Tuesday, September 7, 2010

Tukichagua hovyo, tukitendewa hovyo, tusiseme hovyo

Tukichagua hovyo, tukitendewa hovyo, tusiseme hovyo

Jenerali Ulimwengu
Septemba 1, 2010

VIPINDI vya uchaguzi kote duniani daima huzua mambo yasiyokuwa ya kawaida. Kila aina ya vitimbwi kujitokeza na baadhi ya matukio huwafanya watu wakaonekana kama vile wamebadilika.

Hii ni kwa sababu uchaguzi mara nyingi huibua hisia kali miongoni mwa watu, ama wale wanaogombea nafasi mbalimbali au wale wanaowaunga mkono au kuwapinga. Mara nyingi makundi yanayokinzana huamsha hisia kiasi kwamba hata amani inaweza kuathirika kutokana na matendo ya wanasiasa na mashabiki wao.

Katika nchi za Afrika hali hii ni ya kawaida kabisa kwa sababu kadhaa. Mojawapo ya sababu zinazofanya kwamba hamasa za uchaguzi zivuke mpaka katika nchi za Afrika ni kwamba Waafrika bado hatujaukubali uchaguzi kama zoezi la kawaida la kutafuta ridhaa ya wananchi ili kuwapatia uongozi unaowafaa.

Kwetu sisi Waafrika, uchaguzi bado ni zoezi jingine la kutembeza dhuluma, ujanja, ulaghai, uhuni, ubazazi na kila aina ya uovu utakaotuwezesha kuwapiku washindani kwa njia yo yote ile.

Hali hii bila shaka inatokana na ukweli kwamba wale wanojiita wanasiasa miongoni mwetu hawakuingia katika siasa ili kuwafanyia kazi wananchi na kuwasaidia kuwaongoza katika mapambano ya kuboresha hali zao. Wameingia katika siasa kwa maslahi yao binafsi, na pale wanapokuwa wamesukumwa na watu wengine wanaingia katika siasa kwa kuoanisha maslahi yao binafsi na maslahi ya wale wanaowasukuma.

Kwa hali hii haiwezekani kutaraji kwamba ‘wanasiasa’ wa aina hii watatendeana haki katika mchakato unaoamua ni nani kati yao atakamata usukani wa kuiongoza jamii yake au taifa lake. Kila mmoja atajitahidi kwa uwezo wake wote kupata ushindi kwa njia zo zote, hata zile zisizo halali. Msingi wa hili ni kwamba siasa imekuwa ni mahali pa ulaji na wala si mahali pa kuwapata viongozi wa kuziongoza jamii zetu au kuliongoza Taifa letu.

Medani ni nyingi ambamo ‘wanasiasa’ hawa watafanyiana kila aina ya vituko. Hizi ni pamoja na vitendo vya mabavu, kupigana, kung’oleana mabango ya matangazo, na hatimaye kuiba kura ili kufuta utashi wa wapiga kura. Haya yote yanajulikana na yamelalamikiwa kwa muda mrefu, lakini yanaendelea.

Isitoshe, yataendelea kuwapo kwa sababu sisi Waafrika hatujafikia kiwango cha kujifunza kutokana na uzoefu wetu, hata wa jana. Ukiangalia nchi zilizopitia misukosuko mikubwa ya kutisha, na watu wake wakapoteza maisha kutokana na uvurugaji wa michakato ya uchaguzi inayoendana na uvurugaji wa jumla wa hali, utakuta kwamba hazijajifunza lo lote, na zitakuwa zinaendelea na mambo yake ya ulaghai na kutotendeana haki kama vile hakuna kilichotokea huko nyuma.

Hii ni kwa sababu maisha yetu hayakupangiliwa ili kujenga utamaduni wa upendo, heshima, mshikamano na haki katika kushirikiana katika uzalishaji na kugawana kilichopo.

Utamaduni tulionao ni wa uny’anganyi ambao unatufanya tunyang’anyane vipato katika maisha ya kila siku, na ikifika wakati wa uchaguzi tunyang’anyane katika kinyang’anyiro cha uchaguzi, na tupigane, tuuane, tukashifiane sana katika kufanya hivyo, kwa sababu tunajua kwamba anayeshinda anakuwa amekata leseni ya kuwanyang’anya washindani wake kwa miaka mitano ijayo mfululizo.

Kwa maana hii uchaguzi unakuwa ni zoezi la kurasimisha ulaghai wetu wa kila siku na kuupa mhuri mpya wa miaka mitano. Hili ndilo linalotokea kila baada ya miaka mitano katika nchi nyingi za Afrika, na ndivyo itakavyotokea hadi pale tutakapoamua kutafuta njia mbadala ya kuwapata viongozi wa kweli, kwa mfano kwa ‘kuustarabisha’ mchakato wa uchaguzi kwa kuuondolea misingi yake ya uhuni.

Kwa sasa bado tumekwama katika misingi yetu ya uhuni ndani ya uchaguzi, na kila mmoja anajaribu kuwahi kumkandamiza mwenzake kabla huyo mwenzake hajamuwahi. Katika utamaduni ambao kila mara unawaambia Watanzania, “Kuwa mjanja, pata....” Watanzania tumefanya ujanja ndio ujuzi na ulaghai ndio weledi.

Haishangazi, basi, kwamba tunabakia kuwa nyuma ya wenzetu majirani katika eneo hili, mfano Kenya na Uganda, wanaoingia katika mijadala mizito inayohusu mustakabali wa nchi zao wakati sisi tunakazana kuwa ‘wajanja.’

Juzi nimeangalia televisheni ya Kenya ikirusha kipindi cha vijana wakijadili mustakabli wa nchi yao baada ya kusainiwa katiba yao mpya, nikajisikia uchungu wa ajabu kutokana na ujinga uliopandikizwa miongoni mwetu kiasi kwamba hatuwezi kujadili jambo lo lote kwa kina, kwa sababu tunachotafuta ni “kuwa wajanja.”

Wajanja hufanya mambo yao haraka haraka, kabla ujanja wao haujang’amuliwa na matamko yao kila siku ni mepesi mepesi, na ya haraka haraka. Haya hutoka kila upande, upande wa watawala, upande wa wapinzani wa watawala.

Kwa mfano tunajua sasa kwamba watawala wetu hawajui namna ya kujadili matataizo ya nchi hii ila kwa kutoa ahadi za kufanya hiki na kile, mara nyingi bila tafakuri.

Mara nyingi nimefikiria ile hekaya kuhusu mwanasiasa ambaye katika kampeni kijijini aliwaahidi wakazi wa sehemu hiyo kwamba angewajengea daraja. Walipomuuliza anataka kujenga daraja la nini wakati hawana mto, akawajibu: “msiwe na wasiwasi, mto nitawaletea.” Ahadi, ahadi, ahadi kila mahali.

Kinachojitokeza ni kwamba wanasiasa wetu karibu wote hawana uwezo wa kujadili na kuchambua matatizo ya kimsingi ya nchi, na wakijaribu wanajua watapwaya. Mjadala wa matatizo ya msingi unahitaji ujuzi, na ujuzi hutokana na juhudi za kujielimisha, na kujielimisha hutokana na kujisomea, kujadili na wenza, na kutumia muda kutafakari, kusaili na kudodosa. Haya hayawezi kutokea katika kizazi cha wanasiasa fasta-fasta. Tunachopata ni miyeyusho ya hoja na mipakazo ya tafakuri.

Najua vyema kwamba kila nchi katika kona zote za dunia inao wanasiasa wababaishaji, na sisi hatuwezi kuliepuka hilo, sawa. Lakini hata ubabaishaji wetu umejaa ubabaishaji. Tunao watu wengi wanaojiita wanasiasa na wanaotaka kuwa madiwani au wabunge, hata rais, ambao hawajawahi wala hawana nia ya kujifunza historia ya nchi hii kisiasa na kiuchumi, na wala hawajui mambo ya kimsingi kabisa ambayo mtoto wa darasa la nne angetakiwa ayajue.

Ni wangapi miongoni mwa wagombea (wa vyama vyote) wamejaribu kujifunza juu ya watu wa Tanganyika na Zanzibar: asili zao na huko walikotoka; jinsi walivyojikuta hapo walipo; vita walizopigana na jinsi walivyojenga amani baada ya vita hizo; mahusiano ya ndoa na utani; uzalishaji, ulimbikizaji na utajiri wa mataifa yetu ya asili; utamaduni na malezi ya vijana wa mataifa haya; uhusiano wa yote haya na historia ya ukombozi wa Mtanganyika na Mzanzibari; mapambano dhidi ya ukoloni na usultani; mashujaa wa mapambano haya, mbinu walizotumia na jinsi zilivyofanikiwa au kushindwa?

Najiuliza, na namuuliza msomaji, tuna ‘wanasiasa’ wangapi wanaotaka kuwa hiki au kile ambao tunajua fikra zao kwa sababu waliwahi kuziandika mahali fulani? Sizungumzii kuandika kitabu, tunaweza kupata hata insha iliyoandikwa na ‘mwanasiasa’ huyu wakati akiwa shule ya sekondari? Raia mbumbumbu anayo haki ya kuishi, lakini hana haki ya kuongoza hata mbumbumbu wenzake.

Ni wapi tumemjulia huyu, kwa lipi alilotenda au aliloandika, ili leo tuweze kusema kwamba hatukutaraji angetukatisha tamaa kiasi hiki kama mwenyekiti wa kijiji, diwani, mbunge au rais? Ni kama vile watu wanapiga ramli, au wanarusha shilingi, kisha wanamchagua, lakini wanataraji, kwa sababu zisizoeleweka, kwamba atawafanyia kazi nzuri. Akiwalambisha makombo kidogo, ndiyo kabisa!

Tunachagua kama vipofu, kisha tunalalama kama vichaa. Sasa tuamue: ama tuchague viongozi wetu kwa makini, au tukae kimya wakati wakitunyanyasa. Wachagua hovyo wasiwe wasema hovyo wakitendewa hovyo.

0 comments:

Post a Comment