MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa, amesema kuwa ni maafa kwa Watanzania iwapo watakichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam alipokuwa kwenye mdahalo uliokuwa ukirushwa moja kwa moja na Televisheni ya ITV, ambapo alisema kuwa chama hicho kimewafanya Watanzania wawe maskini, kimeendekeza ufisadi na kimeshindwa kutumia rasilimali za nchi kwa manufaa ya walio wengi.
Dk. Slaa alisema hakuna sababu ya wananchi kuwa waoga wa kuwachagua viongozi wapya kutoka upinzani, kwa kuwa hakuna chuo kinachofundisha urais bali kinachoangaliwa ni busara, hekima, kuwashirikisha wananchi na kuweka mbele masilahi ya taifa.
“Kuichagua CCM ni kutafuta maafa zaidi ya haya tuliyonayo, tuache woga wa kuwachagua viongozi wapya, bila CCM Tanzania inawezekana, hata Mwalimu Nyerere alikuwa mpya wakati huo, lakini tulimpa uongozi kwa sababu tulimuamini atatuongoza vizuri,” alisema.
Dk. Slaa alimtupia lawama Rais Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM kwa vijana wa chama hicho kufanya fujo kwenye mikutano ya kampeni ya wagombea wa CHADEMA.
Alisema vijana hao wa CCM maarufu kama Green Guard wamekuwa wakipata mafunzo ya kijeshi, kinyume cha Katiba na sheria za nchi na baadaye huenda kufanya vurugu katika mikutano ya CHADEMA pasipo askari kuwachukulia hatua zozote.
Alisema Rais Kikwete ana jukumu kubwa la kukomesha kundi hilo la vijana kwa sababu yeye ni Amiri Jeshi Mkuu na Mwenyekiti wa CCM, ambayo inawalea na kuwapa mafunzo vijana hao.
Dk. Slaa alisema wananchi wasidanganywe kuwa vyama vya upinzani vinaweza kuyumbisha au kuleta machafuko hapa nchini, bali hali hiyo itaweza kuletwa na chama tawala, ambacho kinakuwa kimeshikilia serikali na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Mimi sitaki kwenda Ikulu huku damu ya wananchi wangu ikiwa imemwagika au wengine wakiwa na vilema, nataka niende Ikulu kwa amani na furaha ya wananchi wangu walioshiriki kwenye kampeni na uchaguzi uliokuwa na mazingira bora,” alisema Dk. Slaa
Ufisadi
Alibainisha Rais Kikwete na CCM, wameshindwa kuwashughulikia mafisadi kwa sababu wametokana na zao hilo, kwani hata fedha zilizotumika kumuingiza Ikulu zilipatika kwa wizi uliofanyika katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).
Alisema ana ushahidi wa nyaraka wa Kampuni ya Kagoda ambayo ilikwapua zaidi ya sh bilioni 40 na benki zilizohusika katika malipo hayo zinajulikana, lakini mpaka sasa wahusika hawajafikishwa mahakamani.
Alibainisha kuwa Rais Kikwete anahusika na wizi huo, ndiyo maana mpaka sasa hajaweza kumfikisha mahakamani yeye (Dk. Slaa) ambaye alitaja hadharani orodha ya watuhumiwa wa ufisadi akiwamo Rais Kikwete.
“Ninachokisema mimi huwa nina uhakika nacho, kwa sababu nyaraka ninakuwa nazo, mpaka leo hii nadunda mitaani kwa sababu najua Kikwete hawezi kunifikisha mahakamani,” alisema.
Alibainisha kuwa Rais Kikwete hana ubavu wa kupambana na ufisadi kwa sababu hata wale wanaotuhumiwa kushiriki vitendo hivyo huku wengine kesi zao zikiwa mahakamani amewanadi katika mikutano yake ya kampeni kwa kuwaeleza wananchi wawachague kwa madai ni wachapa kazi.
Alisema ni jambo la kusikitisha serikali iliyopo madarakani inabariki wizi wa sh bilioni 155 kupitia Kampuni ya Meremeta ambayo inadaiwa kuwa ilikuwa ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisimama bungeni kutetea wizi huo kuwa fedha hizo zilitumika kwa masuala ya jeshi, ilhali jambo hilo si la kweli, bali zililiwa na wajanja wachache, ambapo fedha hizo zilipitia benki moja ya Afrika Kusini.
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alisema elimu bure kwa Watanzania ni jambo linalowezekana, kwa sababu serikali inazo rasilimali za kutosha lakini kutokana na kutozigawanya inavyotakiwa, jambo hilo limeshindikana.
Alisema Tanzania kamwe haitaweza kujikwamua katika lindi la umaskini kama wananchi wake hawatapata elimu bora kama wanayoipata watoto wa vigogo au wa nchi za Uganda na Kenya.
Alibainisha kuwa hivi sasa hapa nchini kuna matabaka matatu katika sekta ya elimu, ambapo tabaka la kwanza lina uwezo wa kuwasomesha watoto wao nje ya nchi huku lile la pili likiweza kuwasomesha katika shule za kata zilizojengwa hivi sasa.
Tabaka la tatu ni lile ambalo halina uwezo wa kusomesha watoto wao hata katika shule za kata.
Mikataba ya madini
Alisema iwapo atapewa fursa ya kuwa rais ataipitia mikataba yote ya madini na kuirekebisha, ili iweze kuwanufaisha zaidi wananchi kama ilivyo kwa wenzao wa Botswana.
Aliongeza kuwa alikwisha kufanya mazungumzo na watu kutoka nchi za nje ambao walimwambia ni jambo la ajabu kwa Tanzania kupata mrabaha wa asilimia tatu katika sekta ya madini wakati wawekezaji wakipata asilimia 97.
Mabadiliko ya Katiba
Alibainisha kuwa katika miaka yake mitano ya mwanzo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali atahakikisha anaifanyia mabadiliko Katiba ya nchi ili kumpunguzia madaraka rais, ambaye amekuwa akiteua watendaji wengi.
Alisema haoni kazi za manaibu mawaziri, hivyo akiingia madarakani atahakikisha hawateuwi na fedha zilizokuwa zikitumika kuwahudumia zitapelekwa kusaidia ujenzi wa shule, zahanati, barabara na huduma nyingine za kijamii.
Utegemezi wa bajeti
Alisema serikali yake itajitegemea katika matumizi ya kawaida, ikiwemo kulipana mishahara na shughuli nyingine, lakini itaendelea kushirikiana na wafadhili na wahisani ili wasaidie miradi mikubwa.
Aliongeza kuwa serikali yake haitakuwa na kisasi na mtu yeyote, lakini pia haitakuwa na huruma na wanaotumia rasilimali za taifa kwa masilahi binafsi.
Masilahi ya wafanyakazi, wazee
Alisema ataboresha masilahi ya wafanyakazi kwa kupandisha mishahara kulinga na taratibu watakazoziweka lakini pia atashusha gharama za sementi (saruji) na bati, ili wafanyakazi waweze kujenga nyumba.
Kuhusu suala la wazee, alisema ataanzisha utaratibu wa kutoa pensheni bila kujali kama walifanya kazi au la, kwani jambo hilo lilifanyiwa utafiti na watu wa Help Age International Tanzania na likaonekana linawezekana.
Kukubali matokeo ya uchaguzi
Alisema atawaandaa wanachama wake kukubali matokeo iwapo mazingira ya kufanyika kwa uchaguzi yatakuwa huru na haki lakini hawezi kufanya hivyo ikiwa hujuma zitafanyika.
Alisema kocha yeyote ambaye atasema kabla ya kuanza kwa mchezo kuwa timu yake itatoka sare au atayakubali matokeo, atakuwa na matatizo, kwani inawezekana akiingia uwanjani refarii akaipendelea timu pinzani.
Kulinda kura
Alisema jukumu kubwa la kulinda kura ni la mwananchi mwenyewe, kwa sababu kura yake ndiyo maji, barabara na huduma nyinginezo, hivyo ni vema kila mmoja akazilinda kama wakazi wa Kigoma, Karatu, Mpanda Kati, Moshi Mjini na kwingineko.
Aionya NEC
Alisema anashangazwa na majibu ya Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Rajabu Kiravu, kuwa yeye (Slaa) ni muongo, kwa kumpa tuhuma za kuwapo kwa kontena la kura lililokamatwa Tunduma likiwa na kura za mgombea wa CCM.
Alisema alichopaswa kufanya Kiravu ni uchunguzi, si kukurupuka, lakini ni vema akaelewa kuwa Watanzania wa mwaka 2000 si wa sasa, mambo yamebadilika
Alibainisha kuwa Kiravu alipaswa awaeleze wananchi imekuwaje karatasi hizo zichapwe nje ya nchi wakati Waziri anayeshughulikia masuala ya Uratibu na Bunge, Philip Marmo, alisema zitachapishwa na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, lakini hivi sasa zinachapishwa Uingereza.
0 comments:
Post a Comment