Waandishi Wetu
ASKOFU mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe jana aliamua kutoa darasa la elimu ya urais kwa waumini wake na kuwataka kutompima mgombea kwa kuangalia matukio kwenye maisha yake ya ndoa.Kakobe, ambaye aliwahi kumpigia debe Augustine Mrema wakati akigombea urais kwa tiketi ya TLP kabla ya kugeuka na kuisifu CCM, alisema maneno hayo jana wakati akihubiri kwenye ibada iliyofanyika kwenye kanisa lake lililo Mwenge, jijini Dar es salaam.
Pamoja na kutotaja jina, mahubiri ya kiongozi huyo shupavu wa kidini yalionekana kumgusa mgombea urais wa Muungano kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa ambaye amekumbwa na tuhuma za masuala ya maisha yake ambazo zimefika mahakamani ambako anadaiwa fidia kwa madai ya kumtangaza mke wa mtu kuwa mchumba wake.
Dk Slaa, ambaye anawania kuwa mgombea wa kwanza kutoka nje ya CCM kuingia Ikulu baada ya utawala wa miaka 49 wa chama hicho kikongwe, amesema yuko tayari kupambana na mashtaka hayo mahakamani na anaendelea kuzunguka na mwanamke huyo kwenye mikutano yake ya kampeni.
Lakini Kakobe aliwaambia waumini wake kuwa masuala kama hayo yameshawakumba viongozi wengi wa barani Afrika na Ulaya lakini waliongoza mataifa yao kwa ufanisi na kuwa na maendeleo hadi leo, akisema huo ni mfano wa kuigwa kwenye nchi zinazoendelea.
Kakobe, ambaye jana alitangaza kufuta ibada zote zilizopangwa kufanyika Oktoba 31 mwaka huu ili kutoa fursa kwa waumini wake kushiriki uchaguzi mkuu, hakumtaja Dk Slaa kwa jina wakati akihubiri lakini alitumia mifano ya viongozi mbalimbali waliowahi kukumbwa na kashfa hizo lakini wakapewa dhamana ya kuongoza nchi zao.
“Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela alikuwa na kashfa ya kuoa na kuacha na hadi sasa mke wake anayeishi naye ni wa tatu, lakini pamoja na kashfa hizo wananchi wake walimkabidhi nchi na amefanya maajabu na kuifanya nchi hiyo kuaminiwa na mataifa makubwa na hata kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia,” alisema Kakobe.
Mbali na huyo pia alimtaja rais wa sasa wa nchi hiyo, Jackobo Zuma kuwa alikumbwa na kashfa ya kumbaka mwanamke aliyekuwa na Ukimwi kabla ya uchaguzi, lakini wananchi hawakuangalia hayo na badala yake waliona kuwa ana kipaji cha uongozi wakamchagua.
Pia alimtaja rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy aliyedai naye alikuwa na kashfa kuoa na kuacha na hata mke wake wa pili alikuwa mke wa mtu, lakini alioa na kuzaa naye mtoto mmoja halafu wakaachana na sasa mwanamke huyo ameolewa nchini Marekani.
Alisema pamoja na kashfa hizo wananchi wa nchi hizo hawakuangalia hayo na badala yake waliwachagua na kuwapa mamlaka ya kuwatumikia na wakafanya vizuri.
Ufafanuzi huo uliwafanya waumini hao kushindwa kujizuia na kushangilia licha ya Kakobe kuzuia watu kufanya hivyo ili anachokizungumza kiweze kueleweka miongoni mwao.
Kuhusu umuhimu wa kupiga kura, Askofu Kakobe alisema hiyo ni haki na wajibu wa kila raia na kusisitiza hata Mungu anataka watu kujichagulia viongozi wao.
Kutokana na msingi huo wa kutambua umuhimu kwa uchaguzi, kanisa hilo limefuta ibada za siku ya Oktoba 31 ili waumini wake wakapige kura na kwamba ibada hiyo sasa zimehamishwa Oktoba 30.
Alisema uamuzi huo unatokana na vikwazo kadhaa vinavyowakwamisha wakristo wengi nchini kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi kutokana na siku hiyo kuangukia Jumapili ambayo siku ya ibada kwa baadhi ya makanisa ya Kikristo.
“Natangaza rasmi kufunga ibada za kanisa hili nchi nzima Oktoba 31 mwaka huu. Siku hiyo itakuwa maalumu kwa ajili ya uchaguzi mkuu kutokana na umuhimu wa kuchagua viongozi wanye sifa za kuongoza taifa hili,” alisema Kakobe.
Katika ibada hiyo Kakobe alitaja vikwazo vitano vya kitaifa vinavyosababisha watu wengi kushindwa kushiriki katika kupiga kura huku akidai vikwazo viwili vinawahusu wakristo pekee.
Alivitaja vikwazo hivyo kuwa ni dhana ya baadhi ya waumini kuamini kuwa viongozi huchaguliwa na Mungu hivyo kutoshiriki katika upigaji kura, hali aliyosema inachangia kupatikana kwa viongozi wabovu.
Alitaja vikwazo vingine kuwa ni dhana potofu ya baadhi ya wapiga kura ambao hudai kura moja haiwezi kubadili matokea; hofu ya kuibiwa kura na imani ya baadhi yao kuwa hata ukichagua viongozi wengine hali haiwezi kubadilika.
“Dunia ya sasa inazungumzia maendeleo na ndiyo maana mataifa yametengwa katika mafungu matatu, maendeleo katika nchi huletwa na kiongozi bora kwa kuwa kiongozi ni kama dereva mkipata dereva rafu atapitisha gari hata kwenye mashimo na mkipata dereva safi ataifikisha gari mahali panapotakiwa kwa usalama,” alisema.
Kwenye mahubiri hayo ambayo Kakobe aliita ni elimu maalum ya urai kwa waumini wake na wa madhehebu mengine, aliwataka wakristo kutochagua viongozi kwa vigezo vya Biblia au uumini wao bali waangalie uwezo wao wa utendaji katika kusimamia misingi ya katiba.
“Kwenye uchaguzi mkuu hatuchagui malaika wa kutupeleka mbinguni bali kiongozi wa kuliongoza taifa... tuchague kwa kufuata kanuni na taratibu za katiba, kwa kuwa viongozi wote wana sifa, kinachotakiwa ni kuangalia nani ana kipaji cha uongozi,” alisema Kakobe.
Kakobe aliwataka wakristo kuhudhuria kwenye kampeni na kusikiliza sera za vyama ili kubaini ahadi na kuzifanyia utafiti kabla ya uchaguzi.
“Wapo wanaosema msichague viongozi kwa majaribio chagueni wazoefu, hizi ni siasa nyepesi... nani kakwambia Ikulu panahitaji uzoefu? Nelson Mandela alipata wapi uzoefu; Barrack Obama amekuwa rais wa kwanza mweusi nchini Marekani, amepata wapi uzoefu,” alihoji Kakobe na kuongeza kuwa anayekataa mabadiliko anakataa maendeleo.
Alisema kila kitu duniani chenye mafanikio huanza kwa majaribio akitoa mfano wa wanasanyansi ambao alisema hawawezi kuruhusu kufanyika kwa kitu bila majaribio.
Geofrey Nyang’oro, Mussa Mkama na Hermenegildus Rwihula
MWANANCHI
Amka Na BBC
46 minutes ago
1 comments:
Kakobe kasema kweli kabisa! CCM inaonekana kutapatapa, wafa maji! Sababu kila siku ccm inatunga mambo binafsi kumuhusu Dr. Slaa! Kweli naamini always losers turn out haters, ccm now are becoming haters showing they have already lost! Mwacheni Dr. Slaa aingie ikulu bwana, we need serious people like him!
Post a Comment