Thursday, September 16, 2010

Elimu ndogo, umaskini chanzo cha kupanga matokeo - Tendwa

na Moses Ng'wat, Mbeya

MSAJILI wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, amesema kutojua faida na mafanikio ya uongozi, umaskini uliokubuhu miongoni mwa wanachama wa vyama vya upinzani, huenda umesababisha baadhi yao kukubali kushawishiwa kupanga matokeo na wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopita bila kupingwa katika baadhi ya majimbo.

Aliyasema hayo jana katika Hoteli ya Beacco, katika kikao chake na waandishi wa habari baada ya kukamilisha ziara yake ya siku mbili iliyokuwa na lengo la kutembelea vyama vya siasa vilivyosimamisha wagombea katika Uchaguzi Mkuu mkoani hapa.

Aliwataka waandishi wa habari kutumia nafasi zao, kutambulisha umma ofisi za msajili za kanda zilizofunguliwa hivi karibuni kwa ajili ya kutatua matatizo yanayowakabili.

Ofisi hizo, zitakuwa na wajibu wa kuhudumia mikoa yote ya Nyanda za Juu Kusini, ikiwemo Mbeya, Iringa, Rukwa, Ruvuma na mikoa mipya ya Njombe na Katavi.

Baada ya kuulizwa swali ni hatua gani zimechukuliwa na ofisi hiyo juu ya kuwepo malalamiko kuwa baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani waliojitoa dakika za mwisho katika kinyang’anyiro cha udiwani na ubunge kulitokana na kuhongwa na wagombea wa CCM, Tendwa alisema ofisi yake kwa sasa haijapokea malalamiko ya aina hiyo na kilichopo ni hisia tu.

Alisema kutokana na udhaifu huo, inawezekana baadhi ya wagombea wa CCM walitumia hesabu kali za kuwanunua baadhi ya wagombea wa upinzani katika baadhi ya majimbo hayo ili wajitoe na wao kupita bila kupingwa na hatimaye kutangaza washindi.

“Mfumo wa uchaguzi uko hivyo maana waliopita bila kupingwa tunaamini kuwa wangeshinda kwa asilimia 51, ni changamoto kwa demokrasia, lakini sheria zipo hivyo, huwezi kwenda kinyume,” alisema Tendwa.

0 comments:

Post a Comment