Thursday, September 2, 2010

KAMATI YA DR SLAA YABAINI SABABU YA RAIS KIKWETE KUENDELEA KUCHAFULIWA JINA ,YALIA NA MADAI YA WALIMU











Mwenyekiti wa kamati ya bunge hesabu za serikali za mitaa Dr Wilbrod Slaa mbunge wa Karatu akionyesha moja kati ya vitabu vilivyokaguliwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa









Katibu tawala wa mkoa wa Iringa Bi.Getrude Mpaka akifuatilia ukaguzi wa kamati ya Dr Slaa leo



Na Francis Godwin,Iringa

KAMATI ya bunge hesabu za serikali za mitaa inayoongozwa na mwenyekiti wake mbunge wa njimbo la Karatu (CHADEMA) Dr Wilbrod Peter Slaa imeziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha zinapeleka madai ya walimu na watumishi wengine katika ngazi zinazohusika badala ya kuishia ngazi za halmashauri jambo ambalo linasababisha Taifa kwenda vibaya ikiwa ni pamoja na Rais kuchafuliwa jina kwa uzembe wa halmashauri .

Akitoa agizo hilo katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo leo baada ya kukagua mahesabu ya halmashauri ya Manispaa ya Iringa ,mwenyekiti wa kamati hiyo Dr Slaa alisema kuwa imefika mahali Taifa limepelekwa pabaya kwa walimu kutangaza migomo ya kudai haki zao hali ambayo imekuwa ikimchafua jina Rais Jakaya Kikwete.

"Taifa limefika pabaya kutokana na hii migomo ya walimu na ukiangalia sana tunaofanya Rais kuchafuliwa jina ni sisi wenyewe hapa....toka sasa uhakiki wa madai ya watumishi ufanyike katika ngazi zote hapa hapa katika halmashauri husika... tungependa kila mmoja alipwe haki zake kama anavyoidai serikali"

Dr Slaa alisema kuwa kwa sasa sura iliyopo ni kuwa serikali imeshindwa kulipa madai ya watumishi wake wakiwemo walimu kutokana na miaka ya nyuma taratibu za kuhakiki madai ya walimu zilikuwa hazifanyiki hali iliyopelekea baadhi ya halmashauri kuwa na madai ya walimu zaidi ya milioni 500 ila hakuna sehemu yeyote katika vitabu inayoonyesha kuwa wanadaiwa na walimu.

Alisema kuwa kwa kuwa madai hayo ya walimu na watumishi wengine yamekuwa yakijulikana ngazi za chini pekee katika ngazi za juu kama Ikulu na ofisi ya waziri mkuu wamekuwa hawajui madai halisi ya walimu na watumishi wake kutokana na kutokuwepo kwa taratibu nzuri za utunzaji wa madai hayo kimaandishi.

Hivyo alisema kuanzia sasa lazima madai ya watumishi kama fedha za likizo ,matibabu na nyingine zinaonyesha kuwa serikali ilikuwa ikilipa miaka yote japo bado kuna madai hivyo alisema lazima kamati yake iweze kujua fedha hizo zilikuwa zikikwama wapi na kuanzia sasa lazima madai yote yahakikiwe na kutunza katika vitabu .

"Tunatambua kuwa fedha hizo zilikuwa zinatolewa na zinaonyesha kulipwa sasa haya madai ya watumishi sisi tunaendelea kufuatilia na kuona ni nani alichukua fedha hizo na kuzitumia kwa kazi gani na kuwa ikibainika hatua za kuchukuliwa kwa wahusika wa fedha hizo itajulikana"

Hata hivyo alisema kuwa hazina ndio ambao walikuwa wakiweka fedha hizo ambazo zilikuwa hazitumiki kulipwa wahusika hivyo ni wazi suala hilo Ikulu kuwa na taarifa juu ya suala hilo kupitia waziri mwenye dhamana japo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa na waziri mwenye dhamana katika kuijulisha Ikulu.

Kuhusiana na utendaji kazi wa serikali iliyopo madarakani chini ya Rais Kikwete kama inafanya kazi kama wananchi walivyotegemea ama lah Dr Slaa aligoma kulitolea ufafanuzi suala hilo kwa madai kuwa kwa sasa si wakati wake kwa kuwa yupo katika kazi hiyo maalum ambayo ametumwa na bunge hivyo atalitolea jibu siku nyingine.

Kamati hiyo ilifikia uamuzi huo wa kutoa agizo hilo baada ya ofisa elimu wa Manispaa ya Iringa Bi Mary Haule kushindwa kujua madia sahihi ya walimu wa shule za sekondari zaidi ya yale ya walimu wa shule za msingi ambayo ni zaidi ya shilingi milioni 50.

Pamoja na maagizo hayo pia kamati hiyo ya Dr Slaa ilisema kuwa katika madai ya walimu kuna madai ambayo waziri mkuu Bw Mizengo Pinda aliyatoa bungeni kuwa kuna hujuma zilifanyika katika uhakiki wa madai ya walimu ikiwa ni pamoja na wale waliotumwa kuifanya kazi hiyo kuongeza madai kwa lengo la wao pia kuweza kujipatia chochote kauli ambayo inapingwa vikali na halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuwa hakuna jambo kama hilo .

Hivyo alihoji kuwa kama waziri mkuu alitoa kauli hiyo ndani ya bunge pasipo kuwa na uhakika nayo hivyo ni wazi waziri mkuu alilidanganya bunge ama Halmashauri ya manispaa ya Iringa inapingana na kauli hiyo ya waziri mkuu bungeni .

"Sasa kwa kuwa waziri mkuu aliitoa kauli hii bungeni na mbunge Stephen Galinoma wewe ni shahidi juu ya kauli hiyo na leo unashuhudia hapa Manispaa inavyopingwa ....sasa tunakwenda kuifanyia uchunguzi wa kina ikibainika kuwa waziri mkuu alikuwa mkweli tutashughulika na Manispaa ya Iringa haya yote hapa tunayaweka katika kumbukumbu zetu sasa tukimpata mkaguzi mkuu tutakabana koo"

Dr Slaa alisema kuwa lengo la kamati hiyo sio kwenda kuzilipua halmashauri za wilaya bali ni kuhakikisha fedha za serikali zinatumika kama zilivyopagwa na si vinginevyo ikiwa ni pamoja na vitabu kuandikwa katika usahihi zaidi.

Pia hatua ya tatu ya kamati hiyo ni kuhakikisha kuwa madiwani wenyewe wanasimamia vyema fedha za halmashauri rasilimali nyingine ili kamati hiyo ibaki na kazi ya kusimamia maeneo makubwa pekee.

Alisema kuwa matatizo makubwa ambayo wamepata kuyaona katika halmashauri ambazo kamati hiyo imepata kuzitembelea na kufanya ukaguzi ni pamoja na ugeuzaji wa matumizi ya fedha za miradi tofauti na ilivyokusudiwa na bunge.

Hata hivyo alisema kuwa inapobainika kuwa kuna ubadhilifu ambao umefanyika basi kumjulisha mthibiti na mkaguzi mkuu kufanya ukaguzi upya ili kama kuna mtu amehusika na wizi wa fedha za umma kuweza kuchukuliwa hatua na kuwa toka wamefika katika mkoa wa Iringa kuna wilaya moja pekee ambayo imebainika kuwa na makosa hayo ambayo hata hivyo hakuweza kuitaja wilaya hiyo japo hadi sasa wilaya zilizokaguliwa ni takribani zote ukiacha wilaya ya Kilolo ambayo ukaguzi wake kesho ijumaa.

Katika hatu nyingine kamati hiyo ya imetoa muda wa miezi miwili kwa uongozi wa Manispaa ya Iringa kukamilisha ujenzi wa nyumba za walimu ,vyoo na ununuzi wa madawati ya wanafunzi kama walivyoelekezwa na serikali kupitia fedha walizopewa kwa kazi hiyo.

Pia imejenga mashaka na matumizi ya fedha za umma yasiyo na chenji kuwa lazima katika suala hilo uongozi wa Manispaa ya Iringa umekuwa ukifanya kazi ya kublanzisha mahesabu ya fedha za miradi mezani na sio matumizi halisi ya fedha hizo.

Mbali ya mapungufu mbali mbali ambayo kamati hiyo imepata kubaini katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa bado imeweza kumpongeza mkurugenzi mtendaji wake Bi Terresia Mmbando wa wakuu wake wa idara kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi ya serikali kwa kiwango kizuri na kuwa baadhi ya mambo ambayo wamepata kuyaona katika Halmashauri hiyo hayajaonwa sehemu nyingine.

MWISHO

0 comments:

Post a Comment