Friday, September 17, 2010

Wameshindwa miaka 25 wataweza miaka 5?

Na. M. M. Mwanakijiji

Baada ya Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere kusoma alama za nyakati
na kuelewa kuwa kwa uwezo wake wa kibinadamu aliweza kuwafikisha
Watanzania mahali alipowafikisha aliamua kuachia "ngazi" au kama
tulivyoita wakati ule aliamua kung'atuka. Shujaa wangu alitambua kuwa
uongozi una kikomo chake cha uwezo wa mwanadamu na vyovyote vile
ilivyo alitambua kuwa Tanzania ni lazima itakuja kutawaliwa na watu
wengine nje ya yeye mwenyewe.

Hivyo, akaliandaa Taifa kuwa na viongozi wengine na akamuachia Mzee
Ali Hassan Mwinyi kushika usukani. Mwinyi akaingia na Ruksa kwa miaka
kumi ya kile ambacho kinajulikana kama ufunguaji wa uchumi wetu kwa
sekta binafsi. Hii iliaminika kuwa ingekuwa dawa ya kulileta taifa
letu katika mafanikio ya mtu mmoja mmoja. Naye alipomaliza miaka yake
kumi akamuachia Mkapa ambaye naye aliingia kwa kubinafsisha taasisi na
makampuni mbalimbali yaliyokuwa ya umma kwa nguvu kubwa. Mkapa akawa
mtu aliyefungua uchumi wetu kwa wawekezaji wa ng'ambo kwa kiasi
kikubwa akisimamia upitishwaji wa baadhi ya sheria mbovu kabisa kuwahi
kutungwa na watu huru.

Alipomaliza naye miaka yake kumi ya majaribio ambayo iliisha kwa
mlolongo wa kashfa ambazo hazijawahi kutoka katika taifa hili
akamuachia usukani Rais Kikwete ambaye naye aliahidi kuendeleza
"mazuri" yaliyofanywa na serikali zilizopita na kuleta mapya kwa kile
alichokiita "kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya". Kikwete alipoingia
aliingia kwa kujumlisha yale ya Mwinyi (Ruksa) na yale ya Mkapa
(Ubinafsishaji) kwa nguvu zaidi lakini akaongeza na ya kwake ambayo
ameyasimamia miaka hii mitano inayoisha. Yeye kaja na Uchumi wa
Wawekezaji akiamini kabisa kuwa bila ya wawekezaji wa kigeni Tanzania
haiwezi kuendelea na hivyo akitumia nadharia ya ruksa (ya Mwinyi)
amezidi kufungua sekta na sehemu mbalimbali za uchumi wetu kwa
wawekezaji wa kigeni hata katika mambo ambayo ukiyakodolea kwa karibu
yanashangaza (kama uchimbaji wa vyoo vya shule!)!

Kikwete naye kama Mkapa kabla yake amesimamia serikali iliyogubikwa na
mlolongo wa kashfa ambazo kuzirudia tena kunaweza kuwa ni kashfa vile
vile.

Miaka ishirini na mitano ya watawala watatu ilitarajiwa ingeweza
kufuta na kurekebisha matokeo ya utawala wa Rais mmoja aliyekuwa
madarakani kwa karibu miaka 24 hivi. Lakini nusu karne ya watawala
watatu mbalimbali wakiwa na faida ya ulimwengu wa kisasa, uliotulia
kutoka katika vita baridi, chini ya Afrika iliyo na amani zaidi na
mahusiano ya kimataifa ambayo yametengemaa kuliko wakati wowote ule
katika historia yetu. Watawala hawa watoto wamekuja na kila mpango na
miradi ya "maendeleo" ambayo wameijaribisha. Kuanzia mipango ya
"kufufua uchumi" ya miaka ya themanini na mipangao ya MTUKUTA,
MKURABITA na MMEM n.k ya miaka ya 2000!.

Kusema kweli wamejaribu. Wamejaribu kutawala na kufanya yote yaliyo
ndani ya uwezo wao. WAmejaribu kurekebisha muundo wa serikali,
wamejaribu kupigana na rushwa, wamejaribu kubadilisha elimu ya msingi,
sekondari na ya juu, wamejaribu kuleta utawala bora. Naam! Wamejaribu
saana kama timu ambayo licha ya jezi nzuri, na makocha wazuri
imeendelea kufungwa katika mechi zake mbalimbali hata zile ambazo
walitarajiwa angalau kutoka sare. Wamejaribu kuliongoza taifa kwa
miaka 25. Na wamefanikiwa katika kujaribu.

Wamefanikiwa kujaribu kuongeza vitu mbalimbali na ni kweli chini yao
idadi ya vitu mbalimbali imeongezeka. Ukiwasikiliza kwa makini utaona
wanasifia idadi zaidi kuliko ubora. Kwao wao maendeleo ni kuongezeka
kwa idadi. Watasema wameongeza idadi ya vyuo, walimu, shule, majengo,
n.k Wameanza kuwa kama Korea ya Kaskazini! Wanajivuna katik akuongeza
idadi. Lakini macho yetu yanatufanya tuwe mashuhuda wa kushindwa
katika majaribio yao.

Bado jiji la Dar ni miongoni mwa majini machafu kabisa, bado elimu ya
juu ina matatizo makubwa katika ubora na upatikanaji wake, hospitali
zetu bado hazijafikia kiwango cha kisasa zikiendelea kuwa mlundikano
mkubwa wagonjwa, mipango yetu ya uokoaji bado ni mibovu kabisa kama
tulivyoshuhudia juzi mtu aliyekuwa kwenye mtaro kwa masaa ishirini na
nne akiojaribiwa kuokolewa kwa njia za enzi za ujima! Katika miaka yao
ya robo karne bado kuna watoto wetu vijijini na mijini ambao wanasoma
kwa kukalia matofali huku madara yao yakiwa yameezekwa nyasi wakati
mtu mmoja anajengenewa jumba analo"stahili" kwa bilioni 3, huku wao
wakijigawia bilioni karibu thelathini kila mwaka kwa ajili ya samani
na chai huku wakiahidi kuleta bajaji kupeleka mabinti, mama na dada
zetu hospitali wakati wa kujifungua!

Wamejaribu ndugu zangu. Kwa miaka 25 wamejaribu kushindwa na kwa
hakika wameonesha jinsi wanavyozidi kushindwa. Kinachoshangaza ni kuwa
wanataka miaka mingine mitano ya majaribio mengine makubwa. Yaani
wanataka kujaribu kutuahidi kuwa yale ambayo wameshindwa kuyafanya kwa
miaka 25 wataweza kuyafanya kwa miaka mitano kwa kutumia viongozi wale
wale, wenye sera zile zile wakiongoza na itikadi ile ile ya
"majaribio".

Kumbe swali kubwa ambalo wapiga kura wa Tanzania wanakabiliwa nalo na
ndilo kubwa litakalotakiwa kuwaongoza kupiga kura katika uchaguzi huu
mkuu ni hili: Je, wanaamini utawala wa CCM uliodumu kwa miaka 25
katika majaribio yaliyoshindwa unaweza kufanikiwa katika miaka mitano?
Je, kama wameshindwa kuboresha shule za msingi kwa miaka 25 wataweza
kweli kufanya hivyo kwa miaka mitano? Kama wameshindwa kutafuta namna
nzuri ya kutoa elimu ya juu kwa miaka 25 ya uliberali wa kiuchumi
wataweza kweli kufanya hivyo kwa miaka mingine mitano? Je wananchi wa
Dar ambao wanaishi katika mojawapo ya majiji yaliyopangwa vibaya
zaidi, machafu na yenye changamoto za kudumu za maji, umeme na usalama
kwa miaka 25 kweli wanatarajia kuwa maisha yao yatakuwa tofauti na
hali zao kuinuliwa kwa miaka mitano ijayo? Kweli wakazi wa Dar
wanaamini chini ya watawala wale wale hospitali ya Mwananyamala,
Temeke na Muhimbili zitakuwa bora zaidi miaka mitano ijayo kuliko
miaka 25 iliyopita?

Naam, wapo wanaomini kuwa inawezekana. Naam ni imani tu. Na wengine
wataapia kabisa kuwa inawezekana. Lakini msingi wa imani hiyo ni nini
isipokuwa njozi kama za Alinacha? Wale wale walioshindwa miaka
ishirini na mitano wataweza kweli miaka mitano?
Waliokataa kufanya marekebisho makubwa ya Katiba miaka ishirini na
mitano wataweza kuleta mabadiliko miaka mitano bila mabadiliko makubwa
ya Katiba? Walioshindwa kutunga sheria nzuri za uwekezaji na sera
nzuri za misaada ya kigeni kwa miaka ishirini na mitano wataweza kweli
kuleta mabadiliko katika miaka mitano ijayo?

Ndugu zangu, tunapoendelea kutafakari ujio wa uchaguzi mkuu ni lazima
tujiulize katika dhamira zetu kama tunataka mabadiliko makubwa miaka
mitano chini ya uongozi mpya, wenye sera tofauti na za sasa na wenye
maono makubwa zaidi au kuendelea kwa kujaribisha watu wale wale ambao
tunajua tayari wameshatuonesha kuwa wanashindwa?

Kama tumekuwa kwenye basi ambalo dereva wake amekuwa akipata ajali za
mara kwa mara na kusababisha maafa na majeruhi miaka 25 tuendelee
kumchagua dereva yule yule kwa vile ati tumemzoea na kwa vile tayari
tunajua kuwa anaweza kupata ajali nyingine au tuamue kumpatia dereva
mwingine ambaye anakuja na gari jingine na utaalamu mwingine wa
uendeshaji wa gari hilo?

Katika uchaguzi huu wapo watakaoingia kwenye gari la kwanza kwa vile
wamelizoea na wanajua kuwa hata ajali ikitokea wanaweza wasidhurike.
Lakini ni majasiri wale wanaotaka kuingia kwenye gari jipya chini ya
dereva mpya. Hapo pana tofauti kati ya wenye hofu na majasiri.
Kutokana na mazoea wengine watapanda gari la kwanza na hatuwezi
kuwashangaa kwani ndilo gari pekee lililokuwepo kijijini kwa muda
mrefu, lakini nuru mpya na mwanga mpya umeanza kuangaza, gari jipya
lipo kijijini, dereva mpya kashika usukani, anasema twende!

Waliozoea gari la zamani lenye ajali za mara kwa mara na waende
kulipanda kwa furaha, lakini wanaotaka kutafuta njia mbadala
wanalazimika kutafuta usafiri mwingine. Kwani, gari lililoshindwa
kupanda mlima kwa miaka 25 litaweza vipi kupanda kwa miaka mitano
likiwa na dereva yule yule, makonda wale wale na ubovu ule ule? Labda
kuna wakati inabidi hata tutumie pikipiki!

0 comments:

Post a Comment