na Gregori Nyankaira, Musoma
MTU mmoja aliyejulikana kwa jina la Mwita Marwa Msubi (54) mkazi wa Kijiji cha Kyawazaro, anashikiliwa wilayani Butiama, mkoani Mara kwa kosa la kuchana picha ya mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.
Mkuu wa kituo hicho, OCS Onesmo aliiambia Tanzania Daima kuwa Msubi ambaye ni kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mfanyabiashara wa duka la kuuza nyama, alichana picha hiyo iliyokuwa imebandikwa kwenye bucha hiyo.
Alisema mtuhumiwa huyo badaa ya kuichana picha hiyo mbele ya watu, kiongozi mmoja wa CHADEMA wa Kata ya Kukirango aliyekuwepo eneo la tukio, alipiga simu polisi kuomba msaada ambapo polisi walifika na kumkamata kwa ajili ya mahojiano zaidi.
Alisema katika mahojiano hayo, mtuhumiwa alikiri kuchana picha kwa vile si chaguo lake na kwamba ilibandikwa kwenye bucha hiyo bila makubaliano na uongozi wa CHADEMA.
Kutokana na tukio hilo, mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili pindi viongozi wa CHADEMA wa wilaya watakaporudi kutoka kwenye msafara wa mgombea wao wa urais aliyeko mkoani hapa.
0 comments:
Post a Comment