Tuesday, October 12, 2010

Kwanini Dr. Slaa anawakosesha raha?

Mwitikio wa CCM, makada wake na wapenzi wake dhidi ya Dr. Slaa umenishangaza sana. Toka alipotangazwa zimetumika mbinu mbalimbali za kumharibu kisiasa hata kibinafsi na nusura kidogo zifanikiwelakini zilipojibiwa kimahiri ikawa ni kama wao CCM wanamtengeneza shujaa mbele ya macho yetu. Ka nzi kalikopita sehemu mbalimbali mwishoni mwa juma kamejikuta kanashindwa kutoa taarifa ya sababu ya mwitikio huu.

Hata hivyo kanadokeza kuwa kati ya vitu vyote vinavyowatisha ni masuala ya EPA na Meremeta. Masuala haya mawili hawataki kabisa yaangukie chini ya mtu kama Dr. Slaa ambaye tayari amejionesha kuwa licha ya kwamba hana madaraka kuwatolea uvivu watuhumiwa wa uhalifu bila woga jambo ambalo limemshinda mtu aliyeko madarakani.

Lakini japo hilo linaelezea kutishwa kwa waliko madarakani lakini halitoshi kuelezea kutishwa kwa Chama kizima na kuwafanya wawe kama wanapigwa na ubaridi. Ninajiuliza kwa kadiri siku zinavyokwenda yawezekana watawala wakalazimika kuanza kutumia mbinu za wazi za vitisho kama walivyofanya miaka ile walipoanza kuonesha filamu za mauaji ya kimbari ya Rwanda.

Lakini mbinu hiyo wameanza kuhisi haiwezi kufanikiwa kwani walitegemea wakihubiri juu ya umwagikaji damu basi watu wataanza kukwepa mikutano ya Slaa. Kinyume chake imekuwa kweli kwani watu wanachosema ni kuwa "hatudanganyiki".

Lakini ukweli bado unabakia kuwa kuna hofu ambayo haieleweki kwani siyo wana CCM tu bali hata taasisi nje ya CCM zinaanza kuonesha wazi kabisa kuhofia ajenda kali ya mabadiliko chini ya Dr. Slaa ambayo inavutia watu wengi zaidi (popular agenda).

Kilichowashangaza zaidi CCM kwa mujibu wa ka'nzi ni jinsi ambavyo wasomi (mijini) na wananchi wa vijijini wanavyokubaliana katika kumkubali Dr. Slaa. Huko nyuma watawala walitegemea utengano kati ya makundi hayo mawili huku baadhi ya kundi la wasomi likiiunga mkono CCM. Wanachofurahia hata hivyo ambayo inawapa matumaini kidogo ni kuwa bado CCM ni chama kinachokubaliwa na kupendwea na baadhi ya wafanya biashara ambao wanaamini katika chini ya CCM maslahi yao yanalindwa.

0 comments:

Post a Comment