Monday, September 27, 2010

CUF, Chadema zamenyana katika mdahalo

Monday, 27 September 2010 08:39

Salim Said
SERA ya utoaji bure wa elimu na afya jana lilitawala mdahalo wa wagombea ubunge wa CUF na Chadema ambao kwa pamoja walikubaliana kuwa Watanzania hawataweza kupata bure huduma hizo chini ya serikali ya CCM.
Kila mmoja akijaribu kujenga hoja kwenye sera za chama chake, wagombea hao walisema kuwa pamoja na suala hilo kutotekelezeka chini ya chama hicho kinachoongoza serikali, Watanzania wataweza kupata huduma hizo bure iwapo Chadema au CUF itapewa na wananchi ridhaa ya kuongoza nchi.

Mdahalo, uliofanyika juzi usiku kwenye Hoteli ya Movenpick (Royal Palm) na kurushwa moja kwa moja na kituo cha habari cha Independent Television (ITV), haukuwa na wagombea kutoka CCM baada ya chama hicho kuwazuia wanachama wake kushiriki kwenye mdahalo wowote isipokuwa kwa maelekezo.
Mdahalo uliongozwa na mwanataaluma mkongwe wa habari na mawasiliano nchini, Generali Ulimwengu ambaye pia ndiye aliyekuwa mchokozi wa mada katika mdahalo huo.

CUF iliwakilishwa na mgombea ubunge wa Jimbo la Ubungo, Mtatiro Julius na wa Temeke Lucas Limba, huku kwa Chadema ikiwakilishwa na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), John Mnyika (Ubungo), John Mrema (Vunjo), Halima Mdee (Kawe) na Regia Mtema (Kilombero). Pia kulikuwa na wananchi, wapenzi na wanachama wa vyama mbalimbali.
"Naomba nitambue uwepo wa mgombea ubunge wa jimbo la Temeke CUF ambaye amewasili muda si mrefu, lakini pia naomba mwakilishi wa CCM akifika nipate taarifa," alisema Ulimwengu na kufuatiwa na vicheko kutoka kwa watu waliohudhuria.
"Naomba msicheke; nayasema haya kwa sababu nimepata taarifa kuwa, CCM itawakilishwa na Dk Faustine Ndungulilie kwa hiyo atakapofika anione ili nitambue uwepo wake,¡± alisema Ulimwengu lakini hadi mdahalo huo unahitimishwa Dk Ndungulile alikuwa hajafika.

Baada ya wagombea wote kupewa dakika tatu kila mmoja za kujieleza mchokozi wa mdahalo huo alichokoza hoja saba kwa mtindo wa maswali ambayo yalilenga katika elimu, afya, jinsia, ajira, ufisadi, madini na Muungano.
Kuhusu elimu na afya, vyama hivyo vyote vilisema vinakusudia kutoa huduma hizo bure; afya kuanzia kituo hadi ngazi ya rufaa na elimu kuanzia awali hadi elimu ya juu, bila ya kufanya masihara.
"CUF hatuiangalii elimu ya Watanzania kama mzigo, bali tunaiangalia kuwa ni nyenzo muhimu ya kuifikisha Tanzania pale ambapo Watanzania na waasisi wa taifa hili wanataka ifike. Tofauti na CCM ambao wanaiangalia elimu ya Tanzania kama mzigo usiobebeka," alisema Mtatiro.

Mtatiro aliongeza kusema: "Tukishinda na kuingia Ikulu 2010, elimu itakua bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuuu bila ya mjadala. Wapo wanaohoji fedha tutatoa wapi, fedha zipo na elimu na afya bure inawezekana.¡±
"Chini ya CCM asilimia 60 ya bajeti inaendesha serikali kubwa na ya kifahari, lakini chini ya CUF asilimia 67 ya bajeti itaenda katika miradi ya maendeleo na huduma za kijamii. Tutapunguza kama si kufuta kabisa safari za rais nje ya nchi... kama fedha hamna EPA, rada, ndege ya rais zilitoka wapi,¡± alihoji Mtatiro.
"Tunasema chini ya CUF elimu na afya bure inawezekana na fedha zipo lakini chini ya CCM haiwezekani kwa sababu fedha hazipo wanagawana mafisadi."

Mtatiro aliongeza kuwa, iwapo CUF itaingia madarakani hadi kufikia 2013 kila Kata ya Ubungo itakuwa na Zahanati yake iliyokamilika na hatahitajika mzazi kwenda kuteseka Mwananyamala.
Naye Zitto alisema: "Elimu bure na afya inawezekana chini ya serikali ya Chadema kwa kuwa fedha zipo. Asilimia 25 ya fedha inapotea kwa misamaha ya kodi; kuna vyanzo vingi vya fedha havitumiki, huwa tunavionyesha katika bajeti kivuli ya kambi ya upinzani.

"Lakini kama Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliweza kuwasomesha bure na kuwatibu bure Watanzania kwa pamba, kahawa na chai, sisi tutawasomesha na kuwatibu Watanzania kwa dhahabu, tanzanite na gesi asilia, inawezekana," alisisitiza Zitto.
John Mrema wa Vunjo alisema: "Chadema ina mfano... Halmashauri ya Tarime inayoongozwa na chama chetu imeweza kulipia ada wanafunzi kwa miaka yote iliyoongoza kuanzia 2007. Lakini tutajenga maktaba katika kila shule na rais atakuwa na ratiba maalumu ya kukutana na kusoma pamoja na wanafunzi hao katika maktaba hizo.¡±
Alisema elimu ya Tanzania inakabiliwa na matatizo kutokana na shule kutelekezwa na serikali iliyo madarakani, kudhalilishwa kwa taaluma ya ualimu, Watanzania kutojengewa uwezo wa lugha za kigeni hasa Kiengereza na mimba za utotoni kwa wanafunzi.

"Tukiingia Ikulu, kwanza tunashughulikia haya," alisema Mrema.
Naye John Mnyika alisema kwa muda mrefu amekuwa akifuatilia suala la matatizo ya afya kwa akinamama wajawazito kutozwa michango au kutakiwa kugharimia vifaa wakati wa kujifungua, lakini hana meno ya kutosha kuzuia.
"Nipeni meno nikasimamie fedha zenu na matatizo haya katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa sababu hata mabadiliko yaliyofanywa Mwananyama hayaridhishi," alisema Mnyika.

Kuhusu ajira, Mnyika ilisema itabadilisha uchumi wa Tanzania kwa kuimarisha na kuboresha kilimo, viwanda, elimu na kushusha gharama za maisha ili kila Mtanzania awe haki na uwezo wa kufanya kazi apate ajira.
Naye Mtatiro wa CUF alisema serikali yao itaimarisha viwanda vya kusindika matunda, viwanda vya vifaa vya ujenzi ili kutoa ajira na kwamba wale ambao hawana elimu serikali, itawajengea vyuo vya ufundi na kugharamia mafunzo yao.
Kuhusu jinsia Chadema ikiwakilishwa na Regia Mtema anayegombea Kilomberoa ambaye alisema serikali yake itahakikisha kwanza inatambua uwepo wa jinsia na makundi mbalimbali ya watu hasa wanaohitaji uangalizi maalumu.
"Tutawashirikisha katika vyombo vya uongozi kupitia nafasi maalumu na kuwawekea mikakati maalumu ya kuwaendeleza kielimu na kifikra ili wapate kujitambua na kujikomboa," alisema Mtema.

Mgombea ubunge wa Temeke kwa tiketi ya CUF, Lucas alisema serikali yake itatunga sheria maalumu na kali za kudhibiti aina zote za unyanyasaji wa kijinsia na kuhakikisha wazee na wastaafu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wanapata stahili zao miezi sita tu baada ya kuingia madarakani.
"Serikali ya Profesa Ibrahim Lipumba itahakikisha kuwa ndani ya miezi sita ya kwanza inawapatia maslahi yao wazee wastaafu wote wa Afrika ya Mashariki ambao wananyanyaswa na serikali ya CCM na pia tutatoa elimu maalumu kwa makundi haya ya watu wanaohitaji uangalizi maalum," alisema Lucas.

Kuhusu hoja ya ufisadi, Lucas wa CUF alisema jambo la kwanza baada ya serikali yake kuingia madarakani ni kuhakikisha inapambana na mapapa na masangara wote wa ufisadi.
"Jambo la pili ni kuipa meno (Taasisi ya Kuzuiya na Kupambana na Rushwa) Takukuru na tutaiweka chini ya Bunge badala ya rais... itawajibika kwa Bunge na si rais, ili masangara na mapapa wa ufisadi waliopo Ikulu wapate kuchomolewa," alisema Lucas.


Naye Halima Mdee wa Chadema alisema chama chake kina rekodi nzuri ya kupambana na ufisadi na kwamba ikiingia madarakani itabadilisha sheria ili kuhakikisha mali za umma na madaraka hayatumiki vibaya.
"Tutaifanya Takukuru iwe inawajibika kwa Bunge na kuweka mazingira hata kama rais anataka kufanya mabadiliko ya wakuu wa Takukuru hadi yaidhinishwe na Bunge," alisema Mdee ambaye ni mgombea wa ubunge wa Jimbo la Kawe.
Kuhusu hoja ya madini na rasilimali za taifa, Zitto alisemea Chadema imefanya kazi nzuri katika kulinda rasilimali na madini nchini na kwamba yeye ni muathirika wa mapambano hayo baada ya kusimamishwa ubunge kwa miezi mine kutokana na kuhoji suala la Buzwagi.

"Tukiingia Ikulu tutahakikisha mambo haya yanaingizwa katika sheria, mrabaha wenye tija kwetu; mgawanyo wa mapato kwa vijiji vyenye madini; kuundwa kwa mfuko wa madini na kuundwa kwa mamlaka ya madini ili kumwondolea mamlaka kupita kiasi Waziri wa Nishati na Madini," alisema Zitto.
"Pia tutahakikisha sheria ya mafuta na gesi inatungwa haraka iwezekanavyo."

MWANANCHI NEWS PAPER

0 comments:

Post a Comment