Thursday, September 23, 2010

WAKATI NA BAADA YA UCHAGUZI2010: TANZANIA IPI TUNAYOITAKA?


UZINDUZI WA TAMKO LA WANAHARAKATI WASIO WA KISERIKALI 2010;
“WAKATI NA BAADA YA UCHAGUZI2010: TANZANIA IPI TUNAYOITAKA?”

21.09.2010, Hoteli ya Blue Pearl-Ubungo Plaza


Asasi ya Agenda Participation 2000 asasi isiyo ya kiserikali inayofanya kazi ya kuhamasisha
utamaduni wa utawala bora na demokrasia ndani ya Tanzania. Asasi pamoja na mambo
mengine inatoa elimu ya uraia, mafunzo na kuhifadhi masuala ambayo yanaweza kuimarisha
ushiriki wa wananchi katika utawala, demokrasia na michakato ya maendeleo.

AP2000, ikiongozwa na Dira ya; “Kuona jamii ya kidemokrasia na yenye amani na dola au
nchi inayoendeshwa na utamaduni wa misingi au kanuni za kidemokrasia”. AP2000 imekuwa
ikiratibu tangu mwaka 2005 na pia mwaka huu 2010 mchakato wa kukusanya na kuboresha
maoni ya wanaharakati wasio wa kiserikali katika masuala mbali mbali nyeti kwa maslahi ya
Taifa letu.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 31, 2010, AP2000 imehusika kuratibu uandaaji wa Tamko la
Wanaharakati Wasio wa Kiserikali kwa msaada wa mashirika mbalimbali kwa taarifa na ushauri.
Sambamba na mashirika hayo, kwa namna ya pekee Shirika la Kijerumani la Friedrich Ebert
Stiftung, wamehusika kufadhili uchapaji, uzinduzi na usambazaji wa tamko hili.

Tamko la Wanaharakati Wasio wa Kiserikali tunalolizindua leo kupitia mgeni rasmi Mhe. Jaji
Mstaafu Lameck Mfalila, 21.09.2010 katika Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza, Dar-es-Salaam
likishuhudiwa na wanaharakati toka Asasi za kiraia, Balozi, Mashirika ya Kimataifa, Wanahabari,
na wananchi wote kwa ujumla toka kila pembe ya Tanzania limegusa maeneo makuu yafuatayo;

1. Tathmini ya Maendeleo Kiuchumu na Haki

2. Ajira

3. Mazingira na Maliasili

4. Kilimo, Uvuvi na Ufugaji

5. Huduma za Jamii
6. Uongozi na Utawala

7. Rushwa

8. Maisha na Usalama wa Binadamu

9. Maadili ya Uchaguzi

Vipaumbele hivi vilivyofafanuliwa kwa kina sana katika chapisho la Tamko hili, vinaangaliwa
na Wanaharakati Wasio Wakiserikali kama msingi wa kupiga kura wagombea kutoka vyama
vya siasa. Sambamba, kuwataka wagombea ngazi za Udiwani, Ubunge na Urais pia viongozi na
watumishi wa umma kuzingatia maazimio hayo wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu
2010.

Maazimio haya yanabeba uzito na masuala nyeti yanayoikandamiza Taifa na kuzidi kuliweka
katika hali ngumu na kikwazo kuelekea ustawi na maendeleo endapo hayatashughulikiwa kwa
haraka na kiukamilifu

Uchaguzi Mkuu unatoa nafasi adhimu kwa wapiga kura na wagombea kukumbuka malengo
ya msingi ya mfumo wa uchaguzi, yaani kuweka mbele na kulinda maslahi ya Taifa hili. Kwa
mantiki hiyo, tunasisitiza uwepo wa mchakato wa uchaguzi wenye uwazi, haki na amani.Lakini
pia, tunapinga vikali aina yoyote ya vitisho, rushwa, mizengwe au hila kupindisha ushindi
utokanao na kura halali za wananchi.Tunasisitiza katika siasa safi zenye kuzingatia misingi ya
kidemokrasia.

Haya ndiyo tunayoyaamini, tunayoyasimamia, tuna amini yana msingi sasa na hata baada
ya Uchaguzi Mkuu 2010. Wagombea watakaoingia madarakani, viongozi wa umma wote
wanapaswa kuyasimamia kwa vitendo kwa maslahi na ustawi wa Taifa letu.

Tanzania tunayotaka kuiona ni Taifa lenye amani na maendeleo ambalo linaheshimu haki za
wananchi
wake wote bila kujali jinsia, hadhi, dini, kabila, imani ya kundi fulani na uwezo kimwili ama
kiuchumi. Tunataka Tanzania ambayo licha ya kutokuwa na wala rushwa, inaendeshwa na
viongozi wenye uvumilivu na uadilifu, wenye kutumia ipasavyo maliasili na rasilimali hususan
watu. Tunataka Tanzania inayojitosheleza kwa chakula; yenye miundombinu bora yenye misingi
ya kiteknolojia; na yenye kutafsiri maendeleo ya kitaifa kwa kuangalia afya, elimu na ustawi
wa jamii. Tunaomba wananchi wote wayasimamie haya na kuyafatilia, kwa sababu Tanzania
tunayotaka inawezekana!

Ninawashukuru sana kwa kufika kwenu katika uzinduzi huu. Ni matumaini yangu makubwa
mtaupasha umma vizuri juu ya haya tuliyowasilisha kwa umma kupitia tamko hili.

Mungu Ibariki Tanzania!

Imetolewa na;

Prof. Max Mmuya,
Mwenyekiti, Agenda Participation 2000.
Tel: +255 22 2460036/2460039

0 comments:

Post a Comment