Monday, September 13, 2010

Wajibu wa serikali si ahadi za CCM


Juvenalis Ngowi

NILIWAHI kuandika kwamba kati ya mitaji mikubwa inayotumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni ujinga wa wapiga kura kwa maana ya ukosefu wa elimu ya uraia.

Jambo hili linajidhihirisha hata katika kampeni za wakati huu lakini kwa kiasi kikubwa inaelekea Watanzania wameamka na huenda ikawa ngumu kwa chama hiki kikongwe kutumia mtaji huu. Angalia wanavyojaribu kuwafanya watu wajinga au wapumbavu.

Unakuta bango limeandikwa kwamba ili tuwe na amani na utulivu tuichague CCM. Hapa kuna mambo mawili, moja je ni kweli kuna amani na utulivu? Pili, kama kuna amani na utulivu ni kweli imeletwa na CCM?

Tukianza na hili la mwisho lazima tukumbuke kwamba CCM wenyewe wamekuwa wakijanadi kwamba ina wanachama milioni nne. Watanzania tunakadiriwa kuwa milioni arobaini. Hivi katika akili ya kawaida watu idadi hiyo ya wana-CCM ingeweza kusababisha amani na uttulivu kama wengine ambao ni wengi zaidi hawajatulia?

Ni rahisi zaidi kusema Watanzania katika ujumla wao wanadumisha amani na utulivu, kama upo. Nasema kama amani na utulivu vipo kwa kuwa hili suala ni suala la mjadala.

Katika jamii yetu hii iliyozungukwa na matatizo lukuki tunaweza kusema tuna amani?

Utulivu unaweza kuwepo lakini sio kwa sababu ya amani. Watu ambao hawajui mustakabali wao hasa katika hali za kiuchumi hawawezi kuwa na amani. Watu ambao huduma ya afya ni kitendawili hawawezi kuwa na amani.

Watu wanaoishi katika jamii yenye uhalifu, vibaka wakichomwa, watu wakiuawa na kuporwa, ajali zinazosababishwa na uzembe hawawezi kuwa katika amani. Inawezekana kukawepo utulivu lakini katika nafsi za Watanzania wengi hakuna amani. Kila mmoja anahangaika, maana kila ya leo afadhali jana yake!

Ukweli wa kuwepo kwa matatizo mengi katika jamii yetu ni wingi wa ahadi tunazoshuhudia katika kampeni zinazoendelea. Tumeshuhudia ahadi ya bajaji 400 eti zitumike kama magari ya wagonjwa, ambulance.

Wakati wenzetu wanazungumzia mambo ya juu kama kuumba mtu ndani ya maabara, sisi tunazungumzia namna ya kumfikisha mgonjwa hospitalini. Unaweza kusema kwamba hili ni taifa maskini, sawa, kama ni taifa maskini inakuwaje viongozi wetu waishi kitajiri?

Magari ya kifahari yanayotumiwa na kila anayejidhania ni mheshimiwa yangeweza kuokoa maelfu mangapi ya wagonjwa kama viongozi wetu wangetumia magari ya kawaida na fedha za ziada zikanunua magari ya wagonjwa?

Unapotazama mtu aliyevaa nguo zilizoraruka, afya yaje ukiitazama kwa namna yoyote ile inaonekana iko shakani lakini mtu huyu anashangilia hadi kuwa mwehu katika kampeni za wale waliomfikisha katika hali hiyo duni na dhalili, unalazimika kukubali kwamba hakika watawala bado wanatumia ujinga wetu
kuendelea kututawala.

Kama aliyekuahidi maisha bora anarudi leo anakukuta ukiwa umechoka kuliko kabla na kukuambia ameleta mafanikio makubwa, na ukaona watu wanakenua meno na kutoa tabasamu badala ya kuuliza yako wapi yale maisha bora tuliyohaidiwa, basi ujue kuna tatizo.

Anapokuja mtu na kukupa ahadi ambayo katika hali zote zilipaswa ziwe zimeshatekelezwa au walau zimeanza kutekelezwa basi ujue kuna tatizo. Meli iliyohitajika miaka zaidi ya ishirini iliyopita kwa nini inatolewa ahadi leo na waliokaa madarakani walikuwa wale wale?

Ni katika ukosefu huu huu wa elimu ya uraia ndipo anaibuka mtu anajisifu kuleta maendeleo kumbe alikuwa akitimiza wajibu tu. Tukumbuke tuna mkataba na viongozi wetu. Tunawaweka madarakani na kuwalipa mishahara.

Leo hii hawapaswi kutumia nafasi tulizowapa kama sababu ya kuwarudisha tena madarakani. Turudi kwenye mabango ya uchaguzi. Rais Kikwete kwa kuwepo kwake madarakani amekuwa na wajibu wa kushiriki matukio muhimu ya kitaifa.

Unapotumia picha yake akiwa na watoto na kudai kwamba CCM inapenda na kujali watoto hivyo tuichague tena ni kupotosha watu. Picha nyingi za kwenye mabango ya kampeni ni picha za Jakaya Kikwete aliye rais wa Tanzania siyo aliye mwenyekiti wa CCM.

Kutumia picha hizi hata kama siyo za ikulu ni kutumia vibaya ofisi. Ni katika mtiririko huo pia inakuwa si sahihi Jakaya Mrisho Kikwete aliye mgombea urais kusimama wakati wa kampeni na kutumia madaraka yake kama rais kwenye jukwaa hilo hilo.

Tumeshuhudia huko Kagera akitoa maelekezo kuhusu wananchi kurudishwa katika ardhi waliyoondolewa. Hivi ni kweli hakujua kwamba kuna wananchi waliondolewa ili kupisha uwekezaji katika hiyo ranchi? Kama alijua, alijua lini?

Je, mwekezaji huyo ameingia kihalali? Kama siyo, hatua gani zimechukuliwa? Kama yupo kihalali je, maelekezo ya rais hayawezi kuwa yanakwenda kinyume na taratibu na kanuni? Tutafakari.

Angalia bango jingine. Hapa unamwona Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa anakagua gwaride la kijeshi. Picha hii ina uhusiano gani na CCM? Hapa yuko katika shughuli za kiserikali. Je, tukianza kuhoji kwamba wanaoonekana katika picha hiyo nao wanahusishwa na kampeni tutakuwa tumekosea?

Tunajua kwa hakika kwamba wanajeshi wa majeshi yetu yote hawaruhusiwi kushiriki katika siasa moja kwa moja. Unapotoa picha ya kuomba kura huku picha hiyo ikiwa na wanajeshi tunaleta taswira gani?

Hoja ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini John Tendwa haipaswi kuishia tu kwenye picha zilizopigwa ikulu bali picha yoyote ambayo ina maudhui ya kiserikali. Hata picha zinazoonyesha miundombinu iliyojengwa si sahihi kuzitumia kwenye kampeni ya CCM.

Ujenzi wa miundombinu kama barabara ni fedha za serikali zinazotokana na vyanzo ambavyo si vya CCM au ni za wafadhili ambao nao siyo CCM. Ni fedha yangu, yako na ya wafadhili ndio imejenga hivi vichache vilivyopo.

Kujitapa kwamba ni CCM imefanya haya ni kupotosha
umma. Lau kama wanasema haya mazuri wameyafanya wao kwa kuwa wapo madarakani, basi shuruti pia wakubali kwamba hata mabaya yaliyotokea wakati wakiwa madrakani wabebeshwe wao.

Ikiwa tutaweka kwenye mizani mazuri na mabaya ya watu hawa, bila shaka mabaya yatazidi mazuri. Sitaki kurudia ngonjera ya kila siku lakini fikiria mambo tangu uuzwaji wa mashirika yetu, ubinafsishaji, ukwapuaji wa fedha kama zile za EPA na ubadhirifu mwingine mwingi.

Kama wanasema wameweza, tuwaulize liko wapi shirika letu la ndege. Waulize kwa nini tulifikia kutafuta wahindi watuendeshee shirika la reli hata kama ilikuwa kwa ubia, waulize vilikofia vyama vya ushirika. Maswali ni mengi. Waulize tunavyonufaika na rasilimali zetu.

Ikiwa tumeshindwa kuendesha shirika dogo kama la ndege na lile la reli hivi ahadi ya kununua meli na kujenga viwanja vya ndege vya kimataifa inakuwa na mashiko kiasi gani?

Huenda imefika mahali pa kuwaamsha wapiga kura na kuwapa elimu ili wajue nini kinatokana na kipi na kwa nini. Ni pale tu wapiga kura watakaposema hawadanganyiki ndipo tutaweza kuchagua viongozi wanaofaa kwa jamii yetu.

Je, tumewapa wapiga kura elimu ya kutosha ili tuweze kusema bila shaka yoyote kwamba hawadanganyiki?

0 comments:

Post a Comment