Thursday, September 16, 2010

Wanaofanya fujo kwenye kampeni wawajibishwe

Thursday, 16 September 2010 11:09

Mkuu wa Jeshi la Polisi,IGP Said Mwema

Katika toleo la leo, tumechapisha habari zinazoonyesha kutokea kwa uvunjifu wa amani katika baadhi ya sehemu za nchi yetu hapo jana kutokana na kampeni za uchaguzi zinazoendelea hivi sasa nchini kote.

Ni matukio ya aibu ambayo lazima yalaaniwe kwa nguvu zote, kwa wahusika kuwajibishwa kwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili kampeni hizo zimalizike kwa amani na utulivu.

Katika tukio la kwanza lililotokea katika Kata ya Nyambiti, Jimbo la Sumve, mkoani Mwanza, walinzi wa CCM wanaojulikana kama ‘Green Guards’, kwa amri ya mratibu wa kampeni wa jimbo hilo, walimshambulia na kumuumiza mwandishi wa gazeti hili, Frederick Katulanda, baada ya kukataa amri ya kuondoka kwenye mkutano wao wa hadhara wa kampeni.

Na katika tukio la pili lililotokea katika Jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro, wafuasi wa vyama vya CCM na TLP walipambana vikali na kusababisha vurugu kubwa iliyozimwa baadaye na polisi.

Pamoja na kwamba chombo chenye mamlaka ya kutoa hukumu juu ya nani hasa wa kulaumiwa katika matukio yote mawili ni mahakama, maelezo na ushahidi uliotolewa kwa polisi na watu walioshuhudia tafrani hizo yanatuthibitishia pasipo shaka kwamba wafuasi wa CCM wanastahili kubeba lawama.

Kwa mfano, katika tukio la Vunjo, wafuasi wa CCM waliokuwa wanamsubiri mwenyekiti wao wa taifa, Jakaya Kikwete, katika kituo cha Himo ili ahutubie mkutano wa hadhara, walichukizwa na kuwepo bango la kampeni la TLP sehemu hiyo, hivyo kufanya jitihada za kuliondoa.

Baada ya vurugu kubwa, polisi waliingilia kati na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), ilithibitisha baadaye kwamba bango hilo lilikuwa hapo kihalali.

Kwamba matukio hayo yameripotiwa polisi na majalada ya kesi hizo tayari yamefunguliwa, inatupatia imani kwamba watuhumiwa wote watapelekwa mahakamani haraka iwezekanavyo ili haki iweze kutendeka. Ikumbukwe kuwa umuhimu wa kuchukua hatua za kisheria unatokana na ukweli kwamba lazima jamii ielewe kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria na kwamba kujichukulia sheria mkononi ni kosa la jinai.

Jambo linalotusononesha ni kwamba vitendo hivyo vya vurugu katika kampeni za uchaguzi vinaturudisha huko tulikotoka, kwa maana kwamba polisi na mahakama kwa kiasi kikubwa viliogopa kuwachukulia hatua wanachama wa chama tawala waliokuwa wanafanya vurugu au wanavunja sheria siyo tu katika kampeni za uchaguzi, bali pia katika maeneo mengine.

Ndiyo maana tunashuhudia ‘wakereketwa wa CCM` wakiachwa kuvunja sheria kwa kuanzisha vijiwe na kufanya biashara katika sehemu zilizotengwa, ilimradi wapeperushe bendera za chama hicho.

Sisi tulikuwa na matumaini makubwa kwamba demokrasia ya vyama vingi imeanza kueleweka na kukubalika katika nchi yetu.

Jana tulisema kupitia safu hii kwamba tayari yalikuwepo matukio yaliyokuwa yanaonyesha pasipo shaka kwamba nchi yetu imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa demokrasia kwa sababu vyama vyetu vya siasa vilikuwa vinashindana kwa hoja badala ya fujo, na kwamba watendaji wa Serikali walikuwa pia wameanza kuielewa dhana ya mgawanyo wa madaraka miongoni mwa mihimili mitatu ya dola.

Tulitoa mifano kadhaa kama ushahidi wa kuwapo hali hiyo yenye kuleta matumaini, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wakuu wa wilaya kuhudhuria na kuwezesha kufanyika mikutano ya kampeni za vyama vya upinzani, kwa maana ya kuwapa ulinzi na huduma nyingine muhimu.

Tulisema hayo ni mafanikio makubwa baada ya safari ndefu iliyoanza wakati wa mfumo wa chama kimoja ambacho kilikuwa kimeshika hatamu kikiwa juu ya Bunge na wananchi.

Tulisema kwamba wakati ule Watanzania hatukuwa huru kwani, kinyume na sasa, tulikuwa haturuhusiwi kuhoji sera au matendo ya watawala waliokuwa wanaendesha Serikali.

Wakati tukiamini kwamba matukio ya jana yalitokea kwa bahati mbaya, hivyo hayatarudiwa tena, tunayo imani kwamba uongozi wa juu wa CCM mara hii utajitokeza hadharani na kuomba radhi.

MWANANCHI

0 comments:

Post a Comment