Tuesday, September 28, 2010

Hizi ahadi za uongo zinachusha, zinadhalilisha

Hizi ahadi za uongo zinachusha, zinadhalilisha

Jenerali Ulimwengu
Septemba 22, 2010

MAMBO yanayoweza kusababisha kuvunjika kwa amani si yale tu yanayozua ugomvi wa papo kwa papo, kama vile matusi, kejeli zilizopindukia na kadhalika, matendo ambayo kwa silika yake yanao uwezo wa kuibua ghadhabu za ghafla na kuwafanya watu warushiane mawe au mishale au wakatane mapanga. Yako pia mambo yanayoudhi hata kama hayachokozi hasira za yule anayetendewa.

Kwa mfano, kuna suala la ahadi zinazotolewa na wagombea wa kila ngazi. Kampeni hizi za mwaka huu zimejaa ahadi nyingi mno ambazo hadi sasa zinachusha. Nimekuwa nikifuatilia ahadi zinazotolewa mpaka nimechoka kuzihesabu.

Najua ziko asasi zinazofanya kazi ya kukusanya ahadi zinazotolewa na wagombea wa vyama mbali mbali, na ni matumaini yangu kwamba mwisho wa kampeni hizi hizo ahadi zitaorodheshwa na kisha tutakuwa na msingi wa kufuatilia utekelezaji wa ahadi hizo.

Upo umuhimu mkubwa katika kufuatilia ni ahadi gani zitakuwa zimetolewa na wale watakaoshinda na kushika madaraka mbali mbali. Hawa ni pamoja na mgombea atakayeibuka kama mshindi wa urais, ambaye ndiye atakuwa mkuu wa serikali itakayoundwa mwezi Novemba.

Wagombea wa urais watakaoshindwa hawatakuwa na jambo la kujibu kwa sababu hawatakuwa madarakani. Kwa mantiki hii, mshindi ndiye atakayekuwa na mzigo wa kutuonyesha ni vipi anatekeleza ahadi zote alizotoa. Waswahili husema kwamba ahadi ni deni, na wagombea mbali mbali wamekuwa wakijilimbikizia madeni lukuki.

Naamini wanafanya hivyo kwa sababu, kimsingi, wanadhani kwamba hawatatakiwa kujibu maswali yo yote kuhusu ahadi zao na utekelezaji wake. Wanadhani kwamba, kama kawaida, wakiisha kutoa ahadi wananchi walioahidiwa hawatazikumbuka, na kama wakizikumbuka hawataziulizia, na hata wakiziulizia watapewa majibu ya juu juu ambayo yatawaridhisha.

Kwa vyo vyote vile, si tabia yetu kuangalia mbali sana. Tumejenga utamaduni wa kufikiria kile kinachoonekana kinafaa leo bila kujali kesho, keshokutwa na baadaye hali itakuwaje. Ndiyo maana imekuwa haiwezekani kupanga kwa masafa marefu, na tumezama katika utamaduni wa kipuuzi wa fasta-fasta.

Hivyo, tunatoa ahadi fasta-fasta ambazo maelezo yake baada ya muda nayo yatakuwa fasta-fasta. Fasta-fasta moja iliyoniacha hoi ni ile inayosema kwamba yale yaliyoahidiwa miaka mitano iliyopita yametimizwa.

Inawezekana nina tataizo la upofu au uziwi, lakini nadhani kwamba hata kwa fasta-fasta hii ni fasta-fasta zaidi. Yumkin, yako mambo mengi yaliyofanywa, na itakuwa ni ujinga kudai kwmaba hakuna jema lililofanywa, lakini kutamka kwamba yote yaliyoahidiwa yametimizwa, ni aina moja ya utani.

Ingefaa wanasiasa wetu sasa wapunguze ahadi zao kwa sababu hata wao nadhani hawaziamini. Sisemi kwamba wasitoe ahadi kabisa; yale yanayowezekana kufanywa yanaweza kutolewa ahadi, lakini tusizidishe chumvi kiasi cha kuahidi pilau ya kuku kila siku wakati wanachohitaji wananchi labda ni ugali wao na maharage, ambavyo ni vigumu kupatikana.

Naona hata wagombea wa vyama vya upinzani nao wameingia katika mkumbo wa kutoa ahadi za aina hiyo, wakati ambapo labda wao walikuwa na nafasi nzuri ya kuwabana wagombea wa chama-tawala juu ya ahadi zilizotolewa zamani na hadi leo hazijatekelezwa. Inaelekea ugonjwa unazidi kusambaa, na kila siku iendayo kwa Mungu tutasikia mapya.

Binafsi siamini kwamba kutoa ahadi ndiyo njia ya pekee ya kufanya kampeni. Tunachohitaji ni uongozi unaoweza kutuongoza ili tujitafutie maendeleo; hatuhitaji uongozi wa “kutuletea maendeleo.” Katika kugombea urais labda tabia hii inaeleweka, kwa sababu rais anakuwa mtendaji mkuu wa serikali, na katika utamaduni wetu anaweza akaamuru mambo yakafanyika hata kama ni kinyume cha utaratibu alimradi “apeleke maendeleo” kule alikoahidi. Hata hili linatakiwa lipingwe, lakini hatujafika huko.

Lakini bado najiuliza mgombea ubunge au udiwani anayewaahidi wapiga kura wake “kuwaletea maendeleo” anatarajia kupata wapi uwezo wa kufanya hivyo? Kutoa ahadi usizoweza kuzitekeleza huku ukijua hivyo, ni ishara nyingine kwamba wanasiasa wetu wanasumbuliwa na nakisi ya haya, upungufu wa soni.

Nakisi hii inatokana na udhaifu wa jumla katika falsafa za kisiasa miongoni mwetu. Tumezalisha kundi kubwa la “wanasiasa” wanaoamini kwamba siasa ni uongo, jambo ambalo si kweli. Ingawaje ndani ya siasa kuna waongo, mabazazi na walaghai, lakini si wanasiasa wote ni waongo.

Ulaghai tunaouona katika siasa zetu hapa nchini unatokana na hali ya kweli ambayo imetufanya wengi wetu tuwe walaghai katika kila tunalofanya: Biashara zetu zamejaa wafanyabiashara feki na bidhaa feki. Elimu yetu imejaa walimu feki, mitihani feki, wahitimu feki, na vyeti feki.

Hospitali na famasia zetu zimejaa dawa feki. Sekta ya ujenzo imejaa wahandisi feki na michoro ya usanifu feki. Vivyo hivyo, na siasa zetu zimejaa wanasiasa feki wanaotoa ahadi wanazojua hawana nia ya kuzitekeleza.

Mtawala mmoja aliyepita aliwahi kusema ukweli siku moja mara baada ya kuingia madarakani kwa kutamka kwamba ilani ya chama chake iliyokuwa imemwingiza madarakani ilikuwa haitekelezeki.

Hii ilikuwa, bila shaka, ni mojawapo ya zile siku chache sana ambapo mtawala huyu alipata ujasiri wa kusema ukweli kama alivyouona.

Hata hivyo, chama chake kimeendelea kutoa ilani za aina ile ile, nazo hazitekelezeki, na hao wanaozitoa wanajua kwamba hazitekelezeki. Ni mchezo wa kuigiza ambao inaelekea unawafurahisha wananchi wanaofurika katika viwanja vya kampeni kusikiliza ahadi hizo. Hii ni burudani ya bure, na wakati mwingine inakuja pamoja na mlo, au kinywaji, au nguo za kujisitiri wasitembee uchi.

Ahadi za uongo zina madhara ya kweli kwa maana ya kuwafanya wananchi waliochoshwa na ahadi hizo, hatimaye, kukata tamaa juu ya mfumo wa kisiasa na kudharau michakato yake, na badala yake kutafuta michakato mbadala ambayo inaweza ikaleta maafa kwa jamii.

Wananchi wetu ni masikini mno; umasikini wao hauelezeki katikati ya utajiri mkubwa wa nchi yao. Wana hamu kubwa sana ya kupata maendeleo yatakayowaondolea huu umasikini ambao ni aina mojawapo ya udhalilishaji na unyanayasaji, ambao unamnyima masikini uwezo wa kuishi maisha ya staha.

Udhalilishaji huu haukubaliki hata kidogo, hasa ikizingatiwa kwamba mwakani tutaadhimisha miaka hamsini ya Uhuru.

Uchaguzi ni njia mojawapo ya kuwapa tumaini wananchi kwamba matatizo yao yametiliwa maanani, na kwamba uongozi katika ngazi zote unayaelewa matatizo hayo na kwamba uko tayari kushirikiana na wananchi kuyatatua matatizo hayo.

Wasichohitaji wananchi ni hii dhihaka ya kuwapitia kila miaka mitano kuwasimulia hekaya za mambo tunazojua hazina ukweli katika hali halisi. Inatupasa tufanye hadhari na kuhakikisha kwamba utanio huu tunaowafanyia wananchi haufikii kiwango cha kuwaudhi kiasi cha kuwafanya waseme, “sasa basi.”

Wiki ijayo nitajaribu kuangalia ni aina gani za kampeni wanasiasa wanaweza kufanya bila kulazimika kuahidi upuuzi, na taratibu wakawazoeza wananchi wasitarajie ahadi juu ya ahadi. Pia nitaangalia mambo fulani ambayo yana umuhimu mkubwa katika maisha ya taifa kuliko hizo ahadi zinazotolewa, lakini hatuwasikii wanasiasa hata wakiyagusia katika milolongo yao isiyokwisha ya ahadi.

0 comments:

Post a Comment