Monday, September 13, 2010

Njama za CCM zimezidi kumtakasa Slaa

KAMPENI za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu zimetufungua macho na kutufanya tuyaelewe kwa undani mambo mbalimbali tuliyokuwa tukiyachukulia kimazoea kuwa ndivyo yalivyo au ndivyo yanavyopaswa kuwa.

Ndani ya kampeni hizi tumeweza kuuhakiki uthabiti wa vyama vya siasa, uimara wa viongozi wa vyama hivyo, uwezo wao wa kujenga ushawishi pamoja na uadilifu wao katika kuutumikia umma na kadhalika.

Kampeni hizi zinazoendelea zimewavua nguo, hasa wale wanaotumia ukubwa wa vivuli vya vyama vyao kujifanyia mambo yaliyo kinyume na mategemeo ya umma wakiwa matarajio ya kwamba ukubwa wa majina ya vyama husika unatosha kuwapatia umashuhuri usiokuwepo kwa imani kwamba matokeo yoyote hasi, ndani ya umashuhuri huo hewa, yatamezwa ndani ya ukubwa wa vyama vyao.

Tumeweza pia kuona wanasiasa wanaoweza kujenga hoja zinazoendana na mahitaji ya jamii kwa wakati tulio nao, na wenye hoja mfilisi zilizopitwa na wakati lakini zikiwa zinabebwa na majina ya vyama ambavyo ukubwa wake unategemea tu nguvu za dola. Huo ndio uzuri na ubaya wa kampeni unaojionyesha kwa sasa.

Uzuri ni pale kampeni hizi zinapotuwezesha kubaini mbivu na mbichi, na ubaya ni pale waliokuwa wanauaminisha umma kuwa wanazo mbivu wanapogundua kuwa umma umewashitukia na kuanza kusema hovyo kwa tahayari.

Mfano kampeni za mwaka huu, hata kabla hazijafikia katikati ya muda ziliopangiwa, tayari zimeishafichua siri iliyokuwa imefichika kwenye mazoea. Watanzania, kama kawaida yao ya kuzoea na kuamini, walizoea maneno ya makada wa chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM), bila ya kuyaangalia kwa umakini na kuzibaini hadaa zilizo yaremba maneno hayo.

Watanzania wakawa wanaamini kwamba CCM ni chama madhubuti chenye sera imara zisizoyumbishwa kiwepesi. Kumbe imani hiyo ilikuwa inajengwa na utupu, kukosekana kwa chama chenye sera mbadala.

Sasa kimejitokeza Chama cha Demokrasia na Maendeleo na kuitikisa kidogo CCM na CCM ikaanza kupaa kama kishada kilichokwenda harijojo. Kitu hicho kimetuthibitishia kwamba kumbe pale hakuna umadhubuti wowote ila ni umadhubuti wa kufikirika tu uliojengeka katika mazoea ya Watanzania.

Hebu nianzie kwenye majimbo kuuangalia umadhubuti wa CCM. Ni vigumu kuamini kwamba chama madhubuti kinaweza kikauhofia ushindani wa kisiasa kiasi cha makada wake kuzikimbilia pingamizi, tena nyingine zikijionyesha kuwa ni za kughushi, kama njia pekee ya kujinusuru na upinzani.

Tumeona makada wa chama tawala walivyokuwa wakikimbilia pingamizi ili ziwaondoe wapinzani wao kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi na kuwafanya makada wa CCM kupata ushindi wa mezani usiokuwa na baraka za wapiga kura.

Hiyo ni sehemu mojawapo ya uzuri wa kampeni za mwaka huu, uzuri uliodhihirisha kwamba kumbe CCM inawaogopa wapiga kura.

Ndani ya woga huo kuna kitu kingine kilichojificha. Kitu chenyewe ni CCM kujielewa kuwa haiwatendei wapiga kura yale waliyoituma ikayatekeleze.

Kwa maneno mengine ni kwamba CCM imekuwa muda wote ikiwafanyia wananchi usanii, kitu kinachoifanya iwaogope unapofika wakati kama huu wa kusikiliza hukumu yake kutoka kwa wananchi.

Haijawahi kutokea chama kinachojiamini kwamba hakina deni kwa wananchi kikawa kinawaogopa wananchi, wapiga kura, kwa kiasi kile.

Kwa hiyo kwa kutaka kuikwepa hukumu ya wapiga kura CCM ndipo inapokimbilia pingamizi dhidi ya wagombea wa vyama vingine kusudi wagombea wake wapate kile kinachoitwa kupita majimboni bila kupingwa.

Na bila haya chama hicho kinataka watu hao wanaopatikana kwa njia ninazoweza kuziita za kimumiani waitwe wawakilishi wa wananchi! Wawakilishi wa wananchi wanaoogopa kujitokeza mbele ya wananchi.

Jambo jingine lililojitokeza na kuonyesha utupu wa chama tawala katika kipindi hiki cha kampeni ni suala la ndoa ya mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na maendeleo, Dk. Willibrod Slaa.

Baada ya CCM kuhakikisha kwamba imeishiwa hoja zenye uzito wa kukabiliana na hoja za Dk. Slaa ikaamua kuanzisha mchezo mchafu wa kupakana matope, lakini hata hivyo Dk. Slaa hachafuki. Anarushiwa matope ajabu anabaki mweupe! Ndipo CCM wakaamua kuangalia upande wa ndoa yake na kuhamishia nguvu zao zote upande huo.

Japo suala hilo linaonekana ni la kipuuzi, kwa watu walio makini, lakini kwa upande wangu nawashukuru CCM kwa kuliibua. Waswahili wanasema mfa maji haishi kutapatapa.

Mtu anayetapatapa majini kujaribu kuokoa maisha yake anaweza kuiparamia hata maiti ili imuokoe na kwa kufanya hivyo tayari anaonyesha maiti ambayo pengine ilikuwa inatafutwa na ndugu zake.

Kwa hiyo kutapatapa kwa CCM kumekuwa kwa manufaa kwa wapiga kura. Sasa wapiga kura wanaweza wakajiaminisha kuwa wamemuelewa Dk. Slaa kwa pande zake zote hata zile ambazo yeye alikuwa haoni umuhimu wa kuzionyesha.

CCM imemsaidia Dk. Slaa kuwaonyesha wananchi kuwa yeye ni msafi anayefaa kukaa katika sehemu yao takatifu, Ikulu.

Maana mpaka CCM inafikia hatua ya kuibua suala la ndoa ni wazi kwamba imemchezea Dk. Slaa “mduara” kiasi cha kutosha ikitafuta mahali penye dosari ili ikawaonyeshe wananchi, wapiga kura. Dosari imekosekana CCM ikaambulia ndoa na kuamua kuivalia njuga ndoa hiyo.

Lakini wananchi inabidi tujikumbushe kwamba kipindi hiki ni cha Uchaguzi Mkuu. Hiki ni kipindi tunachopaswa kutafakari kwa umakini ni mtu gani msafi anayefaa kuwa kiongozi wetu mkuu. Hiki si kipindi cha kuangalia mambo ya jando na unyago.

Kwa hiyo wanaotuletea masuala ya jando na unyago inabidi tuwachukulie kama wapuuzi wengine wote. Tusiwaachie nafasi ya kuyanajisi malengo yetu.

La kutilia maanani ni kwamba Dk. Slaa si fisadi. Hilo CCM wamelifanyia kazi kwa kutumia kila uwezo unaopatikana, hata kama hawakulitangaza hadharani, lakini kwa kuangalia tu mwenendo wa pilika pilika zao ni rahisi kubaini walichokigundua, Dk. Slaa ni msafi.

Si msafi kwa maana ya kutokuwa fisadi tu, bali pia ni adui wa mafisadi na ufisadi. Na hicho ndicho kitu kinachowafanya CCM wapigane kufa na kupona ili kuulinda ufisadi ambao umeishakiteka nyara chama hicho.

Maana kuondolewa madarakani kwa CCM kunamaanisha kitu kimoja muhimu, kuanguka kwa ufisadi.

Kitu kingine kinachowafanya CCM wapigane kufa na kupona kuhakikisha Dk. Slaa hakanyagi Ikulu akiwa amevaa wadhifa wa mwenye nyumba, ni umakini wake. Kwa hiyo CCM wanatuhakikishia kuwa Dk. Slaa ni mtu makini.

Wanajua kuwa mtu makini ni lazima aongoze nchi kwa kufuata taratibu zote zinazoainishwa kwenye jukumu hilo. Mfano, aliyeiba mali ya umma ni mwizi, pamoja na kutakiwa kukirudisha alichokiiba ni lazima achukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kupewa adhabu kulingana na uzito wa kosa.

Dk. Slaa si mtu wa kusema kwa tabasamu kwamba “walioiba nawafahamu nawapa muda wajirekebishe” bila kuwachukulia hatua yoyote. Hapo ndipo CCM wanapofika wakaona bora wafe na mtu kuliko kumuacha mtu huyo makini akaingia Ikulu.

Wanajua kwamba Dk. Slaa hawezi kuwapa wezi na mafisadi muda wa kujirekebisha badala ya kuwachukulia hatua wanazozistahili.

CCM wanaelewa vizuri umakini wa Dk. Slaa. Wanaelewa kwamba huyu si mtu wa kufanya kitu kabla ya kujiridhisha mwenyewe kwanza kama kinafaa kufanyika ama la. Umakini ambao Dk. Slaa amekuwa akiutumia bungeni na nje ya Bunge kurekebisha mambo mbalimbali ambayo yanakuwa yameamuliwa kwa papara.

Huyu ndiye aliyeonyesha kwamba kilichoitwa ushindi wa kimbunga au sunami, wa CCM 2005, hakikuwa kimbunga wala sunami bali fedha ya EPA.

Aidha, umakini wake ukamfanya agundue kwamba rais alisaini kwa mbwembwe muswada uliokuwa umeghushiwa kuwa Sheria ya Gharama za Uchaguzi. Vile vile akawa wa kwanza kumkamata mtu aliyekiuka sheria hiyo mpya.

Kwa hiyo CCM wenye akili timamu wanawezaje kuwashawishi wananchi wenye akili timamu waamini kwamba mtu makini kama huyo anaweza kumuoa mke wa mtu ambaye bado yuko kwenye ndoa halali?

Pia ikumbukwe kwamba kitendo cha Dk. Slaa kumuonyesha hadharani mchumba wake kinaondoa usiri ulio mafichoni unaotumiwa na baadhi ya vigogo, hususan wa chama tawala, kuwabebesha mzigo walipa kodi wa kuzihudumia nyumba ndogo ndogo zisizohesabika na vimada wasio na idadi.

Na si kwamba ambao hawajaonyesha hadharani wapenzi wao au wake watarajiwa, hawafanyi kinachodaiwa kuwa kosa kwa Dk. Slaa, kuingilia wala kuvunja ndoa za watu.

Mara ngapi tumewashuhudia vigogo wakifumaniwa na wake za watu na kulazimika kuyamaliza kimya kimya lakini baada ya nguvu za ziada kiuchumi kuwa zimetumika?

Kitu kingine kilichojitokeza katika kampeni hizi ni taharuki ya CCM iliyowasahaulisha kuwa wamekaa kwenye nyumba ya vioo na hivyo tapatapa yao kuwafanya waanze kurusha mawe wakidhani wanamkomoa Slaa na CHADEMA yake.

Katika siasa zao za maji taka, kama zinavyochukuliwa na CHADEMA, ndimo tumegundua kwamba kumbe Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba, aliwahi kuwa mwalimu mkuu wa shule ya msingi.

Mimi pamoja na kuwa mpenzi mkubwa wa Makamba, hicho ni kitu nilikuwa sikielewi. Kupitia katika maelezo yake ambayo huwa anayatoa kwa vina kama mashairi ya muziki wa kizazi kipya, nimeweza kumwelewa Makamba kwamba aliwahi hata kutumikia kanisani wakati yeye ni Mwislamu. Lakini ajabu sikuwa na habari kama aliwahi kuwa mwalimu.

Nimefikiria kuwa pengine changamoto aliyopewa na Slaa ya kukitaja kilichomfukuzisha uwalimu ndiyo sababu iliyomfanya akawa anashindwa kuitajataja taaluma yake hiyo.

Hayo ndiyo madhara ya kuanzisha mchezo wa kurusha mawe wakati uko ndani ya nyumba ya vioo.

Mpaka hapo Makamba atakapokiweka wazi kilichomfukuzisha ualimu, tunapaswa tuendelee kumuona Dk. Slaa kama mtu asiye na doa na anayefaa kukabidhiwa funguo za sehemu yetu takatifu, Ikulu.

Utakaso huu wa Dk. Slaa haupaswi kutiliwa shaka kutokana na ukweli kwamba umethibitishwa na mahasimu wake, CCM, ambao kwa vyovyote vile hatuwezi kushuku kuwa wamemfanyia upendeleo.

0 comments:

Post a Comment