Monday, October 18, 2010

Kampeni za vurugu hazitatusaidia, tuziache

HIVI sasa kumekuwapo na taarifa za vurugu za kushambuliwa kwa baadhi ya wanachama wa vyama mbalimbali watokapo au warudipo kwenye mikutano ya kampeni.

Juzi msafara wa magari wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mgombea ubunge wa jimbo la Hai, Freeman Mbowe, umeshambuliwa na kundi la vijana wanaosadikiwa kuwa ni wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wakati tukio hilo likiwa bado kwenye vichwa vya watu, vurugu kubwa zimetokea mkoani Arusha ambapo watu wanaodaiwa kuwa ni wanachama wa vyama vya Tanzania Labour Party (TLP) na Chama cha Demokarasia na Maendeleo (CHADEMA) walipigana baada ya mwanachama mmoja wa TLP kutangaza kuwa vyama vyote vilivyosimamisha wagombea ubunge Arusha mjini vimeungana na kumpigia ‘debe’ mgombea wa TLP.

Siku nne zilizopita mkoani Mara katika jimbo la Musoma Mjini, wafuasi wanaodaiwa kuwa wa CCM, waliwavamia wenzao wa CHADEMA na kuanza kuwakatakata mapanga wakati wakitoka kwenye mkutano wa kampeni ambao ulihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe.

Katika tukio la Hai, magari matatu yakiwemo ya wagombea udiwani kwa tiketi ya CHADEMA, Clement Kwayu na Gilbert Mushi; na la mfanyabiashara wa madini Sadiki Mnenee, yamemvunjwa vioo na pikipiki moja ilikatwa na kitu chenye ncha kali kwenye tanki la mafuta.

Matukio yote haya kwa kiasi kikubwa yametia doa kampeni zinazoendelea hivi sasa na yanaonyesha jinsi wanachama wa vyama walivyokosa uvumilivu wa kupingana bila kupigana kama inavyosisitizwa na viongozi wa vyama vya siasa.

Tunaamini kuwa matukio haya yasipodhibitiwa kwa kiwango kinachostahili dhana nzima ya uanzishwaji wa mfumo wa vyama vingi utatoweka na ile hofu waliyokuwa nayo Watanzania wakati wakipiga kura ya kuukubali au kuukataa mfumo huu utapata mashiko.

Sote tunakumbuka kuwa asilimia 80 ya Watanzania walipinga uanzishwaji wa mfumo wa vyama vingi kwa hofu kuwa utaleta vita na machafuko ya wenyewe kwa wenye kama ilivyokuwa kwa baadhi ya nchi.

Pamoja na upingaji wa uanzishwaji wa mfumo huo, Tanzania iliridhia kuanzishwa kwa vyama vingi kwa lengo la kupanua wigo wa demokrasia pamoja na kuongeza uwajibika wa serikali iliyoko madarakani.

Kwa kiasi kikubwa mfumo wa vyama vingi umesaidia kuchochea maendeleo kwa wananchi hasa kwa serikali iliyoko madarakani kujitahidi kuboresha baadhi ya sekta kwa lengo la kuepuka kuwapa mwanya wapinzani.

Vurugu zilizoanza kutokea hivi sasa inawezekana zinafanywa kwa mkakati maalum uliondaliwa na baadhi ya vyama kwa lengo la kutia dosari jimbo fulani ili kitokee kisingizio cha kutofanyika kwa uchaguzi au kufutwa kwa matokeo husika.

Tunamini kuwa vyama vya siasa na wananchama wake wanapaswa kueleza sera na ilani zao ambazo zitashindanishwa lakini si kuandaa mipango ya vurugu wanapoona wanazidiwa na vyama vingine.

Tunaviomba vyombo vya dola kuwa vikali dhidi ya watu wanaobainika kufanya vitendo hivi bila kujali kama wako kwenye chama tawala au umaarufu wa aliyefanya kitendo hicho.

Kama vyombo vya dola havitakuwa makini katika kuwashughulikia watu hao, wananchi na wanachama watajichukulia sheria mkononi na mwisho wake nchi haitoweza kukalika.

Katika matukio ya Arusha na Musoma Mjini, baadhi ya watuhumiwa wa vurugu hizo wanashilikiwa na jeshi la polisi, hivyo tunaomba iwapo watathibitika kutenda vitendo hivyo wapewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia kama hiyo.

Tunaamini kuwa upigaji wa kura ni muhimu kwa sababu kila mwananchi mwenye sifa zinazotakiwa hupata fursa ya kumchagua kiongozi anayemtaka lakini zoezi hilo lisiwe ndiyo chanzo cha nchi kuingia katika mifarakano kama ilivyokuwa Kenya na Zimbabwe.

Tunaamini Tanzania haitofikia kama Kenya au Zimbabwe iwapo jamii, vyombo vya usalama na viongozi wa siasa watasisiza na kuwawajibisha watu wanaoshiriki kwenye vurugu wakati wa kampeni zinazoendelea hivi sasa.

0 comments:

Post a Comment