Tuesday, September 28, 2010

Elimu, Afya bure vinatekelezeka

WAKATI wagombea wa vyama mbalimbali wanaendelea na kufanya kampeni sambamba na kutoa ahadi, hadi sasa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Rais Jakaya Kikwete anaongoza kwa kutoa ahadi ambapo kwa tathmini ya haraka amefikisha ahadi 33.

Huku akifuatiwa na Chama cha Wananchi (CUF) ambapo mgombea Maalim Seif Sharrif Hamad ameahidi 23 na Dk. Willibrod Slaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ametoa ahadi 11 ikiwa ni pamoja na elimu, afya kuwa bure iwapo atachaguliwa kuongoza taifa hili.

Hii ni moja ya ahadi ambayo CCM imekuwa ikidai haiwezekani kutekelezeka la sivyo lazima baadhi ya sekta zishindwe kuhudumiwa iwapo elimu na afya havitachangia katika mapato ya nchi.

Kwa mtazamo wangu ninaamini kabisa ahadi hii inaweza kufanyiwa kazi si CHADEMA pekee ikichaguliwa kuingia madarakani bali hata serikali iliyoko madarakani ikiwa ingekuwa na mapenzi mema na wananchi wake hasa wa hali ya chini basi asilimia kubwa wangejua kusoma na kuandika.

Nasema hivi kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wasiojua kusoma na kuandika hali ambayo imechangiwa na kuwepo kwa ongezeko la umaskini linalosababishwa na kukosa kipato hivyo baadhi yao kushindwa kuhudhuria masomo.

Ni vigumu kuelewa ninalolieleza lakini zipo baadhi ya familia hasa maeneo ya vijijini, na mjini pia, ambazo baadhi ya wanafunzi wanashindwa kuhudhuria masomo kutokana na kukithiri kwa michango ya shule.

Hiyo familia ukiichunguza utakuta hata mlo mmoja wa chakula ni tatizo wakati mwingine ulazimika kulala njaa kutokana na kukosa fedha sasa itakuwezekanaje kutoa michango isiyo na idadi kwa wanafunzi?

Hata hivyo bado ninaamini kuwa elimu na afya bure vinawezekana kwa kuwa hata ukizungumza na baadhi ya wazazi hasa wa enzi ya utawala wa awamu ya kwanza Mwalimu Julius Nyerere hawasiti kuelezea mazuri ya elimu iliyokuwa ikitolewa kipindi hicho.

Hasa ya kutochagia chochote katika suala la elimu ambapo wanaeleza jinsi walivyokuwa wakipata kila kitu kutoka katika shule walizochaguliwa hapo ndipo ninapojiuliza ni kitu gani kilichofanya sasa elimu kuwa ghali ingawa baadhi ya wataalam wanadai kupanda kwa gharama za maisha.

Lakini je hakuna njia ambayo inaweza kufanywa ili maisha yakapungua ukali ili kila anayehitaji kwenda shule akaweza kupata elimu bila kutoa mchango wa aina yoyote kuliko ilivyo sasa?

Ninaamini kabisa elimu na afya bure zinawezekana ingawa bado serikali itajitetea na kudai kuwa suala la afya kwa upande wa watoto walio na umri wa mwaka mmoja hadi mitano limekuwa likipewa kipaumbele lakini hiyo haitoshi kwani bado kuna rika la wazee hawa nao wanahitaji kuangaliwa.

Sasa basi kuna haja ya masuala haya kuwa bure kama alivyodai Dk. Slaa katika moja ya ahadi zake, kwa kuwa hata baadhi ya nchi za Afrika ambazo zilikuwa chini kwa uchumi zimefikis hatua ya kutoa elimu na afya bure ili kuondoa wimbi la idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika.

Ukichukulia mfano mdogo wa nchi jirani ya Kenya wenzetu hawa wametumia mbinu gani katika kukuza uchumi wao na kuamua kuifanya elimu pamoja na afya kutochagiwa? Basi hatuna budi kujifunza kupitia mifano hiyo.

Wapo wanaodai masuala hayo yakifanywa bure basi uchumi utashuka; hili si kweli kwa kuwa kuna maeneo mbalimbali yanayoweza kuziba mapengo ya fedha iliyokuwa ikipatikana kutoka katika hizo sekta.

Ninaamini kabisa kukiwepo ushirikishwaji wa kutosha hasa kuanzia ngazi ya chini; elimu na afya bure vitawezekana ili kupunguza ama kuondoa kabisa idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika ambayo inatokana na kuwa na kipato kidogo au kukosa kabisa fedha za kulipia.

0 comments:

Post a Comment