| ||||||
Session No | Principal Question No | To the Ministry of | Sector | Date Asked | ||
4 | 12 | AGRICULTURE, FOOD SECURITY AND CO-OPERATIVES | Food/Agriculture | 14 June 2006 | ||
Kwa kuwa tarehe 4/3/2006 Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, alitoa taarifa kwa umma juu ya kuwepo kwa mlipuko wa viwavi jeshi nchini, lakini kukawa na utata mkubwa kati ya taarifa iliyotolewa Wizarani kupitia barua ya Mtabiri wa Viwavijeshi kwa Katibu Mkuu yenye Kumb. Na. KI/PF/ 39097 ya tarehe 27/2/2006 kuhusu ombi la kustaafishwa kwa manufaa ya umma kwa sababu ya ubadhilifu wa fedha zilizopangwa kwa ajili ya viuatilifu kwa msimu wa 2004/2005 na 2005/2006 na kwamba utabiri wake kama mtaalum ulipuuzwa na wahusika kulindwa:- (a) Je, ni kiasi gani cha fedha kilitumika hadi mwisho wa mwaka wa fedha kutoka kwenye Vote 43, Sub-vote 201 yenye shilingi 1,898,720,000 zilizoidhinishwa kwa mwaka 2004/2005 kama ilivyo kwenye kasma ndogo 2611229 Insecticide (OC) na katika kipindi hicho na hadi kufikia tarehe 13/2/2006 kulikuwa na milipuko mingapi, wapi kwa majina na ni fedha kiasi gani zimetolewa kutoka kwenye kasma ndogo kwa ajili ya HQ Kibaha, Morogoro, Arusha, Dodoma, Mbeya, Shinyanga, Kilimo Anga, TPRI, nje ya fedha zilizopelekwa baada ya mlipuko wa Desemba, 2005? (b) Je, ni aina gani za dawa zimeagizwa nje ya nchi na ni waagizaji gani waliopewa leseni ya dawa hizo ikiwa uingizaji wake unasemakana ni controlled na kwamba taarifa ya Katibu Mkuu inaeleza kuwa dawa hizo zimenunuliwa ndani ya nchi, zenye namba zipi katika kipindi hicho hasa zilizo import viuatilifu hivyo? (c) Kwa kuwa Katibu Mkuu katika taarifa yake ameeleza kuwa dawa hizo zimenunuliwa ndani ya nchi, je, Serikali inasema nini kuhusu leseni zilizotolewa na Wizara kuingiza dawa nchini mfano leseni yenye kibali Na. 446 Na.00000446 kati ya tarehe 21/2/2005 na tarehe 21/8/2005 na dawa hizo zilipelekwa kwenye Mikoa ipi kwa mgao gani kati ya kipindi kipi? |
JIBU
Answer From Hon. Chibulunje, Hezekiah Ndahani AGRICULTURE, FOOD SECURITY AND CO-OPERATIVES |
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dr. Wilbrod Peter Slaa, Mbunge wa Jimbo la Karatu, lenye sehemu (a) (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Katika mwaka wa 2004/2005 jumla ya shilingi 1,896,724,100 zilitengwa kwa ajili ya kununua viuatilifu ili kudhibiti milipuko ya visumbufu vya mimea ikiwa ni pamoja na nzige wekundu, viwavijeshi, kweleakwelea, panya na panzi kunuka. Kwa bahati nzuri katika msimu wa mwaka 2004/2005, milipuko ya viwavijeshi haikuwa mikubwa kama ilivyotabiriwa. Kwa hiyo, Wizara ilitumia shilingi 1,412,319,105 kwa ajili ya kudhibiti visumbufu vya mimea. Kati ya fedha hizo shilingi 770,430,969 zilitumika kununua viuatilifu, shilingi 10,000,000 zilitumika kununua mafuta ya ndege, shilingi 330,439,400 zilipelekwa katika vituo vya sehemu ya afya ya mimea Dodoma, Mbeya, Shinyanga, Arusha,TPRI Bio Control - Kibaha na Rodent Control Centre - Morogoro. Aidha, shilingi 301,448,735.9 zilitumika Makao Makuu ya Wizara kwa ajili ya kuratibu na kuendesha operesheni za udhibiti wa visumbufu. Shilingi 484,404,995 zilizobaki zilitumika kukamilisha michango ya mwaka 2004/2005 kwa shirika la kudhibiti nzige wa Jangwa la Afrika Mashariki na shirika la kudhibiti nzige wekundu la Afrika ya Kati na Kusini ambayo nchi yetu ni mwanachama.
Hadi kufikia tarehe 13/02/2006 jumla ya milipuko 26 ya viwavijeshi ilikuwa imetokea katika Mikoa ya Mbeya (Mbarali, Kyela, Rungwe, Ileje, Mbozi, Mbeya Mjini, Chunya, Mbeya Vijijini, katika Mkoa wa Iringa vilitokea (Ludewa, Iringa, Kilolo, Njombe na Mufindi) katika Mkoa wa Ruvuma vilitokea (Mbinga, Namtumbo na Tunduru) na huko Morogoro vilitokea (Kilombero, Ulanga, Mvomero, Kilosa Morogoro Vijijini), katika Mkoa Dodoma (Kongwa) katika Mkoa wa Mtwara (Masasina Newala) na katika Mkoa Lindi (Nachingwea, Rungwa). Kwa kawaida fedha hupelekwa vituoni baada ya ununuzi wa viuatilifu kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2005/2006, hakuna fedha zilizopelekwa vituoni kabla ya mwezi Desemba, 2005 kwa sababu taratibu za ununuzi wa viuatilifu zilikuwa hazijakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2005/2006 Wizara ilitangaza zabuni za ununuzi wa viuatifilifu mbalimbali vikiwemo viuatilifu vya kudhibiti viwavijeshi na makampuni yaliyoshindwa na kutunukiwa zabuni ni kama ifuatavyo:-
(i) Viuatilifu aina ya Chloropyriphos 48% EC na Chloropyriphos 24% ULV vilitolewa na Mukpar Tanzania Ltd. tarehe 10/2/2006 na 18 Aprili 2006. Deltamethrin 0.5% ULV na Chloropyriphos 48% EC zilitolewa na Bajuta Vet. Agro tarehe 06/03/2006 na viuatilifu aina ya Fenitrothion 50% EC na Diazinon 60% EC vilitolewa na Bytrade Tanzania Ltd. tarehe 18/04/2006. Makampuni yote haya na viuatilifu vilivyotolewa vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu haitoi leseni za kuingiza kiuatilifu nchini bali hutoa kibali cha kuingiza kiuatilifu nchini (permit to import pesticide). Kibali Na. 446 anachouliza Mheshimiwa Mbunge ni cha kampuni ya Mukpar Tanzania Ltd. ambacho kilitolewa tarehe 21/2/2005 kwa kipindi cha miezi sita yaani hadi tarehe 21/8/2005. Kibali hiki kinahusu uingizaji nchini wa lita 10,000 za kiuatilifu aina ya Chloropyriphos 24% ULV. Wizara yangu ilinunua lita 8500 tu za kiuatilifu hicho ambazo zilisambazwa kama ifuatavyo: Dodoma lita 1000 tarehe 19/6/2005, Mbeya lita 1000 tarehe 6/9/2005, Dodoma lita 1000 tarehe 31/10/2005, Singida, Tanga na Morogoro lita 500 kila Mkoa na zilitolewa tarehe 7/12/2005, Mbeya lita 1,000 tarehe 3/1/2006, Mtwara lita 400 tarehe 13/1/2006, Lindi lita 500 tarehe 13/1/2006, Mbeya lita 1000 tarehe 19/1/2006 Masasi lita 100 tarehe 26/1/2006 na lita 200 tarehe 28/1/2006.
Aidha, Shinyanga ilipewa lita 150 tarehe 31/1/2006, Morogoro lita 200 tarehe 1/2/2006, Iringa lita 50 tarehe 1/2/2006 na Rwangwa lita 100 tarehe 1/2/2006, Nachingwea ilipata lita 100 1/2/2006, Morogoro lita 40 tarehe 3/2/2006 na lita 100 tarehe 9/2/2006 na Dodoma lita 60 tarehe 20/2/2006.
0 comments:
Post a Comment