Thursday, September 30, 2010

CHAGUA PHILLIP NYANCHINI MOGENDI JIMBO LA KINONDONI

Phillip Mogendi

HISTORIA YA NDUGU PHILLIP NYANCHINI MOGENDI ANAYEWANIA KITI CHA UBUNGE JIMBO LA KINONDONI KWA TIKETI YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO – CHADEMA.

Nilizaliwa tarehe 08/09/1968 katika hospitali ya Lugalo iliyoko Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar-Es-Salaam. Mimi ni motto wa pili kuzaliwa na wazazi Mzee Gregory Mogendi Nyanchini na Mama Aziza Woho Mogendi (Barihuta) ambaye ni marehemu sasa. Baada ya miaka mmoja hivi wazazi wangu walirudi nyumbani kijijini Gamasara, Kata ya Nyandoto, Tarafa ya Inano, Wilaya ya Tarime. Mwaka 1970 Baba yangu Mzee Gregory Mogendi Nyanchini aligombea ubunge wa jimbo la Rorya na kushinda Kiti hicho. Kwa muda wote huu niliishi Kijijini Gamasara nikihudhuria masomo ya shule ya msingi huku baada ya masomo nikishiriki kuwasaidia wazazi kufanya shughuli za kulima na kuchunga ng’ombe. Mwaka 1982 mwanzoni Baba alinitafutia uhamisho kwenda kusoma darasa la sita katika shule ya msingi Isibania iliyoko jimbo la Kusini nchini Kenya. Hii yote ilikuwa jitihada za makusudi za kutafuta elimu bora.

Nikiwa Isibania, Kenya ambayo iko mpakani mwa Tanzania na Kenya yaani upande wa pili mwa Sirari,Wilayani Tarime nilijiunga na Kanisa Katoliki kwa mafunzo ya ubatizo na kubatizwa mwaka huo huo kabla sijarudi Gamasara kumalizia elimu ya msingi. Nilisoma katika darasa la sita shule ya msingi Isibania kwa miezi tisa na baada ya hapo hali ya kifedha haikuruhusu mimi kuendelea na masomo nchini Kenya , hivyo nikarudi Gamasara kumalizia elimu ya msingi. Mwaka 1983 nilifuzu elimu ya msingi katika shule ya msingi Gamasara. Nilibahatika kufanya mitihani miwili ya kufuzu elimu ya msingi, ule wa taifa na ule wa kujiunga na shule ya seminari.

Nilifaulu kujiunga na shule ya kikatoliki ya Mtakatifu Maria ya Nyegezi Seminari ya Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza iliyoko nje kidogo ya mji wa Mwanza. Nilikuwa mwanafunzi pekee kutoka shule ya msingi Gamasara kufauru kujiunga na elimu ya sekondari mwaka huo na pia mtoto wa kwanza kutoka kijijini Gamasara kujiunga na seminari. Namshukuru Mungu kwa mwangozo wake na kwa changamoto kutoka kwa Wazazi wangu. Baada ya kusoma kidato cha kwanza Nyegezi Seminari ulitolewa uamuzi wa pamoja wa majimbo ya Mwanza, Musoma, Shinyanga na Geita kwa shule ya Mtakatifu Maria Nyegezi Seminary iwe ni kwa ajili ya masomo ya sekondari ya kidato cha tano na sita tu na shule ya Mtakatifu Piusi ya Makoko Seminary iliyoko Mkoani Mara nje kidogo ya mji wa Musoma Mjini iwe ni kwa ajili ya masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne. Hivyo basi wanafunzi wa vidato vya mwanzo yaani cha kwanza hadi cha nne tuliokua shuleni Nyegezi Seminary, Mwanza tulihamishiwa Makoko Seminari, Mkoani Mara. Nilisoma Makoko Seminary tangu mwaka 1984 hadi 1987 nilipofuzu mafunzo ya kidato cha nne mkondo wa sayansi na kufaulu kwa kupata daraja la kwanza (Division One) na kuchaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na sita katika shule ya Mtakatifu Maria Nyegezi SeminarI, Mwanza.


Nilichaguliwa kusoma mkondo wa sayansi kwa masomo ya fizikia, Geografia na Mahesabu yaani (PGM) shuleni Nyegezi Seminari, mkoani Mwanza mwaka 1988 hadi 1990. Baada ya kazi ngumu ya kuandaliwa kiroho na kidunia nilifanya mtihani wa kumaliza elimu ya juu ya sekondari. Namshukuru Mungu kuwa nilikuwa kati ya wale wachache tuliofaulu kwa daraja la pili yaani (Division two). Ilikuwa muda nyet maishani mwangu wa kufanya maamuzi kuendelea kwa mafunzo ya juu ya Upadri au kuendelea na masomo ya chuo Kikuu. Ndipo niliamua kuomba nafasi ya kusoma katika chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam.

Mwaka 1990 nilipangiwa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa katika Kambi ya Makutupora, nje ya mji wa Dodoma kwa kipindi cha mwaka mmoja. Nilihamishiwa Mgulani JKT jiini Dar-Es-Salaam kumalizia kipindi cha mwaka mmoja katika jeshi la kujenga Taifa huku nikijitolea kufundisha katika shule ya Jitegemee Sekondari masomo ya Hesabu na Geografia.
Mwaka 1991 baada ya kumaliza mafunzo ya JKT, sikuweza kujiunga moja kwa moja na Chuo Kikuu Mlimani kwa kuwa wanafunzi wa chuo hicho walikuwa wamegoma na serikali ilikifunga chuo kwa mwaka huo hivyo nikachelewa kujiunga kwa mwaka mmoja hadi mwaka 1992. Kwa muda huu niliendelea kufundisha binafsi na kupiga picha mtaani kujipatia kipato nikisubiri kujiunga na Chuo Kikuu.


Nilifanikiwa kuchaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam kusoma katika Kitivo cha Sayansi kwenye mkazo wa masomo ya Mahesabu na Takwimu (Yaani Faculty of Science Majoring in Mathematics and Statistics. Hii ilikuwa kati ya mwaka 1992/93 hadi 1994/95. Tukiwa Mlimani tulikuwa na mwanafunzi mwenzetu mlemavu kwa jina Oscar Paul amabaye kulingana na hali yake ilikuwa vigumu kwake kutembea kuhudhuria vipindi mbalimbali kimasomo hapo Mlimani. Nikiwa kiongozi wa darasa langu ilikuwa vigumu sana kwangu kuona Oscar akihangaika hivyo nikaamua kuunda kamati maalumu kukusanya fedha za kumnunulia kibajaji cha kutembelea. Nikiwa mwenyekiti wa kamati hii nilifanikisha kumwalika Mkuu wa chuo ambaye nilimwomba kuwaalika mabalozi wan chi mbalimbali kuhudhuria siku ya kumchangia ndugu Oscar. Naye kwa akaamua kutowaalika mabalozi hivyo kuamua mwenyewe kuhudhuria na kutoa kibajaji na fedha taslimu tulizokusanya ikatumika kununua petrol. Hivyo basi kumwondolea ugumu wa maisha ndugu Oscar hapo chuoni. Oscar alifanikiwa kumaliza nasi na hivi sasa ni mtaalam katika shirika la NSSF Jijini Dar-Es-Salaam. Nilihitimu na shahada ya Sayansi yenye mkazo wa masomo ya Mahesabu na Takwimu yaani (Bachelor of Science with Honors, majoring in Mathematics and Statistics).


Mara baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu nilitafuta kazi na kati ya sehemu nilizoomba kazi na kuitwa kwenye usahili ni katika Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Dar-Es-Salaam mwaka 1995. Nilifanikiwa kupata kazi hapo kama Katibu Msaidizi wa Katibu wa Bunge daraja la tatu yaani (Clerk Assitant III), kituo changu cha kazi kilikua Dodoma. Nilipata kuhudumia Kamati zifuatazo: Kamati ya Mashirika ya Umma (Parastatal Organization Committee - POC) na Kamati ya Mahesabu ya Serikali (Public Accounts Committee – PAC). Niliteuliwa kuwa Katibu Kamati za Bunge, kazi yangu kubwa ilikuwa kumsaidia Katibu wa Bunge kuongoza Kamati za Bunge, Kuwashauri waheshimiwa wabungekatika vikao vya kamti za bunge kwa kutumia mwongozo wa Kanuni za Bunge, kupanga na kuongoza mikutano ya vikao vya Kamati, kumwakilisha Katibu wa Bunge kwenye misafara ya waheshimiwa wabunge wakiwa na safari za kikazi ndani na nje ya nchi, kuchukua mihutasari ya vikao vya bunge ikiwa ni pamoja na kwenye vikao vya kamati za Bunge, kuandaa taarifa za Kamati za Bunge zinazowasilishwa Bungeni na Mwenyekiti wa kamati husika.

Nilifunga ndoa ya maisha na mpenzi wangu Rachel Nyakuyenga Maingu, ambaye sasa ni Rachel Nyakuyenga Mogendi tarehe 27/12/2007. Hivi sasa Mungu katujalia watoto wawili. Wa kiume tuliyempa jina la Bibi Kizaa Baba- Wambura, (Benedict Wambura Nyanchini Mogendi) Na wa Kike tuliyempa jina la Marehemu Mama yangu Woho, ( Isabelle Woho Nyanchini Mogendi)
Baada ya miaka miaka minne kazini niliamua kutafuta shule Marekani kuchukua shahada ya juu. Baada ya muda mrefu kuuomba uongozi kunisomesha na kushindikana, ndipo nilipoamua kuomba ruhusa kwenda kujisomesha Marekani. Nilifanikiwa kupewa ruhusa hiyo name hapo mwaka 1999 niliondoka kwenda Marekani katika Jimbo la Kansas Mji wa Wichita kusoma. Nilipewa ruhusa ya miaka mitatu. Mwaka 2000 nilianza kusomea shahada ya juu ya Utawala wa mitandao ya Komputa yaani ( Masters in Management Information Systems- MMIS), katika chuo kikuu cha Friends University, Wichita, Kansas, USA. Mwaka 2002 nilifuzu shahada hiyo. Mwaka 2003 nilirudi ofisi ya Bunge Dodoma kuendelea na kazi. Baada ya kurudi nilihamishiwa kitengo cha Utawala wa Kompyuta yaani Information Technology Department ambapo nilitegemea kupangiwa kazi nitumie utaalamu nilioupata Marekani kwa jasho langu kwa manufaa ya Taifa letu change. Baada ya kukaa kwa karibu mwezi mzima bila kupangiwa kazi yoyote, nikaamua kuomba tena ruhusa nikachukue shahada ya udaktari kwa kujisomesha mwenyewe kama ilivyokua awali. Nilikuwa nimefanikiwa kupata ufadhili wa elimu hiyo ya udaktari kwa masharti kuwa narudi kwa wakati uliokubalika. Baada ya ukuritimba uliopo katika ofisi ya Bunge hii ikiwa ni kawaida kwenye maofisi mengi ya serikali, muda ulizidi kuisha nikiambiwa nisubiri maamuzi ya Tume ya Bunge ambayo ilizidi kuchelewa kutoa maamuzi. Ndipo niamua kuandika barua kwa Mwenyekiti wa Tume ya Bunge nikimweleza hali halisi na kutoa taarifa kuwa nimekwisha chelewa na imenilazimu kuondoka nisiikose nafasi ya ufadhili wa kusomeshwa. Bahati mbaya wakati nimerudi Marekani nikawa nimechelewa hivyo kukosa ufadhili niliokuwa nimeahidiwa. Niliamua kujisomea zaidi binafsi ili kufanya mitihani inayotambulika Kimataifa ya Uongozi wa Miradi yaani Project Management. Baada ya muda huku nikifanya kazi katika taasisi mbalimbali, nilifanya mitihani hiyo na kuifaulu na hivyo kuwa na shahada inayotambulika Duniani Kimataifa ya meneja Miradi Mtaalamu yaani Project Manager Professional- PMP.


Nilifanya kazi kwenye Makampuni makubwa ya Hewlet Parkard- HP la Houston, Texas na GuideStone Financial Resources la Jijini Dallas, Texas. Baada ya mikataba yangu kuisha niliamua kutokuiongeza na hivyo kurudi Wichita, Kansas kuungana na familia yangu na hapo nikaamua kufungua Kampuni ya Ugavi inayouitwa Corporate Delivery Service, LLC – CDS. Huu ni mradi binafsi nikuawa nikiuongoza huku nikifanya maandalizi kurudi nyumbani, Tanzania.
Nilishauriwa na marafiki zangu ambao ni raia wa Marekani nichukue uamuzi wa kuwa raia wa Marekani, nami nilikataa kwa kuwa naipenda nchi yangu na pia kwangu mimi naona ni sawa na kuisaliti nchi yangu kwa kuukana uraia wan chi yangu. Marekani mimi nilikwenda kutafuta elimu nayo nimeipata, ni wajibu wangu sasa kurudi nchini kuutumia ujuzi wangu. Hivyo niko kwenye maadalizi ya mwisho kuichukua familia yangu ikiwa ni pamoja na mke na watoto wawili kurejea kwetu.

Mwaka 2009 nilirudi Tanzania na kufungua Kampuni inayouitwa Phinya Group Of Companies Tanzania Limited yenye Ofisi zake Sinza, Jijini Dar-Es-Salaam. Kampuni hiyo imeanza kazi kupitia kitengo chake cha usafirishaji mizigo pande zote nchini,Tanzania.
Baada ya kutafakari kwa makini jinsi nchi yetu inavyoendeshwa, niliamua kwa mara ya kwanza kujiunga na chama cha siasa, ndipo niliamua kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA mwaka jana mwezi wa tisa wilayani kwangu Tarime. Namba yangu ya uanachama ni CDM No. 00675. Ni imani yangu kuwa nina uwezo mkubwa kushirikiana na uongozi wa CHADEMA wilayani hadi Taifa kuwa nianuwezo wa kuleta chngamoto ya maendeleo na kutetea haki ya wanyonge bila kubagua wanyonge hao ni wa chama gani ili mradi haki ya msingi ya kila mwananchi inapatikana bila rushwa. Hivyo basi namechukua fursa hii kujitambulisha kwa umma wa Watanzania hasa wanachi wa jimbo langu la Uchaguzi, Jimbo la Kinondoni, kuwa mimi ni mmoja wa wanachama wa CHADEMA anayewania nafasi ya Ubunge kupitia Tiketi ya chama cha CHADEMA mwaka huu mwishoni. Baadhi yenu mnanifahamu, ila wengi mnahamu ya kunifahamu, tutafahamiana hivi karibuni baada ya kurudi kutoka safarini nitakapo fanya mikutano ya hadhara kwa ajili ya utambulisho Kinondoni na vitongojini mwake.

HII NI HISTORIA FUPI YA NDUGU PHILLIP N. MOGENDI ALIYOITUMA JIMBONI KWA UTAMBULISHO NA NIA YAKE KUGOMBEA UBUNGE KINONDONI. WATANZANIA WA WICHITA, KS; HOUSTON, TX; NA POPOTE MLIPO HUO NI UTAMBULISHO WA NDUGU PHILLIP NYANCHINI MOGENDI (PHINYAMO).

BWANA MOGENDI ANAOMBA USHIRIKIANO WENU WA DHATI KATIKA KUMUUNGA MKONO KWA SALA ZENU, MICHANGO YENU YA KUMUWEZESHA KUFANIKISHA AZMA HII, MAWAZO ILI TUWEZE KUWA SEHEMU YA UFUMBUZI WA MATATIZO YANAYOIKABILI NCHI YETU TANZANIA.
KAMA KUNA SWALI LOLOTE KUHUSIANA NA HISTORIA HIYO FUPI YA MGOMBEA MOGENDI TUMA EMAIL KWA phinya68@yahoo.com AU PIGA SIMU KWAKE 316-519-3810.


PIA WAWEZA KUWASILIANA NA WAJUMBE WA KAMATI NDOGO YA WICHITA, KS NA ILE YA HOUSTON, TX WANAONIFAHAMU VIZURI KAMA IFUATAVYO :

WICHITA, KS:

Lunda Asmani: 316-461-7716

Emelius Mwanache: 316-461-8082

Mwiga Kapya: 316-993-8796

Veronica Hosea: 316-993-1429

Jerry Mkony: 495-694-0631

Angela Kisanko: 316-993-8524


HOUSTON, TX:

Alex Maira: 832-212-2300

Nickson Mlay: 713-966-0185

Anter: 832-646-4557

Arnold Maira: 832-794-4938

0 comments:

Post a Comment