Thursday, September 2, 2010

FOS - TAARIFA MUHIMU

FRIENDS OF SLAA (FOS) NI NINI

Ni muungano wa waTanzania ambao unawajumuisha watu wa makundi yote, bila kujali dini, jinsia, rangi wala itikadi zao. Nia halisi ya muungano huu ni kuleta mabadiliko muhimu ya kiuongozi katika nchi yetu ili kuiwezesha kujenga serikali imara na shirikishi inayowajibika kwa wananchi wake. Ili kufanikisha hayo ni muhimu kuwa na vyama vya siasa makini, vyenye nguvu na uwezo wa kushika dola na kuondoa ukiritimba wa chama kimoja katika kushika madaraka yote ya uongozi wa nchi kila inapotokea uchaguzi mkuu.

Friends Of Slaa (FOS) inaamini kuwa, mgombea wa uRais aliyepitishwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, Ndugu Dr. Wilbroad Slaa, ni mgombea makini, jasiri, na mwenye sifa nyingi za kutosha kuubadili uongozi wa Tanzania kwa kuiongoza na kuifanya iwe na mafanikio makubwa kiuchumi, kidemokrasia, kiulinzi, kisheria, kijamii na katika kuleta mshikamano kati ya wananchi wote na jumuia za kimataifa.

Friends Of Slaa (FOS) inajitolea kwa hiari, kutoa ushirikiano wa hali na mali katika kusaidia ushindi wa Dr. Wilbroad Slaa katika uchaguzi Mkuu wa uRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

NIA NA IMANI YA FOS

FOS inaamini kuwa Tanzania na wa Tanzania wana haki ya maisha bora zaidi yenye uhakika na yanayoweza kudumu kwa muda mrefu. FOS pia inaamini kuwa, Tanzania ni nchi iliyobarikiwa na hazina kubwa ya maliasili, ardhi na watu wenye utashi mwema na wenye uwezo wa kufanikisha malengo ya Taifa endapo watashirikishwa kutekeleza majukumu yao kwa utaratibu unaofaa, wa haki na unaokubalika na jamii nzima.

FOS inaamini kuwa, uongozi wa nchi una mapungufu makubwa ambayo yanahitaji mabadiliko ya haraka. FOS inaamini pia kuwa, msingi ya utawala inahitaji marekebisho makubwa kama sio kuiangalia na kuiunda upya. Mabadiliko ya aina hiyo, hayawezi kupatikana kutokana na chama kilichohodhi madaraka na chenye ukiritimba,.

FOS inaamini kuwa, Dr. W. SLaa ana uwezo, nia, na kila sababu ya kumuwezesha kuongoza Taifa vizuri zaidi na kwa mafanikio makubwa.

FOS inaamini kuwa, iwapo chama kimoja kitaendelea kuwa na nguvu kubwa sana, kupata ushindi mkubwa sana wa Rais, ubunge na madiwani, ipo hatari kubwa ya kujenga udikteta wa kuchaguliwa na wananchi. Hayo yamekwishaanza kuthibitika wazi wazi kutokana na kauli na matendo mbalimbali ya viongozi waliopo madarakani. Chama kimoja kuwa na hodhi kubwa kupindukia, inaondoa uwajibikaji, kusababisha kuzuka kwa vitendo vya rushwa na ufisadi kuzidi kukithiri. Vile vile, ukiritimba wa chama kimoja huzidisha utamaduni wa kulindana na kusafishana na matokeo yake ni tabaka la wachache kuendelea kuneemeka na kukaa madarakani kwa muda mrefu, maswahiba zao, watoto wao, marafiki zao kurithi nafasi mbalimbali za uongozi na kufaidika na rasilimali za nchi na kuwaacha wananchi walio wengi katika ufukara na umaskini uliopindukia.

Lengo letu ni kuondoa hodhi ya chama kimoja kwa manufaa ya watanzania wote bila kujali itikadi zao kwa kutoa ushirikiano wetu kwa kila hali, ili Dr. W. SLaa aweze kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 katika kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

SISI WANA FOS TUNADHAMIRIA KUFANYA YAFUATAYO

  • Kushirikisha kila mtanzania mwenye nia njema katika kuunga mkono juhudi za kusaidia kwa hali na mali ushindi wa Dr. W. Slaa
  • Kukusanya na kuwakilisha michango yote, ya mali, mawazo na kujitolea itakayotolewa na watu wote kwa nia ya kufanikisha ushindi wa Dr. W. Slaa katika kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
  • Kufanya kampeni ya kumnadi Dr. W. Slaa, wagombea wake wa viti vya Ubunge na Udiwani nchi nzima
  • Kumsaidia, kumtetea na kumsemea Dr. W. Slaa katika majukwaa yote nchini na nje ya nchi ili aweze kupata misaada na uungwaji mkono katika kufaikisha azma ya ushindi wa Urais
  • Kutoa elimu, kwa njia mbalimbali, ikiwemo vipeperushi, mabango, majarida na njia zozote zinazokubalika ili kufikisha ujumbe kwa walengwa kwa nia ya kuhakikisha ushindi wa Dr. W. Slaa.

LENGO LA FOS NA MATARAJIO YAKE

  • Kuondoa ukiritimba wa chama kimoja kuhodhi madaraka yote ili kutokomeza vitendo vya rushwa na ufisadi, kuongeza ufanisi na uwajibikaji, kuhakikisha kuwa raslimali zetu zinatumika kwa faida ya wananchi wote
  • Kuondoa hali iliyopo ya chama kimoja kulewa madaraka kwa kukaa madarakani kwa miaka mingi na hivyo kubweteka na kushindwa kuondoa umaskini
  • Kuleta changamoto na ushindani wa kweli katika kuhakikisha kuwa mageuzi ya kisiasa yanamfaidisha Mtanzania wa kawaida kwa kuongozea ushindani wa kisiasa katika kuwaletea maendeleo wananchi
  • Kuleta uwiano wa madaraka ili vyama vyote viweze kushiriki katika ujenzi wa taifa letu na hasa katika vita vya kupambana na umaskini
  • Tunadhamiria kuweka juhudi zetu pamoja katika kujenga serikali shirikishi ambayo kila mwananchi bila kujali itikadi ya chama chake atashiriki na kupewa nafasi ya kutoa mawazo yake
  • Kwa kutambua umuhimu wa mhimili mmojawapo wa utawala bora, tunadhamiria kuboresha utendaji wa Bunge letu tukufu kwa kuongeza wabunge kutoka vyama vingine ili tuwe na Bunge madhubuti ambalo litaweza kufanya kazi yake adhimu ya kuisimamia serikali na na kuiwajibisha pale inapobidi
  • Tunadhamiria kuongeza ufanisi na matumizi mazuri ya fedha katika halmashauri zetu mashirika ya umma na taasisi zingine za serikali katika kuhakikisha kuna ufanisi na matumizi mazuri ya fedha kwa kuhakikisha kuwa Bunge letu tukufu linaundwa na linawakilishwa na wabunge kwa kuzingatia sura ya nchi yetu

WAJIBU NA MAJUKUMU YA MUDA MREFU YA FOS

  • Wana FOS wana jukumu la kutoa michango ya hali mali katika kufanikisha uwiano wa utawala katika nchi yetu
  • Kuwahamasisha wananchi wengine na wapenzi wa uwiano wa utawala kuchangia kwa hali na mali katika kubadilisha mfumo mbaya tulio nao sasa
  • Kueneza sera na kuwahamasisha watanzania waelewe kuwa mfumo tulio nao sasa unafifisha demokrasia, hauleti ushindani na unachangia katika kuleta umaskini. Hivyo hawana budi kuunga mkono juhudi hizi ili kuleta utawala wa uwiano
  • Kujitolea katika kufanya shughuli mbalimbali ili kuwasaidia wagombea wa nafasi mbalimbali ili waweze kutupa utawala wa nchi wenye uwiano
  • Kutoa mawazo, mikakati na mbinu mbalimbali zitakazosaidia kwanza kufikisha ujumbe rahisi kwa wapiga kura, kunadi sera mbalimbali na kuzifikisha kwa wananchi, namna ya kuwafikia na kuongozea idadi ya wapiga kura watakaoleta mabadiko
  • Kunadi sera za wagombea kutoka vyama vingine ili tuweze kuwa na wabunge kutoka vyama mbalimbali vya siasa

MADHUMUNI YA MFUKO WA FOS:

Kugharamia na kulipia shughuli za uchaguzi kama vile gharama za usafiri, matangazo, air time, gharama za uchapishaji na vipeperushi na gharama zote nyinginezo zinazoambatana na shughuli za kampeni na uchaguzi.

UENDESHAJI NA USIMAMIZI WA MFUKO HUU

Ili kuwa na ufanisi na kuondoa urasimu, mfuko utaratibiwa na timu ya watu 4. Timu hii itaongozwa na Mratibu Selemani Rehani na wajumbe Dr Kitila Mkumbo, Steven Mmbogo, na Yona Maro. Ili kuhakikisha kuwa kuna uwazi na taarifa sahihi juu ya michango, matumizi na uendeshaji wa mfuko huu, FOS imefungua account katika benki ya CRDB; Jina la account ni M4C na account namba ni 01J108010100600. Watia saini “signatories” ni Anthony C. Komu na Mwenyekiti Freeman Mbowe. Hawa ndio wenye uwezo wa kuidhinisha malipo. Muhimu tusisitize kuwa tutatoa taarifa ya pesa taslimu, ahadi na matumizi kila wiki. Na taarifa hiyo itawafikia wana FOS wote.

Kwa kufahamu kuwa baadhi ya wananchi hawawezi kuzifikia huduma za kibenki, FOS imeanzisha utaratibu mwingine wa kuchangia kupitia M-PESA na ZAP. Usajili umekwishafanyika na hivi sasa unaweza kuchangia kupitia namba zifuatazo: Namba za M-PESA ni 0764 77 66 73 na inamilikiwa na Dr. Kitila Mkumbo. Namba za ZAP ni 0789 555 333 na inamilikiwa na Steve Mmbogo.

Michango yote itawasilishwa moja kwa moja katika account hii maalum na receipt itatolewa kwa mhusika. Endapo mchangiaji kwa sababu moja au nyingine atapenda kuchangia kwa utaratibu mwingine tofauti na huu wa kupitia katika benki, basi atawasiliana na mratibu au mjumbe kwa majadiliano ya namna nzuri ya kufikisha mchango huo kwa kuzingatia sheria, matakwa ya mchangiaji ikiwa ni pamoja na kulinda usalama wake. Timu hii italipa umuhimu mkubwa sana suala zima la usiri (confidentiality) pale inapokuwa ni muhimu kufanya hivyo.

Aidha, iwapo mchangiaji atapenda kufikisha mchango wake moja kwa moja kwa wagombea au mgombea Urais basi timu hii itajitahidi kuwasiliana na wagombea au mgombea ili kuangalia uwezekano wa kuwasilisha mchango huo kwa utaratibu huo. Mgombea wetu wa urais ametueleza kuwa atajitahidi pale inapowezekana kutenga muda wa kuweza kuwashukuru na kukutana na wale ambao watapenda kuwakilisha michango yao kwake.

Ili kufanikisha malengo yaliyoelezwa hapo juu, FOS imeazimia kufungua Blog ya Friend of Slaa ili kuweza kuwapatia jukwaa wana FOS kufanya kazi ya kuhamasisha na kuongeza idadi ya wapiga kura kwa Dr Slaa na kubadilishana mawazo na kuwasiliana kwa ukamilifu zaidi.

KAZI ZA KAMATI HII:

  • Kuweka rekodi ya ahadi zote zinazotolewa
  • Kuweka kumbukumbu na orodha ya wana FOS wote
  • Kufuatilia ahadi hizo na kuhakikisha kuwa zinatimizwa
  • Kutoa taarifa kwa wana mtandao wote juu ya ahadi, pesa taslimu zilizokusanywa matumizi na kiasi kilichobaki. Hii itakuwa ni pamoja na kueleza kikamilifu kuwa zinatumika kwa matumizi gani
  • Kamati hii itatoa taarifa kwa wiki mara moja

NAMNA YA UCHANGIAJI

Utoaji na uchangiaji wa fedha utafuata utaratibu na kanuni za Chadema. Kamati hii ni lazima ipate ushauri wa kisheria ili iweze kufanya kazi zake kwa mujibu ya sheria za uchaguzi na hasa sheria mpya ya matumizi ya fedha katika chaguzi.

HITIMISHO

Muda haupo nasi. Imebaki miezi mitatu tu. Hatuwezi kusubiri wala kupoteza muda. Tusimsubiri Dr. Slaa au Zitto au Mnyika kufanya haya. Wana majukumu mengi sana. Wakati wa kulalamika na kuorodhesha mapungufu umekwisha. Ni wakati wetu sasa kushiriki katika kuleta siasa zenye ushindani wa dhati. Ni sisi wenyewe ndio tunahitajika kufanya. Kwao tunachohitaji ni mungozo tu na kuhakikisha kuwa hatuleti migongano mbalimbali na tunahakikisha kuna udhibiti wa matumizi mazuri ya fedha.

Kamati hii inaweza kuja na mapendekezo ya events au matukio ambayo tunaweza kuyafanya kwa mfano tunaweza kupanua uchangiaji huu katika mikoa yote ya Tanzania. Tunaweza pia kuandaa tukio kubwa ambalo tunaweza kumkabidhi michango yetu Mhes. Dr. Slaa na tunaweza kulifanya hili katika mikoa mbalimbali.

Raslimali pesa ni muhimu. Lakini raslimali watu ni muhimu zaidi. Mabadailiko haya yanahitaji watu, yanahitaji ‘manpower’ ya kuweza kufanya majukumu mbalimbali. Tuwe tayari kujitolea muda ili tuweze kusaidia. Michango ya mawazo pia vile vile ni muhimu. Kubadilishana taarifa kila pembe ya Tanzania ni muhimu na kujitahidi kutoa elimu kila unapopata nafasi vile vile ni muhimu. Kueleza malengo na shabaha za Chadema ni muhimu zaidi.

KUJIUNGA GONGA


0 comments:

Post a Comment