Tuesday, October 12, 2010

Tamko la TCRA kuhusu ujumbe wa simu unaowachafua baadhi ya wagombea wa Uraisi 2010

Mamlaka ya mawasiliano nchini Tanzania, TCRA, imekiri kupata taarifa za kuwepo kwa ujumbe unaosambazwa kupitia simu za kiganjani ambao umekuwa ukiwahamasisha wananchi kutokuwachagua baadhi ya wagombea wa nafasi ya Uraisi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 31 Oktoba 2010.

Akihojiwa na TBC, Naibu Mkurugenzi wa TCRA, Richard Kayombo amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha namba hizo huku akitoa rai kwa Wananchi kutokuzijibu au kusambaza ujumbe huo.

"Tumepokea malalamiko mengi tu, na ujumbe unakuja kwenye namba ambazo 03588108226 na mwingine kwenye namba 03588976578. Kwa mwelekeo wa haraka haraka, hizi namba zinaonekana ni namba za nje ya nchi. Lakini kwenye teknolojia, chochote kinaweza kikatokea. Inawezekana ni kweli ni namba ya nje ya nchi, lakini laini inayotumika na mtu aliyeko kwenye nchi nyingine. Lakini vile vile, inawezekana ni ujanja wa simu kutoka kwenye mtandao" alisema Kayombo.

Hata hivyo, Kayombo alisema TCRA itazuia matumizi ya namba hizo kwa sasa mpaka uchaguzi utakapokamilika hapo Oktoba 31, 2010.

Aidha, wananchi wameaswa kutojibu wala kusambaza ujumbe wanaotumiwa katika simu zao ili kuepuka uwezekano wa kukumbwa na uchunguzi unaoendelea wa kubaini chanzo cha mtandao huo.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa Taarifa ya Habari ya saa mbili ya TBC, tarehe 11 Oktoba 2010.

www.wavuti.com

0 comments:

Post a Comment