Tuesday, September 7, 2010

Sheria kwanza, utashi baadaye

Sheria kwanza, utashi baadaye

John Bwire
Septemba 1, 2010

KATIKA wiki hizi za awali za kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kumejitokeza hoja zenye mazingira yanayohitaji uamuzi wa kisheria na si utashi wa chama au kiongozi fulani.

Hoja hizo zinahusisha pingamizi kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wa dola. Kuna wagombea waliowekewa pingamizi kwa makosa ya uzembe wa kutokuelewa sheria au kupuuza makusudi.

Wapo pia wagombea waliowekewa pingamizi kwa sababu nyingine zisizotokana na uzembe lakini zikiwa ndani ya wigo au matakwa ya sheria.

Alipata kuzungumza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwamba nchi ni lazima iongozwe kwa mujibu wa Katiba na si kwa shinikizo au ushauri kutoka kwa mke wa kiongozi.

Wito huo wa Mwalimu unapaswa kuzingatiwa ndani ya Uchaguzi Mkuu. Malalamiko au mapingamizi yanapaswa kuamuliwa si kwa kujiuliza kiongozi au chama fulani atakasirika au kufurahi.

Malalamiko au mapingamizi hayo na matukio mengine yanayohitaji matamko au uamuzi wakati huu wa uchaguzi yanapaswa kuamuliwa kwa mujibu wa sheria, si kwa utashi wa viongozi wa taasisi zinazosimamia uchaguzi.

Utashi wa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi au Msajili wa Vyama vya Siasa haupaswi kutumika eti kama kigezo cha kufikia uamuzi wa masuala nyeti ya uchaguzi.

Kinachopaswa kuzingatiwa kama kigezo nambari moja ni matakwa ya sheria. Matakwa ya sheria kimsingi ndiyo milinzi nambari moja wa wa amani na utulivu wa nchi.

Kinyume chake, utashi wa viongozi ni adui nambari moja wa amani na utulivu wa nchi. Tujifunze kuheshimu sheria hata kama zinaathiri kundi fulani linalotunufaisha ilimradi heshima hiyo inalinda maslahi ya nchi.

Kwa kadiri tunavyoruhusu upuuziaji wa sheria kwa kukumbatia utashi wa viongozi ndivyo tunavyoangamiza misingi ya amani na utulivu.

0 comments:

Post a Comment