Tuesday, September 14, 2010

Slaa: Kumrudisha Kikwete ni kulizika taifa kaburini

Aagiza wanasheria CHADEMA kumshtaki Salma Kikwete

na Martin Malera, Mwibara

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amewataka Watanzania kutofanya makosa ya kumrejesha tena Ikulu, Rais Jakaya Kikwete.

Slaa mgombea urais ambaye anaonekana kujenga ushawishi unaoonekana kukitikisa Chama cha Mapinduzi (CCM), alisema Kikwete amekuwa hana uchungu wa kutumia mabilioni ya fedha kwa mambo ya anasa wakati nchi ikikabiliwa na tatizo kubwa la umaskini.

Akitoa mfano wa matumizi mabaya ya serikali ya Kikwete, mgombea huyo wa urais wa CHADEMA ambaye kishindo chake kimesababisha makundi ya propaganda ya CCM yanayohusisha vyombo kadhaa vya habari kuandika habari za kubuni dhidi yake, alisema katika bajeti ya mwaka huu wa fedha (2010/2011) serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 30 kwa ajili ya chai ya vigogo maofisini.

Pia alisema walitenga sh bilioni 20 kwa ajili ya kununulia samani katika ofisi za viongozi wa umma kiwango ambacho alisema kimekuwa kikitengwa kila mwaka hata kama samani zilizonunuliwa miaka iliyopita bado hazijachakaa.

“Nikiwaambia Serikali ya Kikwete ni ya anasa, watu hawanielewi. Mwaka jana walitenga sh milioni 30 kwa ajili ya kujinunulia chai tu maofisini. Wanatenga shilingi bilioni 20 kila mwaka kwa ajili ya kununulia samani za wakubwa.

“Wanatenga fedha hizo kwa anasa wakati Mtanzania wa kawaida hana hata uhakika wa mlo wa siku na watoto wake wanasoma katika mazingira magumu. Huo ni unyonyaji, tuwakatae mwaka huu kwa kuiingiza CHADEMA,” alisema Dk. Slaa na kushangiliwa na umati mkubwa wa watu waliojitokeza.

Akimzungumzia mke wa rais, Salma Kikwete, mgombea urais huyo wa CHADEMA aliwaagiza wanasheria wa chama chake kuanza kumuandalia mashtaka ya matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kumkampenia mumewe.

Slaa alitoa matamshi hayo muda mfupi baada ya Salma kuwasili kwa ndege ya serikali mjini Musoma na kupokewa na msururu wa magari ya serikali akiwamo mkuu wa mkoa, kamanda wa polisi wa mkoa na viongozi wengine wa serikali.

“Mama Salma ni mke wa Rais Kikwete na sisi tuna mkataba na Rais Kikwete, mkewe tunamheshimu. Hata hivyo hana nafasi yoyote kiserikali kutumia fedha na rasilimali za taifa kumfanyia kampeni mumewe,” alisema Dk. Slaa.

Alisema CHADEMA imefikia hatua hiyo baada ya kulalamika bungeni kwa muda mrefu na hata katika kipindi hiki cha kampeni ambapo Salma amekuwa akipita katika maeneo mbalimbali nchini kumfanyia kampeni Rais Kikwete kwa gharama za serikali.

“Jana nilisoma kwenye vyombo vya habari kwamba mke wa Rais wa Zambia, Rupia Banda, amefikishwa mahakamani kwa tuhuma ya kutumia fedha za serikali kumfanyia kampeni za uchaguzi mumewe. Hapa kwetu Mama Salma naye anatumia fedha za umma kumfanyia kampeni mumewe.

“Naagiza wanasheria wetu wa chama, wamfungulie kesi mara moja Salma kwa ufisadi wa matumizi mabaya ya fedha na rasilimali za taifa,” alisema Dk. Slaa na kulakiwa na makofi mazito kutoka kwa umati mkubwa wa wasikilizaji.

Akiendelea alisema Salma akiwa Bunda alifanya mikutano ya kampeni ya kumnadi mumewe na taarifa walizonazo zinadai kuwa aligawa fedha, kanga na vifaa vingine ili kuwarubuni wananchi wampigie kura Rais Kikwete.

Hii ni mara ya pili tangu kuanza kwa kampeni kwa Dk. Slaa kumlalamika kwamba Salma amekua akimfanyia kampeni mumewe kwa fedha za serikali.

Mbali ya kutaka kumfikisha mahakamani mama huyo, Dk. Slaa alitumia nafasi hiyo kuwaambia wananchi kuwa serikali ya Kikwete italifisi taifa kutokana na matumizi mabaya ya fedha za serikali, yakiwemo mabilioni ya fedha yanayotumiwa na mkewe kama vile naye ni kiongozi.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mbunge wa Maswa kwa tiketi ya CCM ambaye sasa ni mwanachama maarufu wa CHADEMA, John Shibuda, aliwaacha hoi wananchi wa Mwibara kutokana na staili yake ya kuzungumza kwa kutumia nahau za vijembe kwa Kikwete, huku akicheza na kuimba kuibeza CCM.

Huku akishangiliwa kwa nguvu na wananchi hao, Shibuda ambaye anawania ubunge katika jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA, aliwataka wananchi hao wasimchague Kikwete kwa madai kuwa serikali yake ni ya wezi tofauti na serikali itakayoundwa na Dk. Slaa aliyoelezea kuwa inajali vipaumbele vya Watanzania maskini.

“Siku zote chafya ya mpishi haiwezi kuzima moto na moto ulioanzishwa na Dk. Slaa, hauwezi kuzimwa na Kikwete.”

“Mimi nilikuwa ndani ya CCM, nikakimbia kutokana na dhuluma na ghiliba zao za ufisadi. Diwani anachaguliwa kwa rushwa, mbunge rushwa, rais rushwa. Ni serikali ya aina gani itakayoundwa katika mazingira ya rushwa ya aina hiyo? Ikataeni CCM,” alisema Shibuda.

Shibuda aliwaacha hoi wananchi hao pale alipoimba moja ya nyimbo maarufu za CCM wa ‘Iyena, Iyena CCM nambari one’ unaotumika kuombea kura.

“Watakuja na wimbo wao hapa wa ‘Iyena, Iyena, Iyena, Iyena, Iyena Iyena, CCM nambari One, wakiwa na maana ya ‘Laleni, laleni, laleni, laleni, laleni, laleni, tuwaibie kura vizuri,’’ aliimba Shibuda huku akicheza jukwaani na kuwaacha maelfu wananchi hao wakiwa hoi kwa kicheko.

0 comments:

Post a Comment