HIVI mpiga kura wa Manyovu, Mpwapwa, Mbinga au hata katika jimbo jipya la Segerea anahitaji kujua nyumba ndogo (kama zipo) za wagombea wa nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31 mwaka huu?
Kutaka kujua ili iweje? Kuna uhusiano gani wa unyumba wa mgombea na sifa na uwezo wake wa kufanya kazi kama Rais wa nchi yetu, kuifanya Tanzania ipige hatua kubwa ya maendeleo kwa faida ya wananchi wake?
Hakika mpiga kura wa Tanzania kwa wakati huu wa kueleka kwenye uchaguzi mkuu, hahitaji kujua wala kusikia mambo hayo ambayo kusema kweli ni ya kibinafsi mno anayoyafanya kwa wakati wake kama binadamu asiye tofauti na wengine.
Inasikitisha kuona kwamba masuala ya unyumba wa wagombea sasa yamekuwa zaidi ya mtaji kwani yamekuwa silaha ya kubomoana na wanaofanya hivyo wakiamini kwamba inasaidia kuvutia au kushawishi kura za wapinzani wao.
Watu wanaacha kufanya shughuli za maana za kuwaelimisha wapiga kura kuhusu sifa za wagombea wao. Wanaacha kueleza watafanya nini kuipaisha Tanzania yetu iwe na manufaa kwa kila Mtanzania ili aishi kwa amani na kwa maendeleo kulingana na maliasili zilizopo.
Ukweli ni kwamba hakuna binadamu aliye kamili chini ya jua hili linalotuunguza na hili linafahamika na kila mtu. Hakuna atakayekuwa msafi kama uchunguzi wa kina utafanyika kwa kila kiongozi wa nchi hii. Suala hilo la usafi labda tuliache kwa vizazi vinavyokuja si hiki cha sasa.
Madai au kashfa za kweli au za kutengenezwa za wagombea zisitutoe katika azma yetu ya kutafuta viongozi wa kweli wenye uchungu wa kuwaona Watanzania wenzao wanafaidi na rasmilimali za nchi hii. Viongozi wenye upeo na uwezo wa kuifanya Tanzania iwe nchi ya sukari na asali kwa kila mmoja.
Tusidanganyike na wala kujisahau kwamba sasa tuko katika mchakato wa kumtafuta au kuwatafuta viongozi wanaopaswa kutushika mkono na kutuongoza katika kazi pevu iliyoko mbele yetu ya kulijenga taifa letu.
Ni wakati wa kila mmoja wetu sasa kutimiza wajibu wake wa kuwapima waliojitokeza kuomba nafasi za uongozi. Wapimwe kwa nguvu za hoja zao za ujenzi wa taifa hili na historia yao ya uadilifu na siyo kwa hoja zao za nguvu dhidi ya wapinzani wao.
http://www.raiamwema.co.tz/news.php?d=2553
0 comments:
Post a Comment