Tuesday, September 28, 2010

Mdahalo wa Dk. Slaa na Sitta haukwepeki


Mdahalo wa Dk. Slaa na Sitta haukwepeki

Padri Privatus Karugendo
Septemba 22, 2010

KAMA bado tuna ndoto za kujenga taifa la uwazi na ukweli, na kama bado tunalenga mwendo wa Kasi zaidi na Nguvu zaidi, hatuna jinsi ya kuukwepa mdahalo kati ya Samuel Sitta na Dk. Slaa.

Tunaweza kuwa salama zaidi kuyafunua yaliyofunikwa; kuyajadili na kutafuta majibu kuliko kuendelea kuyafunika kwa nguvu zote tulizonazo, kwa kiburi na jeuri na wakati mwingine kwa ujinga.

Mtu akificha ugonjwa wake, kifo kinamsaidia kuufichua! Wakati wa mazishi waombolezaji wanajadili juu ya ukimya na usiri wa marehemu na kwamba kifo hakikuwa lazima. Angekuwa wazi angeendelea kuishi.

Hatutaki haya yatokee kwa taifa letu la Tanzania. Kuna uwezekano mkubwa wa kupata dawa nzuri ya kutibu magonjwa ya taifa letu. Muhimu ni Uwazi na Ukweli! Ni lazima tuulizane maswali na kusaidiana kupata majibu.

Bwana Sitta ndiye aliyeomba mdahalo kati yake na Dk. Slaa, na chanzo ni pale Dk. Slaa alipotangaza sera ya CHADEMA ya kutoa elimu bure kuanzia Chekechea hadi Chuo Kikuu.

Sitta anasema hili haliwezekani; maana yeye alikuwa bosi wa kitengo cha uwekezaji: anajua yanayotokea huko kuanzia udanganyifu hadi kuwafukarisha wananchi na kuwatajirisha wawekezaji.

Anasema pia kuwa yeye alikuwa Spika kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita na amesimamia na kupitisha bajeti ya serikali iliyolenga kuwanufaisha viongozi zaidi ya wananchi. Hivyo kwa maoni yake, Tanzania haina uwezo wa kutoa elimu bure. Pia aliongezea kwamba Dk. Slaa amefikia hatua hiyo kwa kuchanganyikiwa!

Kwa upande wake, Dk. Slaa anaamini kuwa Sitta ni adui mkubwa wa Watanzania na maendeleo yake. Kwamba huyu ndiye aliyezima kashfa nzito za ukwapuaji wa mapato ya taifa. Alizima EPA, akazima Richmond, akazima Meremeta.

Dk. Slaa akadai kuwa ufisadi huo tu umeteketeza mabilioni ya fedha ambazo zingeweza kutoa si huduma ya elimu ya bure peke yake bali matibabu, maji, umeme na huduma ya choo!

Tumesikia habari kwamba CCM imemkataza Bwana Sitta kufanya mdahalo na Dk. Slaa; maana sera ya chama hiki kikongwe ni kuendesha midahalo yake majukwaani wakati wa kampeni zake za kuomba kura.

Wao wanapendelea midahalo kama ile ya kanisani au msikitini isiyokuwa na maswali; midahalo kama ile ya enzi za chama kimoja; midahalo isiyoendana na kauli mbiu yao ya Kasi Mpya na Nguvu Mpya.

Lakini sote tunajua ya kwamba huwezi kuwa na kasi mpya ukaikimbia midahalo, huwezi kuwa na nguvu mpya ukaikimbia midahalo.

Ninasema mdahalo huu haukwepeki; maana kila Mtanzania mwenye busara anaona wazi hatari ya kuendelea kufunika bomu linalokaribia kulipuka. Madhara yatakuwa makubwa zaidi.

Badala ya jitihada zinazofanyika kuwasafisha wale wote walioshiriki katika kashfa hizi, ni bora tukawa na mdahalo wa kitaifa ambao ungeongozwa na Sitta na Dk.Slaa.

Bunge lilipoonyesha meno yake na kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa kujiuzulu, Spika Sitta alizoa sifa nyingi sana. Lakini yaliyoendelea baadaye yalifuta sifa zake zote.

Hakika, Sitta hawezi kurudisha heshima yake mbele ya Watanzania bila kukubali kuwa na mdahalo; akajieleza na kuulizwa maswali.

Haitashangaza kusikia kwamba pamoja na tetesi za Edward Lowasa kutaka kugombea urais wa Tanzania mwaka 2015 ( tetesi za kugombea mwaka huu zilizimwa kwa mbinu nyingi ikiwemo na udini), akagombea kiti cha spika mwaka huu.

Hiyo ndiyo Tanzania inayoogopa midahalo yenye maswali na kukumbatia midahalo ya majukwaani. Jinsi Mheshimiwa Rais Kikwete anavyojaribu kumtakasa Lowasa majukwaani bila kuruhusu maswali juu yake, inashangaza.

Watanzania wanataka kufahamu, kama yeye hakushiriki, ni nani aliubeba mradi huu? Mwenye mradi huu ni nani? Ilikuwa vipi ukabadilika kutoka RICHMOND na kuwa DOWANS? Nani anahusika?

Tunatakiwa kuamini kwamba wanachama wa CCM Monduli walimpitisha Lowassa kwa kishindo; ilhali idadi ya wanachama inayotajwa kumpitisha inatia shaka.

Hofu yetu ni kwamba vivyo hivyo Lowassa atatakaswa na anaweza kukikalia kiti cha spika katika bunge letu tukufu lijalo na kujitengenezea njia nzuri ya kuingia Ikulu mwaka 2015!

Na hili likitokea, ni wazi EPA, Richmond, Meremeta ndio mwisho wake, na kusema kweli huo utakuwa mwisho wa ndoto za Dk. Slaa za kutoa elimu bure. Wema wakizaliwa, hoja hii itafufuliwa tena.

Swali la msingi hapa la kujiuliza ni hili: Ni kwa nini nguvu nyingi zinatumika kuwasafisha wale wote waliohusika kwenye kashfa hizi badala ya kutumia nguvu hizo kuhakikisha fedha hizo zilizokwapuliwa zinarudishwa ili zichangie kumwendeleza Mtanzania kwa kutoa huduma ya elimu hadi huduma za vyoo?

Juzi kwenye taarifa ya habari ya BBC, tulisikia jinsi Serikali ya Tanzania inavyoshindwa kutoa huduma ya vyoo kwa wananchi, na jinsi mwananchi wa kawaida asivyo na uwezo wa kulipia huduma hivyo.

Erick David Nampesya, mtangazaji wa BBC kutoka Mwanza, alielezea tatizo la Jiji la Mwanza, jiji lenye watu zaidi ya laki tano, wanahudumiwa na vyoo vichache. Lakini pia jinsi watu wenye kipato cha chini wanavyoshindwa kulipia huduma hiyo na badala yake wanajibanza sehemu nyingine kwa haja ndogo. Wakikamatwa wanatozwa faini.

Tumesikia pia ugumu wa mtu anayepata Sh. 1,500 kwa siku asivyomudu kwenda kwenye choo cha kulipia zaidi ya mara nne kwa siku; maana atajikuta anatumia kipato chake chote cha siku kwa kulipia huduma ya choo.

Nampesa alituelezea pia matatizo ya vyoo kwenye shule za msingi na bila shaka kwenye shule za sekondari. Tatizo la vyoo si la Mwanza peke yake ni tatizo la nchi nzima. Bado taifa letu lina matatizo ya huduma hii muhimu sana katika maisha ya siku kwa siku.

Hivyo mimi binafsi nashindwa kusema kwamba Nampesya ni mzushi. Huyu ni msema ukweli. Labda kwa vile utamaduni wetu ni kutopenda kusikia ukweli ndio maana alishikwa na polisi na kuhojiwa, na sitashangaa akifunguliwa mashitaka.

Hata ikitokea hivyo, ukweli utabaki pale pale kwamba Tanzania bado tunaomba msaada wa fedha za kigeni ili kujenga vyoo. Na jambo la kushangaza sana ni kwamba tunajivunia misaada kama hiyo na kuitangaza kwenye vyombo vya habari! Ni aibu kubwa kupindukia miaka zaidi ya 45 ya uhuru wetu bado tunaomba msaada wa kujengewa vyoo!

Ni bahati mbaya kabisa kwamba sakata hili la vyoo na Nampesya na BBC, ambayo inasikika dunia nzima, linatokea wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu. Dunia nzima inaiangalia Tanzania, vyombo vya habari vinatangaza jinsi wagombea wa Tanzania wanavyotumia helikopta kwenye kampeni, mabango ya wagombea yaliyotengenezwa nje ya nchi kwa kutumia fedha za kigeni yamepamba nchi nzima.

Lakini la kushangaza zaidi ni kwamba vyombo vya habari vinataja kila siku ahadi zinazotolewa na wagombea. Ni ahadi nyingi kiasi cha kutisha: Elimu ya bure, afya ya bure, meli, viwanja vya ndege, ujenzi wa viwanda vipya, ujenzi wa reli, meli mpya nk. Ila kwa bahati mbaya hadi leo sijasikia anayetoa ahadi ya kujenga vyoo vya kisasa kwa kila familia, kwa kila shule na kwa matumizi ya umma kwenye vituo vya mabasi, kwenye masoko na kwingineko.

Wengine wanaotoa ahadi wanatushawishi kwa kusema kwamba watapunguza mishahara ya mawaziri, watapunguza mshahara wa Rais, watapunguza ukubwa wa Baraza la Mawaziri. Tunaweza kushawishika kwamba hata yakitimia, basi, huduma nyingi za kijamii zinaweza kupatikana. Ila kuna wanaotuahidi bila kutuelezea hizo fedha zitapatikana wapi?

Watakwenda kuomba kwa wajomba zetu kule nchi za nje? Wajomba waliowatuma waangalizi wao wa uchaguzi na wanashuhudia mabango ya mamilioni yakiwa yametapakaa nchi nzima?

Wakati wao wanaendesha midahalo na kuwabana viongozi wao, sisi huku tunaikimbia midahalo. Wataukubali umasikini wetu au watakuwa na maswali mengi ambayo kuyajibu ni kujishusha na kuutangazia ulimwengu mzima kwamba sisi hatuwezi kitu? Na kwamba labda Mungu alituumba kwa makosa?

Serikali ya awamu ya kwanza ilijitahidi kutoa huduma nyingi bure; elimu ya bure, afya ya bure na huduma ya vyoo ilikuwa bure. Baadaye ikaja kasumba ya kuzitoa huduma zote hizi kwenye mikono ya serikali ili ziendeshwe na sekta binafsi.

Yakaja mawazo ya ubinafsishaji na kuuza viwanda na mali zote zilizokuwa zikiendeshwa na serikali. Matokeo yake, hata huduma za vyoo zikabinafsishwa. Leo hii tunasikia kule Mwanza jinsi watu wanavyopata taabu kupata huduma hii muhimu.

Tatizo letu kubwa ni kutaka kuiga mambo ya mataifa mengine. Mataifa ambayo watu wake wanachangia kulipia huduma ya elimu, afya, maji, umeme na choo, walianzia mbali. Miaka ya nyuma katika mataifa yao huduma hizi zilikuwa bure na walihakikisha huduma hizi zinamfikia kila mwananchi.

Baada ya kuzisambaza ndipo wakaomba wananchi kuchangia. Sisi hatujasambaza huduma hizi zaidi ya asilimia 40, bado tunataka watu wetu waanze kuchangia!

Tusijidanganye. Ni kazi ya serikali kutoa huduma muhimu kwa watu wake, ni kazi ya serikali kujenga uchumi na kuulinda, ni kazi ya serikali kulinda na kutetea haki za binadamu, ni kazi ya serikali kulinda usalama wa kimwili na kiroho wa watu wote wa Tanzania. Ni kazi ya serikali kulinda na kusimamia mgawanyo wa raslimali za taifa. Ni kazi ya serikali kujenga mashule, mahospitali, barabara na mengineyo.

Serikali ambayo imeshindwa kutoa huduma muhimu kama vyoo kwa wananchi wake inawezaje kujisifia kwa mafanikio? Tunahitaji fedha kiasi gani kujenga vyoo kwa mashule yote ya Tanzania?

Kama tunaweza kutumia shilingi bilioni 50 kwenye kampeni tunashindwa vipi kujenga vyoo? Na baada ya uchaguzi tuanze kutembeza bakuli la kuombea misaada kutoka nchi za nje kujenga vyoo kwenye mashule yetu?

Ndio maana ninaona umuhimu mkubwa wa kuruhusu mdahalo kati ya Bwana Sitta na Dk. Slaa. Huu si mdahalo kati ya watu hawa wawili, ni mdahalo wa kitaifa.

Tuna mambo muhimu ya kujadili kama taifa. Tuangalie utukufu wa taifa letu badala ya kupoteza muda wetu kutengeneza utukufu wa mtu mmoja mmoja. Tunajua kwamba kuna baadhi ya Watanzania wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi na kutenda, lakini wao si muhimu kuliko taifa la Tanzania.

Simu:
0754 633122

0 comments:

Post a Comment