Thursday, September 30, 2010

Slaa aichongea CCM kwa viongozi wa dini

Wednesday, 29 September 2010 18:58
0diggsdigg

Exuper Kachenje
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa jana alikutana na viongozi wa dini na kuwaeleza maoni ya chama chake jinsi CCM ilivyoanza kucheza rafu kwenye mchakato unaoendelea wa uchaguzi mkuu nchini.

Viongozi hao walimtembelea mgombea huyo wa urais kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo kwenye ofisi za makao makuu ya Chadema jijini Dar es Salaam na kumueleza kuwa ziara hiyo ni sehemu ya mpango wao wa kutembelea wagombea urais kwa vyama mbalimbali kwa lengo la kuwafikishia ujumbe wa haki.

Lakini baada ya kuwasikiliza, Dk Slaa alianza kuvurumusha lalamiko moja baada ya jingine.
“Nimefarijika kwa viongozi wa dini kuja," alisema mgombea huyo urais kwa tiketi ya Chadema. "Ni jukumu lao kuangalia amani ambayo huko nyuma ilitaka kuvunjika. Tunajua uchaguzi ni wa muda mfupi na amani haiji kutoka mbinguni."

Dk Slaa, ambaye chama chake kimekuwa kikidai kuwa CCM imekuwa ikicheza rafu dhidi ya Chadema, alianza kueleza mtazamo wake kuhusu mchakato wa uchaguzi.
"Wameeleza; tumetoa mawazo yetu; haki ikikiukwa zaidi hasa kutokana na CCM inavyofanya sasa, sisi hatutakaa kimya. Haki isipopatikana au isipotendeka na polisi kushindwa kuilinda amani na amani ikatoweka; wa kulaumiwa ni CCM,” alisema Dk Slaa.


Alidai kuwa upo ushahidi wa wazi wa CCM kuvunja Maadili ya Uchaguzi na Sheria ya Gharama za Uchaguzi wakati chama hicho ndio msimamizi wa mfumo huo kutokana na kuongoza serikali.
“Tumeeleza kuwa vurugu kwenye uchaguzi huja baada ya matokeo; tumeombwa kuyakubali matokeo baada ya Nec kuyatangaza, lakini tunazo taarifa na waraka tumeunasa kuwa serikali imeagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha chama fulani kinashinda,” alisema Dk Slaa.
Aliongeza kusema: “Ni mwendawazimu kwa mtu kuyakubali matokeo katika uwanja usio sawa. Kwa hiyo viongozi wa dini wachukue jukumu la kuhakikisha uwanja sawa unakuwepo katika kampeni.
“Tunazo pia taarifa kwamba serikali imetuma timu kuzunguka kuwatisha watu, hata viongozi wa dini kwa madai kuwa wanaunga mkono upinzani, hili halikubaliki. Tulichoahidi tutaelimisha watu kwa kuzingatia wajibu wao na kujua haki zao, lakini wanapochokozwa, ninyi mnajua saikolojia ya makundi, hatuwezi kuizuia.”
Ujumbe wa viongozi hao wa dini za Kiislamu na Kikristo waliwakilishwa na ujumbe wa watu 12 ukiongozwa na askofu Paul Ruzoka wa jimbo Kuu Katoliki la Tabora chini ya uratibu wa Peter Maduke, ambaye ni mratibu kamati hiyo.


Viongozi wengine walioshiriki mazungumzo hayo na Dk Slaa jana ni Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Alhadi Salum, Sheikh Abdalah Rashid ambaye alimwakilisha Mufti Issa bin Shaban Simba, Sheikh Thabit Norman Jongo aliyemwakilishi Mufti wa Zanzibar na Askofu Thomas Laizer wa KKKT jimbo la Arusha.


Wengine Askofu Joseph Shao wa jimbo Katoliki Zanzibar, Askofu John Nkola wa Kanisa la Africa Inland Church (Shinyanga), John Mapesa wa Jumuiya ya Kikristo (CCT) Dodoma, Juma Chum (CCK-TC), Padre Daniel Mfowi (Zanzibar), Padre Mbegu kutoka Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC).


Kabla ya Dk Slaa kueleza mtazamo wake kuhusu mwenendo wa uchaguzi, ujumbe huo ambao unaunda Kamati ya Viongozi wa Dini ya Haki na Amani, ulimtaka Dk Slaa kuzingatia haki, maelewano, mshikamano na amani katika kampeni zake za kuusaka urais.


“Dhumuni na shabaha ya kuzungukia vyama vya siasa hasa wagombea urais, ni kuwaomba wahakikishe kampeni zao zinazingatia haki, maelewano, mshikamano amani na utulivu,” alisema Askofu Ruzoka.
Askofu Ruzoka alisema kuwa kamati hiyo imeamua kufikisha ujumbe huo kwa mgombea urais huyo wa Chadema ikiamini utawafikia pia wagombea wote wa ubunge na udiwani wa chama hicho.
Kwa mujibu wa Askofu Ruzoka, kamati hiyo pia imeviandikia barua vyama vingine vilivyosimamisha wagombea urais katika uchaguzi mkuu ujao kuviomba viwape fursa ya kuzungumza navyo, lakini hilo litafanyika kama vyama hivyo vitakubali.


“Ziara yetu imeanzia hapa (Chadema) na kuendelea kwenye vyama vingine kadiri vyama hivyo vitakapotukaribisha,” alisema askofu Ruzoka.


Kwa mujibu wa askofu Ruzoka tayari kamati hiyo imefanya ziara ya aina hiyo visiwani Zanzibar na kukutana na mgombea urais wa visiwa hivyo kwa tiketi ya CUF, Seif Sharrif Hamad na rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Alisema kamati hiyo iliundwa na kuanza kufanya kazi mwaka 2002.


Kamati hiyo ilikemea kampeni za kuchafuana na zinazogusa maisha binafsi ya wagombea wakisema hazipaswi kupewa nafasi katika mchaguzi huo badala yake vyama vitangaze sera na malengo yake ya kuomba uongozi.
Kwa mujibu wa kamati hiyo, si sahihi kwa wagombea kuzungumzia maisha binafsi ya watu katika kampeni zao kwani endapo jambo hilo likiachwa, hakuna mgombea atakayekuwa salama.


“Wagombea waeleze wataifanyia nini nchi hii, wananchi wasikilize sera za vyama. Kila mmoja akiandamwa binafsi kwenye kampeni, hakuna aliye salama," alisema askofu John Nkola.
Aliendelea kusema: "Mambo binafsi hayana nafasi kwenye kampeni, kinachotakiwa ni sera.”
Akizungumzia mkutano huo, Dk Slaa alisema amefarijika na ujio wa viongozi hao wa dini aliowaelezea kuwa wamefanya hivyo kutimiza jukumu lao.


“Nimefarijika kwa viongozi wa dini kuja. Ni jukumu lao kuangalia amani ambayo huko nyuma ilitaka kuvunjika. Tunajua uchaguzi ni wa muda mfupi na amani haiji kutoka mbinguni," alisema Dk Slaa.
Naye mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa waliwaeleza viongozi hao wa dini hofu yao kuhusu mchakato wa uchaguzi na madai yao juu ya jinsi CCM inavyoitumia serikali kuuharibu.

MWANANCHI GAZETI

0 comments:

Post a Comment