Hatimaye Chadema imepitisha majina ya wabunge 105 wa viti maalumu huku ikiwaacha
wanachama wake 42 walioshindwa kukidhi vigezo vya chama hicho.
Majina ya wabunge hao hayakuwekwa hadharani na badala yake yatapelekwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kabla ya Septemba 30 mwaka huu.
Uteuzi wa majina hayo ulifanywa na mshauri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Mkumbo Kitila, ambaye ni mwanachama wa chama hicho na kuthibitishwa na Kamati Kuu katika kikao chake cha Septemba 25 na 26 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Katibu Mkuu wa Chadema ambaye pia mgombea urais, Dk. Willibrod Slaa, alisema baada ya matokeo ya wabunge hao ya Julai kufutwa kutokana na mizengwe, Baraza Kuu lilikasimu madaraka kwa Kamati Kuu kufanya uteuzi huo.
“Kamati Kuu ikaunda Kamati Ndogo ambayo ilimtumia mshauri kufanya uteuzi huo akizingatia vigezo vya elimu, uzoefu wa uongozi kisiasa, uzoefu wa uongozi nje ya siasa; ugombea jimboni mwaka huu; mchango katika operesheni za chama na kampeni zinazoendelea na umri ndani ya chama,” alisema Slaa.
Katika vigezo hivyo, aliyeongoza alipata asilimia 94 na wa mwisho 16 ambapo moja ya sababu za kutumika utaratibu huo ambao Dk. Slaa aliuita wa kisayansi, ni kuondoa uswahiba, wagombea kutoka kanda moja na urafiki.
“Tumeondoa dhana ya mtu kuchagua ‘girlfriend (rafiki wa kike)’ wake, na majina haya hatutayatoa hadharani, kwani wengine waliopitishwa wanagombea majimboni,
hivyo kunaweza kuwachanganya wapiga kura,” alifafanua.
Dk. Kitila alisema katika uandaaji wa vigezo, waliangalia suala la umahiri wa mgombea na kwambambunge atakuwa anawakilisha nchi na kupanua wigo wa ushiriki wa wanawake.
Katika Bunge lililopita, wabunge wa Chadema walikuwa 11 wakiwamo wa majimbo na viti
maalumu na mwaka huu imesimamisha wabunge wa majimbo 185.
0 comments:
Post a Comment