zilizojitokeza kutokana na ‘Hoja yangu ya Kuundwa kwa Kamati Teule ya
Bunge’, kuchunguza matumizi mabaya fedha za umma, uwezekano wa uwepo wa
ubadhirifu, uwizi na ufisadi mkubwa ndani ya BOT ambacho ni kioo cha
uchumi wa nchi yetu, kama ilivyo kwa Benki kuu yeyote duniani. Katika
Mkutano wa Hadhara uliofanyika Jangani tarehe 18 August, 2007 nilitoa
hadi tarehe 15 Septemba kwa Serikali kuchukua hatua mahususi dhidi ya
wahusika. Nilitoa tarehe hiyo makusudi. Leo nina nia ya kutoa ufafanuzi
wa kina zaidi, katika maeneo machache tu katika Tuhuma hizo ili
Watanzania walio wengi waelewe hasa ni nini kilichonisababisha kudai
kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge.
1. Utangulizi:
Kwa kifupi nilitoa Tuhuma nzito dhidi ya BOT na watendaji wake wakuu
ndani ya Bunge letu Tukufu, tarehe 25 June, 2007 wakati wa mjadala wa
Hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu. Jioni hiyo hiyo, wakati wa mafungu kwa
mujibu wa Kanuni ya Bunge ya 104(1)(2) nikatoa Taarifa ya nia yangu ya
kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge.
Tarehe 26 June, 2007 kwa mujibu wa Kanuni hiyo nikawasilisha kwa Katibu
wa Bunge Barua yangu ya Taarifa ya nia hiyo kwa mujibu wa Matakwa ya
Kifungu cha 104(2) ya Kanuni iliyotajwa. Tarehe 8 Julai, baada ya
utafiti wa kina, nikawasilisha kwa Katibu wa Bunge ‘Maelezo yangu ya
Hoja ya Kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge’. Tarehe 13 August, 2007,
mchana nikapokea Barua kutoka kwa Mhe. Spika, yenye Kumb.na
CA.150/277/01/07 ikinitaka niwasilishe ‘vielelezo halisi’ ili yeye
‘akiridhika’ apange muda wa Hoja yangu kuingia Bungeni. Jioni hiyo hiyo
ya tarehe 13 Agosti, 2007 nikawasilisha kwa barua rasmi vielelezo vyote,
vikiwa katika Volumes (lV). Barua yangu iliorodhesha Vielelezo (a) to
(s).
Tarehe 15 Asubuhi, raia mwema, kutoka Usalama wa Taifa, akaniletea
waraka wa kuaminika kuaminika kutoka ndani ya Idara hiyo. Ushauri
uliotolewa baada ya kuchambua mambo mbalimbali unasomeka ifuatavyo:- “
Taarifa ya ukaguzi wa mahesabu ya benki Kuu ilipaswa kuwa siri na
haijulikani ni vipi imeweza kuvuja na kuwafikia wapinzani. Suala hili
likifikishwa bungeni linaweza kuwa na athari mbaya kwa serikali, hasa
kwa kuzingatia kuwa ni vigumu kupata majibu ya hoja hizi za CAG
yanayotosheleza. Ni vema Waziri Mkuu ajulishwe ili itafutwe njia ya
kuzuia hoja hii kuwasilishwa Bungeni. Idara inaendelea kuchunguza chanzo
cha uvujaji wa taarifa hiyo”
Nilitafakari sana hoja hii. Katika akili ya kawaida, ilionenakana
taarifa hii ni ya kweli. Mazingira yaliyojitokeza tarehe 13 Agosti,
ambapo Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM, ikiwa ni wajumbe wote wa
Kamati Kuu ya CCM walioko Bungeni, akiwemo na Spika ilikaa toka saa 5
hadi saa nane kwenye ukumbi wa Spika. Taarifa inayoaminika inasema kuwa
ajenda kuu ilikuwa hoja ya Mhe. Zitto Kabwe, na Hoja ya Dr. Slaa, zote
zikitaka kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge. Kuhusu Hoja yangu
“Maelekezo” mawili inaelekea yaliyotolewa na kikao hicho. Moja ni Spika
kuniandikia na kudai apetiwe ‘vielelezo Halisi’ ili ajiridhishe yeye
kabla ya hoja kuingia Bungeni, na pili, Hoja hiyo isipangiwe katika
Shughuli za Bunge (Order Paper) katika Mkutano huu yaani Mkutano wa Nane
wa Bunge. Hapo nikajiridhisha kuwa ushauri aliopelekewa Waziri Mkuu ndio
unatekelezwa. Na hivyo, nikajua kuwa i)Hoja haitaingizwa Bungeni safari
hii, ina inawezekana isipangiwe kabisa hata kikao kijacho,
ii) Ucheleweshaji wowote, unaweza kuathiri uchunguzi unaotakiwa, kwani
katika Tuhuma yeyote, hatua za haraka ni muhimu ili kusiwe na nafasi
yeyote ya kuingilia uchunguzi.
Kwa vile tuhuma ni nyingi sana, kwa leo naomba niwape mwanga kwenye
maeneo machache tu kama ifuatavyo:
2: TUHUMA ZA MSINGI ZA UBADHIRIFU NDANI YA BOT:
1: BENKI KUU KULIPA DENI LA MERREMETA CO.LTD LA TSHS Bilioni 155 KINYUME
NA
UTARATIBU:
Hapa kuna mambo ya msingi kadhaa Watanzania wanatakiwa kufahamishwa.
Kwa muda wa kama miaka mine sasa Wabunge wa Kambi ya Upinzani tumeihoji
Serikali itueleze
a) Meremeta Co.Ltd. ni mali ya nani na imeandikishwa wapi?
b) Mahesabu ya Kampuni hii yanatolewa kwanani
c) Tanzania inafaidika nini kutokana na Kampuni hii ambayo ilikabidhiwa
Mgodi wa dhahabu wa Buhemba, Mkoani Mara.
Miaka yote, pamoja na kuhoji Serikali ilishindwa kutoa majibu ya
kuridhisha, licha ya kusema tu Meremeta ni Kampuni ya Serikali, na
inaendeshwa na JWTZ, kwa lengo la kuisaidia kikosi chetu cha NYUMBU.
Majibu haya yako kwenye Hansard. Maswali mengine yote hayakujibiwa.
Mwaka jana, baada ya kuibana Serikali ilikiri kuwa Kampuni hii iko
kwenye hatua ya ‘Kufilisiwa’(Liquidation”) Majibu haya ya Serikali
yalileta mashaka makubwa sana. Ndipo ilipokuja nia ya kuundwa kwa Kamati
Teule kupata ukweli na majibu sahihi ya masuali hayo. Sasa basi Utafiti
wangu umeonyesha nini:
a) Meremeta Co.Ltd, tuliyoambiwa ni Kampuni ya Serikali, iliandikishwa
nchini Uingereza kama ‘Offshore Co.’ kwa hati ya Usajili na 3424504 kama
Private Ltd Co., iliyotolewa London, na Ofisi ya Msajili wa Makampuni,
Tarehe 19 August, 1997. Tarehe 3 Oktoba, 1997 Kampuni hiyo ikapata ‘Hati
ya Kutimiza Masharti’ yaani ‘Certificate of Compliance Na 32755.. utafiti
huu unaonyesha kuwa Tanzania inazo hisa 50% katika Kampuni hiyo na Share
mwingine ni Kampuni ya Afrika ya Kusini inayoitwa Triennex Co.Ltd nayo
yenye hisa 50%. Uchunguzi wa ziada unaonyesha Kampuni 2 zaidi zina hisa
moja moja nazo ni London Law Society Ltd (Hisa 1) na London Law
Secretarial Service Ltd yenye hisa moja. Hapa kuna utata mkubwa.
Meremeta ni ya nani? Meremeta ina hisa ngapi? Kama Meremeta
imeandikishwa kama Kampuni ya Kigeni Tanzania ni kwanini imepewa fedha
za Walipa kodi wa Tanzania? Na Iwapo Tanzania siyo peke yake yenye
katika umiliki wake, ni kwanini wakati wa ufilisi wake Benki Kuu ya
Tanzania kwa niaba ya Serikali yaTanzania ililipa Deni lote la Tshs 155,
Billioni, ambazo zilibadilishwa na kuwa Dola za Marekani
118,396460.36 na kuzipeleka kwenye akaunti isiyojulikana ya Nedbank Ltd
ya Afrika ya Kusini kupitia Benki ya HSB ya New York.Zingine
13,736,628.73 zililipwa Kampuni ya Tangold (nayo tutaieleza baadaye
kidogo) kwenye akaunti yake iliyoko Corporate Branch Dar-Es-Salaam. Hoja
hizi zilihitaji Kamati Teule kupata ufafanuzi wa Kina. Kwa kuwa
tumehujumiwa ni vema Watanzania wafahamu kilichoko ndani ya Benki yao
Kuu, na Serikali kwa ujumla wake.
b) Watanzania lazima wafahamishwe, Kampuni hii ilipata faida au hasara
kiasi gani. Taarifa ya Waziri wa Nishati na Madini inaeleza kuwa
Meremeta kwa mwaka 2006/7 imepata Tani 2.7 ya dhahabu. Mapato haya
yemeenda wapi? Utata huu unaelezwa vipi iwapo Serikali inaeleza kuwa
Kampuni ya Meremeta imefilisiwa na shughuli zake kuchukuliwa na TANGOLD
Ltd.
2: KAMPUNI YA TANGOLD LTD:
Bunge tukufu mara kadhaa limeelezwa kuwa Kampuni hii ni mali ya Serikali
ya Tanzania kwa asili mia moja. Hata hivyo utafiti wangu unaonyesha
kuwa;-
a) Kampuni ya TANGOLD Ltd, ni Kampuni ya Kigeni, iliyoandikishwa kwa
mara ya kwanza nchini Mauritius kwa hati ya usajili na. C 205006121
tarehe 8th April, 2005 na kupata Hati ya Kutimiza Masharti ( Certificate
of Complicance) na. 55661 ya 20th February, 2006 hapa Tanzania.
b) Memorandum and Articles of Association ya Kampuni hii, haionyeshi
popote kuwa ni mali ya Serikali wala kuwa ina uhusiano na Serikali.
c) Kifungu cha 7cha Articles hizo zinaonyesha kuwa Hisa zinaweza
kuhamishwa kwa Baba, mama, mtoto, mke, Babu na kadhalika wa wenye hisa
-Hapa kuna zuka utata mkubwa kabisa kuwa Je Serikali inao watu hao
wanaoweza kuhamishiwa Hisa?
d) Isitoshe, Mahesabu ya Kampuni hii iliyoanzishwa 2005 hayako popote?
Je ni kweli ilianzishwa ikakaa tu haikufanya Biashara? Ni kwanini
ilianzishwa ‘Offshore” na kama ilianzishwa kufanya Biashara imelipa kodi
kiasi gani ya Serikali.
e) Uchunguzi wa kina wa Hati zilizoko BRELA hazionyeshi popote kuwa
wakurugunzi wake, wanafanya kazi kwa niaba ya Serikali, kwani FORM zote
za Brela zinaonyesha tu Ukurugenzi au kazi zao kwingineko, lakini siyo
kuwa wanawakilisha Serikali kama Serikali.
f) Msajili wa Serikali ambaye kwa kawaida ni ndiye anayemiliki Mali zote
za Serikali kwa nia ya nchi si mojawapo wa Wakurugenzi.
g) Kampuni hii ndiyo iliyolipwa fedha tulizoona hapo juu? Fedha hizo ni
kwa ajili ya nini?
Je hapakuwa na haja nzito ya Bunge letu kufanya uchunguzi wa kina
kupitia Kamati yake Teule?
3: TUHUMA BOT KULIPA FEDHA KWA KAMPUNI
BINAFSI YA MWANANCHI GOLD CO.LTD.
Mwananchi Gold Co.Ltd. imeandikishwa nchini kama Kampuni Binafsi.
Katika mwaka wa Fedha wa 2004/2005 na 2006/2007 Kampuni hii imelipwa na
Benki kuu jumla ya Dola za Marekani zipatazo 5,512,398.55. Taarifa za
Ukaguzi zinaonyesha kuwa hadi 21 Decemba, Kampuni hii ilikuwa
imelimbikiza Riba ya Dola za Marekani 62,847.91, sawa na Tshs
78,753,459. Hii ni kwa sababu Kampuni hii ilitakiwa kulipa deni lake
ndani ya Miezi 6, na hadi tarehe hiyo ya ukaguzi, yaani miezi 18 baadaye
ilikuwa haijalipa hata senti moja.
Isitoshe, Deni la Dola za Marekani, 2,807,920, linaonekana kwa taarifa
ya ukaguzi kudhaminiwa (secured kwa dhahabu ghafi (raw gold)
iliyonunuliwa kwa fedha hizo hizo za mkopo. Yaani Watanzania tumekaangwa
kwa mafuta yetu wenyewe. Kwa taarifa za BRELA, Benki Kuu inahisa 500 tu
katika Kampuni hiyo, na NDC ina hisa 375. Kampuni ya Mwananchi Trust
Company Ltd ina hisa 1,123 na Chimera Co.ltd ina hisa 500. Kampuni
ilisajiliwa kwa Hati na.44962 ya tarehe 12 Desemba 2002 kama Private
Company, na kwa maana hiyo hairuhusiwi kuchukua fedha kutoka kwa Umma,
yaani kuuza hisa zake kwa Umma wa Tanzania. Kuna utata mkubwa sana
kuhusu hizo kumpanu nyingine za Chimera na Mwananchi Trust, lakini hayo
tuyazungumze wakati mwingine au katika masuali yenu. Taarifa za ukaguzi
zinaonyesha kuwa BOT imelipa pia fedha zifuatazo ambazo hazina maelezo:
Tarehe 17/7/2005 File 18003 Temp f/47 Dola za Marekani 95,000 kwa
Kampuni ya MGCL. Tarehe 29/0/7/2005 ‘Allowances’ dola 7,500 kwa kampuni
ya MGCL bila maelezo. Tarehe 18/01/2006 Transfer( Uhamisho) Tz Embassy,
Kinshasa, Dola za Marekani, 1,500,000.
Kwa chombo kikubwa kama BOT taarifa yeyote inayoacha wasiwasi haitakiwi
kabisa, kwani BOT ndio msimamizi wa Taasisi zote za Fedha, ndiyo
msimamizi wa Uchumi wa Tanzania nzima. Je, Hapakuwa na haja ya Kuundwa
kwa Kamati Teule ya Bunge iwapo Wakaguzi hawajapata hata nyaraka kujua
malipo haya yalikuwa ya nini?
4: TUHUMA ZA JUMLA:
Siku ya Hotuba ya Waziri Mkuu nilitaka pia kupata Ufahamisho kuhusu
taarifa zilizokuwepo katika vyombo vya Habari hasa Gazeti la Serikali
Daily News, Issue no. 0856-3812 na 9315 la 22 June, 2007 taarifa ambayo
haijakanashwa na Serikali hadi leo kuwa kuhusu Fedha zilizolipwa na BOT
kwa makampuni hewa, kiasi cha Tshs 30.8 Billion kupitia Kampuni wakala
ya Kagoda Agricultural Ltd. Sababu ya Mashaka katika malipo haya ni kuwa
Kampuni inasemekana ilisajiliwa Tarehe 29 Septemba, 2005, na ndani ya
majuma 8 ilikuwa imekwisha kupewa mkopo huu. Je, kwa akili ya kawaida,
jambo hili halileti utata wowote, na hapahitaji ukaguzi wa kina wa
Kamati Teule. Wakaguzi wa Serikali CAG hata baada ya utafiti wa kina
hakuweza kugundua Kampuni hizo, Italy, Ufaransa, Ujerumani, Japan na
wala USA. Kwa Taarifa yenu eneo hili pekee ndiyo Serikali ilikubali
kufanyiwa Uchunguzi wa kina na kinachoitwa na Serikali na ‘Forensic
Auditor’.
Kwa kuwa lengo la nyaraka hii ni kutoa picha kwa Watanzania kabla ya
hatua zaidi nitazochukua Tarehe 15 Septemba, nimeona nitoe haya machache
tu ili muyaelewe Hoja ya msingi, utata ulioko, na jinsi Serikali
inavyocheza Rasilimali na Mali ya Watanzania. Narudia kuwa suala hili
halina chembe ya Itikadi hata kidogo bali linaletwa kwenu kwa misingi ya
Uzalendo na mapenzi mema kwa nchi yetu tu.
Naomba kuwasilisha.
Wenu katika ujenzi wa Taifa letu,
Dr.Willibrod Peter Slaa,(MB)
MBUNGE WA KARATU.
1 comments:
Safi sana! sikufananishi na baba wa taifa. ila angekuwepo leo angefurahi sana kuona kuna miongoni mwa vijana wanaofuata nyendo zake kuliko alio waaamini na hawakuaminika na matokeao yake kutufanya tuishi maisha ya dhiki ndani ya nchi tajiri
Post a Comment