Wednesday, September 15, 2010

Arcado Dennis Ntagazwa: Yatima mlala njaa na mchunga mbuzi aliyegeuka kigogo kitaifa

Mwandishi Wetu
Septemba 1, 2010
Ni askari wa mwavuli aliyekwepa kununua nyumba ya Serikali
Sasa atimkia CHADEMA na kuwania ubunge Muhambwe, Kigoma

AGOSTI 16, mwaka huu, Mwandishi Wetu, Godfrey Dilunga, alifanya mahojiano na Arcado Dennis Ntagazwa, aliyekuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Pili na ya Tatu. Aliwahi kuvuliwa uraia na baadaye kukata rufaa na kushinda kesi. Katika mahojiano hayo, Ntagazwa ambaye amehama CCM kwenda CHADEMA na kuteuliwa kugombea ubunge Jimbo la Muhambwe, Kigoma, anazungumzia masuala mbalimbali na kushauri kuhusu mwelekeo wa Taifa…endelea.

Raia Mwema: Kwa faida ya wasomaji wasiokufahamu kwa undani, tueleze kwa muhtasari historia yako.

Ntagazwa: Naitwa Arcado Dennis Ntagazwa. Nilizaliwa Desemba 4, 1946. Ni mtu mzima kimsingi, sidhani kama ni kijana, isipokuwa ukienda kwa Wakorea msemo wao kwamba ujana huanzia miaka 60 basi kwa Wakorea nina miaka yangu minne ya ujana kwa maana hiyo.

Lakini pia tunao msemo katika lugha yetu ya Kiha walituachia wazee wetu wanasema; asazugomba, kusaza ni kuzeeka, kugomba ni kutaka.

Kwamba ukitaka kuzeeka utazeeka lakini kama hutaki hautazeeka, hiyo ndiyo maana ya wazee wetu na nadhani walitaka kutuambia uzee dawa.

Kwa upande wa elimu namshukuru Mungu pamoja na kwamba nimekuwa kwa kudura za Mwenyezi-Mungu kwa sababu marehemu baba yangu Ntagazwa alifariki wakati mimi natambaa.

Na mama kaniacha nikiwa na miaka kati ya mitano au sita kwa hiyo Mungu aliwapenda zaidi wazazi wangu lakini aliwapa watu wenye mapenzi mema moyo wa kumlea huyu kichanga wa Ntagazwa na mkewe walionitangulia mbele ya haki.

Raia Mwema: Pengine kabla hujaendelea, kwa hiyo ulilelewa na mmoja wanafamilia kutoka kwa mmoja wa wazazi wako?

Ntagazwa: Sisi katika mila na desturi zetu tulikuwa na kaka yetu mkubwa katika maana pana kwa sababu mama yake na huyo kaka yetu aliolewa na marehemu baba.

Sasa yeye (kaka) alikuwa ni mtu mzima ana wake zaidi ya mmoja na kwa mila zetu sisi mke mkubwa ndiye anapewa jukumu la kulea kama ilivyotokea kwangu mimi wazazi wangu wote walipofariki na kaka mkubwa akachukua jukumu la kunilea.

Sasa Mwenyezi Mungu wa ajabu na ndiyo maana nasema matendo yake yanatisha kama nini. Mke mkubwa huyo wa marehemu kaka yetu aliyechukua jukumu la kunilea alikuwa ni mama mwema sana kwa sababu alikuwa na wanawe wakubwa tu kama wa miaka 18 na kuendelea.

Kwa hiyo mimi nilikuwa kama kitoto chake kichanga, alinipenda sana mama yule Mwenyezi Mungu amrehemu. Lakini naye nilipofika darasa la pili mama yule naye Mwenyezi-Mungu akamwita.

Kwa hiyo ukawa utaratibu ule ule mke mkubwa zaidi kati ya wale wake zake kaka waliobaki akapewa jukumu la kunilea, yeye alikuwa na wanawe karibu wa rika langu.

Kwa kweli hapo sasa niliipata joto ya jiwe wanasema, kwa sababu kwa kweli moja ya vitu ambavyo vilifanya nikaanza kwenda shule ya bweni kuanzia darasa la tatu hadi namaliza chuo kikuu ni kwa sababu mama yule kwa kuwa alikuwa na watoto wa rika langu nilikuwa nikienda shule kwa kawaida darasa la pili, sisi mwaka 1956 tulikuwa tunaanza masomo kipindi cha mchana baada ya saa sita.

Sasa nikienda shule atawapikia wanawe watakula chakula cha mchana, mimi nikitoka shule naambiwa nikachunge mbuzi, nitakapotoka kuchunga mbuzi tayari wanakuwa wamekwishakula chakula cha jioni.

Kwa hiyo yalikuwa maisha magumu kwa maana hiyo lakini namshukuru Mungu alinipa akili sana kwa wakati huo.

Raia Mwema: Turejee katika elimu sasa.

Ntagazwa: Nilisoma shule ya Msingi inaitwa Kizazi Primary School mwaka 1955 na 1956, mwaka 1956 mwishoni nikaenda kusoma Shule ya Msingi Kabanga wilayani Kasulu darasa la tatu na la nne zote za bweni.

Sasa hiyo ilinipa wanafamilia na wanajamii pale kidogo kwa sababu nilikuwa sipo muda mrefu nyumbani, ninapokuja likizo wanakuwa na hamu ya kuniona lakini ukishapita mwezi tena yanarudi yale yale (kukosa chakula) lakini ilikuwa ndiyo nakaribia kurudi shule baada ya likizo.

Na nilisoma kwa taabu kwa sababu sikuwa na mtu wa kunilipia ada kwa sababu mimi kaka yangu mkubwa aliishia darasa la nne na kwa kweli alikuwa anahangaika sana kutafuta fedha nisome.

Mara alikuwa anakwenda kufanya vibarua Uganda kwenye mashamba ya miwa mara atakwenda kufanya vibarua manamba kwenye mashamba ya mikonge kule Tanga kwa hiyo nilikuwa kama ninavyosema Mwenyezi Mungu alikuwa ananipenda. Kulikuwa na baadhi ya watu wenye nia njema walioamua kuchukua mahala pa wazazi wangu waliokuwa marehemu kwa wakati ule.

Kwa hiyo, baada ya masomo pale Kabanga, nilikwenda darasa la tano na la sita Ujiji-Kigoma, hii ni seminari ndogo, ambako nilisoma darasa la tano na la sita mwaka 1959 na 1960 na baada ya hapo niliendelea na seminari darasa la saba hadi la 12 Seminari ya Mtakatifu Joseph Kaengesa Sumbawanga.

Kwa hiyo Kabanga-Ujiji-Kaengesa hadi darasa la 12 sikuendelea na seminari baada ya hapo nilikuja darasa la 13 na 14 Saint Francis College ilivyokuwa inaitwa siku hizi ni Pugu Sekondari.

Baada ya hapo nilikwenda Jeshi la Kujenga Taifa Mkuyu-Handeni, Tanga na Oljoro Arusha kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Makerere kwa ajili ya mafunzo ya shahada ya sheria.

Raia Mwema: Baada ya safari ya kielimu, kwa faida ya wasomaji turejee safari yako ya kikazi baada ya elimu ya Makerere.

Ntagazwa: Baada ya kumaliza Chuo Kikuu nilibahatika kwa kweli kufanya kazi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais na Waziri Mkuu nilikuwa Idara ya Usalama wa Taifa.

Nashukuru Mungu nilifanya kazi na kiongozi wa Idara hiyo mwadilifu na makini sana (sasa marehemu) Emilio Charles Mzena.

Raia Mwema: Kumbukumbu gani au kuna jambo gani kubwa kutoka kwa marehemu Mzena linalokufanya uamini moja kwa moja alikuwa mwadilifu.

Ntagazwa: Ngoja nikwambie. Unajua Idara ya Usalama wa Taifa ndiyo roho ya nchi na zile taarifa ambazo chombo kile kinakusanya na kuzichambua na kuziwasilisha kwa viongozi wakuu wa nchi ili wafanye uamuzi ndizo zinafanya nchi iheshimike na kiongozi ajue nchi inaelekea wapi na huyu baba alifanya kazi hiyo vizuri sana.

Nakumbuka wakati mmoja alikuwa ananiambia na aliniambia ilikuwa inafika mahali wakati ule Rais ni Mwalimu Nyerere.

Anamwambia ndugu Rais…wakati ule ilikuwa ndugu si mheshimiwa. Kwa hiyo anamwambia ndugu Rais hawa mawaziri wako wanaokwenda kunywa pombe kwa vilabu wanaropoka siri za serikali na wahudumu wa baa na kitu kama hicho mimi utakuta nimekwishawafungia kwenye nyumba za idara za usalama utakuja kuwachukua huko.

Kama wanataka kunywa pombe zao na mambo mengine wakanywe pale Leaders Club (eneo mahususi kwa viongozi Kinondoni-Dar es Salaam, kwa wakati huo) pale watakuwa wanaongea wao kwa wao.

Hiyo inalinda heshima ya serikali na vyombo vyake, siri za serikali hazitavuja kama leo hii. Mimi nadhani gazeti mojawapo nadhani liliwahi kuandika kwamba waziri mmoja wa awamu hii anakwenda kunywa pombe anaropoka na kusema ngojeni nitakapokuwa Waziri Mkuu mtanikoma.

Aah, sasa kwani uwaziri ni kukomoana au kutumikia watu?

Raia Mwema: Kwa hiyo kigezo hicho ndicho dhahiri kinakufanya umkumbuke Elimio kama mwadilifu na mwenye msimamo kikazi asiyebabaishwa na matakwa binafsi ya viongozi.

Ntagazwa: Naam, ni kigezo ambacho nilimwona yule Emilio Mzena kama kiongozi mwadilifu sana.

Raia Mwema: Lakini wanasema wakati mwingine Idara ya Usalama wa Taifa ubora wake unategemea vile vile yule aliyepo juu kwa maana ya Rais…kwamba anafanyia kazi taarifa za idara hiyo au anazipuuza na kufanya anayotaka na hatimaye kuvuruga baadhi ya matarajio ya nchi.

Huoni kwamba wakati ule Mwalimu Nyerere alikuwa mtiifu kwa idara hii na ndiyo maana kulikuwa na udhibiti mkubwa wa maadili?

Ntagazwa: Ni kweli kwamba na Mkuu wa nchi naye alikuwa ni mwadilifu lakini pia zile taarifa za chombo alikuwa anazisoma kwa umakini mkubwa na nina uhakika pia alikuwa na washauri makini sana na waadilifu pale alipokuwa na shaka.

Alipokuwa na shaka kuhusu masuala fulani aliomba ushauri bila hata kuwaonyesha taarifa hizo lakini ni kitu anasema nina suala hili sasa ningependa ushauri wenu.

Mwalimu Nyerere alikuwa na kawaida anamwambia Katibu wake, Joseph Butiku…Joseph hivi mzee Sengerema mnajua yuko wapi…mimi ningependa siku moja ninywe chai naye…ni agizo atatafutwa yuko wapi, kama yuko Mwanza ataulizwa mkuu wa mkoa ataambiwa mkuu wa mkoa mtafute mzee nadhani alikuwa mkoani Tabora yule Mzee Sengerema.

Mtafute huyu mzee Mwalimu Mwalimu anataka kuonana na wewe. Watafanya utaratibu watamsafirisha na watamwambia si kwamba kuna jambo lolote la kutisha au la ajabu usije ukafa kihoro…watamwambia unajua ninyi na Mwalimu ni watu wa rika moja, pengine kwa sababu Mwalimu ni mpenzi wa bao anapenda mcheze wote akafunge.

Kwa hiyo atakuja na akija yule mzee Mwalimu kama anakitu ni kweli watakunywa chai au watakula chakula lakini kwenye maongezi kama kuna kitu atamwambia hivi Mzee Sengerema katika hali ya namna hii mlikuwa mnafanyaje…alikuwa anatafuta ushauri kwa namna ya kawaida kabisa lakini anajua anatafuta ushauri kwa mtu ambaye atampa ushauri wa kweli na wa hali halisi katika hali aliyomweleza.

Nadhani viongozi wengi wanafanya hivyo, najua, ni imani yangu, lakini kama hawafanyi hivi ni shauri yao wenyewe.

Raia Mwema: Lakini wanasema kwa hali ilivyo sasa Idara hii ya Usalama uliyowahi kuifanyia kazi wakati mwingine inatumika kuandaa taarifa za majungu ili kuwakomoa watu fulani fulani?

Ntagazwa: Wala sio uongo. Unakumbuka wakati mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995 iliendeshwa kesi Mahakama Kuu kwamba Ntagazwa si raia.

Kipindi hicho Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ndiye alikuwa kiongozi wetu. Kwa bahati nzuri kipindi hicho mpaka leo ninao rafiki zangu kwenye Idara ya Usalama wa Taifa.

Kwa sababu nasema ni bahati kufanya kazi pale, ukichanganya na kusoma seminari na kufanya kazi pale maisha yakikuchachia kosa ni lako, huna wa kumlaumu ni wewe wa kujilaumu.

Maadili ya kiroho umefunzwa, utendaji kazi serikalini hata kabla hujaingia serikalini umekwishaufahamu. Sasa katika kesi ile, nakumbuka nilisingiziwa kwamba marehemu mama yangu alionekana akitokea Burundi kanibeba mgongoni.

Lakini kesi ile ilikuwa ya kutunga na yuko mama yetu mkubwa hata majuzi wakati wa tarehe mosi mwezi huu (Agosti) nilibahatika kumwona. Yule mama ana miaka zaidi ya 120 sasa hivi, bahati mbaya haoni lakini anatembea na anasikia na kuelewa nani anayezungumza naye…yuko kijijini.

Wakati wa kesi ile aliniambia wewe hivi mwanangu wanaosema marehemu mdogo wangu walimwona akiwa anatoka Burundi amekubeba wewe mgongoni mbona hawakuja kuniuliza?

Siku unazaliwa wewe nilikwenda pale kwenye kitongoji alichokuwa ameolewa mama yako, nimemkuta marehemu baba yako anahaha, hapakaliki kwa sababu mdogo wangu alikuwa katika uchungu wa kukuzaa wewe.

Nilipotokea akasema namshukuru Mungu ndiye amekuleta kamhudumie mdogo wako yuko katika uchungu wa kujifungua. Mimi ndiye nimekukata kitovu, kitongoji kile pale cha Kasana, kijiji cha Nyarugusu, wilayani Kibondo, nani anasema wewe umezaliwa Burundi?

Nikamwambia mama yangu wale walikuwa kwenye mradi wa fedha na ni kweli kabisa zilikuwa zimetumika kama Sh milioni 200 kwa kazi hiyo ya kusema mimi si raia.

Raia Mwema: Kwa nini unaamini walikusingizia, unadhani walikuwa wanalenga nini?

Ntagazwa: Walichokuwa wanalenga baadaye niliambiwa. Unajua nimekwambia nilikuwa nimekua kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa ananipenda, amewapa watu wema kunilea kama mtoto wao, kwa hiyo mimi napenda watu.

Na kwa sababu napenda watu, sipendi kuona watu wakionewa. Sasa katika lile pori la Moyowozi, mimi nilikuwa nasema wananchi wanaokaa vijiji vya jirani na pori lile wafaidike na shughuli zinazofanyika kule na hiyo ndiyo sera ya serikali kwamba rasilimali za Taifa zitumike kupambana na maradhi na ujinga.

Kwa hiyo mimi nikatetea watu wanufaike, sasa, baadaye na kwa sababu wakati huo nilikwishakuwa Waziri wa Ardhi, Maliasili na Utalii najua nini kinaendelea. Unapewa kibali cha kwenda kuwinda wanyama kadhaa, mwindaji au mwenye kitalu kile anawawindisha wale wawindaji aliowaleta zaidi ya idadi ya wanyama walioorodheshwa na kwa maana hiyo huo ni wizi wa rasilimali zetu.

Na mwananchi hapati kile kiasi kinachotakiwa. Sasa mimi kwa kuamua kulizungumzia hili ikaonekana huyu bwana namna ya kumnyamazisha kwa sababu anasema bungeni, ngoja tuseme si raia ili atoke bungeni. Sisi tuendelee kufanya mambo yetu ndiyo ilikuwa jambo hili.

Raia Mwema: Aliyekuwa nyuma ya mpango huo bila shaka alikuwa mtu mzito. Je, alikuwa mwanasiasa au mfanyabiashara?

Ntagazwa: Wakati huo alikuwa mfanyabiashara, siku hizi ni mfanyabiashara na mwanasiasa mkubwa tu nafikiri ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Sitaki kumtaja mimi ni mwanasheria.

Lakini si hayo tu. Unajua baada ya ile kesi Kigoma kuamuliwa kuwa Ntagazwa si raia na kuondolewa kwenye ubunge nilifanya mchakato wa kupinga, kukata rufaa, nikaenda Mahakama ya Rufaa ikasema kesi ile ilikwenda kienyeji mno kwa hiyo tunarudi katika hali ya kabla ya uamuzi wa Mahakama Kuu iliyoketi Kigoma kwa hiyo nikarudi kuwa mbunge.

Niliporudi bungeni nikachaguliwa kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria na baadaye pia nilichaguliwa na wabunge wenzangu kuwa Mwenyekiti wa Bunge, naendesha vikao vya Bunge, siku moja sasa ndiyo nakuja kwenye lile suala la taarifa za ovyo za chombo hiki (Idara ya Usalama wa Taifa).

Siku moja (mwaka 1998, baada ya rufaa ya kesi kukamilika mwaka 1997) wakati naendesha Bunge mheshimiwa Waziri Mkuu Sumaye (Frederick) kaniletea kiji-note…mheshimiwa Ntagazwa baada ya kuahirisha Bunge naomba tuonane nyumbani. Sasa kwa sababu unaendesha Bunge inabidi uwe makini sana pale kwenye kiti, nilichokifanya baada ya ile note ni kumtazama Waziri Mkuu alipokuwa ameketi na kuinamisha kichwa kuonyesha kwamba nimepokea ujumbe wake.

Lakini naona Mheshimiwa Waziri Mkuu haikutosha ile, akaniletea kwa kutumia wale wahudumu wa Bunge maandishi na nilipoletewa pale mezani nikafungua….ni taarifa ya usalama, uraia wa mheshimiwa Ntagazwa.

Niliposoma hivi kichwa cha habari, nilimtazama kwanza Waziri Mkuu aone kwamba nimeipokea, nilipomtazama hivi nikaiweka pembeni (ile taarifa) literary kwa Kiingereza sikuitilia maanani taarifa ile kwa nini kwa sababu wakati ule nadhani ilikuwa kwenye Bunge la mwezi wa 10 au 11 hivi, taarifa ile ni ya uongo iliandikwa na mtu mmoja ambaye nadhani alikuwa bado haamini ushindi wangu kwenye Mahakama ya Rufani hapana kwa sababu ya fedha zilizotumika kuniondoa bungeni.

Sasa taarifa ile mimi nilikuwa nayo tangu mwezi wa nne na ndiyo maana nilipoletewa kwenye mwezi 11 (bungeni na Waziri Mkuu) niliona si lolote si chochote, lakini pia marafiki zangu wakati ule walikuwa wamesema bwana ee sisi tumeambiwa hili suala kwamba Ntagazwa si raia halitakiwi kusikika serikalini si kweli walikwishagundua kuwa ilikuwa hadithi ya kutunga.

Ndiyo nakuonyesha sasa kwamba Idara ile nayo inatumika lakini si hilo tu, Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa wakati ule alikuwa bwana Apson aliniambia bila uficho…Idara ilikuwa wakati wenu (Ntagazwa) na Mzee Mzena.

Raia Mwema: Alidiriki kusema hivyo bila kujali ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara?

Ntagazwa: Ndiyo, aliniambia. Sasa hivi bwana ukituletea taarifa ukiwapa vijana wetu ukasema nao vizuri wataandika taarifa ya ovyo dhidi yako na itapelekwa serikalini.

Sasa nikasema balaa gani hii kwa sababu kile chombo ndiyo roho ya nchi. Ndiyo roho ya serikali, na unasikia siku hizi nani kapeleka hela wapi utadhani ni sadakalawe kama alivyowahi kutueleza Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, pata pataye.

Kwa hiyo kuna vitu vinaogofya kusema kweli, lakini nadhani wanajitahidi lakini bado wamsaidie sana kiongozi wetu (Rais).

Raia Mwema: Kwa uzoefu wako, unadhani nini hasa kimesababisha kupwaya kwa hii Idara ya Usalama wa Taifa kiasi hicho kwa mujibu wa maelezo yako? Nini kimetokea..

Ntagazwa: Nadhani, unajua Baba wa Taifa, nadhani alikuwa anaongozwa na Mwenyezi Mungu. Unajua aliwahi kutuambia hivyo hivyo, alisema ukikuta dimbwi la maji ya mvua, chukua glass ya maji chota kutoka kwenye hilo dimbwi, maji yale hayatakuwa na tofauti na maji yaliyobaki kwenye dimbwi.

Hawa maofisa wa usalama wa Taifa si wanatoka kwenye jamii yetu. Jamii ya Watanzania leo ikoje? Huwezi ukasema ni jamii ambayo tuna uchu wa kuzingatia maadili, ukweli, uadilifu na mema yale unayoweza kusema hapa yapo maadili ya kumpeleka mtu kwa Mwenyezi-Mungu muumba wake. Sidhani kama unaiona hiyo wazi wazi.

Raia Mwema: Katika mazingira hayo, tufanye nini kama Taifa?

Ntagazwa: Katika mazingira haya ambayo maadili yameporomoka ni kama vile utu hauthaminiwi kama ule msemo wa hapendwi mtu inapendwa pochi. Hapendwi mtu kinachopendwa ni fedha. Kinachotakiwa mimi kwa maoni yangu kwa kweli si mapinduzi lakini kuna kitu wanaita moral rearmament sasa Kiswahili chake kwamba katika maadili haya ya dunia na ahera, kuwe na kitu kama mwamko mpya ili ile jamii ithamini utu wa kila mtu na katika kuthamini utu wa kila mtu pia iainishwe kwamba sisi binadamu ni viumbe wa Mwenyezi Mungu.

Raia Mwema: Lakini nani atakayefanya hayo yote, wakati karibu wote tunaonekana tumepotoka kimaadili, tukiongozwa na viongozi.

Ntagazwa: Itabidi wajitokeze wachache wa kujitoa si mhanga lakini kujitoa sadaka kwa sababu tunajua wewe na mimi tukichunguza dhamiri zetu tunajua kwamba tumepotoka.

Sasa tunahitaji watakaokuwa majasiri wa kusema upotofu huu si sawa na waliseme bila haya, bila kuchoka. Ni lazima tuanze mahali.

Raia Mwema: Wapi pa kuanzia kusema hayo kutoka kwa vinywa vya majasiri unaozungumzia. Je, ni kutoka kwenye dini, siasa, taasisi za elimu au wapi?

Ntagazwa: Mimi nadhani tuanzie kwenye taasisi za elimu kwa sababu huko ndiko tunajenga Taifa la leo, kesho na keshokutwa. Najua utaniuliza huko kwenye taasisi za elimu walimu je?

Walimu si hawa wa vodafasta, bado tunao waalimu wastaafu ambao walitufundisha sisi, bado tunao. Lakini lazima tuanze mahali, hatuwezi kuendelea hivi halafu tukajidanganya eti tuko salama kitaifa.

Raia Mwema: Tuje kwenye siasa ingawa tumegusia kidogo. Umewahi kuwa mbunge, waziri na kuwahi kufanya kazi na watu wenye uchungu na nchi ambao baadhi wengine sasa hivi wamegeuka mafisadi, wakiwamo waliowahi kuwa karibu na Mwalimu Nyerere. Unazungumziaje ‘kizunguzungu’ hiki.

Ntagazwa: Kwanza, namshukuru Mungu nimebahatika kufanya kazi chini ya uongozi wa mwasisi wa Taifa letu, Mwalimu Nyerere na kweli kipindi kile nilikuwa mchanga mwaka 1983 nina kama miaka 10 tu nimetoka Chuo Kikuu akaniteua kuwa Naibu Waziri wa Fedha, Waziri akiwa Cleopa Msuya.

Nimefanya kazi pale kusema kweli nashukuru ilikuwa ni shule kubwa ni mahali ambapo nimejifunza mengi.

Moja ya vitu ninavyokumbuka pale wakati ule kuingiza kompyuta nchini ilikuwa lazima vikao vifanyike. Watalaamu kama ninyi ilibidi mkae vikao kwanza.

Mnakaa kwanza wataalamu mnasema huyu anaingiza kompyuta nchini kwa nini na anastahili au hastahili. Mkishamaliza ninyi wataalamu taarifa kikao lazima zije katika dawati la Naibu Waziri atie saini kwamba anaruhusiwa kama mlivyopendekeza wataalamu.

Raia Mwema: Huo ni mchakato unaohusu kuingiza kompyuta za wizara?

Ntagazwa: Hapana ni za wataalamu wa nje waliokuwa wamekuja kufanya kazi za Serikali nchini. Ilikuwa wataalamu wa nje hawaruhusu kuingia na kompyuta mpaka kamati zikae na kujadili.

Sasa baada ya kufanya kazi na Mwalimu, nilibahatika pia kufanya kazi na Mzee Ali Hassan Mwinyi, ni kiongozi ambaye alijitahidi kufanya kazi vizuri.

Unajua nasema kwenye siasa ukali pia unatakiwa lakini usiwe mkali kama nyati aliyejeruhiwa, uwe mkali katika kusimamia misingi hasa ya kutekeleza sera, sheria, kanuni na taratibu, mtu akikiuka mnapambana.

Nilikuwa nasema hivi nilipokuwa serikalini, kuna makosa ya aina mbili. Kuna makosa ya makusudi, hayo hayana maelezo lakini kuna makosa ya kibinadamu kwamba unatarajia katika uamuzi huu tuliofanya matokeo yatakuwa A na uamuzi ule ummeufikia baada ya kuangalia maeneo yote, wanaita scenarios zote na mkakubaliana kwamba tunaamua A na tunarajia matokeo yatakuwa B.

Inakuja kutokea matokeo sio B wala C pengine yanakuwa D lakini kwa sababu mlikwenda kwa utaratibu unaojulikana ambao yeyote angefanya uamuzi kama mlioufanya maamuzi yake yanamaelezo yanayoweza kueleweka.

Lakini makosa ya makusudi unaamua kufanya uamuzi nje ya sheria, kanuni na utaratibu. Utamweleza nani kwamba kosa hili hukulifanya kwa makusudi na kwa malengo mahususi unayoyajua wewe. Haya ndiyo makosa ya makusudi.

Sasa kuna viongozi wengine ni wapole na waadilifu mpaka ukasema pengine siasa si eneo lao kwa Kiingereza ukasema it’s not their way of calling.

Siku moja atanisamehe Makamu wa Rais na mgombea urais wa Zanzibar nimewahi kufanya naye kazi kwa miaka mitano nikiwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira.

Nakumbuka ataniwia radhi lakini si vibaya kusema, nilimwambia mheshimiwa makamu (wa rais) mi nadhani kati ya watakatifu waliopo hapa duniani wewe ni mmojawao.

Ndiyo, baba yule ni mwadilifu, ni mtaratibu hutosikia anapayuka hata kidogo, tunao watu wa namna hiyo. Ni tunu kutoka kwa Mwenyezi Mungu mnapopata viongozi wa namna hiyo.

Raia Mwema: Lakini huo uadilifu na upole tafsiri yake ni nini kwenye masuala ya uongozi, na hasa uongozi tunaotarajia utoe tija kitaifa.

Ntagazwa: Unajua kitu kimoja kizuri, ukiwa na kiongozi mwadilifu, mpole…mtakatifu kama nilivyosema hivi utakapofanya makosa ya makusudi utathubutu kumtazama hata machoni? Hali yake hiyo ya uadilifu…tuseme kama hali ya ukamilifu hivi utathubutu kufanya mambo ya ovyo ukiwa chini ya uongozi wake na ukamtazama usoni…si rahisi kwa sababu uso umeumbwa na haya?

Wanasema ukitaka kujua kama mtu anasema uongo wewe mtazame machoni…ana kwa ana…sasa wewe una kiongozi mwadilifu pengine mtakatifu hivi…mkamilifu, wewe unafanya madudu yako, wanaita mchoro, unafukuzia rushwa na uchafu mwingine katika eneo analoongoza utathubutu kufanya hivi?

Kwa hiyo ule uadilifu wake unafanya na wale walioko chini yake watimize wajibu kama inavyotakiwa na kwa manufaa ya jamii.

Raia Mwema: Hebu sasa jitathmini mwenyewe. Kwa kukaa kwako madarakani, ukiwa waziri au hata Idara ya Usalama wa Taifa. Jambo gani unajivunia?

Ntagazwa: Yapo mengi lakini labda sijui nichukulie wakati ule ulipotolewa uamuzi wa watumishi wa Serikali kuuziwa nyumba. Nilipoteuliwa kuwa waziri baada ya uchaguzi wa mwaka 2000, niliamua kukaa kwenye nyumba yangu, Kimara Temboni.

Niliamua kukaa nyumbani kwangu kwa sababu moja, nyumba ile nimeijenga kwa shida na imenichukua muda sana. Nakumbuka marehemu mke wangu alisema Mungu akituwezesha kujenga nyumba hii si wanaweza kusema tumeiba.

Nikamwambia mwalimu (mke alikuwa mwalimu) atakayesema tumeiba tunaweza kukataa lakini pia shahidi mkuu ni Mwenyezi Mungu na kama ningekuwa mwizi sidhani kama ingenichukua miaka 18 kujenga nyumba moja.

Namshukuru Mungu amenipa uhai mpaka nikakamilisha, nilianza kufyatua matofali mwaka 1986 nikawa najenga taratibu mpaka fremu za madirisha nilizoweka mpaka kumaliza kuta zilibadilika rangi na nilikuja kumalizia kwa mfano kuweka tarazo ni wakati namwoza binti yangu wa kwanza, Chimpaye anasoma Marekani si kwa gharama za serikali licha ya kuwa serikalini.

Nimeanza kufyatua matofali 1986 nilipofanya hesabu nikaona ni miaka 18 mpaka nyumba inakamilika. Ni nyumba ya ukubwa wa vyumba vitano, vyenye kujitegemea kila chumba.

Kuna pia chumba kwa ajali ya kusali, nilifikiria siku nitakapokuwa mzee pengine sitaweza kwenda kanisani kwa hiyo naweza kumwita padre pale nikasali.

Kwa sasa chumba hicho nakitumia kama ofisi. Kwa hiyo niliamua kukaa kwenye nyumba yangu kwa sababu hiyo sasa ilipoamuliwa watumishi na viongozi wa Serikali kuuziwa nyumba mimi sikuwa nakaa nyumba ya Serikali.

Baadaye nilitafutiwa nyumba ya Serikali, nikaambiwa kuna nyumba hapa, nikaenda nikaoina nyumba yenyewe ilikuwa kwenye bonde hivi, nilichofanya ni kwenda kulipia ile offer, nadhani ilikuwa ni Sh 1,500 hivi kuchukua zile fomu baadaye nikaambiwa nahitajika kulipa Sh zaidi ya milioni 30, nikasema yarabi nitazitoa wapi mimi.

Kwa hiyo nadhani kati ya mawaziri waliokuwa wakiitwa askari wa miavuli ni Waziri Ntagazwa ambaye ni mjinga wa kutupa ambaye hakupata nyumba kwa utaratibu huo na namshukuru Mungu maana pengine ingenisumbua kwenye dhamiri yangu kwamba hivi kweli ingawa ulikuwa ni uamuzi rasmi serikalini lakini ulikuwa wa haki bin haki?

Hilo ni moja, lakini la pili, siku moja nadhani ilikuwa mwaka 2007 nilikutana na mtu mmoja akaniambia unanikumbuka? Akaniambia mimi nilikuwa pale Wizara ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakati ukiwa waziri pale anasema mheshimiwa leo hii mimi najiuliza; hivi ungetaka kuwa tajiri wa kutupa nani angekuzuia?

Nikamuuliza, tajiri wa kutupa kwa kufanyaje? Akasema ukiwa Waziri wa Ardhi, Maliasili na Utalii…viwanja viko chini yako, magogo msituni, vitalu vya uwindaji viko chini yako, uvuvi chini yako.

Nikamwambia ningeweza kuwa tajiri wa kutupa lakini dhamiri yangu ningeipeleka wapi? Akasema hiyo dhamiri yako ingekuwa shauri yako wewe.

Kwa hiyo unaona ni vitu ambavyo unakubali kutumikia na sio kujinufaisha lakini watu wanakushangaa. Lakini nina uhakika aliyeniumba (Mungu) hanishangai ndicho anachotarajia nikifanye.

Raia Mwema: Ni jambo gani unalojutia ulilowahi kufanya au kushuhudia katika kipindi chako ukiwa kiongozi kitaifa.

Ntagazwa: Kuna wakati mmoja (enzi za Rais Ali Hassan Mwinyi) alikuja mzee mmoja simkumbuki jina, nikiwa Waziri wa Ardhi, Maliasili na Utalii kulikuwa kumetolewa viwanja eneo fulani na mzee huyo alikuwa amepata kiwanja kihalali hapa Dar es Salaam.

Nakumbuka kiwanja chake kilikuwa namba 163 sasa inaelekea kiwanja namba 161 au 162 aliweka vifaa vya ujenzi asiweze kufika kwenye kiwanja chake.

Sasa unajua katika hali hiyo yanapoanza masuala ya ujenzi kiwanja chake kingeweza kumezwa katika utaratibu wa kupora.

Alikuja kutulalamikia wizarani, niliwaita wataalamu nikawaambia jamani huyu mzee ni sawa na baba yetu kumhangaisha si jambo jema hata kidogo kwa nini tusimtafutie kiwanja cha ukubwa ule ule katika block ile ile.

Kikatafutwa kiwanja akapata akaandikiwa ofa akalipia tukawa tumemaliza tatizo lake. Mheshimiwa Rais Ali Hassan Mwinyi alipoanzisha utaratibu wa kusikiliza kero za watu pale Lumumba (Ofisi za CCM-Dar es Salaam) huyu mzee alikwenda pale kulalamika kwamba mimi Wizara ya Ardhi, Maliasili na Utalii hawakunisaidia chochote kuna mtu aliyepora kiwanja changu.

Sasa uzuri wakati ule Balozi Matern Lumbanga alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambaye baadaye alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Akiwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi baadaye waliondoa maliasili na utalii wakaipeleka kwingine. Kwa hiyo kwa sababu ndiyo ilikuwa wizara inayohusika na suala la mzee huyo Lumbanga akaitwa kutoa maelezo.

Sasa wakati huo Lumbanga, watu hawakujua na wengi hawajui lakini nimesoma naye darasa la 13 na 14 Pugu ni mtu mwenye msimamo na maadili.

Akamwambia mheshimiwa Rais naomba nikwambie kwa dhati mzee huyu hana shukurani. Huyu mzee alichokwambia kwamba kuna mtu ameingilia kiwanja chake na amekuja wizarani kulalamika ni kweli lakini alichokifanya Waziri Ntagazwa alituitisha wataalamu akasema jamani huyu mzee tusiendelee kumsumbua, tafuteni kiwanja cha ukubwa ule ule katika block ile ile ili kama thamani ya eneo isipungue, akapata kiwanja mpaka leo anacho. Kama anakulalamikia huyu hana shukurani. Hiyo ilinisononesha kidogo.

Raia Mwema: Tuingia kwenye siasa. Tueleze kumetokea nini CCM hadi mzoefu kama wewe ukimbie, wengine wanaweza kutafsiri kama umekimbia matatizo badala ya kuyakabili.

Ntagazwa: Nimechomoka kwa sababu ukiisoma Katiba ya CCM katika malengo yale kuhakikisha kwamba rasilimali za Taifa zinatumika kupambana na ujinga, maradhi na umasikini, nikihusisha na pori la hifadhi la Moyovozi linalopakana na Wilaya ya Kibondo na Wilaya ya Kakonko ambayo ni mpya na nadhani mpaka Bukombe huko yale yanayotokea hapana. Haiwezekani yakawa yanatokea na ukasema ni vyombo vilivyo katika Serikali ya CCM hapana.

Kwa nini nasema hivyo; mosi, unapopata taarifa serikalini kwa maana ya wilaya na mkoa na unapata taarifa hizo kwa wanafamilia kwamba zaidi ya watu 21 wameuawa katika pori hilo la hifadhi lazima mshituke. Si kitu cha kujivunia kwamba mmefanya siri, hilo moja.

Februari mwaka jana zilitolewa taarifa baadhi yetu tunaotoka mkoani Kigoma kwamba watu 21 au zaidi wameuawa katika Pori la Hifadhi la Moyovozi. Ni kweli wameingia katika eneo kinyume cha sheria lakini tuna utaratibu wa kisheria. Mtu akiingia kwenye eneo kama hilo anaitwa jangili na anatakiwa kupelekwa kwenye vyombo vya sheria si kuuawa.

Lakini hivi karibuni kitu ambacho kimefikia kunisononesha ni kwamba CCM hii ya leo, mimi nadhani kilichopo ni zile herufi CC na M, si CCM iliyorithi mazuri ya TANU pamoja na CCM ya wakati wa Mwalimu Nyerere.

Ameingia mwananchi katika Pori la Hifadhi la Moyovozi, bahati nzuri maofisa wa wanyamapori wamefanya kazi yao nzuri amekamatwa.

Lakini yule mwananchi amekatwa sikio na ofisa wanyamapori kapelekwa mahakamani kesi inaendeshwa na ni sahihi kabisa ameingia kwenye hifadhi kinyume cha sheria mimi sitetei hata kidogo uvunjifu wa sheria, kapelekwa mahakamani ambao ni utaratibu kabisa unaokubalika katika utawala bora.

Ofisa yule ametoa ushahidi wake kuiambia Mahakama amemkamata wapi na mambo mengine akamaliza, mshatakiwa akamuuliza maswali mawili ninayoyakumbuka.

Mshitakiwa alimuuliza; shahidi nakuuliza uliponikamata nilifanya vurugu yoyote akasema hapana kama ungefanya vurugu ningekushona risasi, akamuuliza sawa kwa nini ulinikata sikio akajibu nilikukata sikio ili niweze kukutambua kama utarudi tena porini.

Nimekwambia nilivyokuwa na nilivyolelewa na nilivyosoma, siamini kama majibu ya namna hii yanaweza kutoka kwa mtumishi wa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Majibu ya namna hii yanaweza kutoka kwa muasi wa Lord’s Resistance Army kule Uganda.

Sasa ukiona mambo ya ovyo ovyo ya kiwango hicho yanafanyika na haya mengine tuliyoshuhudia kwenye mchakato wa kura za maoni wakiimba..tumechoka kuonewa …tunataka haki zetu! Chonde chonde hamko salama.

Amani inakwenda kutoweka. Tuombe Mungu tusifike huko, lakini nimekwambia hivi unafika mahali kila mmoja wetu anakiri kwamba si sawa. Wengi tu katika CCM nina uhakika wanayaona si sawa lakini watakapokaa kwenye vikao rasmi kwa sababu ni mfumo, sasa mfumo unatawala wewe na mimi tunapotoa kasoro moja au nyingine wala, yote weka chini ya busati mnaendelea kama vile hakuna kilichotokea, si sahihi tutauana…haifai, tumuombe Mungu tusifike huko.

Kwa hiyo ni sababu kubwa, nimeona hakuna tegemeo kwa sababu mfumo umekwishakujikita na mfumo huu popote duniani hakuna mfumo unaofanya kazi ya kujimaliza hata siku moja. Mifumo yote inafanya kazi ya kujifanya iwe endelevu.

Raia Mwema: Kwa nini uliamua kwenda CHADEMA badala ya vyama vingine tofauti na CCM.

Ntagazwa: Jibu ni jepesi sana. Nakumbuka kuna wakati nadhani alikuwa anazungumzia juu ya vyama mbalimbali vya siasa, Mwalimu Nyerere akasema ukisoma karibu Katiba za vyama vyote ni Chama Cha Demokrasia na Maendeleo ndiyo Katiba yake inashabihiana na Katiba ya TANU na ile CCM ya wakati wa Mwalimu.

Na ndiyo maana kwenye salamu ya CHADEMA tunasema CHADEMA wanaitika vema, CHADEMA tumaini jipya la Watanzania, tunajivunia nguvu ya umma.

Ni kweli binadamu lazima uishi kwa matumaini kama huna matumaini utajinyonga sasa hivi na katika utaratibu huu, demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya siasa lazima kuwa na chama unakiona ni mbadala ambacho kinaweza kuiondolea jamii mfumo huu wa sasa unaolea uovu.

Raia Mwema: Unakwenda kugombea ubunge kwa tiketi ya CHADEMA Jimbo la Muhambwe, Kigoma. Katika kampeni wewe ndiye utakayekibeba CHADEMA au chama hicho ndicho kitakubeba kwa maana ya nguvu zako kisiasa kwa kulinganisha na mtandao wa CHADEMA huko.

Ntagazwa: Hapana. Unajua ukitaka kulinganisha CHADEMA na CCM, CCM wana mtandao mkubwa tu. Bahati mbaya wanauvuruga kwa kutokukemea maovu ambayo dhahiri yanaonekana na ni kwa sababu watu wetu wanakabiliwa na umasikini wa kipato na hali kwa maana ya weledi wa nini kinapaswa kufanyika na viongozi wetu kwao…viongozi wetu wajibu wao ni upi na haki yangu mimi raia ni nini na vile vile na mimi nina wajibu kwa jamii ili twende pamoja.

Huwezi kulinganisha mtandao wa CCM na chama kingine chochote cha siasa nchini na kwanza ukumbuke kuwa mpaka leo CCM ni chama dola.

Katika suala hili la kwenda kugombea Muhambwe, CHADEMA wana mchango mkubwa sana tutakavyokwenda kumshinda mgombea wa CCM.

Wanajua sifa zake, simjui kwa jina wala sitaki kutaja jina lake lakini moja ya sifa zake wanazopaswa kujua ni katika kura zile za ovyo ovyo za maoni…na mengineyo. Alipata alama nzuri tu kwenye chama, hilo wanalijua, kama hawalijui basi ni mfumo umefunika lakini si kwamba ukweli huo haupo.

Kwamba mgombea wao ametumia haki yake ya kikatiba kwenda mahakamani amekashifiwa na padre katika ibada lakini katika kesi ile kamchukua padre kamjumuisha mwalimu wa msikiti na waumini wengine inajulikana kesi ile imekwisha Mahakama Kuu lakini nadhani utaratibu wa rufani unaendelea siwezi kwenda zaidi.

Lakini nina hakika wakiondoka kwenye mfumo wanamjua mgombea wao na ni ukweli kwamba ahadi moja ya CCM inasema nitajielimisha kwa kadiri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa manufaa ya wote, hii ni ahadi ya CCM na enzi zile wakati wetu ulikuwa unatoa ahadi kwa kiapo.

CCM katika Jimbo la Muhambwe katika karne ya 21 ya Sayansi na Teknolojia, wamemsimamisha mgombea ambaye hakumaliza hata elimu ya msingi ameishia darasa la sita, hiyo ni kweli. Sasa kama ni dharau kwa wapiga kura wa Muhambwe sijui.

Raia Mwema: Lakini hadi hapo hawajavunja sheria na Katiba ya Tanzania inataka mtu anayejua kusoma na kuandika, unasemaje kuhusu matakwa haya ya Katiba.

Ntagazwa: Ndiyo lakini unakwenda na hali halisi katika mazingira. Sheria imepitishwa na Bunge ya Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ninayo imeandikwa Kiingereza, mbunge huyu mtarajiwa wa CCM Muhambwe ataisoma, ataielewa? Ataifafanua na kuitafsiri na kuisimamia?

Raia Mwema: Unakwenda kugombea Muhambwe, wapiga kura wa Muhambwe watarajie nini kama kura zitatosha?

Ntagazwa: Watu wa Muhambwe, kura zitatosha kwa sababu mwaka huu hakichaguliwi chama, anachaguliwa mgombea na hata wizi wa kura uliokuwa ukifanyika tumekwishagundua walikuwa wanafanyaje, tutaweka majeshi ya kulinda kura.

Raia Mwema: Umesema walikuwa wanaiba kura na sasa mtawadhibiti, kwa hiyo ulipokuwa CCM mlikuwa mkifanya hivyo vitendo?

Ntagazwa: Mimi nilikuwa sifanyi wizi kwa sababu kwanza nilikuwa siendi kugombea kwa kujiamulia binafsi. Nilikuwa naitwa, wazee wananiambia walishawahi kuniambia sikiliza mheshimiwa Ntagazwa wewe ni mtoto wetu hata kama una mvi.

Tunasema hivi kama kuna kitu tulichokukosea sisi wazee wa Muhambwe, usichukue fomu (ya kugombea ubunge). Lakini kwamba kuna kitu ulichotukosea wewe hapana, tunakuomba ukachukue fomu.

Mara zote nilizogombea imekuwa hivyo na mimi nimekuwa nikishinda si kwa mbinu za wizi au rushwa, hapana. Safari hii kwa nguvu ya umma salama yetu katika CHADEMA, wapiga kura wa Muhambwe tutashinda.

Kitu ambacho watarajie nimekwishawaambia mambo mawili. La kwanza, wameanza kulima tumbaku na mimi najua kama mwana-mazingira tumbaku ni adui wa mazingira na hasa misitu.

Nimewaambia hivi, kilimo cha tumbaku na hifadhi ya mazingira vinaweza kwenda pamoja. Wanaotaka hiyo tumbaku ni kampuni ya ATTT ya Marekani na wamesema hawajapata tumbaku yenye ubora popote duniani kama tumbaku ya Kibondo.

Sasa nimewaambia kwa kuwa hawa wanataka tumbaku, lazima kuwe na programu ya kilimo cha tumbaku itakayonufaisha wakulima, wanunuzi wa zao hilo na wakati huo huo kulinda hifadhi ya mazingira.

Raia Mwema: Una ushauri gani kwa wanasiasa wenzako, ndani ya kambi ya upinzani na katika CCM.

Ntagazwa: Sote tunatakiwa kuwa na nidhamu katika vyama vyetu lakini isiwe nidhamu inayotuondoa karibu na Mwenyezi Mungu. Siasa si jambo la mwisho bali ni nyezo ya kuturahisishia kwenda kwa Mwenyezi Mungu kwa kadiri tunavyotimiza wajibu wetu. Siasa ni fursa ya kutumikia waja wa Mwenyezi Mungu.

http://www.raiamwema.co.tz/news.php?d=2549

0 comments:

Post a Comment