Dk Willibrod Slaa amecharuka mkoani Mwanza. Akiwa katika majimbo ya Geita, Buchosa na Nyamagana, mgombea huyo ametoa changamoto kali kwa CCM, hasa mgombea urais Jakaya Kikwete ambaye Dk. Slaa alisema ni "saizi yangu." Halafu akatumia fusa hiyo kumshughulikia, akisema rais huyo wa awamu ya nne hana mpango mkakati wala visheni ya kuwakomboa Watanzania. Badala yake, Kikwete amekuwa akitekeleza maagizo yake (Dk Slaa) katika kipindi cha miaka minne iliyopita, hasa kwa kudai anapigana na ufisadi (ulioibuliwa na Dk. Slaa). Hata katika tukio la juzi la Kikwete kumchukulia hatua Meneja wa kiwanda cha Turiani, Morogoro, Dk. Slaa alisema hatua ya Kikwete ilitokana na msisimko wa siasa za uchaguzi, hasa baada ya Dk Slaa kutembelea Turiani, wiki mbili zilizopita, na kutoa kauli kwamba atashughulikia matatizo yao katika siku 100 za kwanza za utawala wake.
Vile vile, alisema Rais Kikwete amevunja rekodi ya kudanganywa kuliko marais wote duniani katika miaka mitano iliyopita. Alisema mwaka mwaka 2007, JK alifungua mradi hewa wa maji huko Pwaga, Dodoma; mwaka 2009 Rais Kikwete aliletewa Ikulu mkurugenzi wa halmashauri isiyohusika na kukabidhiwa gari la wagonjwa; na alizindua hoteli moja ya kitalii mkoani Arusha, kesho yake ikavunjwa uzio na TANROADS, na mwaka huu alisaini kwa mbwembwe sheria iliyochomekwa vipengele ambavyo havikujadiliwa Bungeni; na kwamba hata baada ya matukio yote hayo, hakuna mtu aliyewajibishwa.
Mwaka huu, siku alipozindua kampeni za CCM mkoani Mwanza, JK aliwaeleza wananchi kwa mbwembwe, kuwa Mbunge wa Nyamagana, Lawrence Masha, alikuwa amepita bila kupingwa; jambo ambalo Dk. Slaa alisema si kweli kwani mgombea wa Chadema alikuwa ameweka pingamizi, ambalo hatimaye limemrejesha ulingoni. “Ama JK alidanganywa na Masha au alijidanganya mwenyewe au hakuwa makini…Kikwete si makini. Awaombe radhi wananchi wa Nyamagana kwa kuwadanganya.”
Alisema Kikwete amekuwa rais wa majaribio, na kwamba miaka mitano inatosha. "Imetosha, Kikwete aende akapumzike, muda wake umekwisha, miaka mitano inamtosha. “Hatuwezi kwa miaka mitano kuendelea kuwa na rais mtalii, asiyejua matatizo ya wananchi wake, anayetetea maslahi ya wawekezaji badala ya wananchi, asiye na visheni,” alisema.Dk Slaa alidai hata mipango mkakati kama MKURABITA, MKUKUTA na hata MINI-Tiger, hata na barabara anazojivunia JK kujenga ni za awamu ya tatu ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, si zalo la awamu ya nne.
Akiwa jijini Mwanza, alisisitiza juu ya umuhimu wa viwanda katika kujenga uchumi, ajira na ujira bora; akasema CCM iliua viwanda na makampuni ya umma zaidi ya 450 yaliyoanzishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na hivyo kuua ajira na uchumi wa taifa. Alisema Chadema kinadhamiria kuanzisha viwanda vinavyotegemea mazao ya kilimo na mifugo, ili kuimarisha uchumi wa watu maskini, kwani raslimali zipo. Kilichokosekana, hadi sasa, ni ubunifu kwa upande wa watawala. Alisisitiza pia sera za elimu, afya, na makazi bora wa mujibu wa ilani ya Chadema.
Baada ya mkutano alisindikizwakwa maandamano na umati wa watu wazima na vijana, wakisukuma gari alilopanda kutoka uwanja wa Mirongo hadi Hoteli ya Nyumbani - umbali kwa kilometa zipatazo 5. Polisi walijitahidi kuwadhibiti wananchi hao, ikawa kazi bure. Hakukuwa na fujo yoyote. Walikuwa wakiimba, "rais, rais, Slaa; tumechoka mafisadi..." huku baadhi yao wakiwa na mabango yenye maandishi kuwa, "hatukubebwa na magari, tumekuja ejnyewe."
Amka Na BBC
1 hour ago
0 comments:
Post a Comment