Sunday, September 5, 2010

Dr. Slaa ni Mlei

Dr. Slaa ni Mlei

Dr. SlaaKwa muda mrefu sasa vyombo mbalimbali vya habari na watu binafsi wamekuwa wakieneza habari kuwa Dr. Willibrod Slaa ni Padre wa Kanisa Katoliki na kuwa kwa vile aliwahi kuwa Padre (Kuhani) ndani ya Kanisa hilo ina maana kuwa hadi leo hii yeye ni Padre kama walivyo mapadre wengine. Wengi wanaosema mambo haya wanaonesha kutokujua au hata kujaribu kujua mafundisho ya Kanisa Katoliki juu ya Upadre na jinsi gani mtu anaweza kuwa Padre na akauacha na kuwa Mlei kama Walei wengine.

Kanisa Katoliki linazo Sakramenti saba ambazo ni Ubatizo, Kipaimara, Komunio (Ekaristia), Upatanisho (Maungamo), Ndoa, Upadrisho (Ukuhani) na Mpako wa Wagonjwa. Sakramenti hizo saba zipo ambazo zinatolewa mara moja tu kwa mtu na nyingine ambazo zaweza kurudiwa. Tunaposema "kutolewa mara moja" maana yake ni kuwa mtu anapopatiwa uwezo na nguvu za kuanza kupokea neema za sakramenti hizo hilo hufanywa mara moja tu na hairudiwi tena (isipokuwa kama hakuna uhakika kuwa alishapokea mara hiyo ya kwanza). Hizi ni Ubatizo, Kipaimara na Upadrisho. Zingine ni zile ambazo mtu anapokea mara ya kwanza lakini katika maisha yake ya kila siku anarudia kupokea mara kwa mara kwa kadiri inavyohitajika. Hizi ni Ekaristia na Maungamamo japo nazo huanza kupewa mara moja tu na kutoka hapo ni kuendelea kuchota neema zake kwa taribu zinazotakiwa. Na zipo ambazo hufanywa upya kabisa kama vile hazijawahi kufanywa kabisa; hizi ni ndoa na mpako wa wagonjwa.

Siyo kusudio letu kuelezea Theolojia ya sakramenti hizo ila tunataka kuzungumzia hili ambalo linaonekana kuwashindwa watu kuelewa. Ni kweli Dr. Slaa alipewa Sakramenti ya Upadrisho ndani ya Kanisa Katoliki baada ya kumaliza maandalizi yake ya kazi hiyo. Upadre siyo kama kazi nyingine ambazo mtu "anasomea"; si sawa na Udaktari, Uwakili au Uhasibu. Upadre ni Sakramenti ya Ukuhani ambayo mtu anaandaliwa kuiingia na kuitumikia. Ndio maana kimsingi kabisa, hata mtu ambaye hajasomea kabisa mambo ya Theolojia na Filosofia anaweza akapewa Upadrisho. Lakini kwa miaka mia nyingi Makanisa (Mashariki na Magharibi) yamekuwa yakiwaandaa wale wanaotaka kuingia katika "Daraja Takatifu" kwa mafunzo maalum ya mambo ya dini, falsafa, utawala n.k Ukiondoa mafunzo ya Theolojia ya Katoliki mafunzo mengine ya Falsafa, utawala, au elimu nyingine yoyote ni sawa kabisa na mafunzo yanayotolewa katika vyuo vikuu vingine.

Mtu akishapata daraja ya Ushemasi na baadaye Upadre basi anakuwa ni "Kuhani Milele" na hakuna kitu chochote ambacho kinaweza kufanywa kuondoa daraja hilo. Hii huitwa "alama isiyofutika". Ni alama ile ile ambayo inapatikana katika Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara ambapo mtu akishabatizwa ubatizo wake hauwezi kurudiwa tena kwani alama hiyo ya neema haifutiki. Ni kwa sababu hiyo mtu ambaye ameshawahi kupata upadrisho ataendelea kuwa kuwa na alama hiyo milele.

Kuwa na daraja hilo katika nafsi haina maana mtu ni mhudumu wa altare tena yaani kuhani. Hivyo, mtu anaweza kuamua kuacha kabisa kazi ya upadre, akaamua kuasi, au akaamu kujiunga na dini nyingine au kutoamini kabisa uwepo wa Mungu, lakini ile alama haifutwi na milele anabakia nayo. Kwa maana hiyo, Padre wa Kikatoliki anaweza kuacha, kufukuzwa, kuachishwa kazi za kila siku za kutoa huduma ya Upadre lakini bado anabakia kuwa ni padre moyoni. Hivyo, mtu huyo aliyeacha hastahili kuitwa "Padre X" kwa maana ya mapadre ambao bado wako kwenye huduma. Ni sawa na Daktari aliyeacha kazi ya Udaktari au kufukuzwa Udaktari au Uwakili lakini bado mafunzo na uwezo wa kutoa huduma hiyo akawa bado anao japo haruhusiwi tena kufanya hivyo. Wapo watu ambao kutokana na mazoea wataendelea kumuita "Daktari" japo hafanyi tena huduma hiyo.

Jambo hili ni muhimu kulielewa. Mtu ambaye ameacha yeye mwenyewe upadre bila kurejeshewa hali yake ya ulei (yaani uumini wa kawaida) kwa mujibu wa taratibu za Kanisa basi mtu huyo bado ni Padre na haruhusiwi kupewa Sakramenti ya Ndoa. Hata hivyo, Kanisa Katoliki lina utaratibu wa kumfanya mtu aliyewahi kuwa padre kurejeshwa kwenye hali ya ulei (yaani kuondolewa kabisa kazi na haki ya kufanya kazi za upadre na kuwa muumini wa kawaida kabisa). Mtu ambaye ameondolewa upadre kwa utaratibu wa Kanisa na kibali cha Vatikani anaondolewa haki na majukumu yote ya mapadre wengine isipokuwa mambo mawili tu yaani useja (celibacy) na kusikiliza maungamo ya mtu aliyekaribu na kifo.

Hilo la useja linahitaji kibali kingine kuondolewa ili aruhusiwe kuoa. Hata hivyo kwa vile padre ni padre milele basi mtu aliyewahi kuwa Padre anaweza kusikiliza maungamo na kutoa msamaha kwa mtu ambaye yuko katika hatari ya kifo tu.

Mfano mzuri wa kuelewa hili ni aliyekuwa Askofu Ferdando Lugo wa San Pedro huko Paraguay. Askofu Lugo alitaka kuingia katika siasa kitu ambacho kinakatazwa na Kanuni za Kanisa Katoliki. Askofu Lugo aliomba Kanisa Katoliki limruhusu arejee katika hali ya Ulei ili aweze kushiriki katika siasa lakini Kanisa lilimkatalia lakini Lugo aliendelea kugombea na aliposhinda uchaguzi Mkuu wa Paraguay Kanisa Katoliki lilikubali kumuondolea Upadre wake na kumrejesha katika Ulei. Hivyo, Rais wa sasa wa Paraguay ni Askofu wa zamani wa Kanisa Katoliki ambaye alirejeshwa katika Ulei.

Hii ina maana ya kwamba, Dr. Slaa siyo tu ni mlei lakini anayo haki kama wakatoliki wengine walei kushiriki katika nafasi ya uongozi kwani hajavunja sheria yoyote ya Kanisa, wala hajaenda nje ya haki zake za kikatiba. Dr. Slaa sasa hivi ni muumini Mlei kama wengine na atakapoamua kupata sakramenti nyingine yoyote ya Kanisa ataweza kufanya hivyo kwa uamuzi wake yeye mwenyewe kwani alifuata taratibu za kanisa za kurejeshwa katika maisha ya mlei.

Hivyo, Dr. Slaa siyo mtumishi wa Kanisa Katoliki na siyo padre kwa maana ya kuwa anahaki na majukumu yote ya mapadre wengine. Yeye ni muumini Mlei ambaye kutokana na nafasi yake ya kuwa aliwahi kuwa padre anabakia na haki za waumini wengine walei ndani ya kanisa hilo na vile vile uwezo wa kusikiliza maungamano ya mtu aliye katika hatari ya kifo TU.

0 comments:

Post a Comment