Thursday, September 30, 2010

Upendeleo wa polisi utazusha machafuko

TUNAWASILISHA kilio hiki cha wakazi wa jimbo la Busanda na kote kwenye fujo wakati huu wa uchaguzi, tukisisitiza kuwa kama chombo makini cha habari, kinachotaarifu, kuelimisha na kupigania maslahi ya wote, hatufungamani na chama chochote cha siasa wala upande wowote ule wa kimaslahi.

Hata hivyo tunafungamana na ukweli bila kujali ukweli huo unatokea wapi na unakituhumu chama gani, msimamo wetu ni kupinga kile kisichofaa na kuunga mkono haki na uhuru wa watu kuchagua au kushiriki harakati za kisiasa za chama wanachokipenda.

Ni ukweli usiotia shaka kuwa baadhi ya makundi ya vijana katika baadhi ya vyama vya siasa nchini, hususani kundi la ‘Green Guard’ la Chama cha Mapinduzi (CCM), limekuwa chanzo cha uvunjifu wa amani kwa kuwashambulia wafuasi, viongozi au mashabiki wa vyama vya upinzani, hususan wale wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Gazeti hili jana, lilikuwa na habari kuhusu ukatili uliofanywa na kikosi cha ulinzi cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), ‘Green Guard’ dhidi ya wafuasi na mashabiki wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika jimbo la Busanda, mkoani Mwanza.

Green Guard hao, walitembeza kipigo kwa kuwakatakata kwa mapanga zaidi ya vijana wanne wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CHADEMA, Jumamosi iliyopita, mbele ya mgombea ubunge wa CCM, Lolensia Bukwimba, aliyekuwa akirudi kwenye mikutano yake ya kampeni.

Kwa mujibu wa habari hiyo, chanzo cha tukio hilo la kinyama ni vijana waliokuwa wakimlinda Bukwimba kuwanyooshea alama ya kidole gumba vijana hao ambao walijibu kwa kunyoosha vidole viwili kuashiria kuwa wanaiunga mkono CHADEMA.

Kwa kukerwa na kitendo hicho, walinzi hao wa CCM walishuka kwenye gari waliyokuwemo na kuanza kuwacharanga kwa mapanga vijana hao wa CHADEMA, huku mmoja wao akiwa amekatwa vibaya kichwani na kushonwa nyuzi zaidi 10 na mwingine akiwa amechanwachanwa sehemu za mwili.

Mbali ya unyama huo, kinachosikitisha zaidi ni desturi ya jeshi la polisi wilayani Geita kutoonekana kuchukua hatua zozote stahiki kila inapowasilishwa taarifa ya vitendo vya fujo vinavyofanywa na makada au wafuasi wa CCM.

Ni ukweli usiotia shaka kuwa hata wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge, hali kama hiyo ya vurugu ilijitokeza lakini kila jeshi la polisi lilipotaarifiwa juu ya vurugu hizo zinazofanywa na wana CCM halikuchukua hatua kwani hata baada ya wahusika kuhojiwa baadaye vurugu zilionekana kuendelea.

Vurugu kama hizo pia zimetokea hivi karibuni katika jimbo la Moshi Mjini na Ubungo, jijini Dar es Salaam, zikiwahusisha wafuasi na makada wa vyama hivyo viwili, CCM na CHADEMA.

Tunachukua fursa hii, kulionya jeshi la polisi kuacha kupendelea chama kimoja cha siasa na badala yake lichukue hatua dhidi ya mfuasi wa chama chochote cha siasa anayefanya vurugu au kuchochea vurugu katika wakati huu wa kampeni.

Tunalionya Jeshi la Polisi, kama litaendelea na upendeleo wake kama ilivyojionyesha dhahiri katika jimbo la Busanda, basi upo uwezekano mkubwa kwa wanaofanyiwa vurugu kujichukulia sheria mikononi mwao kwa nia ya kujihami na kujilinda, hali ambayo inaweza kuzusha machafuko au vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Tunalitakia mema taifa letu, tulitaka jeshi letu lilinde Watanzania wote bila kujali tofauti zao za kidemokrasia, tunaamini polisi wakifanya kazi kwa kuzingatia sheria, malalamiko mengi kama haya hayawezi kuwepo.

0 comments:

Post a Comment