi ufuatao wenye lengo la kueleza umuhimu wa ziara za Mheshimiwa Rais nje ya nchi kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika,
Awali ya yote, ningependa kufahamisha waheshimiwa wabunge na wananchi wote kwa ujumla kuwa, ziara anazofanya Mheshimiwa Rais nje ya nchi ni za kikazi na zenye malengo maalum. Matokeo ya ziara hizo yameanza kuonekana yakiwa na faida kubwa kwa nchi yetu. Naomba nitoe mifano michache:

Mwezi Septemba 2006, Mheshimiwa Rais alitembelea nchi ya Marekani. Akiwa nchini Marekani, Mheshimiwa Rais alifanya mazungumzo na Rais wa Marekani na kutokana na mazungumzo hayo, rais wetu ameahidiwa kupata msaada kutoka Millenium Challenge Corporation.

Tanzania itanufaika kwa kupatiwa msaada wa jumla ya fedha ya dola za Kimarekani milioni 800 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maendeleo katika sekta za barabara, maji na nishati.

Msaada huu umeweka rekodi miongoni mwa nchi za Afrika ambapo awali nchi iliyokuwa ikipata fedha nyingi kutoka Marekani ni Ghana ambayo imepata dola za Kimarekani milioni 500.”

Nakubaliana na Waziri Mkuu kuwa, kuna umuhimu wa rais kusafiri nje kwa majukumu yake. Waziri Mkuu angetusaidia zaidi Watanzania kama angetoa maelezo ya ziada kujibu yafuatayo:

Mosi, ni nini hasa gharama halisi za safari za rais na za viongozi wa juu serikalini? Pili, kuna ulazima gani rais kuandamana na msafara mkubwa ilhali nchi yetu ikiomba misaada kila kukicha?

Tatu, kuna ulazima gani wa kusafirisha msafara katika madaraja ya juu ya ndege ilhali safari zenyewe zikiwa za kwenda kuomba misaada?

Nne, kuna sababu gani za msingi kulaza misafara hii katika mahoteli ghali mno wakati serikali yetu ikiwa haina uwezo hata wa kugharamia bajeti yake yenyewe?

Maadam Waziri Mkuu alitoa mfano wa safari hii ya rais kuwa ilituwezesha kupata msaada wa dola za Marekani milioni 800 baada ya mazungumzo na Rais Bush, pengine nieleze taarifa toka vyanzo vingine zinazoonekana kukinzana na ile ya Waziri Mkuu kuhusu hiki kinachoelezewa kuwa matunda ya safari ya rais nchini Marekani mwezi Septemba 2006.

Kati ya mwaka 2002 na 2004, Serikali ya Marekani chini ya utawala wa Rais George W. Bush, uliunda Shirika la Millenium Challenge Cooperation (MCC) kwa lengo la kusimamia mfuko maalum uitwao Millenium Challenge Account (MCA). Vyote hivi vinaratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.

Mfuko huu una kusudi la kusaidia nchi masikini zaidi duniani kujiimarisha kimaendeleo. Tofauti na misaada mingine inayotolewa na wafadhili, vigezo vitatu vikuu vimewekwa na Marekani ili nchi husika ziweze kuingizwa kwenye mpango huu. Vigezo hivyo ni: Utawala wa haki, mipango ya maendeleo yenye kulenga rasilimali watu na sera na mipango ya kiuchumi yenye kuzingatia uhuru wa kiuchumi wenye kulenga kufungua milango ya biashara na uwekezaji.

Mwezi Novemba 2005, chini ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa, Tanzania sambamba na nchi nyingine 22, zilifuzu kufaidika na mfuko huu kwa vigezo vilivyotajwa. Aidha ilikidhi sifa ya msingi ambayo ni umasikini wa kipato kwa watu wake.

Kwa mantiki hii, si kweli kuwa safari ya Rais Kikwete ya mwezi Septemba 2006 ndiyo iliyozaa mpango huu. Katika ziara ya Septemba, rais alikutana na Rais Bush hotelini kwa muda usiozidi dakika 15 na dhahiri haukuwa muda wa kutosha kusalimiana, kupeana taarifa, kuombana misaada na kisha kukubaliana.

Aidha, ni vyema tukajenga utamaduni kama wa wenzetu, ambapo mambo yanayohusu majukumu na mipango ya serikali huwa wazi na kamwe si siri kama inavyolazimishwa katika nchi yetu.

Pamoja na Tanzania kuingizwa kwenye mpango huu, mwaka 2005 wakati Kikwete akiwa katikati ya kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu, Tanzania ilionekana kugubikwa na tatizo kubwa la rushwa jambo lililochukuliwa kuwa ni kikwazo cha msingi katika mipango ya kuleta maendelo endelevu nchini.

Kutokana na udhaifu huu, Tanzania iliruhusiwa kuandaa kwanza mpango maalum wa awali wa kupambana na rushwa chini ya kinachoitwa “threshold program”. Iliahidiwa kupewa dola za Marekani milioni 11.15 chini ya usimamizi wa USAID ili kujenga mfumo wa kukabiliana na rushwa kabla ya kuweza kupata fungu kuu, ambalo tumeahidiwa kama tukikamilisha vigezo na masharti mengine.

Mkataba wa msaada huu wa aibu, ulisainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja kwa niaba ya Tanzania na Pamela White, Mkurugenzi wa USAID Tanzania, Mei 3, 2006, kufuatia kupitishwa rasmi kwa mpango huu wa awali na Bodi ya MCC Januari 27, 2006.

Rais Jakaya Kikwete naye, akiwa ziarani nchini Marekani, Mei 17, 2006 alihudhuria hafla fupi ya kuzindua mradi huu unaoonyesha kuwapo kwa kasoro wa kukabiliana na rushwa nchini kwetu, katika hafla iliyofanyika jijini Washington, Marekani.

Sherehe hiyo vilevile ilihudhuriwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa mfuko huo, balozi John Danilovich, Kaimu Afisa Mtendaji wa USAID, Fredrick Schiek na Katibu wa Hazina ya Marekani, Joln Snow. Balozi wa Marekani nchini Tanzania Michael Retzer na balozi wa Tanzania (wakati huo) nchini Marekani, Andrew Daraja walihudhuria sherehe hiyo.

Nauita mkataba huu wa “threshold program” wa aibu, kwani unathibitisha rushwa yetu, tena ya kujitakia, inavyojulikana kimataifa kuwa ni kigezo kinachokwamisha maendeleo ya nchi yetu. Viongozi wetu wanapodhihakiwa kwa kupewa msaada ili wakasafishe serikali ni aibu kwa taifa na wala si jambo la ujemedari na kujisifia! Ni dhahiri kuwa, serikali yetu haijashindwa kupata dola milioni 11.15 kupambana na rushwa bali tatizo limekuwa kukosekana dhamira.

Katika mkataba huu wa aibu, serikali yetu imeahidi katika kipindi cha miaka miwili hadi ifikapo Juni 30, mwakani, kufanya mambo yafuatayo:

Mosi, kuweka mfumo unaohakikiki manunuzi katika halmashauri zisizopungua 60 nchi nzima.

Pili; kuongeza uwezo wa Takuru kusimamia kesi angalau kati ya 20 mpaka 28 mahakamani katika kila halmashauri.

Tatu; kuongeza uwezo wa vyombo vya habari kuweza kuibua kashfa za rushwa na hivyo kuongeza kesi za asili hiyo kutoka 50 kwa sasa hadi 300.

Nne; kuanzisha na kujenga kitengo cha uchunguzi cha “finance intelligence unit”, kiweze angalau kuchunguza kashfa nzito za fedha zisizo za kawaida; kuweka mpango wa ukaguzi wa angalao idara na wizara zisizopungua 40 za serikali na taarifa hizo kutangazwa kwenye vyombo vya habari.

Serikali yetu bado haijataka kuzungumzia kwa uwazi na kwa kina aibu hii zaidi ya kusema kuwa ni msaada unaolenga kujenga utawala bora!

Sambamba na “threshold program”, Tanzania imeruhusiwa kutengeneza kinachoitwa “country compact proposal”, ambao ni mchanganuo yakinifu unaoeleza ni miradi gani inayokusudiwa kufanywa katika sekta tatu zilizokubaliwa kimsingi kufadhiliwa, ambazo ni miundombinu (dola milioni 387), maji (dola milioni 243) na nishati (dola milioni 131). Utawala wa mradi huu nao umetengewa dola milioni 39; zote jumla zikiwa dola milioni 799.2 za Marekani.

Tangu kusainiwa kwa mkataba wa “threshold program”, yapo masharti mengine kadhaa yameendelea kutolewa na Marekani ili kuwezesha Tanzania kupata msaada huu. Mengine ni ya heri na mengine ni kitanzi kwa wananchi, hasa wale masikini. Zipo hata sheria kadhaa zinatungwa kama sehemu ya masharti haya na wananchi hawaambiwi ukweli wa chimbuko lake.

Baadhi ya sheria zilizoshinikizwa na msaada huu ni ‘Anti Money Laundering Act’ sambamba na uundwaji wa ‘Financial Intelligence Unit’ na sheria mpya za barabara (Roads bill 2007) na sheria ya kuzuia rushwa ya mwaka 2007.

Kadhalika, baadhi ya masharti yanayoambatana na msaada huu, ni pamoja na kuitaka Tanroads kuongeza fungu kwa ajili ya matengenezo ya barabara kuwa asilimia 40 ya bajeti yake.

Masharti mengine ni pamoja na kuwa na mkakati wa taifa wa nishati (National energy stratergy), Tanesco kujiendesha na kujitegemea kifedha, sheria ya umeme kurekebishwa ili kuondoa ukiritimba wa Tanesco, kuongeza bei ya umeme ili Tanesco iweze kujiendesha na kujitegemea na ZECO (Zanzibar Electricity Company) walipe viwango vya kibiashara kwa umeme wanaopata Tanesco.

Mengi ya heri yamefanywa na serikali katika mpango huu. Ni dhahiri mipango kadhaa inayopendekezwa na serikali katika mpango huu inahitaji kupongezwa na kuungwa mkono, kwani pamoja na mambo mengine imeelekezwa zaidi katika maeneo ambayo kwa hakika yanahitaji kufikiriwa kwa kila njia inayowezekana.

Hii ni pamoja na kusudio la ujenzi wa barabara za Tunduru – Songea; Peramiho – Mbamba Bay; Tunduma – Sumbawanga; Manyoni – Itigi – Tabora; Kigoma – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi; Tanga – Horohoro; upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma na Mafia na barabara za Zanzibar vijijini.

Upande wa miradi ya maji, msaada huu unategemewa pamoja na mambo mengine usaidie kuboresha au kuweka mifumo ya maji katika mikoa ya Dar es Salaam, Bukoba, Zanzibar Mjini, miji ya Pemba na Morogoro. Makusudio mengine ni pamoja na Bunda, Bariadi, Same, Misungwi, Tarime, Geita na Zanzibar Vijijini.

Yapo mapendekezo kadhaa ya miradi ya umeme maeneo mbalimbali nchini. Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vya habari, miradi ya nishati ina hofu kubwa ya kufadhiliwa kwa sababu kadhaa zikiwamo; hofu ya uendeshaji wa Tanesco, kukosekana uwazi katika jinsi serikali inavyotoa ruzuku kwenye sekta ya nishati na kukosekana kwa mkakati kitaifa wa nishati.

Pamoja na serikali kuonekana kupata kigugumizi, hasa katika kukabiliana na rushwa, jambo linalozua hofu kwa wafadhili wetu kama kweli serikali ina nia na dhamira thabiti ya kupambana na rushwa, nawajibika kuipongeza serikali kwa jinsi wataalam wake wamejibidisha kwa nguvu kujaribu kutekeleza vigezo kadhaa kuwezesha nchi yetu kupata msaada huu utakaosaidia watu wengi, ukipatikana kwa ukamilifu wake.

Tunaitaka serikali isifanye mzaha hata kidogo kwani rushwa ndiyo hadi sasa inachelewesha utoaji wa kiwango kilichoahidiwa. Serikali nayo isiendelee kutia taifa hili aibu ya kuonekana limejaa wala rushwa kwa wao kufanyia masihara ahadi zake!

WATANZANIA wenzangu, amani iwe kwenu wote.

Nikiwa bado naendelea kupumzisha nyaraka zangu kwa Mheshimiwa Rais, naomba leo nijadili hoja kadhaa zilizoibuliwa na makala ya Prince Bagenda, iliyobeba kichwa cha habari: “Itikadi ya mrengo wa kati si jibu”, iliyochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Mei 9, 2007.

Prince Bagenda ni mwandishi mzoefu na msomi. Naamini bado ni mwanasiasa. Ameandika makala akisema anawatetea Watanzania, tena wale wa kipato cha chini. Ni dhahiri basi, itoshe kusema kuwa kwa sifa hizo, jambo analoibua linahitaji tafakuri ya kina.

Uandishi wa kisomi, ukitumiwa vizuri na kwa nia njema, waweza kuwa wa msaada mkubwa kwa jamii inayohusika.

Aidha, maandishi ya kisomi yanaweza kujengewa hoja yenye kusudio la kulinda masilahi binafsi kwa kuwatumia hao hao wanaodaiwa kutetewa kama daraja.

Maandishi hayo hayo, hata kwa kutokutamkwa bayana, yanaweza kutumiwa kusafisha wanaostahili lawama na hapo hapo kuhukumu wasiostahili.

Naam! Maandishi hayo yanaweza kuvishwa joho la hariri, na kisha yakajenga fikra au wazo ambalo linaweza kuangamiza jamii hiyo hiyo inayodaiwa kutetewa.

Kwa kuisoma katikati ya mistari, sehemu moja ya makala ya Bagenda ilidodosa vitu vingi vyenye kuashiria nia ya kubeza fikra, wajibu na hata visheni ya vyama vya upinzani nchini Tanzania sanjari na viongozi wake.

Mwandishi hata hivyo, aliiwekea makala yake kinga kwa kuandika kuwa hoja anazotoa hazina asili ya “kejeli za kujibizana na waandishi na wanasiasa,” - pamoja na kuwa alikaribisha mjadala wa kitaifa kujadili hoja zake.

Namshukuru Bagenda kwa changamoto zote alizoibua. Kwa msingi huo huo, makala yangu haina nia ya kukejeli dhamira ya mwandishi, kama vile isivyo kuwa na nia ya kusifu na hata kuhoji uelewa wake kuhusu changamoto za kisiasa, kijamii na kiuchumi alizotoa kwa muntaarifu wa dunia ya leo.

Upande wa pili wa makala ya Bagenda, unaibua mambo kadhaa muhimu na ya msingi. Nitashiriki mdahalo huu kwa kujadili hoja hizi za msingi.

Nia yangu ni kujaribu kushiriki kutoa mawazo yangu kwa lengo la kuweka misingi sahihi ya kifikra itakayowezesha Watanzania kuweza kujadili mustakabali wa changamoto za maendeleo nchini, sambamba na mantiki na dhana nzima ya uwepo wa vyama vingi popote duniani.

Bagenda, kwanza, anapendekeza kuwa Tanzania leo iwe na kile anachokiita “itikadi rejea”, akimaanisha itikadi ya ujamaa na kujitegemea ambayo yeye anaiona kama itikadi ya ukombozi dhidi ya mifumo gandamizi ya kibepari.

Pili, anaainisha kuwa leo Tanzania hakuna hata chama kimoja cha siasa chenye programu iliyo wazi ya kutetea na kutekeleza itikadi ya ujamaa na kujitegemea. Anaongeza kuwa CCM wana itikadi hii vitabuni lakini sera zake za serikali zinakinzana na itikadi yake.

Tatu, anapuuza itikadi za kiliberali zenye kukumbatia mifumo ya soko huria na hususan zile za mrengo wa kati katika mizania ya itikadi Tanzania na sehemu nyingine duniani.

Nne, anasema viongozi wa upinzani hawana hoja za kujenga uchumi mbadala wa mfumo tulio nao bali wameelekeza hoja zao kwenye malalamiko juu ya utendaji wa viongozi wa Awamu ya Nne na hoja zao zinaongozwa zaidi na mashambulizi ya lugha kuliko mantiki.

Sasa nijadili. Kwa lugha nyepesi, dhana ya msingi ya kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa katika taifa lolote, ni kutoa uhuru na fursa kwa wananchi wake, kwa ridhaa yao, kuungana na kujiendesha kama kundi lenye madhumuni na malengo ya kisiasa.

Kundi hili, kama chama, linastahili kuwa na uhuru wa kufuata itikadi yoyote wanayoiona inatimiza malengo yao ya kisiasa, kijamii na hata kiuchumi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Tanzania kama taifa, tuliridhia mfumo huu mwaka 1992, na hivyo kufanya marekebisho kadhaa ndani ya katiba na kutunga sheria mpya iliyoainisha masharti na taratibu za kufuata ili chama kiweze kuwa na sifa ya kuitwa chama cha siasa.

Nipende kuainisha hapa kuwa, katiba yetu kama ilivyo leo, inakinzana yenyewe kwa yenyewe. Baadhi ya vifungu vinatoa uhuru wa kuwa na mfumo wa vyama vingi wakati huo huo katiba hiyo hiyo ikilazimisha kufuata siasa ya ujamaa na kujitegemea.

Ni dhahiri kuwa kwa hili, katiba yetu ina upungufu mkubwa ambao ukitafsiriwa kisheria, unatoa uhalali wa kufuta vyama vyote vya siasa ambavyo haviikubali itikadi hii kama msingi wa kuwapo kwake.

Aidha, baadhi ya vifungu vya katiba hii kama vilivyo leo, vinakinzana na sera za serikali ya CCM, kwani baadhi ya sera za serikali hazikidhi matakwa ya katiba. Labda turejee katiba yetu leo inasema nini kuhusu hoja hizi mbili.

Kuhusu vyama vya siasa, katiba yetu sura ya kwanza kifungu cha 3.-(1) inasema: “Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.”

Kwa msingi huu, kifungu hiki cha katiba kinalazimisha vyama vyote kufuata itikadi ya kijamaa.

Katika katiba hiyo hiyo sehemu ya pili inayoainisha malengo muhimu na ya msingi ya mwelekeo wa shughuli za serikali ibara ya 9 na baadhi ya vifungu vidogo inasema:

“Lengo la Katiba hii ni kuwezesha ujenzi wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar au wa chochote kati ya vyombo vyake na udugu na amani kutokana na kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ambayo inasisitiza utekelezaji wa misingi ya kijamaa kwa kuzingatia mazingira yaliyomo katika Jamhuri ya Muungano.

Inaendelea: “ Kwa hiyo, mamlaka ya nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote katika lengo la kuhakikisha –

(b) kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa;

(f) kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu Haki za Binadamu;

(h) kwamba aina zote za dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu au upendeleo zinaondolewa nchini;

(j) kwamba shughuli za uchumi haziendeshwi kwa njia zinazoweza kusababisha ulimbikizaji wa mali au njia kuu za uchumi katika mamlaka ya watu wachache binafsi;

(k) kwamba nchi inatawaliwa kwa kufuata misingi ya demokrasia na ujamaa.”

Naam! Mara kwa mara, umekuwapo utetezi wa kiujanja ujanja wa watawala kuhusu tafsiri halisi ya ujamaa na kujitegemea. Ni dhahiri, tafsiri muhimu kama hii ingestahili kuwa sehemu muhimu ya utangulizi ndani ya katiba.

Kwa kuangalia kwa kina mantiki ya vifungu hivi vya katiba, ni ushahidi ulio wazi kuwa, serikali ambayo inastahili kuendeshwa kwa mujibu wa katiba ambayo ndiyo sheria mama; kwa makusudi ndiye mvunjaji mkuu wa katiba hiyo hiyo, ambayo viongozi wake waliapa kuilinda.

Mara kadhaa nimeandika na kuhutubia kuwa taifa letu linahitaji sana maridhiano ya kitaifa. Hilo halitawezekana kwa kukumbatia itikadi moja, bali litawezekana kwa kwanza kuwa na katiba moja ambayo itaridhiwa na wote bila manung’uniko kama ilivyo leo.

Ni katika katiba ndipo tutakapoweza kuainisha pamoja na mambo mengine, maadili na miiko rasmi ya taifa hili ambayo si tu ibaki kwenye maandishi, bali wananchi wote wakiwemo viongozi waishi kwa ukamilifu wake, na asiwepo yeyote atakayekuwa juu ya sheria. Hapo, tutakuwa tumeweka msingi wa kujenga si taifa na watu wake pekee, bali upendo na amani ya kudumu.

Nikirejea kwenye hoja ya Bagenda, ya kuwa na itikadi moja iliyoridhiwa na vyama vyote, (anayoiita itikadi rejea), si tu kuwa inakinzana na maana halisi ya kuwa na uhuru wa kiitikadi, bali inalirejesha taifa katika mfumo wa chama kimoja.

Katika dunia ya leo, katika nchi yoyote yenye mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, hapajawahi kutokea kulazimisha vyama kufuata itikadi fulani.

Itikadi za kisiasa ziko nyingi na kadiri maisha ya binadamu yanavyobadilika kutokana na misukumo mbalimbali, kunajitokeza vyama vya siasa vinavyowakilisha agenda tofauti tofauti.

Leo ni jambo la kawaida kusikia vyama vinavyotetea sera za mazingira vikishamiri kwenye nchi kadhaa.

Aidha, hakuna ubaya wowote vyama kufanana itikadi ndani ya nchi moja. Mnaweza kuwa na itikadi moja, mkatofautiana katika sera au mifumo ya utawala.

Itikadi ya siasa inakuwa na maana pale ambapo wale wanaoihubiri wanapokuwa kweli wanaitekeleza itikadi yao kisera na kiutendaji, hasa wanapokuwa madarakani. Pungufu ya hili ni utapeli wa kisiasa.

Ni upungufu mkubwa sera na mipango ya serikali iliyopo madarakani inapotofautiana bila kificho na itikadi ya chama tawala, tena katika mazingira ambayo viongozi wakuu wa chama ndio hao hao wa serikali.

Jambo hili mbali na kuwa ni ukiukwaji wa wazi wa katiba yetu ya leo, ni ushuhuda tosha wa jinsi watawala wetu wasivyokuwa wakweli katika fikra na dhamira zao dhidi ya kiapo chao cha utumishi kwa Mungu na umma wa Watanzania.

Vyama vinapokuwa vya upinzani, sera zake hubakia zaidi nadharia hadi pale vinapopata nafasi ya kuongoza dola.

Uwepo wa itikadi nyingi za kisiasa huwa hitaji la muda na mazingira. Hoja kuwa Ujamaa na Kujitegemea ndiyo itikadi anayoiita Bagenda ya “ukombozi” ni hoja tata yenye pia kuhitaji mjadala.

Nchi yetu haijawahi kujitegemea na binafsi sioni juhudi za dhati za kujitegemea kama taifa, bali kuendelea kuwa taifa tegemezi hata kwenye vitu vya aibu kama misaada ya ujenzi wa vyoo kwenye mashule yetu!

Nikubaliane na jambo moja kuwa; kwa nchi masikini kama Tanzania, ni muhimu kuwa na sera za kiuchumi zitakazoweza kusimika mfumo wa uchumi (economic system) ambao utaakisi hali halisi ya umasikini wa wananchi wetu.

Mfumo wa uchumi ninaouzungumzia hapa, unastahili kuweka bayana fursa za ndani na hata za nje za uzalishaji (production) za kuwawezesha na kuwashirikisha wananchi, sambamba na mgawanyo (distribution) wa kile kinachopatikana katika kukidhi mahitaji muhimu ya wananchi.

Sina hakika kama nadharia ya itikadi ya Ujamaa na Kujitegemea bila utashi wa kweli wa watawala inaweza kutoa nchi yetu katika lindi la umasikini unaolielemea.

Si siri kuwa nchi nyingi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, ambazo zilikumbatia itikadi ya ujamaa na hata sasa katika mfumo wa soko huru, matabaka ya watawala na washirika wao ndio wenye kufaidi keki halisi ya taifa ilhali wananchi wengi wakiendelea kuwa maskini wa kutupa. Si siri tena kuwa siasa na vyama tawala vimegeuzwa miradi na vyanzo vya mapato kuliko dhana ya kutumikia umma.

Mfumo wa uchumi ni jambo pana na lina uhusiano wa karibu na itikadi za kisiasa. Katika mifumo mipya ya kisiasa na kiuchumi (contemporary political and economic systems) mbali na itikadi, kuna vigezo kadhaa muhimu vya kuangalia katika kupanga mustakabali wa nchi.

Wanasayansi wa siasa na wanafalsafa wa kizazi kipya kote duniani leo wanajadili kama kweli bado itikadi (ideology) ni dhana ya msingi katika kupanga mustakabali wa nchi yoyote.

Hali hii inasukumwa kwa kiasi kikubwa na kumomonyoka kwa nguzu za ndani za mataifa duniani (nation-state sovereignty) kunakosababishwa pamoja na mambo mengine, mabadiliko makubwa ya mahusiano mapya ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia. (global social, economic and political integration), mashuhuri kama utandawazi (globalization).

Baada ya kuanguka kwa dola ya Urusi katika miaka ya 1980 ambayo ilikuwa kinara wa itikadi za kikomunisti na kijamaa, na hivyo kuashiria mwisho wa vita baridi (cold war), mashindano ya kisiasa (political competition) ya kimataifa sasa yamerithiwa na mashindano ya kiuchumi (economic competition).

Lugha inayotawala dunia leo ni uchumi na demokrasia. Namna kila taifa litakavyoweza kutafsiri fursa zake katika wimbi hili ni changamoto kwa kila nchi.

Hapa ndipo watawala wetu wanastahili kutuaminisha kuwa wanajua wanakotupeleka.

Tanzania si kisiwa. Kwa udhaifu wetu kiuchumi na kiteknolojia hatuna ubavu wa kujitenga na wimbi linalounganisha dunia kupitia mifumo ya kiuchumi (economic globalization) na mpanuko wa technolojia (technological advancement).

Mataifa yaliyoasisi itikadi ya ujamaa, tena yenye nguvu kubwa za kiuchumi, kijeshi, kiteknolojia sambamba na utajiri wa kutisha wa maliasili kama vile Urusi na China, wametambua umuhimu wa uchumi wa soko dhidi ya uchumi hodhi.

Wamekumbatia sera za uchumi zenye kuheshimu uwezo binafsi (individual initiative) dhidi ya mikakati ya pamoja (communal initiative). Kasi yao ya maendeleo sasa ni ya kutisha.

Nchi zilizobaki ving’ang’anizi wa itikadi ya ujamaa ni Korea Kaskazini na Cuba, ambazo hali zao kiuchumi ni mbaya kupindukia.

Ni kweli duniani leo kuna mifumo mingi ya kijamii na kiuchumi inayonyonya nchi masikini zinazoendelea. Hata hivyo ni lazima tukiri kuwa watawala wa nchi nyingi za Afrika sambamba na mifumo yetu ya utawala ni sehemu kuu ya majanga yanayolisibu bara hili na Tanzania hatuna upekee.

Mifumo hii ya unyonyaji wa mataifa yanayoendelea, kwa kiasi kikubwa hupata baraka za watawala wetu pale masilahi yao binafsi yanapotangulizwa mbele kuliko yale ya taifa.

Wote tuna uzoefu jinsi nchi yetu ilivyoporomoka kiuchumi na hata kimaendeleo chini ya mfumo wa kijamaa.

Kinadharia, itikadi hii ni ya kuvutia hasa kwa nchi masikini, ilhali kwa hulka asilia ya binadamu walio wengi iliyojaa ubinafsi, itikadi hii haitekelezeki na muda umedhihirisha hili.

Kama nilivyosema awali, mada hii ni muhimu na ndefu! Niombe radhi kwa kutoimaliza na niahidi akipenda Mwenyezi Mungu nitaendelea wiki ijayo.

Nawashukuru kwa kunisoma.

WATANZANIA wenzangu,

Kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kutupa wengi wetu fursa ya kuonana tena wiki hii kupitia tafakuri yangu. Wako wengi ambao bahati hii hawakuipata na hivyo tuna kila sababu ya kupiga goti kushukuru.

Wiki hii, tafakuri yangu itaendeleza somo nililoanza wiki iliyopita, lililotokana na mjadala wa makala ya mwandishi, msomi na mwanasiasa, Prince Bagenda.

Dhana ya itikadi, vyama vingi na mahusiano yake na mifumo ya kiuchumi na utawala, ni somo pana. Magwiji wa sayansi ya siasa na uchumi wameandika maelfu na maelfu ya vitabu kuhusu somo hili. Hii ni kutokana na ukweli kuwa, sayansi ya siasa ni mada ya kudumu yenye umbo la kubadilika (politics is a game of dynamics).

Neno itikadi (ideology), ni zao la fikra za mwanafalsafa Mfaransa, Antoine Destutt de Tracy, aliyezaliwa mwaka 1754 na kufariki mwaka 1836, katika utafiti na maandiko yake ya “Elements d’Ideologie” wakati wa utawala wa Mfalme Napoleon nchini Ufaransa.

Alikuwa akijaribu kuoanisha mawazo, namna fikra zinavyoweza kuwekwa pamoja kwa njia ya busara na kujengewa utaratibu wa utawala unaoweza kuzaa jamii yenye kuishi kwa utaratibu fulani wa haki na ustawi.

Hii ilifuatia bara la Ulaya kwa karne kadhaa kuwa katika utawala wa ki-imla (anarchy). Mfumo huu uliweka utawala na miliki ya jamii mikononi mwa makundi madogo ya watu kwa misingi ya kidini na hata kifamilia, hali iliyosababisha machafuko na mapigano mara kwa mara katika sehemu nyingi za Ulaya.

Mijadala kuhusu itikadi za kisiasa kwetu Afrika, laweza kuonekana jambo geni. Itikadi zote tunazojaribu kuziishi Afrika leo, sambamba na mifumo yake ya kiuchumi, ni za kuiga.

Iwe ya kiliberali (liberalism) au kijamaa (socialism), ya kikomunisti (communism) au ya kifashisti (fascism), ya kihafidhina (conservatism) au ya ki-utaifa (nationalism).

Kutokana na mahitaji ya wakati na misukumo ya kijamii katika dunia ya sasa, itikadi kadhaa zinazowakilisha makundi ndani ya jamii nazo zimechukua nafasi yake.

Hizi itikadi za “kisasa” (contemporary ideologies) ni pamoja na “jinsia” (feminism) na “mazingira” (ecologism). Itikadi hizi zilizopamba moto kuanzia miaka ya 1970, zimeweza kushika kasi pote duniani na kujipenyeza katikati ya itikadi nyingine.

Itikadi ya “jinsia” kwa mfano, imekuwa ikitetea haki za wanawake, watoto, wazee na makundi mengine yote yanayoonekana “dhaifu” ndani ya jamii. Nafasi ya makundi haya ndani ya siasa za Tanzania leo, ni uthibitisho tosha kuwa itikadi yoyote si umbo la kudumu.

Itikadi zote zimeanza kama fikra na hivyo nadharia (theory) za mtu na si kundi kama Bagenda alivyojaribu kutuaminisha. Fikra hizi hulenga kusudio la mwasisi wake kwa misingi ya jamii ya namna gani anakusudia kuishawishi na kisha kuijenga katika misingi hiyo ya ki-fikra.

Katika historia ya binadamu, siku zote jamii hulishwa na kuaminishwa fikra zilizoibuliwa na mtu mmoja mmoja. Hata kwenye dini, ukweli ndiyo huu. Uenezi wa itikadi nao hutegemea ushawishi wa muasisi kwa jamii anayokusudia kuijenga. Hapa ndipo mahitaji ya jamii yanapojikita na kujisimika katika misingi ya itikadi iliyojengwa.

Itikadi huzaliwa na kwisha kutokana na namna inavyoweza kukidhi matumaini ya jamii husika. Muda umekuwa jibu la kutosha la ni itikadi zipi zimeweza kuhimili misukumo ya mahitaji ya jamii.

Ulazimishaji wa mwendelezo wa itikadi yoyote katika jamii huzaa machafuko, kwani hubaki kuwa hitaji la watawala na si la watawaliwa. Hapa ndiyo dhana ya demokrasia inaposhika mizizi.

Ni kwa misingi hii, leo itikadi kama za kifashisti na kikomunisti zimekufa kifo cha asili bila vita yoyote kupiganwa. Msuguano wa vita baridi kati ya mataifa ya magharibi na mashariki ulikuwa mkali na wenye misingi ya chuki kubwa.

Tafiti za wanazuoni wengi zilihofu kuwa, mvutano huu ungeweza kuzaa vita kuu ya tatu ya dunia. Hili halikutokea na badala yake mabadiliko ya kiasilia (natural evolution) yamechukua mkondo wake.

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia mwaka 1945, dunia ilishuhudia itikadi mbili za ukoministi na ujamaa kwa upande mmoja na uliberali na ubepari kwa upande wa pili zikishika kasi, hususan katika bara la Ulaya, Amerika ya Kaskazini (Marekani na Canada) na Asia.

Afrika, maeneo mengi yalikuwa makoloni ya mataifa ya Ulaya na suala la itikadi halikuwepo kwenye fikra za viongozi wetu wa wakati huo. Kilichotamalaki ni namna ya kupambana na ukoloni na kujitawala.

Ni jambo la msingi kukumbuka kuwa pamoja na maingiliano yote, itikadi zote kuu katika zama zote zina misingi yake. Misingi hii huwekwa na mifumo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Ikiepukwa, haiwezi kuwa yenyewe tena. Hapa ndipo tunapopata uhalali wa kuihoji CCM, serikali yake na Bagenda kuhusu nini haswa wanakusudia wanapodai Tanzania ni nchi ya ujamaa na kujitegemea.

Nifafanue kidogo. Fikra za misingi ya kijamaa kwa kiasi kikubwa zinafanana na zile za kikomunisti. Waasisi wake ni wanafalsafa Wajerumani, Karl Marx (1818 – 1883) na Friedrich Engels (1820 – 1895). Misingi yake ilikusudia kuweka njia zote kuu za uchumi kwenye miliki ya umma chini ya usimamizi wa serikali; si miliki ya serikali kama kwa sehemu kubwa ilivyokuwa hapa kwetu Tanzania.

Ni itikadi inayokumbatia mfumo wa soko hodhi ambapo maamuzi yote ya kiuchumi hayaendeshwi na nguvu za soko bali mapenzi ya walio madarakani.

Kijamii na kisiasa, japo kinadharia, ujamaa ni mfumo unaopaswa kujenga mahusiano ya kijamii yasiyo na matabaka (classless society). Ni mfumo usioamini katika uhuru wa mtu binafsi kupata na kumiliki mali na ukisisitiza mgawanyo wa pato kwa misingi ya usawa.

Upande wa pili, fikra za kiliberali, ziliasisiwa karne ya 16 na kuboreshwa na wanafalsafa kadhaa kama John Locke (1632 – 1704), Immanuel Kant (1724 – 1804), John Stuart Mill (1806 – 1873) na wengineo. Hata hivyo, itikadi hii ilipata msimamo wake wa kiuchumi (uhuru wa soko) toka kwa mwanafalsafa na mchumi kutoka Scotland, Prof. Adam Smith (1723 - 1790).

Ni itikadi ambayo inatoa fursa kwa soko kutawala uchumi, japo haizuii serikali za nchi husika kuweka mikakati yake ya kuhakikisha fursa zinatolewa kwa haki kwa makundi dhaifu ndani ya jamii, ikiwemo huduma za jamii kama elimu, afya, maji, chakula na makazi (welfare states). Aidha, ni mfumo unaosisitiza na kuheshimu uhuru wa kila mtu (individual freedom) katika kupata na kumiliki mali kwa misingi ya halali.

Pamoja na kuwa itikadi kongwe iliyopitia majaribu mengi ya wakati, ni itikadi iliyoendelea kurekebishwa (dynamic transformation) kwa kuzingatia hulka halisi za tabia za mwanadamu na mahitaji ya wakati.

Kisiasa na kijamii, ni mfumo unaoshabikia kikamilifu utekelezwaji wa tamko la dunia la haki za binadamu (Universal Declaration of Human Rights). Tanzania ni mdau wa tamko hili, japo baadhi ya matakwa ya tamko hili hayajazingatiwa katika sheria na Katiba ya Tanzania.

Tamko hili, lenye vifungu 30, lililobuniwa na gwiji la sheria kutoka Canada, Profesa John Peters Humphrey, mwaka 1948 na kisha kuridhiwa na Umoja wa Mataifa, Desemba 10, 1948, linatambua na kuheshimu haki zote za msingi za binadamu.

Itikadi hii ndiyo leo inatawala zaidi ya asilimia 80 kati ya mataifa 197 yaliyo wanachama wa Umoja wa Mataifa, yakiwemo mataifa yaliyoasisi ujamaa.

Ukweli unabakia kuwa, baada ya ushindani wa karne nzima, kutokana na hulka mbalimbali za binadamu na mazingira yake, itikadi ya ujamaa, pamoja na kuonekana kama tamu na safi, imeshindwa kutimiza yale yaliyokusudiwa na waasisi wake. Mfano rahisi ni Tanzania.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ndiye aliyekuwa muasisi wa itikadi hii nchini mwetu. Pamoja na unyofu wa Mwalimu na dhamira nzuri sana aliyokuwa nayo juu ya nchi yake, alijikuta akishindwa kupata mafanikio ya kiuchumi, japo aliweza kwa kiasi kikubwa kupata mafanikio makubwa ya kijamii.

Sasa imedhihirika kuwa, siasa ni uchumi; kwamba uchumi ndiyo nguzo kuu ya utawala wowote. Mipango thabiti ya kijamii ya taifa lolote, haiwezi kusimamiwa na uchumi legelege. Hali hii huzaa utegemezi wa hali ya juu, kama ilivyo kwa nchi yetu leo.

Imedhihirika bila shaka kuwa, watawala wetu leo wameshindwa kuliweka taifa hili kwenye mserereko wa uchumi wenye kutoa matumaini ya kuweza kujitegemea angalau kwa miaka kadhaa ijayo.

Nimalizie hoja kuhusu itikadi kwa kumweleza ndugu yangu Bagenda kuwa, hatuna sababu ya kubeza hali halisi ya dunia. Itikadi zote (iwe ujamaa au uliberali), zimeasisiwa na mataifa ya Ulaya. Changamoto yetu, iwe ni tutumiaje uzoefu wao (empirical experience) na tuijengee mazingira ya kwetu, tujenge dhamira safi tulijenge taifa letu!

Mataifa yao yamedumu katika harakati hizi za fikra kwa karne kadhaa, tangu enzi za wanafalsafa mahiri kama Socrates na Plato waliozaliwa na kuishi miaka zaidi ya 300 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo.

Katika mifumo ya dunia ya leo (New International political order), dhana ya kulazimishwa itikadi imepitwa na wakati. Ni jukumu la kila chama cha siasa kuwa na itikadi yake ambapo raia hupewa fursa ya kuchagua kupitia chaguzi zilizo huru na za haki, ni itikadi na kisha ni sera zipi wanazoona zinakidhi mahitaji yake sambamba na uhalisia wa mazingira yake, kwani kila nchi ina upekee wake (nation-state peculiarity).

Ni dhahiri, makala chache ndani ya gazeti haziwezi kutoa elimu ya kutosha kwa jamii yetu kuweza kupata ufahamu wa kina wa ni nini itikadi, asili yake wapi na tafsiri zake zikoje sambamba na dunia ya leo inakwenda kwa kasi gani!

Tukubaliane jambo moja! Elimu ya uraia itakayojumuisha elimu ya siasa ya itikadi zote (comparative political studies), ni muhimu sana katika nchi yetu. Lazima tufike mahali tutoe elimu hii kuanzia hatua za kwanza kabisa za elimu ya watoto wetu, ili tujenge taifa lenye kujielewa na wakati huo huo lenye kuelewa nchi nyingine zinaishi vipi, na hivyo changamoto inayolikabili.

Miaka kadhaa iliyopita, Watanzania tulifundishana siasa ya upande mmoja. Kila mtu alifundishwa mazuri ya ujamaa sanjari na utukufu wake na madhila ya itikadi nyingine sanjari na “unyama” wake. Hizi zilikuwa, kinachoitwa kwenye siasa, propaganda ambapo fikra za upande mmoja hupandikizwa kwa kila fursa ipatikanayo (indoctrination).

Leo sehemu kubwa ya kizazi chetu imechanganyikiwa. Wanajiuliza bila majibu kutoka kwa watawala: Iweje itikadi tuliyoaminishwa kuwa ndiyo sahihi, leo tunaikana kisiri siri? Iweje wale wote tuliowabeza na kuwatukana leo ndio kimbilio letu?

Naam, Bagenda analalamika kuwa vyama vya upinzani leo vimejikita katika kukosoa utendaji wa serikali ya awamu ya nne, tena kwa lugha ambayo yeye haipendi. Huko nyuma tulikuwa naye wakati tukikosoa utawala wa awamu ya pili na tatu! Sijui mwenzetu kimemkumba nini ghafla! Mbona CCM ni ile ile na watu wake ni wale wale, tena sasa ikiwa na mtandao hatari zaidi?

Kumbe vyama vya siasa baada ya uchaguzi vifanye nini? Mbona huu ni utaratibu wa kawaida dunia nzima? Nina hakika Bagenda anajua wajibu wa vyama vya siasa visivyo madarakani, ni pamoja na kuwa “watch-dog” wa serikali iliyoko madarakani katika kuhakikisha “checks and balances”.

Pengine Bagenda angetusaidia zaidi kama angetushauri kuwa jukumu hili litekelezwe vipi.

Taifa hili chini ya Mwalimu, lilijengwa likajiamini sana kwani kiongozi wetu naye alijiamini. Alisimamia kile alichokiamini, potelea mbali kama ni sahihi au hapana. Alitenda alichohubiri na alihubiri alichoamini!

Taifa halizuki. Hujengwa na viongozi. Viongozi wenye inda, waso-kauli, waso-misimamo, waso-dhamira ya kweli na waso-fikra huru, nao hujenga taifa legelege, tegemezi na lenye hofu.

Ghafla leo, kujiamini kwa Tanzania kumekwisha! Utawala wetu si kisima cha fikra tena, bali ni kisima cha kumeza fikra za wengine. Uimara wa taifa huonekana kwa ulinganisho na nchi nyingine. Tunaweza kujidai ndani ya mipaka yetu, lakini tukipambanishwa na nchi nyingine tunanyong’onyea kwa woga na hofu!

Mfano rahisi, angalia jinsi tulivyokumbwa na hofu ya Shirikisho la Afrika Mashariki. Sasa hatuogopi tena mataifa makubwa, bali tunaogopa mataifa madogo madogo, tena majirani zetu. Bila aibu, tunajifungia ndani ya sanduku. Tunahofia Kenya, Uganda na hata Burundi na Rwanda! Hapa ndipo tulipofikishwa na CCM.

Vyama vingi ni fursa ya kuwepo utajiri wa fikra. Bagenda anapaswa kufahamu kuwa, mazingira ya Tanzania hayatoi fursa ya utajiri huu wa fikra kulijenga taifa kama inavyostahili kutokana na mikakati ya makusudi ya ukandamizaji na unyongaji wa wazi wa demokrasia inayofanywa na serikali.

Ni fursa tunayoshindwa kuitumia na badala yake imegeuzwa chimbuko la chuki ya watawala na washirika wao dhidi ya viongozi na wanachama wa vyama vya siasa.

Huko nyuma, niliwahi kuandika sana kuhusu fursa na athari za mfumo wa siasa ya vyama vyingi. Ni mfumo mzuri ambao ukiwekewa misingi mibaya, unaweza kuwa wa maafa makubwa kwa nchi na watu wake.

Maafa ya mfumo huu hutokea pale ambapo waliopo kwenye madaraka ni viongozi dhaifu, wenye madhambi na hivyo waoga wa kuondolewa kwenye utawala. Hofu ya kupoteza madaraka hutamalaki.

Hali hii ikishajengeka, watawala hujiona salama zaidi ndani ya chama chao. Hutumia vibaya mamlaka ya serikali kujijengea uzio utakaofunika maovu yao. Hutumia fursa hii ya tofauti za kisiasa baina ya vyama kuhalalisha misingi ya kujenga chuki za kiitikadi, ambazo humomonyoa umoja wa kitaifa.

Muda si mrefu, chuki hii husambaa na kuwa chuki taasisi, yaani chuki iliyojisimika katika ngazi zote za uongozi wa kisiasa na kushuka kuanzia taifa hadi kwenye kaya.

Kumepandikizwa chuki za kushangaza na kutisha katika nchi hii. Chuki hizi si rahisi kuziona katika mazingira ya kawaida, kwani taifa letu limejengwa na linaendeshwa katika misingi ya kinafiki na hofu. Bagenda anajua kuwa kukabiliana nazo tu, ni jambo lisilo masihara.

Inahitaji watu wenye busara, fikra pana na subira kweli kweli kusimamia jitihada za kusimika mfumo wa vyama vingi ndani ya jamii yoyote. Tanzania ni mwathirika mkubwa wa mfumo wa vyama vingi. Madhara yake kwa nchi hii ni makubwa na mapana sana. Inahitaji ujasiri kutanabaisha madhara yake.

Viongozi makini wanapokuwa madarakani, huelekeza nguvu kubwa katika ujenzi wa taifa na si chama cha siasa. Hutoa nafasi kwa vyama vyote kukua, kwani huongozwa na matamanio ya ujenzi wa taifa lote, vikiwemo vyama vya upinzani.

Waliotutangulia katika ujenzi wa demokrasia ya vyama vingi, waliliona hili na kujiwekea utaratibu wa kutenganisha utendaji wa serikali na ule wa chama tawala. Sisi tunakazana kuunganisha!

Taifa letu liko njia panda. Linahitaji maamuzi magumu sana. Tunaweza tukaendelea kudanganyana, kupongezana, kusifiana, kuchekeana na hata kuoneana haya, lakini tujue kwa kuendeleza hulka hizi, tunakaribisha maangamizi ya taifa letu, na si ya Mbowe, Lipumba, Mbatia au Mrema!

Nawashukuru kwa kunisoma!

WATANZANIA wenzangu, naendelea kumshukuru na kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika kila hatua ya maisha yetu, kwani bila yeye ndani ya “mji”, wote waulindao wafanya kazi bure.

Wiki iliyopita, nilimalizia tafakuri yangu kwa kusema, taifa letu liko njia panda. Maamuzi magumu sana yanastahili kufanywa kama kweli tunakusudia kuukubali ukweli wa mazingira ya dunia ya leo, ilhali, taifa likikubali kwa dhati na kwa dhamira kuwa sasa njia pekee kwenda mbele ni kwanza kubalisha fikra zetu na mazoea yetu.

Ndiyo, viongozi wa vyama vya siasa wote, wanaotawala na wasiotawala, wana kila sababu ya kubeba lawama kwa taifa letu kukwama na kukosa mwelekeo. Kila mwananchi ni mbia katika lawama hizi. Kila Mtanzania, kwa nafasi yake ana mchango kwa njia moja au nyingine kwa hali yetu kuwa hoi kama ilivyo leo, pamoja na kuwa tumepishana kwa viwango – lawama zaidi zikistahili kuelekezwa kwa wenye dhamana ya kutuonyesha njia.

Aidha, kila Mtanzania, bila kujali chama chake cha siasa, dini yake, jinsia, rangi, kabila na hata uwezo wake kiuchumi, ana uwezo wa kuwa wakala wa mabadiliko ya kwenda kwenye neema tunayostahili. Kila mmoja wetu ajiulize, kaifanyia nini nchi hii, hatua ya kwanza ikiwa ni kufikiri amewasaidiaje au amewalemaza vipi walioko madarakani kutekeleza wajibu wao?

Watanzania wenzangu, hakuna njia ya mkato. Maisha bora kwa kila Mtanzania yatabakia ndoto na vibwagizo vya uchaguzi kama wote kama taifa hatutaona tuna wajibu wa kujiondoa katika umasikini uliopo kuanzia kwenye kaya zetu.

Kwa wenye mamlaka ya juu, hatua ya kwanza ni kupata muafaka wa kitaifa, kisha kwa pamoja tukubali kusota juani ili tuchumie kivulini. Hii ndiyo changamoto kubwa inayomkabili Rais Kikwete na serikali yake, kwani wao ndiyo wenye dhamana ya kuongoza vita hii.

Kila siku tunatumia neno vita kama msamiati wa kudumu na wa masihara huku tukicheka! Vita dhidi ya umasikini! Vita dhidi ya rushwa! Vita dhidi ya dawa za kulevya! Vita dhidi ya ukimwi n.k. Vita haipiganwi milele. Huwa ni mkakati wa muda mfupi wenye kusudio la kuleta matokeo ya haraka.

Sasa naona msamiati unabadilishwa na kuwa “vita hii ni ya kudumu”. Hii ni ishara ya kukata tamaa na kutojua tuendako kama taifa. Huku ni kuwapa adui nafasi ya kudumu kunakoweza kutafsiriwa kama watawala kukosa dhamira, malengo mahsusi na mwelekeo na wengine wote kama taifa kubweteka kwa kudhani kweli kuna juhudi za dhati.

Kutangaza vita dhidi ya jambo lolote ni kutangaza mapambano na mapambano ni maumivu. Vita, kwa maana yeyote ile ni hali ya kutumia nguvu dhidi ya adui na penye matumizi ya nguvu siku zote kubembelezana hakupo!

Taifa letu leo limegeuka popo. Kwamba, taifa lolote linapokuwa na watawala wasioweza kusema bayana ni mfumo gani wa taifa wanakusudia kuujenga, na kisha wakaongoza azma hiyo, si kwa kauli na maandiko pekee, bali kwa vitendo, ni ishara ya taifa popo.

Katika makala zilizopita, nilieleza kinagaubaga kuwa msingi wa itikadi yoyote hatma yake ni jinsi inavyojielekeza kwenye mfumo wa uchumi na mahusiano ya kijamii.

Si dhambi kwa chama chochote kubadilisha itikadi yake. CCM ina haki hiyo. Kinachogomba ni usiri na ubabaishaji unaoandamana na azma hiyo. Hapa ndipo dhana ya upopo inapotamalaki.

Kama CCM imeona mapungufu katika mfumo wa kijamaa ilivyoshindwa kuujenga, isione haya, ikiri, itoke hadharani iliambie taifa. Haya ndiyo maamuzi magumu tunayostahili kuyakabili bila woga wala kuchekeana. Pungufu ya hili ni kuwa na utawala wa ghiliba, unaodanganya raia wake na unaokosa uhalali (legitimacy) wa kuongoza.

Nchi yetu leo inaelekea kuzama kwa kasi katika kinachoitwa katika siasa “itikadi ya sifa” (Populist Ideology). Chini ya itikadi hii, msingi mkuu wa ujenzi wa taifa huwa matakwa na kauli tamu (rhetorics) za kiongozi mkuu na wasaidizi wake wa karibu na kamwe si mifumo ya utawala iliyopo kwa misingi ya sera. Katika hali hii, umashuhuri wa kiongozi huonekana kama sifa ya taifa.

Itikadi hii isiyo rasmi, huibuliwa na kundi la tabaka la kati (middle class) linalowakilisha maslahi ya wafanyabiashara na watu wenye nafasi zaidi katika jamii, hasa wale wanaoishi katika maeneo ya miji (urban elites). Hawa hutumia nyenzo kadhaa, haramu na halali kujihalalishia nafasi za utawala kwa lengo kuu la kugeuza utawala chanzo chao cha sifa, utajiri na mamlaka.

Kundi hili hujisimika ndani ya chama cha siasa kinachotawala kupitia mtandao usio rasmi. Huu ndiyo mtandao tunaoshuhudia nchini mwetu leo. Hugeuza chama cha siasa kama chombo cha uchaguzi (electoral machinery) na hutegemea sana haiba binafsi ya kiongozi mkuu (personal charisma).

Ni rahisi kwa viongozi katika mazingira haya kulewa sifa zitokanazo na umashuhuri wao. Nao kwa upande wa pili huendeleza mfumo huu kwa kukumbatia kwa kiasi kikubwa yale mambo mepesi mepesi yenye kusudio la muda mfupi la kuongeza umashuhuri wao na washirika wao.

Taratibu kundi hili hujenga mikakati ya kunyonga demokrasia kwa kudhibiti fursa zote huku likijijengea uhalali wa kutawala kwa kukita mipango yote ya utawala kwenye malengo ya muda mfupi yaliyojikita katika chaguzi (electoral politics). Mipaka na mipango mingi ya utawala wa aina hii hulenga ushindi kwenye uchaguzi unaofuata na ni nadra kwa utawala wa aina hii kufikiria mipango ya muda mrefu nje ya kipindi cha utawala wao.

Kwa nia ya kutokutaka lawama, viongozi hufumbia macho usimamizi wa sheria na taratibu (law and order) huku wakiacha mambo yaserereke yenyewe. Hawako tayari kukiri na kuusimamia ukweli, kwani azma ya kudumu madarakani kwa wanamtandao ndiyo kielekezi cha utendaji wao wa kila siku. Hawako tayari kuchukua waziwazi “risk” ya kubadilisha mfumo na huachia mambo yajichukulie mkondo wake yenyewe.

Kauli nyingi za Rais Jakaya Kikwete kila akipata fursa, ni kuwakumbusha wana CCM wenzake kuhusu lengo lao la kushinda uchaguzi ujao – kwa udi na uvumba. Katika hali hii, agenda kuu ya utawala inakuwa ni kuwa madarakani kuliko kujenga taifa.

Ni rahisi wengine kusema Mbowe anamhukumu Rais na wenzake. Wengine wanaona makala zangu ni hasira za kushindwa uchaguzi. Ni haki yao. Aidha, yaweza kuwa ni wajibu na kazi yao kujenga taswira hiyo. Vyovyote watakavyosema, tayari nimeanza wajibu wangu wa kuwasaidia viongozi wetu.

Mpango wa kinachoitwa “Mabilioni ya Kikwete” kama mkakati wa kuondoa umasikini na mipango ya kuileta timu ya Real Madrid kama mkakati wa kuendeleza michezo na sifa za taifa, ni baadhi tu ya mipango isiyo endelevu inayoweza kughilibu raia na wakakosa kujikita katika mambo ya msingi yenye “serious impact” kwenye maisha na nchi yao.

Leo ni jambo la kawaida kusikia vilio vya wananchi: Kikwete tukomboe, Lowassa tusaidie. Ukweli ni kuwa tunawachosha viongozi wetu hawa. Wajibu wao si kusimamia kila kitu, bali kusimamia vyombo vilivyo chini yao kutekeleza majukumu yao. Hata hivyo, kinachowaponza ni azma yao ya kujijenga “kibinafsi” (personal institutionalization) badala ya kujenga mfumo mzima (system institutionalization).

Baadhi ya vyombo vya habari navyo kwa kujua au kutokujua, vinaendeleza utamaduni huu kwa kuona kuwa rais, makamu wa rais na waziri mkuu hawastahili lawama yoyote pale panapotokea udhaifu ndani ya serikali yao. Lawama nyingi zimekuwa kimkakati zinaelekezwa kwa mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na watendaji wengine wa chini.

Hata hivyo, huwamiminia sifa viongozi hawa pale jema lolote linapotokea ndani ya nchi hata kama jema lenyewe limesabababishwa na chanzo kingine chochote nje ya serikali. Hali hii husababisha “kuwinda” ni nini cha kusema au kuwaeleza wananchi ambacho watasikia raha na hatimaye sifa za viongozi kuongezeka!

Mengi yanafanywa na serikali yetu leo, hususan katika kuimarisha huduma za jamii. Pamoja na huduma hizi kuwa muhimu, ni ukweli usiopingika kuwa, huu ni msukumo wa matumizi (consumption economy) ambao hauwezi kuwa endelevu (sustainable) kama kipaumbele chetu, kama taifa, hakitaelekezwa kwenye mikakati sahihi ya kuongeza pato la taifa kwa njia za uzalishaji na huduma (production and service economy).

Katika kufikia azma hii, ni vyema viongozi wetu wawe na uwezo wa kufikiria mbali zaidi ya uchaguzi. Uchaguzi ukiwa ndicho kigezo cha mipango yetu ya uchumi, karne ijayo itatukuta hapa hapa. Viongozi wetu wana woga usio sababu. Lazima wajipe ujasiri wa kuwa tayari kutawala hata kipindi kimoja, ili kuweza kufanya maamuzi magumu ya kulikwamua taifa hili.

Kinachohitajika ni kuthubutu. Tukitaka kwenda peponi, ni lazima tukubali kukabiliana na kifo. Ndiyo ukweli wenyewe. Matamanio ya maisha bora kwa kila Mtanzania, lazima yaandamane na viongozi wetu kukusanya kila nguvu ya taifa hili (ya akili na ya msuli) na kuitumia kwa azma hii bila kuoneana haya.

Katika makala zilizotangulia, nilisema uimara wa taifa lolote ni uimara wa uchumi wake. Uchumi wetu ni dhaifu ajabu na unategemea misaada toka nje kwa kiasi kikubwa. Leo hatuna jeuri ya kuwakatalia “wafadhili wetu” kwa chochote kwani hatuna ubavu wa kujitegemea.

Tafsiri yake ni kuwa, hatuna ubavu wa kujitawala. Cha kutisha zaidi, mbali na kauli za hapa na pale, sioni mkakati wowote wa makusudi wa kujitoa kwenye utegemezi huu kwa kushona suti yetu kwa kitambaa tulicho nacho.

Mara nyingi imenishangaza kuona kipimo cha ukuaji wa uchumi wetu kikipimwa na kuongezeka kwa mapato ya serikali kupitia kodi! Kila makusanyo yakiongezeka, serikali inajipongeza!

Nieleweke hapa! Maongezeko ya makusanyo ya kodi yanaweza yakatokana na kupanuka kwa uchumi wa taifa (economic base). Hata hivyo, maongezeko ya makusanyo yasiyoshabihiana na pato halisi la wananchi, ni ushuhuda wa kutosha kuwa umasikini unaongezeka ndani ya taifa. Wataalam wa uchumi wanasema hakuna kodi ndogo kwa mtu masikini. Kila kodi kwao ni mzigo.

Suala moja hapa ni wazi. Kwa uchumi kama wa kwetu ambao ni wa ndani (inward or import based economy) kuliko wa nje (outward or export based economy), makusanyo ya pato kubwa la taifa hutokana na kodi wanayolipa walaji wa ndani ya nchi (consumer based tax). Cha kusikitisha, wananchi wetu walio wengi hawajui kama wanalipa kodi.

Kampuni za simu, sigara, bia n.k zinaweza kuonekana zinalipa kodi kubwa kwa serikali. Ni sahihi, lakini kinachostahili kujulikana ni kuwa, kodi hii uhamishiwa kwa walaji na mwisho wa siku kampuni hizi kubwa (ambazo nyingi husamehewa kodi wanazostahili kulipa) hubakia kuwa mawakala wa kukusanya kodi (collection conduits) toka kwa watumiaji wa huduma au bidhaa zao, ambao wengi wao ni wananchi masikini.

Wakati hatuwezi kujitenga na mifumo na misukumo ya kimataifa, ni ukweli usiopingika kuwa, kila taifa lina wajibu wa kutambua nafasi yake katika jamii ya kimataifa na kisha kujiwekea mikakati yake ya kukabiliana na changamoto zake katika azma yake ya kufikia malengo yake.

Maendeleo kwa taifa ni jambo lenye sura mbili. Uimara wa uchumi unaofaidisha raia wake. Takwimu za kukua kwa uchumi bila vigezo vya kuboreka kwa maisha ya raia kamwe hakuwezi kuakisi maisha bora.

Ningependa kuhitimisha mchango wangu katika mjadala huu wa itikadi kwa kuzungumzia mtazamo mpya wa kiitikadi (contemporary thinking) wa “The Third Way”, ambao kimsingi unashabihiana na itikadi ya mrengo wa kati, ambao ninaamini ni suluhisho la ujenzi wa mfumo wa kiuchumi na kijamii unaojali na kutoa fursa kwa watu wote. Mtazamo huu ni mgeni hivyo kwa wale wataalam wetu wa enzi za Kivukoni wanaweza kuwa hawakuipitia enzi zao.

Ni dhahiri kila itikadi ina uzuri na ubaya wake. Ujamaa una sifa kubwa ya utu, kwamba kinadharia, ni mfumo unaojali watu wa tabaka la chini. Upande wa pili, uliberali una sifa kubwa ya mfumo wenye kuwezesha uchumi endelevu.

“The Third Way” ni mtazamo unaochukua yale yote mema ndani ya ujamaa na kuyaunganisha na yale yote mema ndani ya uliberali, huku ukikubali changamoto za mabadiliko ya kiuchumi na kiteknolojia.

Kwa mujibu wa Antony Giddens, mwanafalsafa wa kizazi kipya anayepigia sana chapuo mawazo haya, kupitia kitabu chake cha ‘The Global Third Way Debate’, anaainisha sifa kuu nne zinazostahili kuunda taifa la kisasa.

Kwanza, ni kukubali ukweli kuwa dunia sasa imeunganika kimfumo (interdependence) na hivyo kuwa na ulazima wa kujenga mifumo ya ushirikiano wa kimataifa ya kuwezesha kufanya kazi na kusaidiana pamoja.

Sifa ya pili ni uwajibikaji (responsibility). Kwamba kila mtu anastahili kupata haki zake za kijamii, lakini wakati huo huo akitambua haki hizo zinastahili kwenda sambamba na yeye kutimiza wajibu wake kwa jamii.

Sifa ya tatu ni fursa ya ushawishi (opportunity based incentives). Kwamba kutokana na mabadiliko ya kasi ya jamii, kila mtu ndani ya jamii anastahili kupewa fursa zilizopo zikiambatana na ushawishi unaoweza kusaidia watu kujiendeleza. Fursa hizi ni pamoja na elimu, afya nk.

Sifa ya mwisho, ni mamlaka kwa jamii (devolution). Kwamba enzi za serikali kujiamulia itakavyo zimekwisha. Jamii, kwa misingi ya kidemokrasia, zina haki ya kushirikishwa katika kuendeleza taifa lao.

Mawazo haya yanatambua na kuheshimu ukweli kuwa, uchumi imara ndiyo hujenga jamii imara na kuwa kwa hulka ya binadamu, matakwa ya pamoja (collective interests) hujengwa kupitia yale mambo yote ambayo binadamu wote wanayahitaji.

Taifa letu sasa linatakiwa litoke katika ndoto na likabiliane na changamoto za dunia. Zama za kubweteka na kujisifu kuwa maliasili nyingi tunazo zimepitwa na wakati. Mchango wa malighafi katika uchumi wote wa dunia (global economy) ni pungufu ya asilimia 20!

Mifumo mipya ya uchumi wa dunia inajikita kwa kasi katika uchumi wa huduma na teknolojia (service and information age economy). Mataifa yasiyo na maliasili kama Singapore na Hong Kong yameweza kutumia fursa hizi. Hata mataifa yaliyoendelea nayo sasa yanajielekeza kwenye sekta hizi za uchumi. Siri yake ni moja tu: ELIMU ELIMU ELIMU!

Tunahitaji kupaa na si kutembea au kukimbia. Wakati ilichukua mataifa ya Magharibi karne vizazi (generation) zaidi ya 10 kusimika mapinduzi ya viwanda (industrial revolution), dunia ya leo imeshuhudia mapinduzi ya teknolojia ya habari (information age revolution) ikijisimika na kutawala uchumi wa dunia katika kizazi kimoja.

Viongozi wetu wasipofanya maamuzi magumu leo na kupandikiza fikra na mikakati mipya ya kupambana katika dunia ya leo, hakika tutaendelea kulalamika na tutakaposhtuka, tutakuwa kwenye dunia yetu wenyewe!

Haya ndiyo maamuzi magumu, Kikwete na wenzake wanastahili kufikiria na si namna ya kugawa kadi za CCM na “vijembe”.

Nawashukuru kwa kunisoma!

Tuonane kwenye bajeti!

0 comments:

Post a Comment