Lula wa Ndali-Mwananzela | Septemba 8, 2010 |
KATI ya mambo mengi ambayo yanavutia katika Ilani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni uelewa wao wa jambo moja kubwa sana na muhimu sana kwa mustakabali wa Taifa.
Hilo ni kuelewa kuwa kama Taifa hatuwezi kujenga Taifa la kisasa lenye uchumi wa kisasa huku tukitumia namna ya ulinzi wa kizamani na vyombo vya usalama vya kizamani ambavyo havijafanyiwa mabadiliko makubwa.
CHADEMA wanaonyesha kuelewa kuwa Tanzania ina haja ya haraka la mfumo mpya wa usalama wa vyombo vya usalama ili kuweza kukabiliana na changamoto na matishio ya ulimwengu wa kisasa.
CHADEMA inasema hivi katika suala la ulinzi na usalama wa Tanzania: “Katika miaka ya karibuni, utendaji wa Usalama wa Taifa umedorora sana kutokana na kuingiliwa na wanasiasa wa chama tawala. Matokeo yake chombo hiki muhimu kimeanza kupoteza imani, heshima na hadhi yake katika jamii na kuanza kuonekana kuwa kipo hapo kwa ajili ya Usalama wa CCM na wanasiasa wake, badala ya usalama wa Taifa.”
Wameweza kutambua mojawapo tu ya matatizo katika mfumo wetu na nadharia yetu ya ulinzi na usalama. Na wanaelewa msingi wa nadharia iliyomo katika Ilani yao. Wao wanasema: ”Kwa kutambua changamoto mbalimbali zinazokabili vyombo vyetu vya usalama, Serikali ya CHADEMA inakusudia kufanya mabadiliko makubwa ya mfumo wetu wa ulinzi na usalama ili hatimaye tuweze kujenga vyombo na mfumo wa kisasa wa kiusalama na kuondokana na mfumo wa zamani ambao bado una mabaki ya fikra za enzi za ukoloni na masalia ya vita baridi. Tanzania tunayoitaka ni lazima iwe tayari kulinda watu wake, uchumi wake na maslahi yake pasipo kuwa na hofu.”
Ni hatua wanazozipendekeza kushughulikia changamoto hizi zinawafanya watofautiane kwa kiasi kikubwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) au vyama vingine. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu ajenda ya Usalama wa Taifa inaangaliwa kwa upana wake na kwa uwazi inaostahili.
CHADEMA wana mapendekezo makubwa ya mabadiliko katika jeshi la Polisi na Magereza. Kwa mfano, baadhi ya mambo ambayo wanayataja ni pamoja na ujenzi wa vituo vya kisasa vikubwa vya Polisi ili kukidhi mahitaji ya kiusalama ya Jiji la Dar es Salaam.
Wanasema kuwa kuanzia Bajeti ijayo ya 2011/2012 watatenga fedha ili kuanza ujenzi wa vituo vikubwa vya polisi katika maeneo ya Ubungo, Kawe, Mbagala na Magomeni.
Mmoja wa mipango mipya kabisa ambao haujawahi kubuniwa na Serikali ya CCM uko katika kuundwa kwa vikosi vya uokoaji vya halmashauri. Kwa miaka kadhaa sasa kazi ya uokoaji imebinafsishwa kwa vyombo binafsi. Lakini CHADEMA wanasema kuwa katika mpango wao “Kila Halmashauri itakuwa na wajibu wa kuunda kikosi chake cha Uokoaji na Dharura (rescue and emergency services) ili kuhakikisha kuwa kila mji una maafisa wa kutosha na vifaa vya kutosha kukabiliana na majanga mbalimbali.”
Hii itaondoa moja ya matatizo makubwa tuliyonayo katika idara ya uokoaji kwa vile jukumu hilo linaangaliwa na wizara ya kitaifa badala ya kuachwa mikononi mwa mamlaka za mahali.
Kwa upande wa ulinzi wa majini wamekuja na wazo hili “Tutaondoa kikosi cha Polisi cha Majini (Police Marine) na kutokana nacho tutaunda kikosi kipya cha Ulinzi wa Pwani na Fukwe (Tanzania Coast Guard). Kikosi hiki ndicho kitakachokuwa na nguvu za kipolisi katika maeneo ya pwani na fukwe za maji yetu katika Bahari ya Hindi na maziwa yetu pamoja na mito mikubwa. Tutakipatia kikosi hiki zana mbalimbali na vitenda kazi vya kisasa. Mpango wa kuundwa kwa kikosi hicho utaanza kufanyiwa upembuzi yakinifu katika Bajeti ya 2011/2012 na utekelezaji wake kuanzia mapema 2012 ili hatimaye ifikapo 2014 Kikosi hiki kiwe tayari kuanza kazi kama Jeshi la Ulinzi wa Pwani na Fukwe. Kikosi hiki kitapewa jukumu la kusimamia uhalifu unaofanyika majini usiohusiana na masuala ya mapigano ya kivita.”
Lakini mawazo makubwa ambayo naamini ni mapya sana ni haya yanayohusu Idara ya Usalama wa Taifa na taasisi zinazoshughulikia ukusanyaji wa taarifa za kijasusi.
Kwanza wanasema hivi kuhusu idara hii: Idara ya Usalama wa Taifa inatakiwa kuwa ndiyo chombo ambacho kinaweza kukusanya taarifa za kijasusi na hata kuzuia matukio mbalimbali kabla hayajatokea. Tumeshuhudia kwa miaka zaidi ya 15 idara hii ikiwa imemomonyolewa na kuvurugwa kwa maamuzi ya kisiasa na hivyo kuifanya ibakie kama isiyo na uongozi na uelewa wa kisasa wa majukumu yake.
Mapendekezo yao ya kuboresha na kubadilisha Idara ya Usalama wa Taifa ni ya kimapinduzi sana. Ni mapendekezo ambayo yataifanya idara hiyo kuwa ni ya kipekee katika bara la Afrika.
Wanasema watafanya yafuatayo:
- Kufanyia mabadiliko sheria iliyounda Usalama wa Taifa (TISS) ya 1996 sasa ili kuunda chombo kipya kitakachosimamia masuala ya inteligensia nchini.
- Katika mabadiliko hayo Wakala wa Usalama wa Taifa (National Intelligence Agency) utaundwa na kuwa ndicho chombo cha juu kabisa cha masuala ya inteligensia nchini. Chombo hiki ndicho kitaratibu ukusanyaji, uchambuzi, ugawaji na ufuatiliaji wa taarifa mbalimbali za kijasusi. Mkurugenzi Mkuu wa NIA atapendekezwa na Rais na kupitishwa na Bunge.
- Idara zote hizo za chini ya NIA zitaongozwa na wakurugenzi ambao watateuliwa na Rais na kuidhinishwa na Bunge.
- Makao Makuu ya NIA yatajengwa huko Kigamboni na idara hiyo itakuwa huru kutoka Ikulu. Ujenzi wa Makao Makuu ya Idara hii yatafanywa kwa kushirikiana na Idara ya Uhandisi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania na vyombo vingine vya Usalama.
- Tutapitia mfumo wa mafunzo na upatikanaji wa watumishi wa NIA ili kuhakikisha kuwa wanaoingia katika Idara ya Usalama wa Taifa ni wale tu ambao watakuwa wamewahi kupitia vyombo vya kijeshi na wale ambao watakuwa wameshaajiriwa bila mafunzo hayo kuhakikisha wanapitia mafunzo ya kijeshi kwa utaratibu utakaowekwa.
Tukilinganisha hayo na yale yaliyopo kwa Ilani ya CCM kuhusu masuala hayo ya Usalama wa Taifa tofauti ni kubwa mno. Chama cha Mapinduzi katika Ilani yake hakina mpango wowote rasmi na mahsusi unaoonyesha kutambua changamoto za Idara hiyo wala kulieleza Taifa ni kwa namna gani idara hiyo itabadilishwa na kuwa ya kisasa. Kwa maneno mengine CCM na uongozi wake hawatambui udhaifu uliopo kwenye idara hii. Ninafahamu kisingizio (si sababu) ya kwanza kutolewa itakuwa ni ile ya kuwa hilo ni suala la nyeti na haliwezi kujadiliwa hadharani. Matokeo yake ni mwendelezo wa lile lile lililopo.
Idara ya usalama wa taifa ya nchi yoyote ndiyo mlinzi asiyeonekana wa taifa hilo wakati jeshi la nchi hiyo ndiyo mlinzi anayeonekana. Ni uongozi wenye hekima unaotambua changamoto ya walinzi hao wasioonekana na jinsi gani kutengeneza mazingira ya utendaji wao kazi kukabiliana na changamoto za kisasa.
Wiki ijayo nitajaribu kuangalia tena tofauti katika masuala mengine ya Ilani za CCM, CHADEMA na CUF. Ni katika kuangalia ilani hizo ndipo mpiga kura ataweza kupata mwanga zaidi wa kuelewa ni wagombea wa chama gani wanastahili kupewa nafasi ya kuongoza Taifa.
http://www.raiamwema.co.tz/news.php?d=2555
0 comments:
Post a Comment